Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WAISLAMU mkoani Mwanza wametoa wito kwa Waislamu kote nchini kujiandaa kuonyesha kanda ya mauaji ya Mwembechai katika mikutano ya hadhara ya kampeni za uchaguzi 2000.
Wamesema kwamba hiyo itakuwa ni fursa kwa Waislamu kuihoji serikali iliyopo madarakani juu ya ahadi zake za kuwa na utawala wa sheria; uadilifu na kulinda uhai wa watu na mali zao.
Waislamu kadhaa wa mjini Mwanza wametoa wito huo baada ya kuona kanda ya mauaji hayo huku ikiwa ni mwaka mzima tokea mauaji hayo na serikali haijachukua hatua yoyote.
Imeelezwa kwamba wakati wa kampeni za mwaka 1995 katika baadhi ya sehemu kanda za mauaji ya Rwanda zilionyeshwa na CCM kujenga hoja kwamba endapo wananchi watachagua vyama vya upinzani, basi vitaleta yale ya Rwanda. Kwa hoja hiyo CCM ilidai kwamba ndiyo yenye uwezo na dhamira ya kuleta amani na kulinda uhai na mali za watu.
Mkanda wa mauaji ya Mwembechai umekuwa ukionyeshwa kwa makundi mbalimbali mjini Mwanza ambapo wananchi wamekuwa wakihoji kwamba mwelekeo huu hasi wa serikali dhidi ya Waislamu unakusudiwa uzae nini baadae nchini.
Katika onyesho la mwisho wa wiki iliyopita kwa akina mama wa maeneo ya Kirumba na Nyamanoro, baada ya vilio vikali akina mama hao walitoa wito kwa Waislamu kuondoa woga katika kupigania ukombozi wao.
Walisema kwamba "kama ni kufungwa watu washafungwa na kama ni kuuliwa ndio huku washauliwa, kipi tena cha kuogopa?", walihoji akina mama hao.
Aidha, wamewataka Waislamu wazingatie motisha uliopo ndani ya Qur'an kwamba wanaokufa katika njia ya Allah si wafu; bali wa hai kwa Mola wao wakiruzukiwa.
Ni katika onyesho hilo ambapo akinamama
walitoa wito kwamba kanda ziandaliwe kwa wingi kwa ajili ya kuonyeshwa
wakati wa kampeni za uchaguzi 2000.
|
|