Shule zisizoruhusu Hijab Tanga kuwakosa Waislamu
 

Na Abu Abdullah, Tanga

MIKAKATI inapangwa mjini Tanga kuhakikisha kuwa amri ya Allah (s.w.) kuhusu vazi la stara (hijab) linatekelezwa na kila Muislamu.

Hilo lilikuwa ndilo azimio kuu mwishoni mwa mkutano wa kusisimua baina ya wazazi wa Kiislamu na viongozi wa TAMSA uliofanyika Machi 7, mwaka huu kwenye shule ya Jumuiya ya mjini hapa.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti na Katibu wa TAMSA waliwasilisha mbele ya wazee malalamiko yao, kubwa ikiwa ni suala zima la hijab.

Walizitaja shule za sekondari za Eckenford, Sahare na Popatlal kuwa zimewakatisha tamaa katika utekelezaji wa amri hii ya agizo la serikali.

Shule ya Eckenford ilitajwa kwa ubaya zaidi, kwa kuwa kaidi pamoja na malalamiko haya kupelekwa huko kwa njia nyingi, ya karibuni zaidi ikiwa ni karipio la ana kwa ana kutoka kwa Sharif Hussein Hashim.

Vipindi vya dini kwa shule hii vimewekwa siku ya Ijumaa wakati wa sala, hivyo wanafunzi wa Kiislamu wamelazimika kutafuta muda wao siku ya Jumamosi ili wasome somo hilo.

Akitoa nasaha zake, Mwalimu Mkuu wa Jumuiya Ustadh Kimangale Hassan alisema "nashangazwa na hoja za Maprofesa Wakristo, kwamba eti kuvaa Hijab kwa Waislamu ni kupenyeza Uislamu mashuleni. Je, kuzifanya Jumamosi na Jumapili kuwa siku za mapumziko si kupenyeza Ukristo nchini", aliuliza.

Kuhusu hoja ya kuwa watoto wa Kikristo watajiona wanyonge, alisema haina mantiki yoyote.

Alitoa ushauri kwa TAMSA kufanya Ijtamai za mara kwa mara kuzungumzia masuala nyeti ya Kiislamu kama la Hijab ili wale wasioyafahamu vyema, wapate fursa za kuyaelewa kwa upana wake na ukubwa wa ukosaji kwa kutokutekeleza.

Mwishoni mwa kikao hicho, wazazi walitoa hoja ya kuunda kamati ya wazee wapatao saba ili watembee mashule yote na kutathmini utekelezaji wa agizo hili miongoni mwa walimu wakuu.

Shule zote zitakazogunduliwa kuwa vipingamizi zitatangazwa Misikitini na mitaani ili wazazi wasiwapeleke watoto wao au wawatoe wale walioko tayari kuwahamishia shule nyingine.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook