Msiipalie makaa nchiyetu - Ilunga
  Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imetakiwa kuacha kuyumbisha hakika kwamba Waislamu wananyanyaswa na kuonekana raia daraja la pili nchini mwao, badala yake ichukue hatua za makusudi kusitisha ukandamizaji huo.

Hayo yametamkwa na Sheikh Ilunga Kapungu kwa niaba ya maelfu ya Waislamu waliofurika katika viwanja vya Msikiti wa Mtambani Jijini ambako kulifanyika Baraza la Idd Jumapili iliyopita.

Mbele ya umati mkubwa ambao haujapata kuonekana siku za hivi karibuni, Sheikh huyo aliiasa serikali kutokucheza na hakika ya uonevu dhidi ya Waislamu.

Aliwaomba waandishi wa habari na watu wa Usalama wa Taifa wasaidie kulinusuru taifa na maafa yatakayoweza kusababishwa na watu kunyanyaswa kwa muda mrefu.

"Si tabia ya binadamu kukubali kunyanyaswa", alisema Sheikh Ilunga.

Huku akirejea matamshi ya aliyekuwa Rais wa Marekani Bwana Abraham Licoln, Sheikh Ilunga alisema wale wanaopuuza malalamiko ya Waislamu wanaipalia mkaa nchi yetu.

"Inawezekana kuwanyanyasa watu wote kwa kipindi fulani na inawezekana kuwanyanyasa baadhi ya watu kwa kipindi chote, lakini haiwezekani kuwanyanyasa watu wote kwa wakati wote", alikariri Sheikh huyo ambaye ni mkazi wa Mwanza.

Akirejea hatua ya kujifunga mabomu wanayoichukua Wapalestina leo hii dhidi ya Waisraeli, alionya isifikie binadamu kunyanyaswa mpaka akaona kufa ni bora kuliko kuishi.

"Atakachohakikisha hafi peke yake bali na japo wachache aliowakusudia", alisema kwa uchungu Sheikh huyo.

Aidha, alisema kwa bahati mbaya serikali inajaribu kupuuza ukweli huo na kuendeleza "sera za nguvu mali" za kupeleka bataliani za mapolisi Misikitini.

Alisisitiza kuwa binadamu si swala; hufika mahala akajiuliza kwanini ananyanyaswa na afanye nini ili aondokane na kunyanyaswa.

" Hizi ni dalili za kuchoka, Muslims now becoming tired (Waislamu sasa wamechoka), watu wa magazeti kama mtalifikisha mtakuwa mmelinusuru taifa hili", alisema Sheikh Ilunga.

Katika hotuba hiyo iliyoonekana kuvuta hisia za waisikilizaji, Sheikh Ilunga aliikumbusha serikali kuwa Waislamu wana malalamiko yao yenye ushahidi mzito.

Alihoji ni kwanini Mtanzania Muislamu aishi kama raia daraja la pili katika nchi yake ilhali Katiba ya nchi inawalinda Watanzania wote.

Aliyataja baadhi ya madhila wanayofanyiwa Waislamu kuwa ni pamoja na uenezaji wa mabucha ya nguruwe, kukatazwa kuhubiri dini yao, kuzuia mavazi ya stara kwa wanafunzi Waislamu na muda wa swala (hasa Ijumaa) mashuleni na maofisini.

Sheikh Ilunga alisema kadhia ya mabucha ya nguruwe mwaka 1993 iliashiria udhia mkubwa uliopo hapa nchini dhidi ya Waislamu.

Katika kadhia hiyo Masheikh na wahadhiri walikamatwa kwa kuhusishwa na uvunjaji wa bucha za nguruwe huku serikali ikiwa imekalia madai ya Waislamu karibu mwaka mzima.

"Vipi serikali inakuja kuwakamata walioua nguruwe badala ya kumshughulikia mfungaji na muuzaji wa nguruwe", alihoji Sheikh Ilunga.

Alisema hata katika ukamataji hapakuwa na heshima kwa Masheikh kinyume na ambavyo wangefanyiwa Maaskofu.

"Askofu hawezi kukamatwa hivyo, hata akikamatwa anakamatwa kwa heshima, 'tafadhali baba Askofu unaitwa kituoni".

Kuhusu suala la Mwembechai, Sheikh Ilunga alisema hadhani kuwa mauaji yale yalifanyika kwa bahati mbaya.

"Mwembechai ni hatma ya maonezi ya Waislamu nchini", alisisitiza.

Kuhusiana na ruhusa ya vazi la hijab mashuleni, Sheikh Ilunga alihoji ujasiri wa mwalimu mkuu wa shule ya msingi kupinga amri ya mkuu wake wa kazi.

"Katiba inasema uhuru wa kuabudu, mtu anazuia nini anapovaa hijab, midhali ni vazi la Kiislamu anachukia", alisema kwa mshangao.

Akielezea kuhsu jitihada ya baadhi ya watu kupeleka masuala ya Waislamu ngazi za juu na Bungeni alisikitishwa na namna masuala hayo yanavyojibiwa na baadhi ya Waheshimiwa.

Alisema wakati Rais akipokea malalamiko ya Waislamu Mheshimiwa mwingine alisimama Bungeni na kuyaita kuwa ni udini ambao unaotakiwa kuangaliwa kwa tahadhari.

"Waislamu wanapeleka matatizo yao bungeni unaitwa udini, wakizungumza wenyewe Misikitini inaitwa uchochezi, wakasemee wapi?" alihoji kwa hisia Sheikh Ilunga.

Akimaliza hotuba yake kwa kuwataka Waislamu nchini kote kuitafakari hail waliyonayo na wazungumze matatizo yao kwenye mikusanyiko ikiwa ni pamoja na vikao vya kahawa wakilengaa kuleta mabadiliko mwakani.

Baraza la Idd Mtambani lilifanyika huku kukiwa na ulinzi mkali wa vyombo kadhaa vya dola.

Mbali ya maaskari kanzu waliofurika mahali hapo kwa "miavuli" tofauti, magari madogo (gofu) kadhaa yalikuwa yakizunguka eneo zima la Kinondoni.

Karandinga lililojaa polisi waliokuwa na silaha liliwekwa tayari katika bonde la barabara ya Kawawa (Moroco) kuelekea Magomeni.

Aidha, kulipatikana taarifa kwamba Land Rover 12 zilizojaa askari wa kutuliza ghasia (FFU) zilikuwa zikivinjari barabara ya Mwenge.

Polisi wengine walionekana kufanya doria za miguu na kila kona iliyopo eneo hilo ilikuwa na maaskari kadhaa waliokuwa tayari kutekeleza amri kutoka juu.

Pamoja na hali hiyo ya kutisha, Waislamu waliendelea kumiminika katika Baraza hilo wakiyapiga pande mabaraza mengine yaliyoandaliwa siku hiyo. 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook