Ndugu Mhariri
WAKATI ambapo kila Muislamu anatafakari hali itakavyokuwa mwaka 2000 na kujiandaa ili kuhakikisha hafanyi makosa kama yaliyofanyka mwaka 1995, sisi hapa Mwanza tumepata dosari na bahati mbaya sana katika jitihada yetu ya kuhakikisha hatufanyi makosa kipindi kingine, ambao Salimu Mswabaha alituingizia fikra ambazo ukweli ni kwamba zimepitwa na wakati.
Fikra hizi amebahatika kuzipenyeza kwa Waislamu wakati wa ziara yake hapa Mwanza iliyochukua takriban siku tano, ambapo kwa kupata wenyeji wenye mrengo kama wake, alifanikiwa kuandaliwa mazingira ambayo yalipelekea kila alilosema lionekane la kweli.
Ukweli ni kwamba ziara hiyo ilikuwa ni ya ghafla mno kiasi ambacho Waislamu tulio wengi tumeshindwa kuelewa kama ziara yake ilikuwa ya kisiasa au ilikuwa ya kidini.
Lakini kwa waliomfuatilia baadae waligundua kuwa ziara yake ilikuwa ni ya kisiasa zaidi kuliko kidini. Katika ziara yake amebahatika kuongea katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa, Msikiti wa Rufiji, Msikiti wa Arafa Mabatini na Thaqafa shule ya Sekondari. Mimi nilipata bahati ya kumsikiliza pale Msikiti Mkuu wa Ijumaa na pale Thaqafa shule ya Sekondari.
Tukiwa Msikitini aligusia suala la umoja ambapo alisema : "Wengi huzungumzia suala la umoja au tatizo la kutokuwepo umoja lakini hakuna anayezungumzia sababu zinazopelekea kutokuwepo umoja", naye akasema "sababu ziko nyingi lakini ninatazama hizi: kwanza, viongozi wana ubinafsi, pili, upeo mdogo, tatu, Waislamu hawana uwazi na ukweli".
Haya aliyazungumza akiwa Msikitini.
Tukiangalia sababu ya tatu aliyoitaja ya Waislamu kutokuwa na uwazi na ukweli. Mimi na Waislamu wengine waliohudhuria muhadhara uliofanyika Thaqafa tunaweza kukubaliana kuwa ukweli na uwazi anaouzungumzia Bw. Mswabaha hauna tofauti na ule unaozungumzwa na wanasiasa wengine.
Kwa mfano, suala la Mwembechai wanasiasa walio wengi wanadai kuwa walioua Waislamu pale Mwembechai hawana makosa, walikuwa na haki ya kuua kwa sababu askari sio mbwa, mwanasiasa mmoja alishawahi kusema hivyo.
Sasa Bw. Mswabaha akiwa katika uwanja wa siasa na ukizingatia kuwa alikuwa akiwazungumza Waislamu ilimbidi atumie ujanja aliodhani kuwa kwa ujanja huo atakayozungumza hayataleta madhara pale aliposema eti waliouawa katika kile walichokifia wana ujira mkubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na akasema walioua ni watu wasiojua kitu ambao wanahitajia kuelimishwa.
Hapa ndipo Waislamu wa Mwanza na wa kwingineko wanatakiwa kumuelewa Mswabaha kuwa ukweli na uwazi anao uzungumzia hauna tofauti na wanasiasa wengine.
Anasema Gewe hajui kwa hiyo Waislamu wakamuelimishe kuwa Waislamu hapa nchini ni raia kama raia wengine, tukamuelimishe kuwa yeye ni Mkuu wa Usalama katika Mkoa wa Dar es Salaam, hivyo usalama wa taifa huondoka pale Waislamu wanapodai haki zao na kupatikana kwa kuwafyatulia Waislamu risasi za moto na kuwaua?
Sehemu nyingine alipoonyesha kuwa yeye si muwazi na mkweli ni pale alipojaribu kuwalaghai na kuwapotosha Waislamu kuwa wapo Waislamu wanaotaka Tanzania itawaliwe na sheria ya Kiislamu pale alivyoonyesha isivyo wezekana kwa kusema kuwa hakuna chama chochote kinachoweza kuongoza kwa sera za kidini hata iweje?
Lakini tukichunguza fikra zake hizi tunaona kuwa hazina pakushika kwani haya yote aliyoyadai sio Waislamu wanayoyataka serikali iwafanyie bali wanayoyataka ni haki zao za kimsingi; kama Waislamu watambuliwe kuwa na wao ni raia kama raia wengine wenye haki ya kupata elimu, wenye haki ya kuwa na uhuru wa kuabudu, Waislamu waruhusiwe kuvaa hijab mashuleni na makazini bila bughudha wala mizengwe, kuwe na uwiano katika uongozi wa nchi yetu. Ieleweke wazi kuwa Waislamu hawataki upendeleo bali wao wanataka haki zao za kisheria.
Sisi hatuna haja na Rais atakayetawala nchi yetu halafu awe Imamu au Msoma khutba, bali tunataka Rais atakayetuthamini kuwa sisi ni miongoni mwa raia ambao wanachangia kuleta maendeleo ya nchi hii na atakayekuwa tayari kufuata na kuilinda Katiba pale inapoonekana kukiukwa.
Utawala wa awamu ya tatu ni kama tunavyo ushuhudia hatuna sababu ya kusema mengi juu yake. Hivyo ndugu Waislamu wote wa nchi nzima na hasa wa Mwanza jihadharini Maswabaha wengi watakaokujieni na watakuja kwa mbinu mbalimbali.
Na nina penda kumzindua Bw. Mswabaha kwamba Waislamu wa Mwanza sio mazezeta kama alivyodhania kuwa watakuwa ni ngazi.
M. Rugayangabo,
Mwanza.
Ndugu Mhariri
KUTOKANA na mjadala unaoendelea hivi sasa nchini Tanzania wa kwamba Kiswahili kiwe ni lugha ya kufundishia mashuleni na vyuoni, yaelekea hautakwisha kwa sababu ya woga wa wasomi.
Kwa mfano, mvutano unaoendelea kwa muda mrefu sasa wa kuvuna waumini kati ya dini kuu mbili nchini. Ukizingatia kwamba Kiswahili kinachukua sehemu kubwa ya hazina ya maneno katika lugha ya Kiarabu ambayo ni lugha mama ya dini moja katika dini hizo mbili.
Hivyo, watu wa dini inayotegemea sana lugha ya Kiingereza wanapinga Kiswahili kutumika kufundishia wka kuhofia kutoweka kwa dini yao.
Ahmad Hussein,
P.O. Box 2251,
Tanga.
Ndugu Mhariri
TUKIO la ziara ya Salum Msabaha Machi 13, mwaka huu mpaka Machi 14, mwaka huu mkoani Mwanza ni ya kuwadumaza Waislamu akili.
Tujihadhari sana Waislamu na watu wanasiasa kama kina Salum Msabaha, 2000 karibia wameishaanza kampeni wana CCM. Lengo ni kuwafanya Waislamu wasidai haki zao kuwadumaza kwa akili.
Ismail Katabalo,
Nyamanoro,
Mwanza.
|
|