WIKI KWA WIKI
Na Robert Makange
Congress ivunje chama
Mwafrika na Taifa Novemba 10, 1962
UCHAGUZI wa Rais wa Jamhuri umekwisha, na Dr. Nyerere amepata kura zaidi ya milioni wakati mpinzani wake, Bw. Mtemvu akipata kura zaidi ya 20,000. Kiasi hiki cha nusu pasenti. Hakuna kinyume kwamba wananchi wameamua hawataki upinzani katika nchi hii.
Kwa kufuata matokeo ya uchaguzi huu sina njia nyingine ila kuwashauri wakuu wa Congress wavunje chama chao kwa sababu chama hicho sasa kimekuwa kama jahazi bovu katika bahari yenye mawimbi. Kuzidi kushikilia ni kuzama nacho.
Rais Mtemvu wa Congress amekwisha kusema kwamba yuko tayari kuvunja chama hicho na kwenda kusaidia TANU ikiwa wanachama wake wataona hakuna haja ya upinzani.
Rais Mtemvu hana haja ya kuwauliza watu kama wanataka au hawataki upinzani. Watu wamekwisha kuyasema hayo katika uchaguzi.
Matokeo ya uchaguzi huu yanaonyesha kabisa kwamba watu hawataki Congress wala upinzani. Matokeo ya uchaguzi huu yanaonyesha wazi kwamba hata ikawaje, Congress haingeweza kupata hata mjumbe mmoja. Kwanini basi Congress iendelee?
Isitoshe mara tu baada ya ushindi, baadhi ya wale wale ambao walijidai ni Congress walikuwamo katika maandamano kuicheka Congress na Mtemvu.
Mtemvu mwenyewe alitengenezewa ‘jeneza’ la kumzika, kitendo ambacho kinahitaji roho ngumu ama sivyo mtu anaweza kudhoofika.
Mimi mwenyewe sikupendezewa na kitendo cha kumbembea mtu ‘jeneza’ kwa sababu huu ni uchuro -wachilia mbali uchokozi, lakini wengi wakiwa wamefurahi, kulalamika kwa watu kidogo kunakuwa hakusikilizwi.
Yote haya, yanaonyesha kuwa watu hawaipendi Congress. Narudia tena kwama kuvunjwa kwa chama hiki ndio utabibu bora uliosalia kwa faida ya wanachama wa Congress.
Hii ni dawa ambayo itaondoa manung’uniko, chuki, upinzani wa kupiganishana makelele na kuleta shabaha moja tu ya kujenga nchi.
Tamaa
Kwenye mkutano wa kufungua Umoja wa Akina mama wa Tanganyika, Dr. Nyerere, aliwaambia mabibi hao kwamba waache tamaa wajenge ujamaa.
Tamaa hiyo ni yale mavazi yasiyokuwa na mwisho. Wafanya biashara nao siku hizi wametukalia vibaya. Kila mwezi hutumiminia,hata majina yake yanakuwa magumu kutamka. Mara imekuja ‘nailoni’ siku nyingine ‘shifoni’ na kuendelea.
Wakina mama wakiziona hizo basi wakina dada hawalali nyumbani. Watu wanaridhiwa kulala na njaa ili mradi mama apate fashioni mpya.
Mimi nafikiri sasa wakina mama wangeanza
mashindano ya namna nyingine ya kulitumikia Taifa. Lakini tusiwaonelee
wanawake peke yao, mambo ya kutimua fedha pia yako kwa akina baba. Pombe
hunywewa hata kama watoto hawajala au hawana nguo. Labda wote tukisadiana
tutajenga ujamaa bora.
Afrika imeingiliwa na shetani
Uhuru Na. 560 Ijumaa, Novemba 11, 1966
RAIS Mwalimu Julius K. Nyerere ameyaomba mataifa huru ya Kiafrika kueleza kinagaubaga iwapo yanataka kushirikiana na wakoloni waliokuwa wakiyatawala mataifa hayo ama wanataka kuudumisha umoja wa nchi huru za Kiafrika. Aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mara tu baada ya kuwasili katika kiwanja cha ndege mjini Dar es Salaam kutoka Addis Ababa alikokuwa akihudhuria mkuano wa viongozi wa nchi huru za Kiafrika.
Mwalimu aliongeza kusema kuwa mkutano huo wa viongozi uliomalizka juzi ulidhihirisha kwamba Ufaransa na Uingereza zina sauti zaidi katika Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) kuliko mataifa ya Kiafrika yenyewe yenye umoja wao. Alieleza kwa masikitiko kwamba mkutano haukuonyesha kuwa ulikuwa ni mkutano wa viongozi hasa kwa vile viongozi wengi waliususa
***************************
Mwalimu alipokuwa akivuka mpaka wa Ethiopia akiwa hewani kurejea Tanzania almtumia salamu Mfalme Haile Selassie zisemazo. "Kwa niaba ya ujumbe wangu na mimi mwenyewe binafsi, ningependa kukutolea shukrani zetu kwa mapokezi bora mliyotufanyia wewe binafsi pamoja na wananchi wa Ethiopia wakati tulipokuwa nchini humo.
"Wakati huu ambapo tunavuka mpaka wa Ethiopia, napenda kukutakia wewe Mfalme pamoja na watu wa Ethiopia heri na mafanikio mema. Ni tegeme langu kwamba chini ya uongozi wako shupavu, Ethiopia itaendelea kuwa katika mstari wa mbele katika Umoja wa Afrika"
**************************
hawakuhudhuria kabisa, na kwa hivyo haukuleta mafanikio yoyote.
Alisema kwamba jambo la kushangaza ni kwamba ni viongozi wachache tu waliohudhuria mkutano huo na ikaonekana kana kwamba mkutano huo ulikuwa wa Mawaziri wa nchi za kigeni.
Mwalimu alisisitiza kwa kusema Mataifa ya Kiafrika ni lazima yaeleze kinaganaga kama yatakubali kuendelea kupokea amri kutoka kwa wakoloni waliokuwa wakiyatawala mataifa hayo ama yataacha na kufuata matakwa yao bara letu la Afrika. Alisema kuwa baadhi ya viongozi walifika katika mkutano huo huku wakiwa na barua za utambulisho zizotiwa sahihi na mataifa ya nje. "Kuna shetani ambaye amejificha katika sehemu fulani ya Afrika anayejaribu kuyavuruga maendeleo ya umoja wa Afrika", alisema kwa hasira.
Akijibu maswali iwapo alifanikiwa
katika kuwahimiza viongozi wenzake juu ya udumishaji wa umoja, Mwalimu
alisema kuwa hakufaulu. Aakasema pia kwamba mgogoro wa Ghana na Guinea
ulivuruga kabisa mkutano. Alisema kuwa mpaka sasa haelewi maisha ya Kamati
ya Ukombozi yatakuwaje hapo baadaye.
Mwafrika, Ijumaa Oktoba 5, 1962
"HATUKUBALI hata kidogo kuwaruhusu Wazungu na Wahindi kuingia chama cha wafanyakazi relini, na niko tayari kwenda jela kulikosemwa na mtu akipingapinga atapelekwa".
Hayo aliyasema Bw. Samuel Katungutu, Mwandishi Mkuu wa TRAU katika mkutano wa hadhara Mjini Dar es Salaam jana jioni. Bw. Katungutu alieleza kwamba majadiliano yao na viongozi wenzake kutoka Kenya na Uganda, mbele ya Mwamuzi, Chifu Lugusha hayakufanikiwa.
‘Wiki mbili zilizopita, majadiliano hayo yalikuwa yakiendeshwa mjini Nairobi, lakini yalipokwama ilishauriwa wajumbe waje Dar es Salaam kwenye nchi huru, huenda wakafanikiwa; kumbe jana yakakwama kabisa’.
"Kwa hiyo", alisema Bwana Katungutu, jambo lililobakia ni kuanzisha mastaplani yetu ya pili, ambayo hatutaitangaza magazetini wala magazetini ili kuwapa ‘maadui’ wetu faida; bali tutawaarifu wanachama wetu tu".
Akamaliza kutamka kwamba iwapo Wahindi na Wazungu wanapenda kujiunga na vyama vyetu, basi waende TFL kunakoruhisiwa mseto.
Katika mkutano huo, Bw. Walter Otenyo, mwandishi mkjuu wa chama cha wareli nchini Kenya alitamka kwa nguvu; "Adui ni adui wa Waafrika wenzake, kwa sababu, wakati yeye anapata zaidi ya shilingi 6,000 kwa mwezi, anapendekeza mikutanoni kwamba Waafrika wanapaswa kupata mishahara ya chini ya shilingi 101 tu kwa mwezi.
Akasema: Hii si ajabu kwamba mtu anayeshiba kuwasahau wenzake wenye njaa kwa sababu hata akina mzee Kenyatta na Bw. Sagini (waziri wa elimu wa Kenya) wamepeleka watoto zao kwenye shule za Wahindi na Wazungu baada ya waalimu wa Waafrika kugoma kutaka haki zao. ‘Je, huo ndio umoja"’ aliuliza.
Bw. Otenyo aliwashauri kwa nguvu viongozi wenzake wa Tanganyika wasikubali Wahindi na Wazungu kuingia katika TRAU au jamaa hao watabakia watu wa juu siku zote.
Bwana Abdalla Mwamba, Mwenyekiti wa tawi la Dar es Salaam la TRAU alisema kwa huzuni: "Tumwachie Mungu taabu zetu na shida zetu".
Mwafrika, Ijumaa Oktoba 5, 1962
RAIS Mdogo wa Chama cha Zanzibar and Pemba Peoples’ Party, Sheikh Ameri Tajo akionana na mwandishi wetu mjini Dar es Salaam alimwambia kwamba chama chake kitatoa msaada kuipa African National Congress ya Tanganyika kama TANU inavyosaidia Afro-Shirazi huko Unguja.
Sheikh Ameri Tajo alisems kwamba chama cha TANU kiliipa Afro-Shirazi Party motokaa ambazo ziliwasaidia katika kupigania uchaguzi na kueneza siasa ya Afro-Shirazi.
Sheikh Ameri hakutaja msaada wa aina gani chama chake kitaipa Congress.
Kuhusu uchaguzi, Unguja Sheikh Ameri alisema kwamba utafanyika katika 1964, na kuongeza kusema "sioni kwa nini uchaguzi huu umewekwa mbali namna hiyo".
Katika uchaguzi uliokuwepo Unguja katika mwezi wa Januari, 1962 Sheikh Ameri ailpoteza kiti cha Makunduchi kwa Mjumbe wa Afro-Shirazi Party Bw. Hasnu Makame.
Katika uchaguzi wa Juni alishindwa tena.
Sheikh Ameri Tajo ni Mjumbe
wa kuteuliwa wa Baraza la Kutunga Sheria Unguja. Yeye amekuwa mjumbe wa
baraza hilo tangu 1946.
Mwafika, Jumanne Aprili 28, 1964
MAELFU ya watu waliojaa katika kiwanja cha ndege kumpokea Rais wa Unguja Sheikh Abeid Karume wakati alipowasili mjini Dar es Salaam.
Njiani mamia ya watu wengine waliokuwa na matawi ya majani walijazana katika njia aliyopita wakimpungia mikono na kumpigia makofi.
Mara tu baada ya ndege yake kufika kiwanja cha ndege mizinga 21 ilipigwa, na baada ya kulakiwa na kuamkiana na Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Tanganyika, Marais wote, pamoja na Makamu wa Rais wa nchi zote mbili walikagua jeshi la askari wa Nigeria.
Wakagua
Baada ya kukagua gwaride hilo walirudi hadi kwenye jukwaa na nyimbo za taifa za nchi hizo zilipigwa.
Kisha wakuu hao walianza kujulishwa kwa Mawaziri, Mabalozi na wakuu wa TANU.
Baada ya sherehe hiyo fupi motokaa zilianza kuendelea mjini na mstari mrefu wa maandamano yalifuata nyuma hadi Jumba la Serikali.
Maandamano yalipofika State House wageni
toka Unguja na wenyeji wao walikaribishwa kwa vinywaji.
|
|