MAKALA
 
Umuhimu na nafasi ya Ibada ya Hija katika Uislamu-3
 

Kafara kwa mwenye kuvunja masharti ya Ihram

Allah (s.w) kwa Urehemevu wake, ametoa nafuu kwa wale watakaovunja masharti ya Ihram kwa kutoa fidia isipokuwa kwa kosa la jimai. Tunafahamishwa katika Qur-an:

"... Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au ana vya kumuudhi kichwani mwake (akafanya yaliyokatazwa, kama vile kunyoa), basi atoe fidia kwa kufunga au (kwa kutoa) sadaqa au kuchinja mnyama ..." (2:196)

Katika Hadith tunafahamishwa:

Ka'ab bin Ajra (r.a) ameeleza: "Nilipokuwa katika (hali ya) Ihram kwa ajili ya 'Umra nilisumbuliwa sana na chawa kichwani mwangu. Mtume wa Allah (s.a.w) akaniambia ninyoe kisha nifunge siku tatu au nichinje mbuzi wa sadaqa au niwalishe maskini sita. (Bukhari, Muslim, Abu Daud).

Kwa hiyo kwa Muharim atakayevunja sharti lolote la Ihram atalazimika kutoa kafara kwa ama (i) kufunga siku 3 au (ii) kumchinja mbuzi na kuitoa nyama yake sadaqa au (iii) kulisha maskini sita.

Kufanya tendo la ndoa ni kosa lisilosameheka kwa kutoa kafara bali hubatilisha Hija au 'Umra moja kwa moja. Ama kwa mume aliyefanya mapenzi na mkewe kwa kubusiana na kumkumbatia bila ya kufanya kitendo cha ndoa, atatoa kafara ya ngamia (au thamani yake) kama atatokwa na manii na kama hatatokwa na manii, atatoa kafara ya mbuzi.

Kafara kwa mwenye kuwinda au kuonyesha windo akiwa katika Ihram ni mbuzi iwapo mnyama huyo ana ukubwa wa mbuzi, au mdogo zaidi kuliko hivyo; vinginevyo atatoa kafara ya mnyama aliye sawa na huyo aliyemuwinda au atatoa thamani yake anunue vibaba vya chakula kinacholiwa sana katika sehemu hiyo, na kumlisha kila maskini kwa vibaba vitakavyopatikana. Hivi ndivyo tunavyoagizwa katika Qur-an:

Enyi mlioamini! Msiue mawindo na hali ya kuwa mmo katika Hija au 'Umra. Na miongoni mwenu atakayemuua makusudi basi malipo yake yatakuwa kwa (kuchinja) kilicho sawa na alichokiua katika wanyama wanaofugwa kama watavyohukumu waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama huyo apelekwe ilipo Ka'aba (akachinjwe na kutolewa sadaqa huko) au badala ya hayo ni kufunga, ili aonje ubaya wa jambo lake (hili). Mwenyezi Mungu ameyafuta yaliyopita; lakini atakayefanya tena Mwenyezi Mungu atamuadhibu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye Nguvu na Mwenye kuadhibu. (5:95).

Aina za Hija

Kuna aina tatu za Hija ambazo kila mwenye kuhiji ana uhuru wa kuchagua mojawapo kulingana na uwezo wake wa kukidhi masharti ya kila aina. Aina hizi ni (i) Ifraad, (ii) Qiran na (iii) Tamattu kama zianvyoelezwa katika hadith ifuatayo:

Amesimulia Aysha (r.a): "Tulitoka na Mtume wa Allah (s.a.w) (kwenda Makka) katika Hija ya Mtume ya kuaga. Miongoni mwetu tulivaa Ihram kwa nia ya kufanya `Umra tu (al-tamattu) wengine kwa Hija na `Umra pamoja (al-Qiran) na kwa wengine kwa Hija tu (al-Ifraad). mtume wa Allah (s.a.w) alivaa Ihram kwa nia ya Hija tu. kwa hiyo kwa yule aliye vaa Ihram kwa hija tu au kwa Hija na `Umra pamoja, hakutoka katika Ihram mpaka siku ya kuchinja (kutoa muhanga yaani siku ya mwezi 10 Dhul-Hija). (Bukhari).

(i) Ifraad: Ni aina ya Hija ambapo, "Hajj" anavaa Ihram kwa nia ya kufanya Hija tu bila ya "Umra na katika ( ) Talbiya ataanza kutikia mwito wa Allah (s.a.w ) kwa:( ) yaani "Nimeitika kwa Hija." Hajj hatavua Ihram yake mpaka amalize matendo yote ya Hija yanayomlazimu kuwa katika Ihram. Hija huruhusiwa kuvua Ihram na kutoka kwenye masharti yake baada ya kutupa mawe kwenye mnara na kunyoa au kupunguza nywele siku ya mwezi 10 Dhul-Hija. Kwa yule aliyechagua aina hii ya Hija halazimiki kuchinja siku ya mwezi 10 Dhul-Hija.

(ii) Qiran: Ni aina ya Hija ambapo Haji huvaa Ihram kwa nia ya kufanya Hija na 'Umra pamoja na katika talbiya ataanza kutikia mwito wa Allah kwa: ( ) - yaani "Nimeitika kwa Hija na 'Umra'. Hajj katika aina hii ya Hija hatavua Ihram mpaka baada ya kuchinja na kufanya Tawaful-Ifadha (tawafu ya nguzo) siku ya mwezi 10 Dhul-Hija.

Aina hii ya Hija inafanywa na wale wanaokuja Makka na wanyama. Katika Hija yake ya kuaga, baada ya kumaliza ibada ya 'Umra, Mtume (s.a.w) aliwaamrisha watu wote wavue Ihram ila kwa wale waliokuja na wanyama.

(iii) Tamattu: Katika aina hii ya Hija, Haji anapofika katika Miiqaat yake huvaa Ihram kwa nia ya kufanya 'Umra tu na ataitikia mwito wa ( ) - yaani "Naitikia kwa 'Umra'. Baada ya kumaliza 'Umra atanyoa au kupunguza nyewele na kuvua Ihram au kuwa huru na miiko yote ya Ihram. Atavaa tena Ihram kwa nia ya Hija mnamo mwezi 8 Dhul-Hija, na atabaia na Ihram mpaka amalize Hija ya mwezi 10 Dhul-Hija kama ilivyo katika aina nyingine za Hija.

Katika aina hizi tatu za Hija, At-Tamattu ndio aina bora zaidi na yenye nafuu kubwa kwa wale wanaotoka mbali wasioweza kuja na wanyama, ama kwa wakazi wa Makka au majirani wa Makka ambao wana uwezo wa kwenda na wanyama, Hija iliyo bora kwao ni hii ya Al-Qiran. Lakini wenye kuhiji Hija ya Tamattu wanalazimika kununua mnyama na kumchinja siku ya mwezi 10 Dhul-Hija kama tunavyofahamishwa katika Qur'an:

"... Na mtakapokuwa kwenye salama, basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya `Umra kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliyesahilika (mbuzi au kondoo). Na asiyepata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba atakaporudi (kwake; hizi ni kumi kamili. Hayo ni kwa ajili ya yule ambaye watu wake hawako karibu na msikiti Mtakatifu wa Makka. na mcheni Mwenyezi Mungu na jueni ya kuwa Mwenyezi Mungu ni Mkali wa Kuadhibu." (2:196).

Matendo ya Hija na Umra

Matendo yote yanayokamilisha Ibada ya 'Umra na aina zote za Hija ni haya yafuatayo:

1. Ihram na nia ya Hija na 'Umra

2. Talbiya

3. Tawaf

4. Sa'i

5. Matendo ya siku ya Tarwiya (8 Dhul-Hija)

6.Siku ya Arafa (9 Dhul-Hija)

7.Kulala Muzdalifah (usiku wa kuamkia 10 Dhul-Hija)

8.Matendo ya siku ya kuchinja (siku ya Idd - 10 Dhul-Hija)

9.Matendo ya siku za Tashriq (11, 12, 13 Dhul-Hija)

10. Tawaful-Widaa (Tawaf ya kuaga)

1. Ihram na Nia ya Hija au 'Umra

Matendo ya Hija au 'Umra huanza rasmi kwa kuvalia vazi la Ihram. Kama tulivyoona Ihram huvaliwa nyumbani au katika vituo maalum - Mawaaqiit - vilivyowekwa na Mtume (s.a.w) kabla ya kuingia kwenye uwanja Mtakatifu wa Makka. Wakazi wa Makka huvalia Ihram nyumbani kwao.

Utaratibu unaofuatwa ni kwamba Hajj, kabla ya kuvaa Ihram, ni sunna kunyoa nywele za makwapani na sehemu nyingine za mwili, kupunguza nywele za kichwani, kunyoa ndevu na kukata kucha. Kisha ni sunnah kukoga, kutawadha na kupaka manukato ndipo uvalie Ihram. Ni vyema kuvaa Ihram wakati wa swala mojawapo ya faradhi. Mtume (s.a.w) katika Hija ya kuaga alivaa Ihram wakati wa swala ya Adhuhuri.

Kabla ya kutia nia ya aina ya Hija au 'Umra, Haji ataswali rakaa mbili za sunnah, kisha mara tu baada ya kutoa salaam atanuia aina ya Hija anayokusudia kuifanya, na ataitikia wito wa Allah (s.w) kulingana na nia yake.

Kama nia yake ni ya kufanya I'Umra (At-Tamattu) ataitika:

Ee Allah nakutikia kwa 'Umra.

Kama nia yake ni ya kufanya Hija na 'Umra (Al-Qiran) ataitika:

Ee Mola. Naitika kwa Hija na 'Umra.

Kama nia yake ni ya kufanya Hija tu (Al-Ifraad) ataitikia:

Ee Mola, Naitika kwa Hija

2. Talbiya

Talbiya ni maneno ya kutikia wito wa Allah (s.w) pale alipomuamrisha Nabii Ibrahim (a.s) kuwaita watu kwa Hija:

"Na (tukamwambia Ibrahim): Utangaze kwa watu habari za Hija, watakujia (wengine) kwa miguu na (wengine) juu ya kila mnyama aliyokonda (kwa uchovu wa safari ndefu). Ili washuhudie manufaa yao na kulitaja jina la Mwenyezi Mungu katika siku zinazojulikana ..." (22:27-28).

Maneno ya kuitikia wito huu wa Allah, yaani maneno ya Talbiya, kama yalivyo katika hadith iliyosimuliwa na Abdullah bin Umar (r.a) ni haya yafuatayo:

"Labbayka Allaahumma labbayka. Labbayka laashariika laka labbayaka. Innal-hamda wanni-i-mata laka wal-mulka; laashariika laka".

Tafsiri:

"Naitika wito wako Ee Allah, Naitika. Naitika, Ewe Usiye na Mshirika, Naitika. Hakika sifa zote njema na neema zote ni zako na Ufalme ni Wako, Ewe Usiye na Mshirika" (Bukhari na Muslim).

Wanaume wataitika kwa sauti ya juu na wanawake wataitika kwa sauti ndogo. Kwa wale walionuia kwa Hija tu au Hija na 'Umra, talbiya huanza mara baada ya kuvaa Ihram na kunuia, mpaka watakapotupa jiwe la kwanza katika mnara mkubwa -"Jamratul'Aqaba" siku ya mwezi 10 Dhul-Hija.

Talbiya ya 'Umra huanzia kwenye Miiqaat baada ya kuvaa Ihram na kutia nia ya 'Umra mpaka kwenye Nyumba Takatifu ya Ka'aba. Kwa wale walionuia Hija ya "Tamattu", wataanza Talbiya tena baada ya kuvalia Ihram kwa nia ya Hija siku ya mwezi 8 Dhul-Hija, na wataendelea mpaka wakati watakapoanza kutupa jiwe la kwanza kulenga mnara mkubwa siku ya mwezi 10 Dhul-Hija.

Wakati wa kwenda Makka talbiya itarudiwa tena na tena. Isomwe kila baada ya swala ya faradh, kila Hajj anapopanda na kuteremka katika kipando au chombo anachosafiria, na kila akipanda na akiteremka mlima, kila anapokutana na msafara mwingine. Mtume (s.a.w) alifanya hivyo pamoja na maswahaba wake alioongozana nao katika Hija ya kuaga. Kila alipotaka Waislamu wasome talbiya aliwaamrisha kwa kusema "Takbiir". Kisha Masahaba wake na yeye mwenyewe walianza kusoma Talbiya kwa nguvu.

3. Tawaf

Kutufu ni kitendo cha kuizunguka Ka'aba mara saba kuanzia kwenye Jiwe Jeusi (Hajaral aswad). Wakati wa kuzunguka Ka'aba inakuwa upande wa kushoto, yaani mzunguko ni kinyume na ule wa saa (anti-clockwise). Kutufu ndio Ibadah ya kwanza anayoifanya mwenye kuhiji au kufanya 'Umra mara tu baada ya kuizuru Ka'aba na kubusu Jiwe Jeusi.

Masharti ya Tawaf

Mwenye kutufu hana budi kuwa twahara. Yaani awe ameepukana na najisi na aina zote za hadath - asiwe na janaba, hedhi wala nifasi na awe na udhu.

Kwa wanawake wenye hedhi wanaruhusiwa kuingia katika Ihram na kufanya vitendo vyote vya Hija isipokuwa kutufu kama tunavyofahamishwa katika hadith ifuatavyo:

Amesimulia Aisha (r.a): Nilikuwa katika hedhi nilipoingia Makka, kwa hiyo sikuweza kutufu wala kusali. Kisha nilimfahamisha Mtume wa Allah, akaniambia, 'fanya vitendo vyote vya Hija kama wengine lakini usitufu mpaka uwe twahara.: (Bukhari).

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook