CHAKULA NA LISHE
 
Waislamu watalishwa nguruwe kisayansi kama hawakujiandaa
 

Na Mjahid Mwinyimvua
 
KWA mujibu wa dini ya Kiislamu baadhi ya wanyama ni haramu (siruhusa) kwa Muislamu kuwala, mfano wa wanyama hao ni nguruwe (kiti moto), simba, chui, nyani, nyoka, mijusi n.k.

Kwa upande wa watu wasiokuwa Waislamu, wengi, wao hawana 'mwiko' huo. Yaani kwao wao kila mnyama ni ruksa. Na nguruwe na wengine humwita mkuu wa meza sasa kiti moto!

Katika karne zilizopita Waislamu ndiyo waliokuwa wanaongoza katika medani za vita, sayansi, siasa, utamaduni n.k.

Hata hivyo, dunia sasa inashuhudia kuwa Waislamu wako nyuma katika fani hizo wakilinganishwa na wale wasiokuwa Waislamu.

Vile vile, dunia sasa inashuhudia kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia yake ni makubwa sana.

Wakati wanasiasa (na wataalamu wengine) wa Kiislamu wanaongoza dunia, sayansi ilitumika vizuri kwa maendeleo ya wanadamu na pia sayansi ilitumika kuwafikisha wanaadamu kwenye imani ya Mungu Muumba.

Hata hivyo, neema hiyo haikudumu. Baada ya wanasayansi Waislamu kuporomoka na wale wa nchi za Magharibi kuchukua nafasi yao, historia ikabadilika. Kwa kifupi ni kwamba wanasayansi wa nchi za Magharibi (na wengine) ambao wazazi wao karibu wote wanaimani ya kidini ya Kikristo wanauona Ukristo ni kitu kilichopitwa na wakati, na sayansi ni silaha kubwa inayotumika kupinga imani siyo tu ya dini ya Kikristo bali pia dini zote zilizoko duniani, na imani ya Mungu Muumba kwa ujumla.

Hoja ya hapo juu (kwanini wanasayansi wengi wa leo wanachuki na dini na pia imani ya Mungu Muumba) ni nzito, na inahitaji makala maalum, yaani siyo katika sehemu hii ya chakula na lishe.

Baada ya utangulizi huo, ni vyema sasa tutazame kiini cha makala hii. Ili kuifikia azma hiyo, nitafanya rejea ya gazeti la Alasiri la Machi 23, mwaka huu (No. 0737). Katika gazeti hilo ukurasa wa kumi kulikuwa na makala iliyotafsiriwa kutoka gazeti la Daily Mail la Uingereza (mfasiri hakutaja tarehe ya gazeti hilo).

Kwa kifupi makala hiyo inatupa habari kuwa, wanasayansi nchini Uingereza na Marekani wanafanya uchunguzi ambao wanyama kama vile nguruwe, ng'ombe, kuku, sungura, nyani, panya, kondoo, panya buku, samaki n.k. wanabadilishwa baadhi ya viungo vyao vya mwili ili waweze kukua haraka na kuwa wakubwa kimaumbile au kuzaa watoto wengi.

Gazeti la Alasiri linaripoti kuwa "kwa mitaji (utafiti) huo sasa mtu unaweza kula steki ya binadamu, pengine kupitia steki ya ndafu au samaki au hata kuku wa nyama".

Makala hayo linaendelea kutupasha kwamba, wiki mbili zilizopita mwanasayansi wa Kiingereza aliyeko Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani alieleza jinsi majaribio ya kijenetiki yalivyosaidia kuzalisha kuku wenye miguu mitatu".

Zaidi ya hayo, Alasiri limeripoti kuwa "Samaki ambao wapo karibu kuingia sokoni ni wale wa aina ya Salmor. Hawa wamepandikizwa 'jini' inayopepesuka (Staggering gene) ambayo huongeza ukuaji wa samaki huyo kwa asilimia 400".

Hata hivyo, gazeti hilo linaripoti kuwa, "baadhi ya majaribio ya wanyama waliobadilishwa kimaumbile tayari wameshakuwa na matokeo yanayoogopesha na matokeo ambayo hayatabiliki".

Wasomaji wangu, mkirejea maelezo yangu ya awali (sayansi ya sasa ni zana inayotumika dhidi ya Imani ya Mungu Muumba) mtaelewa muelekeo wa wanasayansi (wenye nguvu) wa zama zetu hizi.

Kwa kweli kuna mengi yanayofanyika. Wanasayansi (wenye nguvu) sasa wanafanya utafiti ili kuondoa kifo! Pia wanafanya utafiti ili binadamu awe anachapa kazi kama nyuki. Kwa maneno mengine wanataka kuumba ulimwengu mpya na viumbe wapya.

Kama Waislamu wataendelea kuchagua mafundisho ya dini ya Kiislamu. Kwa mfano Qur'an inasema: "Na utafute kwa yale aliyokupa Mwenyezi Mungu - makazi mazuri ya akhera, wala usisahau sehemu yako ya dunia,..." (28:77)

Lakini Waislamu wengi wa leo wanashughulikia akhera tu, kwa mfano wanaswali, wanafunga, wanakwenda Makkah kuhiji, wanatoa zaka, wanasoma Qur'an na wanafanya mambo mengine ya kiroho lengo ni kupata thawabu tu.

Ajenda ya kushughulikia na mambo ya dunia (kama Qur'an inavyosema) wameitupilia mbali. Yaani, Qur'an inawataka Waislamu wa 'balansi' akhera na dunia.

Kwa hiyo, ninaona kwamba kama mambo yatakwenda hivyo itafika wakati Waislamu watakao kwenda kuhiji watalazimika kutumia (kwenye ibada ya kuchinja) wanyama wenye mchanganyiko na wale wa haramu (mfano nguruwe na ngamia, au nguruwe na kondoo, n.k.)

Mambo yakifikia hapo, sijui Masheikh watadai kuwa hiyo ni dharura. Kama baadhi yao wanavyodai wa kadhia wanayopata wanawake (wanawake kutibwa magonjwa ya kike na madaktari wanaume), kadhia ya benki za riba, kadhia ya dawa zenye pombe (alcohols), kadhia ya sabuni zilizotengenezwa kwa kutumia mafuta ya nguruwe, n.k.

Namalizia makala hii kwa kuwaomba Waislamu wazingatie Qur'an, Hadithi na usia huu wa Mtume Muhammad (s.a.w.) alipomwambia mkewe Bi Khadija (lakini lengo ni Waislamu wote) "Muda wa kulala sasa umekwisha".

Yaani Mtume (s.a.w.) aliyasema maneno hayo katika siku za mwanzo wa Utume wake, ambapo ajenda yake ilikuwa kusimamisha Dola ya Kiislamu ili Mwenyezi Mungu aabudiwe ardhini kama vile anavyoabudiwa mbinguni.

Lakini alijua kuwa makafiri hawataridhia sheria ya Mwenyezi Mungu itawale uchumi, siasa na mambo yote ya maisha kwa ujumla. Siku hizi anaetaka sheria za Mwenyezi Mungu anaambiwa asichanganye dini na siasa.

Kwa hoja hiyo basi, Waislamu waanze sasa kuandaa vijana tangu shule za awali (chekechea) mpaka Chuo Kikuu ili waweze kuwa na watalaamu wa kila fani watakaofanya utafiti ili kumjua zaidi Muumba na kuleta amani na utulivu wa kweli katika ardhi.

Kinyume na hivyo, siyo tu watalishwa nyama ya nguruwe (na wengine wa haramu) kisayansi bali pia dunia itaangamia.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook