Na Abu Saad
ZAIDI ya asilimia 80 ya wananchi wa Kosovo ni Waislamu. Albania nchi iliyo jirani na Kosovo pia ina idadi ya raia zaidi ya asilimia 80 ambao ni Waislamu, Waserbia ni Wakristo wa madhehebu ya Orthodox ambao ni asilimia zaidi ya 70 ya wananchi wa Serbia.
Urusi ambao ni marafiki wakubwa wa nchi ya Serbia nayo pia wananchi wake ni Wakristo wa madhehebu ya Orthodox kwa zaidi ya asilimia 80. Hali kadhalika ndivyo ilivyo kwa Croatia ambayo ina idadi kubwa ya Wakatoliki kama ilivyo kwa Wapambe wao wa Italia na sehemu ya Ujerumani.
Licha ya ukweli huo hapo juu, hakuna anayedai kwamba kuna Waserbia wenye asili ya Urusi au Wacroatia wenye asili ya Italia. Kusema kuwa Wakosovo ni watu wenye asili ya Albania ni hoja ya kipropaganda inayolenga kuhalalisha dhuluma dhidi ya haki ya Waislamu kuwa na madaraka ya kinchi.
Albania yenyewe imekuwa ikikandamizwa na mashinikizo tangu enzi za Ukomunisti ya kutojinasibisha na Uislamu kama inavyoshinikizwa Uturuki. Bosnia - Herzigovina ambako kuna Waislamu wengi walishindwa kuwatafutia nchi ya kwuanasibisha nayo kwa sababu wako katikati ya iliyokuwa Yugoslavia.
Waliamua kuwaua tu kwa dhana kuwa wangewamaliza. Kosovo wanawaua na kuwashinikiza wakimbie waende Albania ili nchi yao itekwe na Waserbia kama Mayahudi walivyowafanyia Wapalestina.
Ukweli huo unajulikana na mataifa yote viongozi wa NATO. Ajenda ya kuangamiza Waislamu wasiwe na nchi Ulaya ni ajenda isiyokataliwa na NATO.
Katibu Mkuu wa NATO aliyemtangulia huyu aliyepo sasa hivi alikiri kutamka kwamba baada ya kuanguka kwa Ukomunisti adui yao mkubwa aliyesalia ni Uislamu.
Mara tu NATO walipoanza kuipiga mabomu Serbia hivi karibuni Naibu Waziri Mkuu wa Serbia aliwaambia NATO kwamba msisahau mnaotupiga ni Wakristo wenzenu na kwamba mataifa yote ya Magharibi yanatambua kwamba haikubaliki kuwa na nchi ya Waislamu Ulaya.
Kwa kuwa NATO inadai kwamba inaipiga Serbia ili kuzuia mauaji yanayofanywa na Waserbia Kosovo, ingelitegemewa kuona NATO inapeleka majeshi Kosovo kunakofanywa mauaji. NATO inajua kwamba Waserbia wamekuwa wakiua watu Kosovo zaidi ya miaka mitano iliyopita na baada ya kuona ulimwengu utawashangaa wakaamua kuzidisha mashinikizo yao ya kumtaka Milosovic kuacha mauaji Kosovo kama vile walikubaliana na Milosovic, NATO ilipoanza kutangaza azma yake kuipiga mabomu Serbia hatua zilizochukuliwa za kuandaa mazungumzo yaliyopoteza muda mrefu, zilitoa pia muda wa kutosha kwa Milosovic kupeleka majeshi na silaha kali ndani ya Kosovo.
Hivyo upigaji wa mabomu ya NATO katika maeneo ya Serbia mbali ya Kosovo ulikwenda sambamba na kasi ya Warsebia ya kupora mali zao Waislamu, kuangamiza miji yao na kuwachinja Waislamu ambao hawakuweza kukimbia nchi yao. Ni dhahiri mabomu ya NATO hayakulenga kuwanusuru Waislamu wa Kosovo.
Pamoja na unafiki huo, NATO imetumia fursa ya vita hiyo ya Kosovo kuangamiza mabaki ya silaha na viwanda vya silaha vya Wakomunisti vilivyoko Serbia. Ukaribu wa Serbia na Urusi ni moja ya sababu ya NATO kuhofia kibri cha Milosovic kwamba huenda kinatokana na kumiliki baadhi ya silaha kali na watalaamu wa utengenezaji wa silaha hizo kutoka Urusi iliyokuwa ya Kikomunisti.
Mtu angelitegemea NATO kuua
ndege wawili kwa jiwe moja. Lakini NATO haifanyi hivyo kwa kuwanusuru Waislamu
wa Kosovo. Wao wanaua ndege mmoja tu yaani silaha za Serbia. Na katili
Milosovic anawaulia ndege wa pili kwa kuangamiza Waislamu Ulaya.
|
|