]
Na Kipondo wa Changarawe
NAPENDA kuwakaribisha tena ndugu wasomaji kwenye hii safu ya kutafakari Qur'an kwa pamoja ili tuweze kupata mafunzo yatakayotuongoza kwenye njia ya haki iliyofundishwa na kufuatwa na Mitume wote kuanzia Adamu (a.s.) hadi kipenzi chetu Mtume Muhammad (s.a.w.). Katika maudhui yaliyopita, dodoso la kutafakari Qur'an lilijihusisha katika kuzingatia aya zinazozungumzia ahadi za kilaghai zinazotolewa na watu wa aina mbalimbali tunaoishi nao kwenye jamii; wanasiasa wakiwa ni vinara wanaoongoza kutoa ahadi hizo. Kwa maneno machache niliziita kuwa ni ahadi za peremende.
Kwa leo dodoso letu linahama kutoka kwenye ahadi za peremende kuelekea kwenye maudhui yenye anuani isemayo "Cheo kilichotelekezwa". Kutokana na ukaribu uliopo baina ya maudhui hizi mbili ni vyema tukiwa tunazishughulisha akili zetu katika kuzipambanisha ili tuone kiini cha upogo.
Ni ukweli usiopingika kuwa tangu ilipoteremka mpaka sasa Qur'an ndiyo mwongozo usio na upinzani ambao ukifuatwa ndipo yatakapostawi maisha ya amani na uadilifu katika jamii na kila mtu atalindwa, ataheshimiwa, atapewa haki zake zote zinazostahiki bila ya kuathiri uhuru wa mwingine.
Hii inatokana na ukweli kwamba sambamba na jukumu la ujumla la kuwaongoza wanadamu, Qur'an inajukumu la kuwaandaa viongozi waadilifu watakaowaongoza na kuwasimamia watu katika kufanya haki, uadilifu na usawa utendeke kwenye jamii. Kwa kupitia kanuni na sheria madhubuti zinazozingatia barabara "fitra" ya mwanadamu (mwili na roho) Qur'an humnyanyua mpaka kufikia cheo cha kuwa Muttaq hadhi ambayo humwezesha kuongoza kwa haki na uadilifu bila ya ubinafsi wala upendeleo.
Katika Istilahi za Qur'an, neno Muttaq hutafsiriwa katika lugha ya Kiswahili kwa maana ya mtu mcha Mungu. Natumaini kuwa neno "mcha Mungu" si geni kwako msomaji ama umekwisha sikia likitamkwa na watu au kulisoma katika sehemu mbalimbali. Nisingelipenda tuendelee kutumia neno 'mcha Mungu' na badala yake tutumie Muttaq au Muttaqun (wingi).
Akili ya mwanadamu ina kawaida ya kutaka sababu pale mtu anapotakiwa aachie jambo fulani na afanye jambo fulani badala yake. Huenda ukadai sababu za kutumia Muttaq badala ya mcha Mungu. Hebu sikiliza: Katika sura ya pili aya ya mia moja na kumi na nne, Qur'an inatutaka tutumie neno "Undhurna" badala ya neno "raa'ina". Maneno yote mawili yalikuwa na maana ya kumtaka mtu unayemheshimu akusikilize (Please look at us/Attend to us; showing politeness), lakini neno "raa'ina" lilikuwa likitumiwa vibaya na baadhi ya watu hivyo kupoteza maana iliyokusudiwa.
Kwani hili neno mcha Mungu lina maana gani nyngine katika jamii yetu? Aha! Vyema. Nafikiri utakumbuka kama una kumbukumbu nzuri kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu zilivyokuwa zikishika kasi, neno mcha Mungu lilikuwa likitumiwa na "wenzetu" kutuashiria tuwachague watu wenye moyo safi, wakarimu, wenye huruma, wa kweli na waadilifu. Lakini kutokana na uhalisia wa mambo yanavyokwenda; ukitajiwa neno mcha Mungu, taswira inayokujia kichwani ni ile "Operesheni choma moto majumba ya Nzasa, matingatinga yakibomoa bomoa majumba maeneo ya Ubungo na Yombo Vituka Lumo, choma ngano ya Bakhresa, mauaji ya Mwembechai n.k..
Pia zinakujia taswira za wachapakazi wenye hasira wakiwapa mkong'oto Waislamu, wakiwatungua wengine kwa risasi pale Mwembechai, wakiwadhalilisha akinamama na kuwasaka Masheikh nyumba hadi nyumba. Kisha zinafuatia kauli za shutuma na kuwapaka matope waliopigwa risasi kuwa "wanatumiwa na balozi za nje, alikutwa na karatasi na makaratasi ya uchochezi".
Nafikiri mpaka hapa imekwisha kukudhihirikia kuwa ni kwa kiwango gani mcha Mungu lilivyopoteza maana inayokusudiwa. Ni kwa msingi huu dodoso letu tunatumia stilahi ya Muttaq na kumchosha ili ajulikane kuwa ni nani hasa mtu huyo.
Muttaq ni kiongozi anayejitambua kuwa yeye si bwana aliye juu ya sheria na kuwa hawajibiki kwa yeyote, bali hufahamu vyema kuwa Allah (s.w.) ndiye Bwana na yeye anawajibika kwake. Hivyo; uwezo, mali, mamlaka, wakati, fursa pamoja na uhai alionao atahakikisha kuwa anautumia katika kusimamisha haki na uadilifu utendeke kwenye jamii.
Daima Muttaq ni mwenye kujihesabu na kujitathmini mwenendo wa matendo yake akizingatia kuwa lazima ataulizwa na Allah (s.w.) namna alivyotumia nguvu, uwezo, mali, mamlaka, fursa, wakati na uhai wake katika kuvifanya haki na uadilifu viongoze maisha ya jamii.
Kwa kuwa anajua kuwa hakuna njia wala namna atakayotumia kumkwepa Allah (s.w.), Muttaq kamwe hatofumbia macho dhulma wanayofanyiwa viumbe kwenye jamii wakati yeye akiwepo, atafanya jitihada kwa kutumia kila kilichopo mkononi mwake ili kuhakikisha kuwa inakoma. Huona kuna thamani kubwa kwake kuendelea kupambana na dhuluma mpaka iondoke au akutane na Allah (s.w.) katika hali hiyo kuliko thamani ya kuishi na kumwinamishia kichwa mwenye kudhulumu.
Taratibu na mifumo mbalimbali iliyofumwa na wanadamu ina nidhamu ambayo huwafanya wale wanaoandaliwa kuwa ni wa binafsi wasiojali utu kuliko matumbo yao na matashi mengine ya kinyama. Hii inatokana na dhana inayopandikizwa vichwani mwao kuwa ulimwengu hauna Muumba na kwamba maisha na kustarehe ni hapa duniani tu. Kutokana na msingi huu, lengo la maisha kwa hawa waandaliwa ni kujitahidi kwa gharama yoyote ile waweze 'kuyabojoa mapochopocho' na starehe za kimwili.
Kanuni yao ni sera ya nguvu mali (The Survival of the Fittest). Hebu sasa jaribu kuvuta fikra kuwa hali itakuweje watu wa mlengo huu wakiwa ndio wao wanaomiliki viwanda vya silaha. Je, ikiwa ndio hawa wenye kauli ya kutoa idhini katika masuala ambayo ni tete jamii inakuwaje. Hivi itawawia vigumu nafsini mwao kuanzisha mapigano na kuua mamia ya watu ili watwae madaraka yatakayowapa fursa ya kustarehe. Ni kitu gani kitakachowazuia wenye mamlaka wasifanye ujanja wa kujiongezea kura za ziada ili waendelee kuwepo pale wapaonapo pana wafikisha kwenye lengo lao la maisha.
Kinyume na hawa wenye kuyatazama maisha kwa jicho moja la kushoto, Muttaq huyatazama maisha katika upeo unaovuka mipaka ya haya maisha ya muda ya kidunia ambayo ndio msingi wa kushindwa au kupata mafanikio yasiyo katika maisha ya kudumu yaliyo usoni mwetu. Huyaangalia matatizo yote yanayoisibu jamii kuwa yana muhusu na kwamba liko mabegani mwake jukumu la kuyatatua, hatuacha kuyashughulikia eti kwa sababu yeye siye aliyesababisha yatokee. Hasha wakala! Anaogopa kuulizwa na Mola wake kwanini aliitekelekeza jamii katika makucha ya watu wanayotazama maisha kwa jicho moja la kushoto.
Vile vile anafahamu fika kuwa kutokuwa salama ikiwa hatofanya jitihada za makusudi katika kusimamisha Haki na uadilifu katika jamii inamoishi. Muttaq ni kama daktari mweledi aliye muadilifu ajuaye jukumu na wajibu wake, katu hatokaa kimya pindi unapofumuka ugonjwa wa hatari wa kuambukiza; iwe kajuwa kuwa umetokea kutokana na ujinga wa watu, uzembe au makusudi ya wachache miongoni mwa wana jamii. Atakachofanya ni kutumia ujuzi, muda, nguvu na zana alizonazo katika kutoa matibabu pamoja na kuwaelimisha juu ya chanzo, namna unavyoambukizwa, dalili zake na hatua za tahadhari za kuuzuia usitapakae.
Imekuwa ni bahati mbaya cheo cha Muttaq hakipatikani kwa kuchaguana, kurithi, kununua, kujipachika na kuitwa bali hufikiwa kwa kupitia Qur'an na hakuna njia ya mkato. Qur'an inalia na kutusisitizia kuwa "Muttaq ndiye mwenye kufuzu". Lakini wapi. Cheo kimesahaulika, kimetelekezwa na badala yake matwaghuti wametufunga kamba shingoni wanatuburuza tu kwenye uozo.
Kama hivi sivyo, ni wangapi katika sisi wakitembea wanaona? Ni wangapi miongoni mwetu wakiamshwa kwa maji baridi au kwa kijinga cha moto waamka? Ni wangapi wakipigiwa tarumbeta masikioni mwao wanasikia? Ni wangapi ambao wanaposoma Qur'an wanakiona hiki cheo? Wengi misahafu yetu imejaa mavumbi.
Inatosha, sitaki kusema sana. Hebu tuzitafakari kwa pamoja aya zifuatazo:
"Na wanapoambiwa msifanye uharibifu katika ardhi, husema: Hakika sisi ndio tutengenezao. Kwa hakika wao ndio waharibifu hawajui". (2:11-12)
"Na Allah ndiye mlinzi wa walioamini, huwatoa kutoka katika giza na kuingiza katika nuru; lakini wale waliokufuru viongozi wao ni matwaghuti, huwatoa kutoka katika nuru na kuwaingiza gizani. Hao ndo watu wa motoni humo watakaa milele". (2:257)
"Enyi mlioamini! Kuweni
wenye kusimamisha uadilifu, mshuhudiao kwa ajili ya Allah (s.w.)..." (4:135).
|
|