Kadhia ya 'Sheikh' kuritadi Mwidu:
 
Markaz Gongo la Mboto yalaumiwa kukanusha ukweli
 

Na Mussa Ally, Morogoro

VIONGOZI wa Msikiti wa Kijiji cha Mwidu wametoa lawama kwa viongozi wa Markaz Gongo la Mboto kwa kuukanusha ukweli na kughushi barua kwa kutumia jina la Imamu wa kijiji hicho.

Wakiongea na Mwandishi wa habari hizi Kijijini hapo Jumatatu wiki hii, muasisi wa Msikiti huo Bw. Shaaban Machupa na Imamu Sheikh Hassan Said Hassan walionyesha masikitiko makubwa juu ya taarifa za Fysabilil-lah Tabligh Markaz Gongo la Mboto, na ile iliyodaiwa kuwa ni barua ya Imamu wa Mwidu kukanusha habari (zilizochapishwa na gazeti hili toleo namba 192 ukurasa wa 15 la Machi 12-18, 1999, Dhulkada 1419 zikikanusha habari (sio makala za toleo) zilizoelezea kadhia ya "Wakristo kuritadisha Waislamu Mwidu" akiwemo 'Sheikh' Nadhiru Mohammed Lutta.

Viongozi walisema kuwa ' Nadhiru aliye "murtad" sasa aliletwa na aliyekuwa kinara wa Tabligh za Markaz hiyo katika eneo la Mwidu Bw. Ameir Baba na kumtambulisha kwa Waislamu hadi walipokwaruzana ndipo Nadhiru alipohamia kwa Mwanafiysabilil-lah mwingine Sheikh Mzee, huku akifanya shughuli mbalimbali za Kiislamu pamoja na mwenyeji wake Sheikh Hassan Said Hassan kama vile kusalisha, kuhutubu na kufundisha darasa la watu wazima na watoto wasiopungua 60.

Naye Bw. Shaaban Machupa aliikosoa Markaz Fiysabilil-lah kwa kuwanukuu visivyo katika barua zao (Markaz) gazetini.

"Sisi tulimwambia mjumbe wa Markaz kuwa Nadhiru ameritadi kwa njaa yake, ametukuta na ametuacha tulivyo.Hakuna Muislamu 'muumini' aliyemfuata au atakayemfuata Nadhiru ila wale wasio na msimamo na wenye mwelekeo wa kipagani. Na tukamtaka aonane na mwandishi wa habari husika endapo kuna kitu alichoandika kimegusa kituo chao (cha Markaz); hawakufanya hivyo, badala yake wanatugonganisha na Waislamu wenye nia ya kutusaidia", alisema mzee Machupa.

Wakati huo huo, chama cha waalimu wa Madrasa Morogoro kimeitikia kilio cha Mwidu kwa kutuma mwalimu Jumamosi iliyopita ambaye amepokelewa na Waislamu wa Mwidu na amekwisha aanza kazi rasmi kijiji hapo.

Mwalimu huyo Bw. Moshi Juma amepewa kazi ya kufunza maarifa ya Kiislamu na kufanya shughuli zote zinazohusiana na Uislamu kijijini hapo akisaidiana na uongozi wa Msikiti.

Nao viongozi wa chama cha waalimu wa madrasa Morogoro wamewaomba Waislamu kumpa nguvu kwa hali na mali mwalimu huyo na ikiwezekana waongeze waalimu wengine wasaidie kuliendesha jahazi la Mwidu.

Halikadhalika viongozi wa Msikiti wa Mwidu wametoa shukrani zao za dhati kwa ANNUUR kutangaza hali halisi ya Mwidu, jambo ambalo limewasaidia kupata mwalimu toka Morogoro atakayewaongezea nguvu ya kuinua na kuuhami Uislamu kijijini hapo.

Muasisi wa Msikiti wa Mwidu Bw. Shaaban Machupa ameliambia gazeti hili kuwa walikuwa na gari iliyokosa mwelekeo hasa kwa vizazi chipukizi, hivyo akawaomba Waislamu wa Morogoro na nchi nzima kwa ujumla wasiridhike tu kutuma mwalimu, bali pia washirikiane na wana Mwidu kuangalia maslahi ya mwalimu na kuweka mipango imara ya baadaye ya kuboresha Uislamu Kijijini hapo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Msikiti Mkubwa wa kudumu, shule ya watoto wadogo, msingi, sekondari na kituo cha Kiislamu cha kutoa huduma za kijamii kiujumla.

"Hapa mwanangu tunayo ardhi ya kutosha, ila usaidizi ndiyo tatizo", alisema Bw. Machupa.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook