HALI ya mapambano kati ya Waislamu na vijana wa Daniel/Pius inahofiwa kuibuka wakati wowote lau hatua za haraka hazitachukuliwa kutatua mgogoro wa nyumba za Wakfu.
Fukuto la hatari hiyo limechochewa na taarifa zilizopatikana kwamba msimamo wa serikali ya mkoa ni kwamba nyumba ya Wakfu yenye mgogoro ni mali "halali" ya Bw. Pius Kipengele.
Imearifiwa kwamba msimamo huo wa serikali umeegemea hoja kwamba Bw. Pius alinunua nyumba hiyo kutoka kwa Bw. Daniel japo ni ya Wakfu kwa Masjid Mwinyi toka kwa marehemu Hajat Aziza Omar.
Kufuatia msimamo huo wa serikali kama ilivyoarifiwa kwamba ulitamkwa na Mh. Yusufu Makamba; polisi wameagizwa kumshughulikia Muislamu yeyote atakayeonekana katika nyumba hiyo.
Tangu agizo hilo litolewe Waislamu wamekuwa wakikamatwa mmoja mmoja na kufunguliwa kesi ya kuvamia nyumba ya Bw. Pius Januari 24, mwaka huu. Tarehe hiyo ndipo Waislamu walipokusanyika na kuisafisha nyumba hiyo pamoja na kumwombea dua Hajat Aziza bint Omar.
Aidha, vijana wa Daniel/Pius wakisaidiwa na polisi wamekuwa wakiweka doria katika nyuma hiyo No. 58 Mtaa wa Somali ambapo wamekuwa wakiwatia matatani wapita njia waliovaa kofia au akina mama wenye hijab.
Katika tukio moja kijana mmoja wa Kiislamu Bw. Mauji ilibidi apambane na kundi la vijana hao ambapo aliishia kujeruhiwa mkono.
Katika tukio jingine mama mmoja akiwa na hijab yake alifungiwa ndani toka saa 10 hadi saa 12 jioni ambapo wengine wawili waliwekwa juani masaa mawili.
Baadhi ya vijana wanaosaidiwa na polisi kulinda nyumba hiyo wamedai kwamba wao wamepewa ajira na Mchungaji Mtikila kulinda Kanisa lake.
Gazeti mmoja liliwahi kuripoti kwamba Mchungaji Mtikila amedai kwamba nyumba No. 58 (ya Wakfu) ni Kanisa lake na limevamiwa na Waislamu.
Ni maoni ya Waislamu wengi walioongea na gazeti hili kwamba lolote laweza kutokea mtaa wa Somali kupambana na vijana wanaojiita wa Mchungaji Mtikila kuizuia nyumba ya Wakfu kugeuzwa Kanisa.
Habari ambazo gazeti hili imezipata zinaeleza kwamba hivi karibuni kilifanyika kikao katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mh. Yusufu Makamba kuzungumzia mgogoro huo.
Pamoja na Bw. Makamba walikuwepo maafisa usalama wa taifa; makamanda wa polisi na viongozi wa Masjid Mwinyi.
Katika kikao hicho, uongozi wa Masjid Mwinyi ulitoa Hati ya kiapo yenye muhuri wa mahakama pamoja Stamp ya malipo ya Hajat Aziza, pamoja na nyaraka nyingine muhimu kuonyesha kwamba nyumba hiyo ni ya Wakfu.
Hata hivyo, mwisho wa mazungumzo Mh. Makamba anadaiwa kutoa agizo kwa polisi kumshughulikia Muislamu yeyote atakayeisogelea nyumba hiyo kwani ni ya Pius kwa vile kauziwa.
Ilipoulizwa iwapo ni halali mtu kununua mali ya wizi na kwamba je mtu akikamatwa na mali ya wizi nini hukumu yake, hapakuweza kupatikana jibu lenye kueleweka.
Aidha, Bw. Makamba amearifiwa kuwahimiza Waislamu kwenda mahakamani kwani ni kupitia mahakama Bw. Daniel alipewa nyumba hizo na yeye asingeweza kuingilia mahakama.
Hata hivyo Waislamu walioongea na gazeti hili; ni maoni yao kwamba Mh. Makamba bado angekuwa na uwezo wa kuutatua mgogoro huu hasa baada ya kupata vielelezo vyote muhimu.
Habari zaidi zimeeleza kwamba Mh. Makamba ameagiza apewe taarifa kwa maandishi ya nyumba hizo ili awasilishe tatizo hili kwa Mh. Rais Mkapa.
Gazeti hili liliwasiliana na Mh. Makamba kwa simu jana ofisini kwake ambapo Katibu Muhtasi wake alimwelekeza mwandishi awasiliane naye saa nane mchana.
Hata hivyo, mwandishi wa habari hizi
alipopiga tena simu saa nane mchana aliambiwa kwamba Mh. Mkuu wa Mkoa kaenda
kwenye zoezi la upandaji miti na hatapatikana ofisini hadi kesho (leo).
|
|