Kwa tishio la kupiga marufuku mhadhara
Polisi Dar lawamani
 

Na Mwandishi Wetu

KAIMU Kamanda wa polisi mkoa wa Dar es Salaam Bw. Boke Kibona amelaumiwa na kutakiwa kuweka bayana kauli yake ya kuzuia mhadhara katika Masjid Haqqi kama alivyoitoa mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita na kuripotiwa na vyombo kadhaa vya habari hapa nchini.

Wito huo umetolewa na viongozi wa Masjid Haqq uliopo Buguruni karibu na Maghorofa wanayoishi maafisa wa Polisi barabara ya Uhuru Jijini.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini Masjid Haqq, viongozi hao walionyesha kukanganyikiwa kutokana na taarifa ambayo wameieleza inawapa wasiwasi.

Mmoja wa Maimamu wa Msikiti huo Ustadh Ibrahim Al-Ghulaam alimweleza mwandishi wa habari hizi kwamba kauli ya Bw. Kibona haikuwa wazi jambo ambalo limewaletea mshituko mkubwa.

Akitoa mfano Ustadh Al-Ghulaam alisema katika taarifa yake Bw. Kibona amejaribu kutoa picha isiyo sahihi, kama kusema kwamba muhadhara huo ni mkutano na kutokuweka wazi wapi palilengwa kufanyika mhadhara huo.

Pia Ustadh Ibrahim alisema "tendo la Bw. Kibona kuelezea kwamba waaandaaji wa muhadhara huo ni chama kisichosajiliwa, inatupa ile taswira ya kuwa mpambwa sifa mbaya ili umuue", alimalizia Ustadh Ibrahim bila kufafanua.

Nae Katibu Mkuu wa Masjid Haqq Ustadh Said Mshaka alimtaka Bw. Kibona aweke wazi kauli yake ili viongozi wa Msikiti waelewe ni ipi sheria inawaruhusu kutekeleza na ipi sheria inayowakataza.

"Sisi ni viongozi wa Kiislamu, ambao tunawajibika kutekeleza uongozi wetu kwa mujibu wa Qur'an na Sunnah na kwa hili hatuoni popote ambapo tumekiuka Katiba ya nchi. Hii ni ofisi ya Msikiti, lakini kama unavyoona ndugu mwandishi, vipengele kadhaa vya Katiba vinavyowaruhusu waumini wa dini kutangaza dini yao na vile vile kukusanyika pamoja kwa kuzungumzia mambo yao yanayowahusu, sasa sisi tumefanya kosa gani", alisema.

"Amekuja Muislamu mwenzetu ametutaka kama viongozi ruhusa ya kukusanyika na wanawake wenzake ndani ya Msikiti ili wapeane nasaha na kuzungumzia mambo yanayowakabili wanawake wa Kiislamu, kama Waislamu hatukuona sababu za kuwakatalia. Tangazo limetoka kwamba akinamama watafanya muhadhara katika Masjid Haqq, vipi leo Bw. Kibona anauita huu ni mkutano, tena ulioandaliwa na chama ambacho hakikusajiliwa? Tangazo limejieleza wazi kabisa kwamba waandaaji ni Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu, hivi ni kweli kwamba kila kamati lazima isajiliwe?", aliuliza kwa mshangao Ustadh Mshaka.

Nae Imamu Mkuu wa Masjid Haqq Sheikh Rashid Mpota amewataka watendaji wa serikali na taasisi zake kuacha tabia ya kutoa mamuzi ambayo yanawafanya Waislamu wajihisi ni raia wa daraja la pili katika nchi yao.

Mwandishi wa habari hizi alijitahidi kumtafuta Mwenyekiti wa Masjid Haqq Mzee Ally Nassoro Semboga ili kupata maoni yake lakini mpaka anaondoka katika ofisi za Msikiti huo Sheikh Semboga alikuwa hajatokea.

Hata hivo, waumini kadhaa waliozungumza na mwandishi wa habari hizi, maoni yao yalifanana na ya viongozi wao, ingawa baadhi yao walionyesha jazba.

Kauli hiyo ya Bwana Kibona ilikuja siku moja baada ya viongozi wa Msikiti ambao ni Mwenyekiti Mzee Semboga, Katibu ustadh Mshaka na Mzee Mohamed Mtakata kuitwa kituo cha polisi cha Buguruni ambapo walihojiwa kwa zaidi ya masaa matatu tokea saa 10:30 - 2:00 usiku na kuandika maelezo, ambapo hatimaye walitakiwa wafike kituo cha polisi cha Msimbazi, ambapo walipofika hakuna mambo yoyote muhimu walioyazungumza pamoja na mkuu wa polisi wilaya ya Ilala mbali ya kuulizwa majina na vyeo vyao katika Msikiti.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook