Historia: Form One
Maana ya Historia (4)

(c) Suala la maisha ya Akhera

Kwanza mtazamo wa makafiri, ulimwenguni na vyote vilivyomo umetokea kibahati nasibu na hivyo hivyo ndivyo utakavyotoweka yaani, makafiri wanadai kuwa hapana Muumba wa ulimwengu na vyote vilivyomo na hakuna maisha mengine baada ya kufa. Mwisho wa maisha ya mtu ni pale anapokufa. Kwa mtazamo wa makafiri, ulimwengu utakuja toweka kama ulivyoibuka kibahati hapo awali. Hivyo wanadai kuwa maisha ya akhera ni jambo la dhana tu lisilokuwa na uthibitisho wowote.

(d) Umuhimu wa kujifunza Historia

Kwa kuwa Historia ni kumbukumbu ya harakati za wanaadamu waliotangulia katika harakati zao za kuzalisha mali, kujifunza historia kwa mtazamo wa kikafiri ni muhimu kwa sababu:

(i) Kunawawezesha makafiri waone ni wapi watu waliopita walifanikiwa na wapi walifeli katika harakati za uzalishaji mali ili wajifunze kutoka kwao. Waige njia zao zilizowapelekea kufanikiwa na wajiepushe na udhaifu wao uliosababisha kufeli kwao.

(ii) Pia historia inasaidia kurekebisha mahusiano kati ya mtu na mtu katika harakati za uzalishaji mali.

2. Mtazamo wa Uislamu juu ya Historia

Kuna tofauti kubwa sana za kimtazamo kati ya Uislamu na Ukafiri juu ya Historia na umuhimu wake. Hili linadhihirika wazi tunapozingatia "chanzo cha ulimwengu na asili ya mwanadamu, lengo la maisha ya mwanadamu, hadhi ya mwanadamu hapa ulimwengu na suala la maisha ya akhera.

(a) Chanzo cha Ulimwengu

Tunafahamishwa katika Qur'an kuwa Muumba wa ulimwengu na vyote vilivyomo ni Allah (s.w.). Hebu turejee aya chache zifuatazo:

"Yeye Allah ndiye Muumba wa mbingu na ardhi pasina ruwaza; na anapotaka jambo basi huliambia tu, "kuwa" nalo huwa. (2:117).

"Bila shaka Mola wenu ni Allah ambaye ameziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya arshi (yake). (10:3).

(b) Asili ya Mwanadamu na hadhi yake hapa ulimwenguni

Maelezo ya uhakika juu ya asili ya mwanaadamu yamepangwa katika Qur'an tukufu. Mtu wa kwanza mwenye ukamilifu wa kimwili, kiakili na kitabia aliumbwa moja kwa moja na Muumba. Kuumbwa kwake, kuoa kwake, kukosea kwake, kupata kwake msamaha wa Mwenyezi Mungu, kufanywa kwake Mtume, kuja kwake duniani, na juhudi zake za kuitangaza dini ya Allah (Uislamu) ni maelezo yasiyo na shaka au utatanishi.

Hivyo kutokana na mtazamo wa Uislamu asili ya mwanadamu si nyani wala hadhi yake hapa ulimwenguni si sawa na ile ya mnyama. tunafahamishwa katika Qur'an kuwa watu wote ni ndugu wa baba na mama mmoja, Baba Adam na Mama Hawwa. Tunakumbushwa katika Qur'an:

Enyi watu mcheni Mola wenu ambaye amekuumbeni katika nafsi (asili) moja. Na akamuumbia mkewe katika nafsi ile ile. Na akaeneza wanaume wengi na wanawake kutoka katika wawili hao. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana. Na (muwatazame) jamaa. Hakika Mwenyezi Mungu ni mlinzi juu yenu (anayaona kila mnayoyafanya).

Enyi watu kwa hakika tumekuumbeni (nyote) kwa (yule) mwanaume (mmoja, Adam) na (yule yule) mwanamke (mmoja, Hawwa). Na tumekufanyeni mataifa na makabila (mbalimbali) ili mjuane (tu basi sio mkejeliane). Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi katika nyinyi, kwa yakini Mwenyezi Mungu ni mjuzi na mwenye habari (za mambo yote). (49:13).

Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa watu hutokana na kizazi cha Adam (a.s.) na Hawwa na wote ni sawa mbele ya Allah (s.w.) bila ya kujali tofauti za ukoo, ukabila, utaifa au rangi zilizopo. Mwenye hadhi na heshima mbele ya Allah (s.w.) ni yule amchaye ipasavyo.

Pia tunajifunza katika Qur'an kuwa mtu wa kwanza kuumbwa ni Adam (a.s.) ambaye pia alifanywa Mtume wa Allah kwa wanawe. Adamu (a.s.) ameumbwa kutokana na udongo kama tunavyojifunza katika Qur'an:

"Na (kumbuka) Mola wako alipowaambia Malaika: Hakika mimi nitamuumba mtu kwa udongo mkavu unaotoa sauti wenye kutokana na matope meuisi yaliyovunda." "Basi nitakapomkamilisha na kumpulizia roho inayotokana na mimi, basi mumuangukie kwa kumtii." (4:1).

"Na Allah amekuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha akakufanyeni wanaume na wanawake. Na Mwanamke yoyote hachukui mimba wala hazai ila kwa ilimu yake.... (35:11).

Baada ya ya kuzingatia aya hizi ya kwanza ya An-Nisaa (4:1) tuliyoinukuu awali binadamu ni kiumbe aliyeumbwa kutokana na mfinyango wa udongo, kisha akapuliziwa roho itokanayo na Allah (s.w.) kisha akaumbiwa mkewe Hawwa, kutokana na asili hiyo hiyo ya udongo na roho kisha kutokana na wawili hao, uzazi ukaendelea kwa njia ya kawaida tunayoitumia mpaka hivi leo. Ni kwa msingi huu watu ni wana wa Adam au kwa ufupi "wanaadamu" au Binadaamu yaani "bin Adam" (watoto wa Adam).

"(Wakumbushe watu habari hii) wakati Mola wako alipowaambia Malaika mimi nitamleta Khalifa katika ardhi..... (2:30).
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook