Na Mwandishi Wetu
IDADI ya waliokufa kufuatia uvamizi wa jeshi la polisi Mwembechai mwaka jana inahofiwa kuwa kubwa kinyume na ilivyotangazwa awali baada ya mtu mwingine zaidi kuripotiwa kuuawa katika kadhia hiyo.
Omar Rajab aliyekuwa mkazi wa Magomeni Mikumi Kisiwani ametajwa kuwa miongoni mwa waliouawa na maiti yake kusafirishwa na kuzikwa kimya kimya nyumbani kwao Muheza mkoani Tanga.
Mara baada ya Msikiti wa Mwembechai kuvamiwa na polisi mwaka jana vyombo vya habari viliripoti kuuawa watu wawili na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Aidha, majeruhi walifikishwa vituo vya polisi na kufunguliwa mashitaka kisha kuwahishwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu wakiwa chini ya ulinzi mkali.
Akifahamisha kifo cha Bwana Omar Rajab, mama mmoja aliyefika katika ofisi ya gazeti hili akiwa na mtoto wake mdogo begani na kujitambulisha kuwa ni mjane wa marehemu, alieleza kuwa siku ya tukio mumewe ambaye alikuwa dereva wa magari yanayokwenda mikoani alirejea safarini na kumuaga kwamba angekwenda kuswali sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Mwembechai.
Mama huyo aliyejifahamisha kwa jina la Maryma Rashid mkazi wa Manzese, Jijini, aliendelea kueleza kuwa ilipofika jioni ya siku hiyo rafiki wa marehemu mumewe alifika nyumba waliyokuwa wakiishi na kumfahamisha kwamba mumewe ni mahututi Muhimbili.
Asubuhi ya siku iliyofuata (Jumamosi Februari14) rafiki huyo wa mumewe alifika tena na kuwachukua yeye na ndugu wa kiume wa marehemu hadi hospitali ambako amedai mama huyo kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi ambao hawakuruhusu kwa urahisi kuingia Wadi waliyolazwa majeruhi.
Bi. Maryam ameeleza licha ya kuzuiliwa mara kadhaa walifanikiwa kuingia Wodini na kumkuta mgonjwa (majeruhi) akiwa katika "sakaraat mauti, hivyo hawakuweza kumsemesha.
"Kwa kweli ulinzi ulikuwa mkali, tulipita alipokuwa mgonjwa kama wapita njia", amedai mama huyo.
Aliendelea kueleza kuwa walilazimika kurejea nyumbani ili kusubiri kipindi cha jioni, hata hivyo wakati wajikitayarisha kwenda hospitali nyakati za jioni jamaa yule(ambaye hakutaka kumtaja jina) alifika tena na kuwaeleza kuwa Bwana Omar amekwisha fariki dunia.
"Tuliongozana na pamoja na ndugu wa marehemu mume wangu hadi Muhimbili ili tukachukue maiti kwa ajili ya mazishi", ameeleza Bi. Maryam ambaye kiasili ni mwenyeji wa pangani.
Hata hivyo, amedai mama huyo mazingira ya siku hiyo yalikuwa ya "mizengwe" mingi iliyoandamana na masharti kadhaa kabla ya kukabidhiwa maiti usiku wa siku hiyo.
"Kwanza tulizuiliwa tusichukue maiti lakini baada ya jitihada ya huku na kule tukapewa, tukatakiwa tuzike kimya kimya na tusitangaze kuwa amekufa kutokana na vurugu za Mwembechai", amedai Bi. Maryam huku akiwa akionekana mwenye hofu kubwa.
Kuhusu mazishi ya marehemu, mjane huyo amesema walikodi gari kwa kushirikiana na ndugu mkubwa wa mumewe aliyemtaja kwa jina la Juma Rajab na kusafirisha maiti hiyo hadi wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga ambako walizika siku ya Jumapili.
Mwandishi wa habari hizi alipomuhoji kwa nini alisita kutoa taarifa hizi kwa muda wote huo, Bi. Maryam alidai kuwa aliogopa vitisho walivyopewa wakati wakikabidhiwa maiti.
"Nimevumilia lakini kutokana na hali ngumu inayotukabili mimi na watoto wangu nililazimika kwenda Msikiti wa Mtambani mtu mmoja mrefu ambaye sikufahamu anaitwa nani wala wadhifa wake pale Msikitini akaniambia nije nieleze hapa", amedai mama huyo.
Amesema hivi sasa amelazimika kujihifadhi kwa jamaa yake maeneo ya Friends Corner baada ya kule walikokuwa wakiishi na marehemu mumewe kuhama kutokana na kushindwa kumudu kulipa kodi.
Uchunguzi zaidi juu ya taarifa za bi maryam unaendelea
Wakati huo huo, mtu mwingine amedaiwa kuuawa kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na polisi Mwembechai.
Marehemu huyo alizikwa kimya kimya na jamaa zake maeneo ya Mwananyamala Jijini siku chache baada ya tukio mapema mwaka jana.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umeonyesha marehemu huyo aliyekuwa akifahamika kwa jina la Bakari (Mluguru) alikufa baada ya kushindwa kupumua kutokana na hewa ya sumu ya mabomu ya machozi yaliyolipuliwa bila idadi katika kadhia hiyo.
Ndugu wa karibu wa marehemu Bakari wanaoishi Manzese jijini ambao ni wenyeji wa kata ya Mkoya milima ya Uluguru mkoa wa Morogoro wameliambia ANNUUR kuwa walilazimika kufanya mazishi haraka na kimya kimya kwa kuogopa kukamatwa kwa kuhusishwa na vurugu nyingine walivyoidhania ingetokea wakati wa mazishi.
Katika baraza la Id el fitr mwaka huu kamati ya kutetea haki za Waislamu ilionyesha kanda ya video iliyonasa matukio mengine ya mauaji yaliyofanywa na polisi Mwembechai februari 13, mwaka wa jana.
Katika matukio hayo wanaonekana polisi wakifyatua risasi za moto kadhaa na kuuwa watu wapatao wanne.
Wito umeendelea kutolewa kwa viongozi wa juu kuharakisha kuwachukulia hatua wale waliokiuka haki za binaadamu kwa kuuwa raia wasio na hatia.
Nayo ripoti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imelitaja jeshi la polisi Tanzania kuwemo katika orodha ya wavunjaji wa haki za binadamu duniani.
Ripoti hiyo imetaja matukio kadhaa likiwemo la Mwembechai, yanayodhihirisha uvunjaji wa haki za binaadamu wa jeshi hilo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari wiki hii, matukio mengine ni pamoja na ukamataji na utesaji wa watuhumiwa hadi kusababisha vifo.
|
|