Zanzibar tukate kamba
 

Tumesikia hivi karibuni kutoka katika Idhaa ya Iran mazungumzo ya Mabwana wawili wenye nyadhifa muhimu katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mazungumzo hayo yametupa moyo wa tamaa sana. Mabwana hawa maneno yao bila ya kusema kuwa wanaisemea serikali yao, basi ni ndivyo kufahamika kuwa ikiwa sio wanaisema serikali yao basi kwa uchache wanasema kwa ridhaa ya serikali yao, hivi ni kutokana na nyadhifa na mwahala mwao muhimu katika serikali na katika chama.

Kwa hivyo basi, tunaweza kufahamu kuwa maneno yao ndio fikra za serikali yao au kwa uchache ni fikra za juu katika serikali yao. Mabwana hawa kwa ufupi wote wawili walisema kutilia nguvu dharura ya kuwepo serikali ya Zanzibar yenye uhuru wake na madaraka yake kamili, yaani kama vile ilivyokuwa kabla ya Januari 12, 1964 au pale Aprili 24, 1964 ilipotawaliwa Zanzibar na kupotezewa udola wake kwa jina la Muungano.

Bwana Dorado hiyo sio kauli mpya kutokana na yeye, hayo ndio maneno yake tangu zamani; daima hiyo kauli yake. Msimamo wa Bwana Dorado juu ya muungano na juu ya uhuru kamili wa dola ya Zanzibar unafahamika vyema na wengi wetu. Lakini basi, imetupa moyo wa tamaa zaidi kwa vile mara hii kauli hii imetokana na bwana mwingine kabisa, bwana mwenyewe wadhifa na pahala pa juu kabisa katika chama; kwa hivyo maneno yake yataongezea uzito juu ya kilio hichi cha Wazanzibari kutaka kurejeshewa uhuru wa dola yetu ya Zanzibar.

Kutokana na maneno yao haya, sisi; tunawapa mkono wa pongezi na heko ndugu zetu hawa kwa kitendo chao hiki cha kiwananchi na cha kishujaa. Vile vile tunawahakikishia ndugu zetu hawa, pamoja na serikali ya Zanzibar kuwa sisi Wazanzibari tulioko nje tukishirikiana na ndugu zetu walioko visiwani tuko pamoja na wao bega kwa bega katika msimamo wao huu.

Isitoshe, tunachukua fursa hii kwa kukumbushana kuwa kutaka Zanzibar irejee kuwa dola huru hivyo sio kuwa Wazanzibari wanaomba kutendewa ihsani kutoka kwa yoyote yule, sivyo hivyo hata kidogo. Uhuru wa Zanzibar ni haki ya Zanzibar, ni haki yetu ya kuzaliwa nayo.

Mwalimu Nyerere kwa kuyafahamu haya vyema ilisema jahara kuwa wao Wazanzibari watataka kujirejeshea uhuru wao basi sito wapiga mabomu (kuwazuilia haki yao hii). Kutokana na maneno haya ya Mwalimu ni juu yetu Wazanzibari kuzindukana na kuzidi kutambua kuwa hapana mwenye haki ya kutuzuilia uhuru wetu, kwa hivyo basi, ni wajibu wetu tuungane na tuichukue haki yetu hii na kuirejeshea Zanzibar uhuru wake bila ya kusita-sita au kuchelewa.

Baada ya kurejea uhuru wetu na kuwa na dola huru kamili hapo tena ndio tutaweza kuingia katika mazungumzo na dola yoyote ile ulimwenguni. Hichi ndio kilio cha Wazanzibari tangu siku ile Zanzibar ilipopotezewa udola wake na kutiwa chini ya utawala wa nje kwa jina la Muungano.

Haki ya Zanzibar

Tukichukua fursa hii vile vile tunapenda kukumbushana zaidi kwa kuelezana haya machache yafuatayo:

Nchi ya Zanzibar ilikuwa huru miaka na miaka, bila ya kutawaliwa na dola yoyote ile ulimwenguni. Lakini basi, msiba ulitushukia pale Zanzibar ilipopotezewa uhuru wake mwaka 1890 ilipotiwa katika Himaya ya Muingereza.

Kwa kuwa ni Himaya, wala si koloni, Zanzibar iliendelea kuwa na mfalme wake na wananchi wakabakia na uraia wao wa asili, yaani wakabakia kuwa ni Wazanzibari walio kuwa wakihamiwa na Muingereza, si raia wa Muingereza, kama ilivyo kuwa hali yao katika koloni za Muingereza.

Hali kadhalika bendera ya Zanzibar ikaendelea kupepea juu ya ardhi ya Zanzibar. Lakini jukumu la uendeshaji wa nchi lilikuwa juu ya Muingereza, khasa katika usalama wa ndani na nje, mahusiano na nchi za nje, fedha na kadhalika; yote haya yalikuwa chini ya Muingereza, kwa vile yeye ndiye aliye kuwa mtawala wa Zanzibar.

Tangu mwezi wa Novemba mwaka 1886 eneo la Zanzibar lilipunguzwa kwa maonevu ya madola ya Kiingereza, Kijerumani na Kifaransa. Badala ya dola ya Zanzibar kutanda kote tangu Somalia, Kenya, Tanganyika mpaka Zaire, Zanzibar ikabakishwa visiwa vya Unguja na Pemba na na Mwambao wa Kenya ambao ulikodiwa kwa kahari na Waingereza. Mlima wa Tanganyika ulikodiwa na tena ukanunuliwa kwa kahari na Jarumani kwa Pauni 200,000, thamani ya shamba moja tu katika Ujerumani. Na hata hizo hazikwenda Zanzibar, bali zilikwenda Uingereza, ati zilikopwa! Zanzibar ikilipwa riba yake tu, riba ya 3% miaka nenda miaka rudi; japokuwa kila siku kima cha riba kilipanda zaidi ulimwenguni.

Kwa juhudi za Wazalendo wa Zanzibar himaya hiyo ya Muingereza juu ya Zanzibar ilikomeshwa taarikhi tisa, Desemba mwaka 1963. Tangu siku hiyo Zanzibar ikarejea kuwa huru kamili. Baada ya wiki moja, yaani taarikhi 16 Desemba mwaka 1963 Zanzibar ikapokelewa kwa furaha na kwa jumla na mataifa yote duniani kuwa ni mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa, yaani United Nations Organization.

Sheikh Muhammad Shamte kwa kuwa ndiye Waziri Mkuu wa Zanzibar huru aliipandisha bendera ya Zanzibar huru, bendera nyekundu yenye karafuu mbili za kikonyo kimoja, kumathilisha Unguja na Pemba - Zanzibar, tangu wakati huo ikarejea Zanzibar kuwa ni dola huru sawa na dola yoyote ulimwenguni.

Kwa niaba ya Zanzibar Sheikh Muhmmad Shamte alitoa khutba iliyosisimua, na itaendelea daima kusisimua nyoyo za kila Mzanzibari; kwa kila mwenye uchungu na kila mwenye kuitakia kheri na mafanikio Zanzibar.

Lililopita limepita, na maziwa yaliomwagwa hayazoleki. Lakini palipobomoka hujengwa. Palipoporomoka hunyanyuliwa ijapo kwa kuwekewa mwega. Mambo yamevurugwa, yamevurugika. Baaada ya wiki tatu tu baada ya kwishatoa khutba yake hiyo Waziri Mkuu wa Zanzibar huru, mambo yakawa juu chini.

Ufisadi ukatumiminikia kama mvua ya masika. Na baada ya miezi minne tu, yaani hapo Aprili 24, 1964 Dola ya Zanzibar ikapotezwa kwa kutiwa Zanzibar chini ya Muungano. Kwa kupoteza Dola ikawa Zanzibar haina chake yenyewe chochote, hata huyo Rais ikawa ni Rais jina tu; sawa na kanzu ya kuazima haitekelezi haja. Hali kufika hivi ikawa Zanzibar hali yake afadhali pale ilipokuwa katika hali ya serikali ya Madaraka, yaani kabla ya uhuru wetu.

Kwani wakati wa serikali ya Madaraka tulikuwa na bendera yetu nyekundu. Tulikuwa na mkubwa wetu wa nchi. Tulikuwa na uwananchi,uraia wa Kizanzibari uliokuwa ikitambulikana ulimwenguni kote, vyote hivi vimepotea - ilikuwa Zanzibar na ilikuwa Wazanzibari.

Badala yake imekuwa ni Tanzania na Utanzania tu,Uzanzibari umepotezwa kama ilivyopotezwa Zanzibar. Tumemezwa na kutawaliwa. Hatuwezi kufurukuta, hatuwezi hata kukata shauri nani wa kutusaidia bila ya kunyoonyeshwa ufito kutoka Dodoma na kulazimishwa tukae kitako bila hata kwikwi.

Hayasahauliki yaliotufika pale tulipotaka kujiunga na ndugu zetu katika OIC. Tulitaka kujinga na OIC nasie tupate kutononoka kama vile wanavyotononoka wenyewe huko Bara kwa vile wanavyonyooshewa mikono na makanisa na jumuia mbalimbali za makanisa kwa kila misaada. Sisi tuliambiwa Katiba haituruhusu kutenda hivyo! Sisi natutote!

Kamba ilioko shingoni inatukaba, Wazanzibari na Watanganyika; sote tumo katika mateso ya huu unaoitwa Muungano. Kwa nini basi tukiutua Muungano huu tuliotwikwa na mabwana wawili itubidi tutafute Muungano wa Serikali Tatu watakaouzua mabwana kama hao, au mfumo mwingine wowote wa khadaa wa kuendeleza kututia shemere?

Kwanini hivi sasa hatukati kamba na minyororo yote hii, minyororo ya kutawaliwa, minyororo ya madhila na ufukara; tukarejesha uhuru wetu ule ule wa Tanganyika na Zanzibar tulipoingia katika UNO hali ya kuwa kila moja ni dola huru kamili yenye kila lake na kila chake?

Wazanzibari tuzinduke! Kwa umoja wetu tuungane! Tusahau tofauti zetu zote zilizotiwa kati yetu na wale wasiotutakia kheri ya nchi yetu! Tudai uhuru wa nchi yetu Zanzibar. Irejee kuwa ni dola huru kamili. Tuwe na mkubwa wa nchi yetu. Tuwe na Paspoti yetu. Tuwe na kiti chetu katika UNO, bendera yetu ipepee mbele ya Makao Makuu ya UNO, New York. Tuwe na mabalozi wetu. Tuwe na kila kitu chetu sawa na dola huru yoyote ile ulimwenguni. Tuwe huru, tupate heshima za kibinadamu.

Wazalendo wa Zanzibar
Ijumaa, 4 Shawwal, 1419
Januari 22, 1999
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook