Mashairi ya zamani
Uhuru, Jumanne Agosti 5, 1969
Mzazai hana kinyongo, kwa
wanao wacha inda,
Ukawatenga mtengo, kuchagua
wa kupenda,
Huo ndugu si mpango, usijaribu
kutenda,
Hachagui wa kupenda, mzazi
mwenye busara.
Mzazi mwenye busara, uwa
hodari kuunda,
Huunda kama Sonara, unyosha
kilicho pinda,
Ndipo upewa hongera, kwa
ujuzi wakufunda,
Hachagui wa kupenda, mzazi
mwenye busara.
Mungu kakupa bahati, kuzaa
watoto kenda,
Wavulana na binati, wako
nyumbani waranda,
Baba uwe katikati, hadabu
njema kudunda,
Hachagui wa kupenda, mzazi
mwenye busara.
Usichague kikundi, wengine
wabaki munda,
Kwa sababu si washindi,
miili yao imekonda,
Mzazi haitwi fundi, kwa
Majura ni Kamanda,
Hachagui wa kupenda, mzazi
mwenye busara.
Ewe mzazi mwenzangu, sikia
ino agenda,
Unao gawa mafungu, watoto
kama matunda,
Hapendezwi bwana Mungu,
kwa hayo unayotenda,
Hachagui wa kupenda, mzazi
mwenye busara.
Chonde ninakuchondela, moyo
wako wachainda,
Baba usiwe nahila, kama
mti na maganda,
Huo ni ukabaila, Tanzania
twauponda,
Hachagui wa kupenda, mzazi
mwenye busara.
Hivyo ukiwa tajiri, umeanzisha
kiwanda,
Watumishi tawadhiri, kuwafanya
makinda,
Wengine nguo nzuri, wengine
wavae gwanda?
Hachagui wa kupenda, mzazi
mwenye busara.
Hapa ndio kaditama, sifikishi
beti kenda,
Siku nyingi sijasema, nafasi
inanishinda,
Leo ninaunguruma, katu simba
hawi punda!
Hachagui wa kupenda, mzazi
mwenye busara.
H.S. Kibugo (Nkojabuli)
S.L.P. 20592,
Dar es Salaam.
Mwafrika na Taifa Novemba 10, 1962
Leo napiga kilemba, nitoe
wangu undani,
Nina wimbo naimba, umenijaa
kinywani,
Nacheza huku nayumba, furaha
tele moyoni,
Ahadi kuitimiza, dunia huwa
ni pepo.
Dunia huwa ni pepo, ahadi
ikitimizwa,
Na akherza uendapo, pema
utapokelewa,
Wallahi nala kiapo, motoni
hutochelezwa,
Ahadi kuitimiza, dunia huwa
ni pepo.
Ahadi unapotowa, yangojea
kutimizwa,
Thawabu utapewa, duniani
utapendwa,
Uwongo ukiutoa, madhambi
utavishwa,
Ahadi kuitimiza, dunia huwa
ni pepo.
Ndugu ahadi ni deni, kuna
msemo wasemwa,
Na asolipa deni, daima atasakamwa,
Abishae ni nani, apinge
yalosemwa,
Ahadi kuitimiza, dunia huwa
ni pepo.
Ahadi ni hazina, duniani
na akhera,
Yaleta mengi mema, kuonekana
ni bora,
Utakumbukwa daima, ulalapo
akhera,
Ahadi kuitimiza, dunia huwa
ni pepo.
Leo nasema hivi, na kesho
wabadilisha,
Bure utaota mvi, wacha kujiabisha,
Ahadi ya hivi hivi, motoni
utakawilishwa,
Ahadi kuitimiza, dunia huwa
ni pepo.
Muhakikishe mwenzako, ndivyo
ilivyo dunia,
Uwache urongo wako, kheri
utajipatia,
Timiza ahadi zako, usije
kuangamia,
Ahadi kuitimiza, dunia huwa
ni pepo.
Kaditama washairi, dunia
huwa ni pepo,
Eewo ndugu muhariri, ufanye
maakuli,
Niwache ninakiiri, chipukizi
ndilo hili,
Ahadi kuitimiza, dunia huwa
ni pepo.
Athumani A. Kido,
El Baajuny,
Tanga.
Kwa jina la Rahmani, Ya Illahi
Ya Rabuka,
Wa mbingu na ardhini, yu
pweke amepwekeka,
Njema zote shukurani, Yeye
anawajibika,
Iwe Iddi - Mubaraka, wa
mina-lifahizina.
Wa mina-lifahizina, iwe Iddi
Mubaraka,
Kwa mabibi na mabwana, wote
Makka walofika,
Aidha ajimaina, Mungu alipe
baraka,
Iwe Iddi - Mubaraka, wa
mina-lifahizina.
Wote walokwenda hiji, kule
na huko kutoka,
Kwenye miji na vijiji, India
na Amerika,
Urusi China na Fiji, Ulaya
na Afrika,
Iwe Iddi - Mubaraka, wa
mina-lifahizina.
Zifaulu zao sai, Marwa Swafa
kutimka,
Shetani kwa kutumai, eti
watu kupotoka,
Kimpate kipapai, fudifudi
kuanguka,
Iwe Iddi - Mubaraka, wa
mina-lifahizina.
Twaomba Ya Jabari, Mungu
wetu mtukuka,
Iwe Hija mabururi, isiyo
na shakashaka,
Wao uwalipe kheri, tusokwenda
kadhalika,
Iwe Iddi - Mubaraka, wa
mina-lifahizina.
Waliokwenda Madina, pale
walipomzika,
Tumwa wetu Seyyidina, Muhammad
mtajika,
Wape wao Subuhana, kila
lenye kupendeza,
Iwe Iddi - Mubaraka, wa
mina-lifahizina.
La Muhammad kaburi, naomba
kueleweka,
Khalifa Abubakari, karibu
yamepangika,
Na la Khalifa Umari, kuzuru
yakubalika,
Iwe Iddi - Mubaraka, wa
mina-lifahizina.
Mahaji na Mahujaji, tawafu
na kuzunguka,
Na kwenda kwao matiti, labeka
wakiitika,
Na kupiga jamarati, radhi
ya Mungu kutaka,
Iwe Iddi - Mubaraka, wa
mina-lifahizina.
Kaditama nilitinde, shairi
latamatika,
Waliokwenda washinde, hija
iwe muafaka,
Na sisi tuombe twende, nasi
tukahiji Makka (Amina)
Iwe Iddi - Mubaraka, wa
mina-lifahizina.
(Mshairi - Bora)
Amiri A.S. Andanenga
S.L.P. 4775,
Kinondoni Shamba,
Safarini Mvuti Kijijini
- Dar es Salaam.
Nakwita Maji ya Ndimu, labeka
uniitike,
Kwa swali lako muhimu, imefanya
niinuke,
Kukujibu yalazimu, kutojua
kukutoke,
Dafu ndivyo kula kwake,
kunywa maji kisha nyama.
Kunywa maji kisha nyama,
dafu ni hivyo huliwa,
Sababuye ya hekima, hii
hapa unapewa,
Kwanza ‘kiu’ kukizima, nyama
hula ukipowa,
Dafu inavyotakiwa, kunywa
maji kisha nyama.
Dafu ni kitu azali, ndivyo
inavyotumika,
maji hunywewa awali, ukisha
kuburudika,
Nyama yake hukabili, kilaji
cha kupendeka,
Dafu inavyotumika, kunywa
maji kisha nyama.
Aidha nakupa usi, maji ya
ndimu yashike,
Dafu inavyo halisi, ukivunja
maji yake,
Siyo katika gilasi, unywee
dafuni mwake,
Dafu ni mwenendo wake, kunywa
maji kisha nyama.
Nakwambia yapasayo, madafu
yaek dhamiri,
Uanze kupoza moyo, itoweke
yote hari,
Mwisho wake nyama ndiyo,
ule dafu kwa uzuri,
Dafu yake fakhari, kunywa
maji kisha nyama.
Dafu sikio la mbuzi, ni nyama
yake laini,
Hilo ni dafu azizi, linalopita
kooni,
Linafanya utelezi, halitati
abadani,
Dafu ni yake kanuni, kunywa
maji kisha nyama.
Na swala la ukwamaji, ajali
hailindiki,
Unaweza kwamwa maji, ajali
haiepuki,
Ajali usiihoji, kamwe haiepukiki,
Bali ni yake kanuni, kunywa
maji kisha nyama.
Isiwe maji ya dafu, utie
kwenye kikombe,
Ili uyanywe halafu, nyama
kwanza uirambe,
Mwendo utauhalifu, maji
yatakuwa pombe,
Dafu ili ulipambe, kunywa
maji kisha nyama.
Ubeti huu shairi, usemi wangu
nafunga,
Mtungaji ni Amiri, maarufu
Andanenga,
Mbora wa Washairi, pembe
zote nimezinga,
Dafu katika kupanga, kunywa
maji kisha nyama.
Amiri A.S. Andanenga,
S.L.P. 4775,
Kinondoni - Shamba,
Dar es Salaam.
Dama umesema kweli, faraja
wawe wawili,
Ni ruhusa ya Jalali, kuikwepa
udhalili,
‘Wallah’ wake wawili, ni
raha sio mithili,
Wake wawili faraja, bora
iwe kwa nikaha.
Ameagiza Jalali, Mola mwenye
kutukuka,
Tuanzie na wawili, moyo
pate burudika,
Watatu pia halali, mwenyewe
keshatamka,
Wake wawili faraja, bora
iwe kwa nikaha.
Ukewenza maumbile, ndiyo
maana ni faraja,
Mola wetu wa milele, hutujuwa
wake waja,
Singeruhusu jambo lile,
pasingekuwa na haja,
Dama umesema kweli, faraja
wake wawili.
Mke mmoja karaha, kwa mwanamume
‘rijali’,
Roho inakosa raha, kutamani
walo mbali,
Tusijinyime furaha, faraja
wawe wawili,
Dama umesema kweli, faraja
ni ukewenza.
Ni ruhusa ya Muumba, kuoa
wake wawili,
Sharti lake ni kwamba, uadilifu
wa kweli,
Usiye kuwa mshamba, haki
kufanya batili,
Wake wawili faraja,bora
iwe kwa nikaha.
Waume hufarijika, wanawake
kadhalika,
Aibu husitirika, mabinti
hunusurika,
Jamii uhifadhika, na zinaa
hutoweka,
Wake wawili faraja, Dama
umesema kweli.
Faraja ukewenza, Dama nakupasulia,
Ni uadilifu kwanza, na siyo
kukimbilia,
Unaweza kujiponza, motoni
ukatupiliwa,
Wake wawili faraja, bora
iwe kwa nikaha.
Mhariri beti nane, sioni
pa kuongeza,
Tuwaoe mpaka wanne, Rabbi
ameelekeza,
Wembamba pia wanene, hata
wenye makengeza,
Wake wawili faraja, Dama
umesema kweli.
Said Rajab,
Box 16000,
Dar es Salaam.
Yaillahi Rahmani, Mola uso
mshirika,
Mjuzi wa kila fani, wewe
ndiwe msifika,
Nijaalie Manani, ujumbe
uweze fika,
Haipo mbali safari, yapasa
kujiandaa.
Ni mpito duniani, hilo linatambulika,
Kwa mfano majumbani, kwa
kweli tumepunguka,
Wanetu na majirani, duniani
wametoka,
Haipo mbali safari, yapasa
kujiandaa.
Na Mitume kadhalika, mingi
imetangulia,
Hawa wailchagulika, kwa
Mola wtu Jalia,
Mola hakuacha katu, roho
zao kuchukua,
Haipo mbali safari, yapasa
kujiandaa.
Yu wapi Adam wetu, Mungu
alimjalia,
Na mkewe mama yetu, peponi
wakatulia,
Mola hakuacha katu, roho
zao kuchukua,
Haipo mbali safari, yapasa
kujiandaa.
Nuhu pia yupo wapi, na umri
alopewa,
Pia Musa simtupi, na Mungu
alijaliwa,
Jabarini mara ngapi, ujumbe
alipatiwa,
Haipo mbali safari, yapasa
kujiandaa.
Daudi namkumbuka, chuma kwake
kukifuwa,
Mikononi akishika, huyuyeka
kilikuwa,
Roho yake imetoka, Mola
ameichukuwa,
Haipo mbali safari, yapasa
kujiandaa.
Muhammd Rasuuli, huyu pia
katutoka,
Ni kipenzi cha Jalali, Miraji
kampeleka,
Hilo Mungu hakujali, roho
yake kaitaka,
Haipo mbali safari, yapasa
kujiandaa.
Waislamu wenzangu, tutendeni
mambo mema,
Roho kutoka uchungu, tena
sana inauma,
Tusije muasi Mungu, motoni
atatuchoma,
Haipo mbali safari, yapasa
kujiandaa.
Nyoyo zetu ngumu sana, wala
hazisikilizi,
Makatazo yake Bwana, yamekuwa
simulizi,
Na mifano twapeana, ya adhabu
za Mwenyezi,
Haipo mbali safari, yapasa
kujiandaa.
Hapa mwisho namaliza, ujumbe
wangu mfupi,
Mambo mema kuhimiza, umri
wangu mfupi,
Kama tutayapuuza, tutasalimika
vipi?
Haipo mbali safari, yapasa
kujiandaa.
Hamis M. Rutengo,
Ubungo Islamic High School,
S.L.P. 55105,
Dar es Salaam.
|
|