Waislamu Kusini wahimizwa kuchangia mfuko kusaidia wanafunzi
 

Na Mwandishi Wetu

WAISLAMU wilaya za Masasi na Newala wamehimizwa kuchangia mfuko wa kusaidia wanafunzi wa Kiislamu wanaosoma nje ya mkoa wa Mtwara.

Hayo yamesemwa na Sheikh Yousouf Kayungilo akiwahutubia waumini baada ya swala ya Isha katika Msikiti wa Al-Azizu mjini Masasi hivi karibuni.

Sheikh Yousouf ambaye ni Imamu wa Msikiti huo na msimamizi wa vituo vya Kiislamu Al-Azizu Islamic Centre Masasi na Darulfurqani Islamic Foundation Newala, alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuchangia mfuko huo ili kuwasaidia wanafunzi wa Kiislamu wanaosoma Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Arusha wanaotoka katika shule za Masasi na Newala.

Sheikh Yousouf aliendelea kusema kuwa kuchangia mfuko huo ambao una lengo la kusimamia utatuzi wa matatizo ya vijana wao kimasomo kutatoa changamoto kubwa kwao na kuwawezesha kumudu shughuli zao za masomo, kwani wao tegemeo lao kubwa liko katika kuinua hadhi na heshima ya Uislamu mikoa ya Kusini baada ya kumalizia masomo yao.

Akisisitiza juu ya swala la umuhimu wa elimu, Sheikh Yousouf alisema kuwa "kuwa siyo wakati wa kubishana kwa maneno bali Waislamu tunatakiwa kuonyesha vitendo hivyo tuna jukumu kubwa la kuwaelimisha Waislamu wanielewe vilivyo Uislamu ili waweze kuishi na kuabudu kuhukumu na kuhukumiwa Kiislamu ni kwa njia hii ya kuelimisha jamii ndiyo dawa pekee ya kupunguza migogoro na matatizo baina ya Waislamu".

Sheikh Yousouf pia alisisitiza kuimarisha kwa jumuiya za akina mama wa Kiislamu zilizoanzishwa Masasi na Newala kwa kuwaandalia semina, warsha na makongamano mara kwa mara ili kuwajenga katika msimamo wa kidini.

Aidha, Sheikh Yousouf alisema kuwa kumekuwa na juhudi za kuunda timu hiyo ya vijana ishirini na tano na kuwapeleka katika shule za Mutawasitah na Thanawiy ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa wataalam wa kidini unaoikabili mikoa ya kusini.

Sheikh Yousouf alimaliza hutuba yake kwa kuwaomba Waislamu kujitahidi na kuwa na moyo wa kuchangia kwa wingi mfuko huo kwa kutoa zakah na sadaka zao ili kufanikisha zoezi hilo la kuwasaidia vijana hao.

Michango hiyo inaweza kupitia uongozi wa taasisi hizo:

(i) Al-Azizu Islamic Centre S.L.P. 284 A/C Na. Mas/10/252 NMB tawi la Masasi.

(ii) Darulfurqani Islamic Foundation S.L.P. 365 Newala.
 
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook