MAKALA
 
Pasaka siyo kufa na kufufuka

Na Muhibu Said

KATIKA toleo lililopita, tuliona kwa undani kuwa kinyume na wanavyodai Wakristo, pasaka ni mnyama (kondoo, ng'ombe au mbuzi) ambaye katika zama za Nabii Musa (a.s.), Mungu aliwaamuru wana wa Israeli wamchinje na wamle kila ifikapo tarehe 14 ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa kutoka kwao nchini Misri. Tukaona pia kuwa mwezi huo (wa kwanza) ulioitwa "mwezi wa Abibu". Ulianza kuhesabiwa kabla hata Nabii Issa au Yesu (a.s.) hajazaliwa (B.C.); na kwa hiyo ikadhihirika kuwa pasaka ilikuwepo kabla hata mimba yake (Yesu a.s.) haijachukuliwa. Aidha kwa mantiki hiyo, pasaka kuwekewa tarehe 2 mwezi wa Nne (Aprili) wa kalenda ya kuzaliwa Yesu (a.s.) yaani A.D.kama wanavyofanya Wakristo leo, ikadhihirika pia kuwa si katika mafundisho ya Mungu (kama tulivyoona) bali ni uzushi uliobuniwa na wanadamu! Sambamba na ukweli huo, tuliona pia lengo la Mungu kuwawekea wana wa Israeli sikukuu hiyo (ya pasaka), ilikuwa ni kwa ajili ya kukumbuka siku aliyowakomboa kuwatoa nchini Misri chini ya utawala wa Farao (Firauni) ambako walikaa katika hali ya utumwa kwa muda wa usiopungua miaka 430. Aidha, lengo lingine la Mungu kuwawekea wana wa Israeli sikukuu hiyo (ya pasaka) tuliona ilikuwa kama desturi yake kujenga uhusiano mzuri baina yake na wanadamu endapo watatii amri zake. Pamoja na ukweli huo kama nilivyoahidi katika toleo lililopita, endelea kufuatana nami sehemu ya pili na ya mwisho ya mada hii uweze kuangalia angalau kwa uchache udhaifu na upotofu wa dhana nzima ya kufa na kufufuka kwa Yesu, jinsi dhana hiyo isivyohusiana kamwe na pasaka wa Mungu na pia ushuhudie mapinduzi na mhusika mkuu wa mapinduzi hayo dhidi ya pasaka huyo sahihi aliyefundishwa na Mungu.Hakuna uhusiano wowote kati ya Pasaka na "kufa na kufufuka kwa Yesu"

Kama tulivyokwisha kuona katika shuhuda zilizotangulia kuwa sikukuu ya Pasaka imekuwepo kabla ya Yesu kuzaliwa, kwa hiyo basi kabla sijaonyesha mapinduzi na mhusika mkuu wa mapinduzi hayo dhidi ya Pasaka hiyo iliyofundishwa na Mungu ni vyema hapa kwanza tukauangalia kwa undani kidogo usahihi wa dhana ya kufa na kufufuka kwa Yesu ili tuone kama ina uhusiano wowote na Pasaka hiyo ya Mungu.

Dhana ya kufa na kufufuka kwa Yesu si mafundisho ya Mungu

Kwa kweli, zaidi ya masimulizi ya Wainjilisti na wanaadamu wengine kwa ujumla, hakuna kamwe mafundisho sahihi ya Mungu yanayothibitisha kufa na kufufuka kwa Nabii Isa au Yesu (a.s.). Kinyume chake, tunaona maandiko mengi ya Mungu yanashutumu vikali tendo zima la mtu kusulubiwa kwa kutundikwa mtini, kama lile linalodhaniwa kufanyika kwa Bwana Yesu (a.s.)

Na ndio maana sambamba na kutoa amri ya Pasaka kabla ya kuzaliwa Yesu, tendo hilo (la mtu kutundikwa) mapema Mungu alilishutumu vikali kwa kusema:

"...kwa aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu..." (Kumbukumbu la Torati 21:22-23).

Aidha, kabla ya shutuma hiyo (ya Mungu) dhidi ya mtu aliyetundikwa (aliyesulubiwa), Mungu alieleza bayana wasifu wa laana kwa mtu, kwa kusema:

"Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, niwaagizapo leo; na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine". (Kumb. 11:26-28)

Kuhusu laana, Mungu pia hakuacha kuelekeza mahali ambako laana yake hupatikana kama tunavyosoma maandiko yafuatayo:

"Laana ya BWANA i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki". (Mithali 3:33).

Kwa shuhuda hizo, tunachojifunza hapa ni kwamba yeyote aliyetundikwa (aliyesulubiwa) basi anahesabika kuwa amelaaniwa, asiyesikiza maagizo ya Mungu na kukengeuka njia yake, mshirikina (anayemuabudu Mungu pamoja na miungu mingine) na kwa ujumla mtu huyo ni mwovu (rejea Mithali 3:33).

Zaidi ya hivyo, kwa maandiko hayo, yaonyesha wazi Mungu hafurahishwi na kwa ujumla hapendi tendo la mtu kusulubiwa. Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kuwa dhana ya kusulubiwa Yesu ingelikuwa sahihi iwapo tu Mungu asingelishutumu tendo la mtu "kusulubiwa" kwa kiwango hicho, hasa unapolinganisha shutuma hizo (za Mungu) na hadhi, utukufu na ucha Mungu kwa ujumla wa Bwana Yesu (a.s.) mbele ya Mwenyezi Mungu. Isitoshe, Mungu asingeacha kueleza tukio zito na 'muhimu' kama hilo kwa ufasaha, kwa uwazi na kwa maelezo ya kukinaisha.

Aidha, dhana hiyo ya kusulubiwa Yesu pia ingelikuwa ni sahihi na tendo la wokovu, iwapo tu Yuda Iskariote angeliitwa "mwokozi wa kwanza" kwa 'kuharakisha' wokovu wa walimwengu, kinyume na anavyoitwa mpaka sasa kwamba ni "msaliti" aliyemsaliti Yesu! (tazama Mathayo 26:25). Kwani inasimuliwa kuwa ndiye aliyewaonyesha maadui wamuue Yesu baada ya kuahidiwa fedha (tazama Mathayo 26:14-15). Ni ajabu watu wa timu moja wamshutumu mtoa pasi kwa mchezaji aliyeifungia goli timu yao!

Vile vile dhana hiyo (ya kusulubiwa Yesu) ingekuwa sahihi na tendo la "ukombozi" wa wanaadamu, iwapo tu Yesu asingemkemea mapema yule atakayemsaliti kwa kumwambia:

"...Lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa". (Mathayo 26:24)

Kinyume na andiko hilo juu, dhana ya kusulubiwa Yesu ingekuwa sahihi na nzuri iwapo Yesu angelimpongeza yule atakayemsaliti, kwa kumwambia:

"Heri yake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa vibaya kwake mtu yule asingezaliwa". n.k.

Na kubwa zaidi, masimulizi ya Mwinjilisti Mathayo ya kudai kuwa eti Yesu alipokuwa msalabani alisema: "... Eloi, Eloi, lamasabakhtani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?" (Tazama Mathayo 27:46) yanapingwa vikali na mwenyewe Bwana Yesu (a.s.) kwa kusema:

"Naye aliyenipeleka yu pamoja nami; hakuniacha peke yangu, kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo". (Mathayo 8:29).

Kwa kauli hiyo peke yake ya Yesu inadhihirisha wazi kuwa yule aliyekuwa akilalamika kuachwa na Mungu hapo msalabani hakuwa Yesu. Yesu hawezi kuachwa na Mungu kwa sababu kama mwenyewe anavyoeleza katika andiko hilo hapo juu kwamba siku zote hufanya yanayompendeza Mungu.

Na kwa ujumla ukombozi wa wanaadamu kamwe haupatikani kwa njia ya laana (kusulubiwa) ambayo i katika nyumba ya waovu. (Mithali 3:33).

Na ndio sababu, kutokana na uzito wa shutuma za Mungu dhidi ya mtu anayesulubiwa (kama tulivyoona hapo awali), Mwenyezi Mungu katika Qur'an Tukufu akaeleza wazi kwamba:

"Hawakumwua wala hawakumsulubu". (Qur. 4:158).

Kwa maandiko haya na mengine mengi ni dhahiri kuwa dhana ya kufa na kufufuka Yesu katu haimo katika mafundisho ya Mungu. Na kwa mantiki hiyo, Pasaka iliyofundishwa na Mungu haina uhusiano wowote na dhana ya kufa na kufufuka kwa Yesu hasa ukizingatia kuwa Pasaka hiyo (ya Mungu) imekuwepo kabla ya Yesu kuzaliwa, na pia kufa na kufufuka kwa Yesu ni jambo lililozuliwa na wanaadamu baada ya Yesu kuondoka kama tutakavyokuja kuona hapo baadae, InshaAllah.

Yesu mwenyewe aliwahi kumla Pasaka

Ili kuonyesha zaidi kwamba Pasaka haina uhusiano wowote na dhana potofu ya kufa na kufufuka kwa Yesu, maandiko ya Biblia yanaeleza wazi kuwa Bwana Yesu naye kabla ya kuondoka aliwahi kumla Pasaka. Maandiko yafuatayo yanathibitisha ukweli huu.

"Hata siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja Pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile Pasaka? Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amechukua mtungi wa maji; mfuateni; na popote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, ki wapi chumba cha wageni, niile Pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu? Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni. Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka. Basi ilipokuwa jioni yuaja na wale Thenashara, wakila, Yesu alisema, Amin, naawaambieni, mmoja wenu, naye anakula pamoja nami atanisaliti". (Marko 14:12-18)

Kufuatana na maandiko hayo juu, tunaona hapa kwamba Bwana Yesu aliwatuma wanafunzi wake wakaandaa mahali atakapomla pasaka na wala haielezwi kwamba aliwatuma wakaandaa mahali "yeye atakapokufa kwa pasaka". Aidha, haielezwi kwamba wanafunzi wake walipochinja, walimchinja Yesu kuwa Pasaka. Lakini tunaona kuwa baada ya kupatikana hicho chumba na maandalizi kwa ujumla kukamilika, naye Yesu pia alimla Pasaka. Hii yote ni kudhihirisha kuwa Pasaka ni mnyama anayechinjwa na kuliwa na siyo binadamu. Na kwamba Pasaka ilifanyika mwenyewe akiwa hai na wala hajafundisha kwamba Pasaka ni kufa na kufufuka kwake.

Mapinduzi ya Paulo dhidi ya Pasaka aliyefundishwa na Mungu!

Pamoja na Mungu kufundisha wazi kwamba Pasaka ni mnyama (kondoo, ng'ombe au mbuzi) anayetakiwa achinjwe na kuliwa kwa utaratibu na kwa lengo maalum kama tulivyoona hapo awali, lakini Paulo hakukubaliana kabisa na mafundisho hayo ya Mungu. Yeye alikuja na mafundisho mapya kabisa. Tofauti na Pasaka yule aliyefundishwa na Mungu, Paulo alikuja na Pasaka wake, kama mwenyewe anavyosema hapa chini:

"Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani Kristo". (1 Wakorintho 5:7)

Kulingana na maelezo yake hayo juu, mbali na kuwataka watu waache kufuata anavyokiri kuwa ni kuishika sheria za Torati (angalia Wagalatia 3:10-13 na Warumi 7:14), katika juhudi zake hizo za kupindua mafundisho ya Mungu, Bwana Paulo amejaribu kumgeuza Yesu kuwa ndiye Pasaka badala ya mnyama (kondoo, ng'ombe au mbuzi) aliyefundishwa na Mungu, na Yesu mwenyewe kabla hajaondoka!

Kwa shuhuda hiyo, ni dhahiri kuwa Bwana Paulo ndiye muasisi mkuu wa dhana ya kuchinjwa (kusulubiwa), kufa na kufufuka kwa Yesu. Vinginevyo asingethubutu kumwita Yesu kuwa ni "Pasaka" kwani hilo siyo fundisho la Mungu.

Azma ya Paulo dhidi ya mafundisho ya Mungu tangu awali

Hapo juu tumeona jinsi Bwana Paulo alivyogeuza Pasaka wa kweli aliyefundishwa na Mungu. Pamoja na mapinduzi yake hayo, Bwana Paulo tangu awali hakuficha azma yake juu ya Bwana Yesu. Mara tu alipofika hakuhofu kuutangazia wazi umma kwa kusema:

"Basi, ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima. Maana naliazimu nisijue neno lolote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulubiwa". (1 Wakorintho 2:1-2).

Kwa maelezo yake hayo, kikubwa alichoazimia Paulo kukieneza kwa watu si kingine isipokuwa "kusulubiwa tu kwa Yesu"! Ambapo msingi wa kusimamisha dhana yake hiyo aliona aanze kumwita Yesu kuwa ni pasaka. Dhamira yake ikiwa ni kupotosha mafundisho sahihi ya Mungu kuhusu pasaka apate kumchinja Yesu kinadharia ili dhana yake (ya Yesu kusulubiwa) isimame!

Hitimisho

Kama tulivyoona shuhuda nyingi za maandiko ya Biblia, jambo la kusisitiza hapa ni kwamba, sikukuu ya Pasaka iliwekwa na Mungu kwa ajili ya kumbukumbu ya kukombolewa wana wa Israeli kutoka nchi ya Misri (tazama Kumbukumbu la Torati 16:3); na siyo kufa na kufufuka kwa Yesu kama inavyodaiwa na Wakristo.

Aidha, tumeona kuwa dhana ya kufa na kufufuka kwa Yesu haimo kabisa katika mafundisho ya Mungu, bali ni katika mafundisho ya Paulo ambayo mara nyingi amekuwa akieleza wazi kuwa mafundisho yake ni ya kibinadamu (tazama Wagalatia 5:15)

Aidha, dhamiri ya Bwana Paulo kuibua mafundisho yake hayo kama tulivyoona ilikuwa ni kufanya mapinduzi dhidi ya mafundisho ya Mungu.

Kwa mantiki hiyo basi, ni wazi kuwa imani hiyo (ya msalaba) haitomsaidia kitu mwanadamu hasa kwa kuwa lengo lake ni kutaka watu waache kufuata amri na sheria za Mungu (kama atakavyo Bwana Paulo), badala yake wategemee damu bandia ya Yesu!

Umefika wakati wa wanaadamu kujiepusha na imani potofu (kama hizo za kusulubiwa Yesu) na badala yake waanze mara moja kufuata maamrisho ya Mungu kwani hata Yesu mwenyewe alipoulizwa na mtu mkubwa mmoja "nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele?" Yesu hakumwambia "nitakaposulubiwa na kufa ndiko kutakakofanya upate uzima wa milele", hapana! Lakini Yesu alimwambia hivi:

"...wazijua amri; usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo... Viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate". (Luka 18:18-22)
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook