Na Mwandishi Wetu, Geita
WIMBI la wasiokuwa Waislamu kuufahamu na kuufuata kumeibuka kwa nguvu katika wilaya nzima ya Geita na kupokea idadi ya wasiokuwa Waislamu kusilimu.
Katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka jana, ANNUUR ilipokea taarifa mbalimbali za makundi kuingia katika Uislamu wakati wa mfungo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo ANNUUR imezipata kutoka wilayani Geita ambapo imepatikana orodha ya majina ya waliosilimu majina yao ya zamani, dini (madhehebu) zao za zamani ni kama ifuatavyo.
Kwa jumla yao Wakatoliki 27, African Inland Church (AIC) wanane, Tanzania Assemblies of God (TAG) watu 13, Evangelical Assemblies of God (E.AG) watu sita, na madhehebu ambayo Mwandishi hakuweza kuyafahamu kirefu chake.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Bakwata Wilaya ya Geita Ustadh Mikidadi Juma Feruzi kwa furaha, alipinga vikali propaganda zinazoenezwa na vyombo vya habari na wasiopenda maendeleo haya ya wananchi kupokea maoni ya upande wanaopingana nao,
Alisema wote waliosilimu walikataa wazi kabisa kwamba hawakushawishiwa wala kuahidiwa chochote, ila baada ya kuona ukweli ndipo walipoamua kwa hiari yao.
Aliwaomba wahadhiri wa dini zote kuwa na nidhamu bila ya jazba kuelimisha, kwani mambo ya imani sio ya haraka.
Ustadh Mikidadi Juma Feruzi alitoa wito kwa vikundi mbalimbali vya ulinganishi wa dini kuiga mfano wa AL-MALLID tawi la Mwanza.
Alisema kuwa mafanikio hayo yote ni mara baada ya kundi hili kuweka kambi na kufaulu kuzungumza na waumini wa madhehebu mbalimbali wilayani Geita.
Alisema kuwa binadamu wana akili zao zinazopima ukweli na kutoa uamuzi kwa mujibu wa imani zao. "Hakuna kulazimishana ndani ya dini", alinukuu kipande cha aya ya Qur'an.
Baadhi ya watu waliotoa maoni yao mjini Geita walishangazwa na taarifa za mara kwa mara kuwa amani na utulivu vitavurugika kama mihadhara itaruhusiwa kila mahali.
Walisema maadili yamevurugika kwa kuwa kweli haisemwi, watawala na wanasiasa wanasema yanayowafurahisha watu waovu, hakuna anayepigia kelele ulevi, uzinzi na mambo machafu yanayohimizwa ndani ya jamii yetu.
Shukrani za jumla zilitolewa kwa kundi la AL-MALLID - Mwanza na kuwaomba wazidi kufikisha ujumbe wa Allah (s.w.) kwa watu wote na waungwe mkono wa hali na mali.
Walisema kuwa ni lazima mali
zitumike ili kuhakikisha ujumbe muafaka kwa walengwa wote, dini bila ya
kutumia mali zetu haendi.
Na N. Omary
KUNDI jipya la mihadhara ya dini ya Kiislamu la Umatil-Istiqama la jijini hivi karibuni limekuwa likiendesha mhadhara maeneo ya Kigamboni wilaya ya Temeke na kufanikiwa kuwarejesha Wakristo 11 katika Uislamu.
Akiongea na mwandishi wa habari hizi Katibu Mkuu wa kikundi hicho Ustadh Swalehe Rashid aliwataja Waislamu hao kuwa ni pamoja na Abdallah Bernard (zamani aliitwa John Bernard) aliyekuwa muumini wa dhehebu la Katoliki ambaye baada ya kuingia katika Uislamu alipata misukosuko mingi toka kwa jamaa zake na wakafikia hatua ya kutangaza kumuua kwani ameasi dini ya Yesu na ameingia dini ya mashetani.
Hata hivyo Ustadh Swalehe alisema kwa hivi sasa yuko mikononi mwa Waislamu na watamlinda.
Aidha Waislamu wengine wameomba
majina yao yasiandikwe gazetini kwa kuhofia vibarua vyao visipotee baada
ya kusikia wamesilimu.
Na Muhibu Said
WAKATI serikali ikiendelea kuhaha kupiga marufuku mihadhara ya Waislamu, Kituo cha Kiislamu cha Khidmat Da'awat cha jijini kinachoongozwa na Ustadh Magezi Shabani kinaendelea na mihadhara yake katika wilaya za Temeke na Kinondoni ambapo hadi sasa Wakristo zaidi ya 80 wameripotiwa kusilimu.
Idadi hiyo inayoelekea kwenye mamia ya Wakristo wanaorejea kwenye Uislamu wilayani Temeke, inajumuisha Wakristo 16 waliosilimu kufuatia mhadhara uliofanywa na kituo hicho katika uwanja wa Temeke Mwisho mnamo mwezi Januari, mwaka huu.
Wengine ni Wakristo waliosilimu kufuatia muhadhara uliofanyika katika uwanja ulio jirani na shule ya sekondari ya Nurulyakin Temeke - Yombo, mwishoni mwa mwezi Februari na mwanzoni mwa mwezi Machi, mwaka huu na 10 waliokwisha kusilimu katika mhadhara unaoendelea hivi sasa katika Msikiti wa Hijra uliopo Mbagala Zakhem, Jijini Dar es Salaam.
Aidha, idadi ya Waislamu hao wapya imekuwa ikiongezeka kadri mihadhara inayofanywa na kituo hicho inavyoendelea kushamiri siku hadi siku.
Wakati juhudi za kituo hicho kuwarejesha walioghafilika kwenye Uislamu zikifanyika, serikali kupitia Kamanda wake wa polisi wilaya ya Kinondoni (SSP) A.N. Magoti katika kile kilichotafsiriwa na wengi kama juhudi za kulihami Kanisa, imepiga marufuku mhadhara wa kikosi kilichopo katika Msikiti wa Mikocheni 'B' hivi karibuni.
Akipiga marufuku mhadhara
huo ambao unafanyika Msikitini, Kamanda Magoti kupitia barua yake Kumb.
Na. KIN/A.24/60/Vol.111/3 ya Machi 22, 1999 amedai kuwa "kwa mujibu wa
K/F 40 (3) cha Police Force Ordinance Cap 322 kama ilivyofanyiwa marekebisho
na sheria Na. 3 ya 1995, kibali cha mhadhara wa kidini mlichoomba kimekatawaliwa
kufuatia sababu za kiusalama".
|
|