Windows: Mambo Mazuri ya Kuyajua
 

Leo tena tunaendelea na msururu wa makala zetu zenye lengo la kuelezea mbinu mbali mbali za kumuwezesha mtumiaji wa Windows 95/98 aweze kufanya mambo kwa ufanisi zaidi.
 

Kufungua mafaili kwa kutumia programu unayoitaka

Anaweza mtu akakuletea faili lenye maandishi aliyoyaandika kwa kutumia Microsoft Word, lakini faili hilo likawa halina extension ya .DOC. Ukitumia Windows Explorer kufika mahali ulipoliweka faili hilo, hutaweza kulifungua moja kwa moja kwa kutumia Microsoft Word kwa kutumia njia ya kulibonyezea mouse mara mbili (double-click). Hii ni kwa sababu, faili ni lazima liwe na extension ya .DOC ndio kompyuta ijue kuwa faili hilo linahitaji kufunguliwa kwa kutumia Microsoft Word. Hali ni hiyo hiyo kwa mafaili mengine kama yenye extesion .XLS ya kuhitaji kufunguliwa kwa kutumia Microsoft Excel, yenye .TXT ya kufunguliwa kwa kutumia Notepad, n.k.

Njia moja ya kutumia kulifungua faili lililotayarishwa kwa kutumia Microsoft Word lakini lika whalina extension .DOC, ni kwanza kuanzisha Microsoft Word na kisha kulifungua faili hilo kwa kutumia File -> Open. Lakini njia hiyo ni ndefu na inapoteza muda. Ipo njia fupi zaidi. Kwa kutumia Windows Explorer, ukishaliona faili lilipo, kwanza libonyezee kifungo cha kushoto cha mouse (left mouse button), halafu bonyeza Shift na uishikilie wakati ukilibonyezea faili lako kifungo cha kulia cha mouse (right mouse button) na uchague Open With. Ukifanya hivyo, kitatokezea kisanduku chenye picha na majina ya programu kadhaa. Chagua programu unayoitaka (kwa mfano huu Winword, yaani Microsoft Word) ili itumike kufungulia faili hilo.

 
Kutumia "Send To" kurahisisha mambo

Ukiwa kwenye Windows Explorer, ukilibonyezea faili lolote lile kifungo cha kulia cha mouse, na ukachagua Send To kwenye kidirisha kitakachojitokeza, na ukaendelea kuchagua 3 ½ Floppy (A), faili hilo litaingizwa kwenye disketi mara moja, kama kwenye floppy drive A umechomeka disketi. Unaweza pia kuipata Send To kwa kupitia kwenye File menu badala ya kubonyeza kifungo cha kulia cha mouse.

Kama una jalada (directory) lolote lile ambalo mara kwa mara unapeleka mafaili yako kwenye jalada hilo, ni jambo la busara kuliweka jalada hilo kwenye Send To menu. Kufanya hivyo ni kazi rahisi sana. Tumia Windows Explorer mpaka ulione jalada C:\Windows\SendTo. Libonyezee jalada hilo kifungo cha kushoto cha mouse, kisha bonyeza File -> New -> Shortcut. Ukifanya hivyo utapata dirisha la Create Shortcut na kwenye kisanduku cha Command line andika kwa ukamilifu jina la jalada lako, kwa mfano C:\Mybackup. Jalada hilo linapaswa kuwepo tayari. Baada ya hapo bonyeza Next

na utapata dirisha la Select a Title for the Program. Kwenye dirisha hilo andika jina unalopenda lionekane kwenye Send To menu kwa ajili ya jalada hilo, baadaye bonyeza Finish. Kuanzia hapo, ukiwa kwenye Windows Explorer na ukataka kulipeleka faili kwenye jalada lako hilo, basi ni kiasi cha kulibonyezea kifunguo cha kulia cha mouse na kuchagua Send To na baadaye jina la jalada kama ulivyotaka lionekana kwenye Send To menu.

Tumia njia hiyo hiyo kuweka programu yoyote ile unayoitaka kwenye Send To menu. Kwa mfano, kama unataka programu ya Wordpad iwe kwenye Send To menu ili ikurahisishie kazi ya kuyasoma mafaili ya matini (text) tupu, basi kwenye Windows Explorer bonyeza kifungo cha kushoto cha mouse kwenye jalada la C:\Windows\SendTo na uchague File -> New -> Shortcut kama ilivyoelezwa hapo juu. Kwenye dirisha litakalojitokeza la kukutaka ujaze nafasi ya Command line, bonyeza Browse na uende moja kwa moja mpaka kwenye faili C:\Program Files\Accessories\Wordpad.exe na ukishalibonyezea faili hilo kifungo cha kushoto cha mouse, bonyeza Open kisha bonyeza Next. Kwenye kisanduku cha Select a name for the shortcut unaweza kuandika "Wordpad", kisha bonyeza Finish. Baada ya hapo, faili lolote unalotaka kulifungua kwa kutumia Wordpad basi ni kiasi tu cha kulibonyezea kufungo cha kulia cha mouse na kuchagua Send To -> Wordpad.
 

Unahitaji nafasi zaidi kwenye hard disk drive yako?

Ungependa kuongeza nafasi tupu (free disk space) kwenye hard disk drive (HDD) yako kwa kiasi cha kama 14 MB? Aha! Ombi lako limekubaliwa! Angalia kama unalo jalada "C:\Program Files\Online Services". Kama unalo lifutilie mbali. Nadhani unaikumbuka njia ya kufuta jalada au faili kwa uhakika kwa hatua moja tu? Kama huikumbuki, ukiliona jalada au faili kwenye Windows Explorer, libonyezee kifungo cha kushoto cha mouse, kisha shikilia Shift na ubonyeze Delete.

Jalada hilo lina mafaili ya "Online Services" kama vile America Online, Compuserve, n.k. ambayo kwanza yote ni ya zamani na hayatumiki tena na pili si watu wengi wanaotumia huduma za makampuni hayo. Na wale wanaotumia huduma hizo wanaweza kupata mafaili mapya kutoka kwa makampuni hayo moja kwa moja. Unaweza pia kufuta picha (icon) ya Online Services inayoonekana kwenye Desktop. Unaweza pia kufuta "program group" ya Online Services kwa kupitia Start -> Settings -> Taskbar –> Start Menu Programs -> Remove.

Kama unataka nafasi zaidi, basi yafute mafaili yote yaliyo kwenye jalada C:\Windows\Temporary Internet Files, lakini usilifute jalda lenyewe. Kwenye jalada hili hutunzwa kumbukumbu (cache) za sehemu za web ulizozitembelea kwa kutumia Internet Explorer. Baada ya muda, jalada hili hujaa sana na huna budi kulifuta mafaili yake. Kama unatumia Netscape hali ni hiyo hiyo. Tafuta jalada lenye jina "cache" lililo ndani ya jalada la Netscape na uyafute mafaili yake yote.

Sehemu nyingine ni Recycle Bin. Uwe na mtindo wa kufuta mafaili uliyokuwa huyahitaji tena kuemo kwenye Recycle Bin. Kwenye C:\Windows\Temp angalia pia kama kuna mafaili ya zamani na uyafute mara moja. Kama kuna mafaili ambayo yameingizwa kwenye jalada hilo baada ya kuiwasha kompyuta, basi mafaili hayo usiyafute. Ukimaliza kufanya usafi wa namna hiyo si ajabu kuongeza nafasi kwenye kompyuta yako kwa zaidi ya 30 MB!
 

Kufunga madirisha yote kwa mpigo

Ukiingia kwenye My Computer, kwa mfano, kila unachokifungua hufungua dirisha lake. Baada ya muda unakuwa na utitiri wa madirisha kwenye kioo cha kompyuta yako. Unaweza kuyafunga madirisha hayo yote kwa mpigo kwa kuishikilia Shift na kubonyeza kifungo cha kushoto cha mouse kwenye alama ya X iliyo kwenye pembe ya juu ya kulia ya dirisha la mwisho lililofunguliwa.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook