Na Dkt. Abdallah J. Saffari
Dibaji
KATIKA kitabu chake hiki, Bwana A. J. Saffari ameelezea kwa kirefu na kwa ufasaha hatua zinazohusu mashitaka na utetezi katika mashauri ya jinai kuanzia upelelezi, wajibu wa mpelelezi, na haki ya mshukiwa katika hatua hiyo. Pia ameelezea uendeshaji mashitaka yenyewe; vitu muhimu katika hati za mashitaka ya makosa mbalimbali, na utaratibu wote wa kuendesha mashitaka. Ushahidi, maana ya ushahidi, aina mbalimbali za ushahidi, na utaratibu mzima wa kutoa na misingi ya kutathmini ushahidi pamoja na masuala ya utetezi vimejadiliwa vizuri.
Kitabu hiki kinazungumzia pia wajibu wa mahakama katika hatua mbalimbali za usikilizaji wa haya mashauri ya jinai na misingi ya hukumu na adhabu inayotolewa mwishoni.
Kwa jumla, kitabu hiki ni cha manufaa kwa wale wote ambao kwa aina moja au nyingine wanahusika na suala zima la utoaji haki katika mashauri ya jinai. Kwani Bwana Saffari hakuorodhesha hatua na taratibu tu, bali amejaribu katika sehemu mbalimbali kuzungumzia chimbuko na misingi ya taratibu hizo na katika sehemu kadhaa ametoa maoni na mapendekezo yake. Inawezekana mtu asikubaliane naye katika sehemu kadhaa, lakini amejaribu kuangalia mambo aliyoyazungumzia kwa makini. Amefanya utafiti wa kutosha ili kutilia uzito mawazo aliyotoa.
Kwa kifupi hiki ni kitabu kinachofaa kusomwa na watu wote wenye hamu ya kujifunza au kuzidi kuendeleza majadiliano katika suala hili la haki na misingi inayoendelea kujengeka hapa kwetu nchini kuhusu utaratibu wa kutoa haki hasa katika mashauri ya jinai.
Jaji William K. Sekule.
Mashitaka ya Jinai na utetezi
Utangulizi
TAALUMA ya sheria imegawanyika katika matawi mawili makubwa: Madai na Jinai. Sheria za mikataba, ndoa, kazi na kadhalika ni mfano wa tawi la kwanza ambapo sheria zote ambazo zikikiukwa kosa hufanyika na adhabu hutolewa ni mfano wa lile tawi la pili. Aidha liko tawi jingine muhimu mno linaloelezea mwenendo yaani uendeshaji wa mashauri yote katika mahakama pamoja na kanuni za ushahidi. Kitabu hiki kinahusiana na tawi hili la mwisho.
Mwenendo wa mashitaka ya jinai ni utaratibu mzima wa upelelezi wa kosa, kushukiwa na kutiwa nguvuni kwa mtuhumiwa, kupekuliwa, kuandikisha maelezo, kufunguliwa mashitaka, kuwekwa mahabusu, kusikilizwa kwa shauri lenyewe, kuita mashahidi na kadhalika. Utetezi ni hatua inayofuatia mashitaka. Upande wa mashitaka unapomaliza kuita mashahidi wake mahakama huamua iwapo mshitakiwa, kwa ushahidi uliopo dhidi yake, anawajibika kujitetea.
Hivyo basi kujitetea, kama ilivyo kuendesha mashitaka, ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa haki katika mashauri ya jinai. Muhimu vile vile ni uamuzi wa mahakama baada ya kuupokea na kuupembua ushahidi wa pande zote mbili.
Kwani huo ndio upeo wa shauri na sio siku zote mahakama huwa sahihi katika hukumu na adhabu inayotoa. Ndiyo maana kuna utaratibu wa rufani na masahihisho mahususi kwa kuangalia uhalali wa uamuzi wa mahakama ya daraja mbalimbali.
Kila mwanasheria, na hakika yeyote yule aliye na uzoefu wa mahakama, anaelewa kuwa mwenendo wa mashitaka ya jinai ni mithili ya mtambo unaoendesha chombo cha haki katika mashauri haya ya jinai yanayojadiliwa hapa. Kabla, na hata baada ya kukamatwa na kushtakiwa rasmi, kuna utaratibu ambao daima lazima ufuatwe kuhakikisha kuwa haki inatendeka hasa kutokana na dhana kwamba kila mtu hana hatia mpaka pale inapothibitishwa hivyo bila ya shaka yoyote ya maana.
Pamoja na mwenendo wa mashitaka ya jinai, kanuni za ushahidi ni muhimu kwa kiwango kile kile katika hatua mbili: Kabla ya wakati wa mashitaka. Kabla ya mashitaka kanuni za ushahidi ni zana muhimu ya kuamua iwapo kuna ushahidi wa kutosha dhidi ya mtuhumiwa kuweza kumfikisha mahakamani na wala sio kumshitaki tu na kumtesa. Wakati wa kusikiliza shauri lenyewe kanuni za ushahidi zinabainisha iwapo mshitakiwa ana hatia au la. Kwa bahati mbaya Sheria ya Ushahidi ni ngumu na inawatatiza hata baadhi ya wanasheria wa siku nyingi.
Hivyo basi azma ya kitabu hiki ni kumpa mwongozo kila mmoja mintaarafu ya utekelezaji haki katika mashitaka ya jinai. Kimekusudiwa kwa wanasheria na wasiokuwa wanasheria. Jitihada imefanywa kukiandika kwa wepesi bila ya kuzama katika tata za kitaaluma ambazo huweza kuwakanganya wasomaji wa kawaida. Lakini taratibu zote muhimu za kuandika kazi za kitaaluma, pamoja na tanbihi na istilahi za kutosha ziemzingatiwa hasa kwa faida ya watendaji katika mahakama na wanasheria.
Natumaini kuwa kitabu hiki
kitaondoa dhana ya wale wenye taasubi ya Kiingereza kwamba sheria ni taaluma
ambayo haieleweki wala kufundishika kwa Kiswahili ila Kiingereza pekee.
Upelelezi
MARA tu kunapotokea malalamiko ya kutendeka kwa kosa hatua ya kwanza muhimu ni kufanya upelelezi ili kupata ushahidi unaomhusisha mtu anayeshukiwa na kosa linalohusika. Upelelezi sio lazima uanze baada ya kupokea malalamiko ingawa hiyo ndiyo njia kuu ya kuanzisha upelelezi: yaani mtu anatendewa kosa na mtu anayemfahamu au asiyemfahamu na kwenda kituo cha usalama kutoa taarifa ya tukio hilo. Lakini, mathalan hata polisi wenyewe wanaweza kukuta mtoto mchanga ametupwa ndaniya pipa au mtu ameuawa na kutupwa kando ya barabara. Hiyo huwa namna ya pili ambayo husababisha upelelezi kufanyika.
Katika nchi nyingine upelelezi huweza kufanywa na mtu binafsi ambaye analalamika kutendwa kosa linalohusika au anaweza kumwajiri mtaalamu wa shughuli hiyo. Hali hiyo hufanyika zaidi kwa kuwa na imani kubwa juu ya uwezo wa mtaalam fulani kuliko kuliacha suala lote la upelelezi mikononi mwa polisi. Kinadharia, hapa Tanzania, mlalamikaji dhidi ya kosa la jinai hakatazwi kufanya upelelezi wake binafsi kumpata mhalifu. Lakini kwa kawaida kazi hiyo iko mikononi mwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai kwenye Jeshi la Polisi.(Sheria ya Jeshi la Polisi, Sura ya 322)
Haikusudiwi kuingia katika mjadala wa mbinu zenyewe za upelelezi wa makosa ya jinai ambazo hutegemeana sana na aina ya makosa na mazingira yenyewe. Badala yake masuala muhimu kuambatana na hatua hii ya upelelezi yatajadiliwa. Nayo ni mtuhumiwa na mshitakiwa, hati ya kutia nguvuni, hati ya kupekuwa, hati ya kuita shaurini, maelezo ya mshitakiwa na mashahidi, pia dhamana.
Mtuhumiwa na Mshitakiwa
Mara nyingi upelelezi unapoanza huwa kuna mtu anayetuhumiwa kwamba ndiye aliyetenda kitendo kilichosababisha kosa linalohusika. Kunaweza kuwa na ushahidi wa mazingira au hata wa moja kwa moja kwamba mtu fulani ametenda kosa hilo. Mpelelezi anayehusika na kesi yenyewe hukusanya ushahidi wote huo na kutoa maoni yake kwa kiwango gani mshukiwa anahusika na ushahidi huo.
Iwapo ushahidi unaonekana kumwelemea na kumhusisha mtuhumiwa na kosa linalohusika basi hufunguliwa mashitaka naye huitwa mshitakiwa. Mashitaka huanza pale hati ya mashitaka dhidi ya mshitakiwa inapowasilishwa mahakamani.
Uamuzi sahihi wa kumfungulia mashitaka mtuhumiwa hutegemea sana kiwango cha uwezo wa anayechukua uamuzi huo katika kuupima ushahidi uliopatikana katika upelelezi dhidi ya mtuhumiwa. Kinadharia mtuhumiwa hufunguliwa mashitaka pale ambapo ushahidi wa kutosha umepatikana kiasi cha kuweza kufungua na kuendesha mashitaka dhidi yake kikamilifu. Lakini kwa bahati mbaya, kiutendaji, hivyo sivyo kama ambavyo itaonekana sura inayofuatia.
Hati ya kupekua
Ili kupata ushahidi dhidi ya mtuhumiwa mara nyingi inabidi apekuliwe mwenyewe au sehemu anamoishi. Kitendo cha kumpekua mtu huingilia uhuru na hata hadhi yake hivyo ni lazima kifanywe kwa mujibu wa masharti ya sheria.
Kuna namna mbili za kufanya upekuzi kwa njia ya halali. Kwanza ni kupata hati ya kupekua kutoka mahakama yoyote iliyo karibu na tukio lenyewe (F. 40, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, Na. 1, 1985).
Pili kupata hati ya kupekua kutoka kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi. Kwa kawaida hati hizi za njia ya pili hutolewa kwa Polisi. (F. 38, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Hati ya kupekua inaweza ikatolewa na kutekelezwa siku yoyote ile hata Jumapili. (F. 40, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Kwa kawaida upekuzi hufanyika asubuhi hadi jioni lakini mahakama huweza kuamuru upekuzi ufanywe saa yoyote ile kama yanaona sawa kufanya hivyo.
Inatokea kuwa wakati wa kutaka kufanya upekuzi jengo au sehemu ya kupekuliwa imefungwa na mtuhumiwa hayupo. Ikiwa atakuwepo mtu mwingine yeyote anayeishi ndani ya jengo au sehemu hiyo au ana milki yake, mtu huyo atatakiwa kumpa polisi au yeyote mwenye hati hiyo, (baadaya kuonyeshwa), ruhusa na msaada wa kufanya upekuzi. (F. 43, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Polisi au mtu mwenye hati ya upekuzi anaweza kutumia nguvu za kutosha kama vile kuvunja na kuingia au kutoka ndani ya jengo linalohusika kutekeleza amri hiyo. (F. 43 (2), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Licha ya majengo, mtuhumiwa mwenyewe anaweza kupekuliwa. (F.42, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Iwapo mtuhumiwa ni mwanamke atapekuliwa na mwanamke mwenzake. Mwisho wa upekuzi hati itarejeshwa mahakamani ikionyesha kitu au vitu ambavyo vimepatikana. (F. 45(2), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Vitu hivyo vilivyopatikana vitahifadhiwa hadi mwisho wa upelelezi au shauri lenyewe. Kama mtuhumiwa atashitakiwa na kupatikana na hatia kitu hicho (ambacho kitakuwa kielelezo) kitashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Na kama mshitakiwa amekata rufaa basi kitahifadhiwa hadi wakati wa kusikiliza rufani hiyo. Iwapo mshitakiwa amepelekwa Mahakama Kuu hicho kitahifadhiwa hadi wakati wa kusikilizwa shauri lake. (Hapa inahusiana na mashitaka ambayo husikilizwa na mahakama Kuu tu, kama vile kuzinga na maharimu, mauaji, uhaini na kadhalika).
Maelezo ya Mtuhumiwa, Mshitakiwa na Mashahidi
Mtuhumiwa, mshitakiwa na mashahidi wanaweza kutakiwa kutoa maelezo polisi ili kusaidia upelelezi na uendeshaji wa mashitaka. Utaratibu wa kuandika maelezo ya watu hao unatofautiana kama ambavyo itaelezwa hapa chini.
Tukianza na mashahidi ni kuwa polisi wana uwezo wa kumwita na kumhoji mtu yeyote ambaye wanaamini anaweza kutoa taarifa kusaidia upelelezi wa kesi inayohusika. (F.32. Sheria ya Jeshi la Polisi, i.h.j. Pia F.46 (1) Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Kama ni lazima maelezo ya mtu huyu yatanakiliwa na polisi. Maelezo hayo yanaweza baadaye kutumika katika kuendesha na kuthibitisha shitaka dhidi ya mshitakiwa. Kwa kawaida polisi huandika maelezo hayo wenyewe kadiri shahidi anavyoeleza. Mwisho humsomea Shahidi maelezo hayo na kumtaka afanye masahihisho yoyote kama yapo. Shahidi hutakiwa kuweka saini katika maelezo yake pamoja na saini ya mwandishi wa maelezo hayo. (F.48, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Itabidi amfungulie mashitaka rasmi mtuhumiwa huyo halafu amhiarishe kama bado anapenda kutoa maelezo yake au la. (F.52(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Katika kufanya hivyo ni lazima mahakamani. (F.32(4), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Pia amueleze kuwa iwapo atakataa kumpa maelezo yoyote yanayoweza kuwa ushahidi kuhusiana na shitaka lenyewe atafikiriwa kuwa amefanya hivyo kwa nia ya kujiepusha na shitaka hilo. (F.52(4), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Maana ya mashauri hayo dhidi ya mshitakiwa ni kujaribu kupata ushahidi muhimu kutoka kwake bila ya vipingamizi, lakini kwa hiari. Kwa kawaida polisi hawamuachii mshitakiwa atoe na kuandika maelezo yake mwenyewe bali humhoji na kuyaandika maelezo hayo. Askari wengine wanadai kuwa bila ya kumhoji mshitakiwa huwezi kupata ushahidi muhimu na wala huwezi kujua kama anasema kweli au anadanganya.
Utaratibu huu una tatizo moja kubwa katika utoaji haki kwa mujibu wa sheria. Ni hivi: polisi na upande wa mashitaka wanapoamua kuendesha kesi mahakamani huwa wanao ushahidi muhimu (kama mshitakiwa hakutoa maelezo ya uwongo) dhidi ya mshitakiwa. Lakini mshitakiwa huwa haelewi hali na uzito wa ushahidi wa upande wa mashitaka. Jambo hili lastahili kurekebishwa ili kumwezesha mshitakiwa aandae utetezi wake vizuri. Hivi sasa utaratibu huo unafanyika katika mashauri ambayo yanatanguliwa na Uchunguzi wa Awali kabla hayajasikilizwa na Mahakama Kuu.
Aidha, huweza kutumika katika mashauri ya madai. Pengine inasahauliwa kwamba baadhi ya mashauri katika mahakama ya wilaya ni magumu kisheria na kiushahidi kuliko hata yale yanayosikilizwa na Mahakama Kuu kwa mara ya kwanza. Na kwamba mashauri ya jinai huadhibiwa kwa kifungo au faini au vyote pamoja, hivyo kuna haja kubwa ya kumpa mshitakiwa kila nafasi ya kuandaa utetezi wake vizuri.
Itaendelea toleo lijalo
|
|