Kubomolewa kwa Madrasatil - Az-Hra Shariff Arusha hukumu yake Aprili 21
 

HUKUMU ya kesi inayowakabili Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha, Alhaj Mohammed Mollel na Baraza la Wadhamini itasomwa Aprili 21, mwaka huu katika mahakama ya Mkoani hapa.

Hakimu wa Wilaya Bw. Phares Mbuge baada ya kusikiliza kesi hiyo zaidi ya masaa mawili hapo Machi 9 alisema kuwa ameridhika na maelezo ya pande zote mbili zinazovutana.

Katika kesi hiyo ya madai Namba 8/99 iliyowakilishwa Februari 11 mwaka huu na Waislamu wapatao 50 wakiongozwa na Abduwel Mohammed wa mjini hapa wanadai kuwa Katibu wa Bakwata mkoa Alhaj Mollel na Baraza la wadhamini kuamua kuivunja Madrasatil-A-Har Shariff bila kufuata taratibu za sheria (Katiba ya Bakwata) ni kuwaburuza.

Akiwasilisha malalamiko ya Waislamu mahakamani, Wakili anayewatetea Bw. Kinabo alisema kuwa jengo hilo lilijengwa kwa ajili ya kutoa taaluma ya kidini na si kwa lengo la biashara.

Akitoa ufafanuzi zaidi Wakili huyo alisema Waislamu wote wanayo haki ya kufuatilia na kudai jambo lolote linalohusika na ustawi, maendeleo na maslahi ya Waislamu.

Aidha, Wakili huyo aliiomba mahakama kutupilia mbali ombi la walalamikiwa (Alhaj Mollel na Baraza la Wadhamini) walioitaka mahakama kubatilisha Hati ya kusimamishwa ubomoaji (Injuction Order) iliyotolewa Februari 11, mwaka huu hivyo itupiliwe mbali na ubomoaji uendelee.

Naye Wakili wa upande wa utetezi Bw. Loumi Ojare akijibu hoja, aliiambia mahakama kuwa walalamikaji hawana uhusiano wowote na mali inayogombaniwa, si kweli kwamba ni wawakilishi wa Waislamu bali ni kikundi kidogo cha watu wachache. Hivyo hawana haki wala mamlaka yoyote juu ya Bakwata.

Aliendelea kuifahamisha mahakama hiyo kuwa hatua zote za kisheria zilifuatwa na wateja wake ikiwa ni pamoja na kupata vibali vya kubomoa na kujenga.

Aidha, Wakili huyo aliiomba mahakama hiyo itupilie mbali hoja zote zilizowasilishwa na Waislamu hao kwa sababu baadhi ya walalamikaji wa kesi hiyo walishajitoa akiwemo Bw. Abduwel Mohammed.

Akikamilisha hoja zake, Wakili huyo alisema kuwa anaiomba mahakama itupilie mbali Hati ya Kusimamisha ubomoaji na ujenzi wa madrasa hiyo na kwamba kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo gharama za ujenzi zinazidi kupanda.



Waislamu watakiwa kutangaza kashfa ya Mwembechai

WAISLAMU nchini wametakiwa kutoingia woga katika uangaliaji wa mikanda ya video inayohusu mauaji ya Mwembechai kwani suala hilo siyo kosa ndio maana Rais kalipokea na kwenda kulifanyia kazi na Mawaziri wake.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni mjini hapa na Katibu wa Msikiti wa Mafiga (Manzese) Ustadh Said Ramadhani wakati wa Itikafu maalum iliyofanyika Msikitini hapo kwa ajili ya kukumbushana ibada ya Hija, makumbusho ya funga ya Ramadhani na kutazama mkanda wa video wa mauaji ya Waislamu yaliyofanyika Februari 12, mwaka jana jijini Dar es Salaam.

Katibu huyo alisema kuwa moja kati ya malalamiko aliyopewa Rais wakati wa Baraza la Idd mwanzoni mwa mwaka huu ni suala la mauaji ya Mwembechai ambapo Rais hajatoa jibu bado kama suala hilo, hivyo hakuna mwenye haki ya kuzuia suala hilo lisizunguzwe au matukio yake yasikumbukwe.

"Inashangaza ndugu zangu watu wanatishwa hata kuzungumzia mauaji ya Mwembechai kwa madai ya kuogopa kukamatwa, msiogope, zungumzeni suala hili popote pale", alisema Katibu huyo huku akito wito kwa Waislamu wote kupata kanda ya video ya mauaji hayo ili iwe historia yao pamoja na vizazi vijavyo kwa lengo la kukumbuka dhulma wanazofanyiwa Waislamu ndani ya nchi yao.

Aidha, Katibu Said ametoa changamoto Waislamu kuacha kupiga kelele tupu kuhusu kuzuiwa kuvaa hijabu, bali amewataka Waislamu wote kwa umoja wao kuwashonea watoto wao vazi hilo na kuwapeleka shule na mwalimu atakayekataa basi huyo ndiyo atakuwa ni mwenye kuulizwa mbele ya sheria.

"Rais Mkapa aliwahi kutulaumu kama madai yetu Waislamu yanakuwa hayana ushahidi wa kisayansi kutokana na kusema maneno matupu, sasa tuwavishe watoto wetu hijabu yule atakayewavua ndiye atakuwa shahidi wa madai yetu mbele ya serikali", alisema.

Naye Ustadh Rajab Salum wa kikundi cha mihadhara ya Khidmat akitoa mchango wake Msikitini hapo amewaasa Waislamu kuwa macho na wanasiasa wa serikali hii kwa kuandaa na kuwafanya wajishughulishe na mambo ya mwaka 2000 wakati Waislamu hawatakiwi kuwepo au kufanya mambo yao kwa ajili ya mwaka huo.

"Mauaji ya Mwembechai yamefanyika kwa madai ya mihadhara inayodaiwa ya kashfa, leo mihadhara hiyo hiyo inafanyika tena bila ya vikwazo, tofauti na siku za nyuma kwa madai serikali ipo pamoja nasi katika kutupa uhuru wa kuabudu lakini hapo lengo likiwa mwaka 2000", alisema.

Pia Ustadh Salum amesema kinamama wa Kiislamu kutotetereka na kutumbukia katika fitna za wanasiasa waliowatuma watu kwenda kuwadhalilisha wanawake wenzao pale Mwembechai, badala yake amewataka wawe katika kamba moja tu ya Uislamu.

Awali katika itikafu hiyo Ustadh Seleman Kiriri aliwasilisha mada ya ibada ya Hija ambapo amewaasa Waislamu na hasa wale wanaokwenda kuhiji kuwa lengo la kwenda huko siyo kupata jina au kuchonga mhuri wa Alhaj fulani, kwani kwa kufanya hivyo itakuwa ni kucheza (Riya) na hakuna muendaji atakayekipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Mwisho katika itikafu hiyo iliyohudhuriwa na Waislamu kutoka Misikiti mbalimbali mkoani hapa kulitolewa maazimio kadhaa ikiwa ni pamoja na Waislamu kutosahau mauaji ya Mwembechai na wote wametakiwa kutangaza suala hilo kwa kuongea au kutazama kanda za video majumbani, Misikitini na hata sehemu za wazi.

Azimio lingine lililotolewa ni pamoja na Waislamu wote kuwashonea watoto wao hijab na kwenda nao shule na watoto watakaofukuzwa suala hilo lipelekwe Misikitini ambapo viongozi watalishughulikia kwa mujibu wa sheria.



Imarisheni hadhi ya Misikiti - Sheikh

WITO umetolewa kuipa hadhi Misikiti na heshima zake kama ilivyokuwa wakati wa Mtume Muhammad (s.a.w.).

Sheikh Ally Koyogole alitoa wito huo katika khutba ya swala ya Ijumaa ndani ya Msikiti wa Al-Kadiriya Temeke hivi karibuni.

Katika khutba hiyo iliyokuwa na anauni ya "Nafasi na Hadhi ya Misikiti katika Uislamu", Sheikh Ally alionya kutoifanya Misikiti mahala pa vurugu au kuanzishia vurugu, badala yake aliwataka Waislamu kuifanya mahala pa upendo na kushauriana kama ilivyokuwa wakati wa Mtume.

Sheikh Ali aliendelea kusema kuwa Msikiti ni taasisi muhimu sana katika Uislamu na ndio maana Mtume (s.a.w.) alipohamia Madina hakujenga nyumba yake isipokuwa Msikiti.

Akifafanua Qur'an 9:18, Sheikh Ally alisema "Kuimarisha Misikiti ni pamoja na kuswali swala tano Misikitini, usiposwali umevunja hadhi na heshima ya Msikiti".

Alihitimisha kwa kuwataka Waislamu kurudisha hadhi na heshima ya Misikiti kwani kwa kufanya hivyo Waislamu watafanikiwa katika mambo yao yote.



Muuza kanda za dini Moro atishiwa maisha
 

LICHA ya serikali kudai kuwa haiwanyanyasi watu wa dini yoyote, Afisa Mtendaji wa Kata ya Uwanja wa Taifa mjini hapa amemtishia kumfunga Bw. Hamza Rajab kwa madai ya kupiga kanda za mawaidha ya Kiislamu yenye kutukana Ukristo.

Afisa Mtendaji huo Bw. Boneventura Shelu inadaiwa kuwa mara kwa mara amekuwa akimsumbua muuza kanda huyo anayeuza karibu na shule ya msingi Kiwanja cha Ndege na kumtishia kumfunga jela.

Akielezea mkasa huyo mapema wiki hii, Bw. Hamza alisema kuwa vitisho vya Afisa Mtendaji huyo vilizidi wiki iliyopita alipofika katika kibanda chake na kuondoka na kanda ya mawaidha iliyokuwa inapiga kwenye kaseti iliyokuwepo kibandani hapo.

Bw. Hamza ameendelea kusema kuwa aliamua kumfuata Afisa huyo ofisini kwake ili amueleze sababu ya kuchukua kanda yake ambapo wakati kitendo hicho kinafanyika Bw. Hamza hakuwepo katika kibanda chake na alimuachia mtu anayemuuzia kwa muda.

Alipofika ofisini kwa Afisa huyo, alipewa majibu ya vitisho kuwa aache mara moja kupiga kanda hizo na hasipoacha basi atachukuliwa hatua kwani suala lake hilo wakazi wanaoishi maeneo hayo tayari wameshalipeleka kwa Mkurugenzi wa Manispaa. Hata hivyo Afisa huyo hakuweza kutoa kanda aliyoichukua.

Bw. Hamza ameendelea kusema kuwa kesho yake aliamua alipeleke suala hilo kwa viongozi wa Tawi la AL-MALLID mkoa wa Morogoro hata hivyo walienda kumuona Afisa huyo ambapo alikataa kutoa ile kanda na kumlazimisha aache kupiga kanda zile.

Ameendelea kusema kuwa viongozi wa AL-MALLID walimtaka Afisa huyo awape maandishi kama kachukua kanda na hataki eneo la kata yake kuwekwa kanda za mawaidha ya dini ya Kiislamu.

Muuza kanda huyo alisema kuwa baada ya kuambiwa maneno hayo Bw. Shelu akanywea na kuwaambia viongozi hao kuwa hilo ni suala dogo tu na hasingependa liwe kubwa na mwisho akatoa ile kanda bila ya masharti yoyote.

Wakati huo huo, mwanzoni mwa wiki hii katika viwanja vya Kikundi kulifunguliwa rasmi tawi la AL-MALLID mkoa Morogoro ambapo ilifuatia na kufanyika mhadhara mkubwa ulioendeshwa na kikundi cha AL-MALLID Taifa.

Akielezea sababu ya kuanzisha tawi mjini hapa, Makamu wa Mwenyekiti mkoa Ustadh Hussein Al-Bashir amesema hiyo imetokana na masikitiko mengi ya kufa kwa Uislamu vijijini yanayotolewa na gazeti hili.



Waislamu watakiwa kuhifadhi mazingira

WAISLAMU mjini hapa wametakiwa kuzuia kwa uwezo wao wote uharibifu mkubwa wa mazingira unaotishia kumhilikisha mwanadamu leo, kwa kushikamana na kutekeleza vilivyo mafundisho ya Uislamu pamoja na kutekeleza vyema jukumu lao la kuamrisha mema na kukataza maovu.

Hayo yamo katika hotuba ya Ijumaa iliyotolewa hivi karibuni na Amiri Mohamed Isa katika Msikiti wa Al-Farouq uliopo eneo la majengo, mjini hapa.

Akielezea nukta hiyo, Amir Mohammed alisema kuwa wasio Waislamu wanayachukulia mazingira kuwa ni anga, ardhi na vilivyomo katika ardhi kama vile milima, misitu, maji ya bahari na mito na hivyo kuelekeza nguvu na juhudi zao zote katika kuhifadhi vitu hivi tu.

Alisema kuwa katika Uislamu msamiati huu "mazingira" unajumuisha hayo yote yaliyotajwa pamoja na mwanaadamu mwenyewe kama khalifa wa Allah (s.w.) hapa ulimwenguni.

Aliendelea kusema kuwa mazingira mazuri na salama kwa mwanadamu ni kule kuishi kwa mujibu wa lengo la kuumbwa kwake, bila kujidharau yeye mwenyewe na vile vile bila ya kuyadhuru mazingira yanayomzunguka ambayo yapo tu kwa faida yake yeye.

Alisema kuwa mazingira mazuri na salama kwa mwanaadamu ni kule kuishi kwa mujibu wa lengo la kuumbwa kwake na si vinginevyo. Akizungumzia kuharibika kwa mazingira kukubwa kuliko leo.

Amiri Mohamed alitoa mfano wa kuharibika kwa maadili kwa kiwango kikubwa sana kufikia hatua ya maovu yaliyoenea kuonekana kuwa ni kitu cha kawaida tu.

Aliyataja baadhi ya maovu hayo kuwa ni wanawake kwenda uchi hadharani, ulevi kutangazwa na kushindaniwa hadharani, zinaa kufundishwa, kuchochewa na kudhaminiwa bila haya, rushwa kuachiwa kuwa kitanzi cha haki ya wanyonge, kukosekana huruma na mapenzi katika nyoyo za watu na mengine mengi yanayomhilikisha mwanadamu leo.

Alisema kuwa huu ni uharibifu mkubwa wa mazingira na wa hatari zaidi kuliko jangwa, kuliko kukata misitu na hata kuliko kuchafuliwa bahari.

Aliwaonya wale wote wanaochangia kwa namna moja au nyingine kuharibika kwa mazingira (maadili) kama vile kuwashindanisha mabinti katika mashindano ya kwenda uchi hadharani, ambapo wakati mwingine wageni rasmi huwa ni viongozi wenye dhamana serikalini, wale wanaoendesha kampeni za uzinzi "salama" huku wakijali tu kushibisha matumbo yao kupitia kampeni hizo, wale wanaowahimiza watu kulewa kwa matangazo ya redio, televisheni na mabango ya mitaani yaliyoandikwa "Urithi Wetu" (utadhani wananchi wote wa nchi hii ni walevi) n.k. waache tabia hizo ambazo leo zinamfanya mwanaadamu kutokuwa tofauti na mnyama.

Hata hivyo, alisema Amir Mohamed jukumu hili ni la Waislamu. "Ninyi ndiyo mlio na mwongozo unaosema hili baya na hili zuri, ninyi ndio mlioamrishwa kuamrisha mema na kukataza maovu, hivyo ni jukumu lenu la kidini kukemea kwa nguvu zote uovu huu", alisema.

Aliendelea kusema kuwa Waislamu wapambane kukemea maovu haya kwa kuwaelimisha watoto wao, wake zao na Waislamu wenzao kupitia mafundisho sahihi ya Uislamu, kutekeleza Uislamu wao kwa vitendo na kushirikiana pamoja na umma kuyakemea maovu yote yanayohubiriwa na kufanywa hadharani hata kama mfanyaji ni mfalme.

Alinukuu Hadith ya Mtume (s.a.w.) isemamyo kuwa, "mwenye kuuona uovu miongoni mwenu auondoe kwa mkono wake, ikiwa hawezi basi kwa ulimi wake na ikiwa hawezi basi achukie kwa moyo na (hatua hiyo) ni katika udhaifu wa imani".



Waislamu watakiwa kufanya kazi

WAISLAMU nchini wamehimizwa wafanye kazi kwa bidii na waachane na uvivu na uzembe kwani huo sio msingi wa dini ya Uislamu, sababu mwanaadamu ataulizwa na Allah (s.w.) neema alizopewa alizitumiaje.

Hayo yalisemwa katika hotuba ya sala ya Ijumaa hivi karibuni katika Masjid Al-Haramain mjini Moshi.

Hotuba hiyo imebainisha kwamba wanaadamu wamekuwa Makhalifa hapa ardhini na kuna wachunga ili wasimamishe uadilifu katika maendeleo na uchumi thabiti hayawezi kupatikana bila ya kufanya kazi kwa bidii kwa kutumia nguvu.

Hotuba iliendelea kusema "kazi maana yake ni kudumisha uhai wa mwanaadamu na kuendeleza ubora wa maisha yake kidunia na hasa Muislamu amelazimishwa kufanya kazi na Mola wake kama Mtume (s.a.w.) anavyosema: Hakika Mwenyezi Mungu anampenda mja anayekula kwa kutumia jasho lake katika kazi ya halali", ilisema.

Aidha, hotuba ilisema katika Uislamu kuna nguzo za zaka katikanguzo tano, hivyo ni vigumu kwa Muislamu kutoa hiyo zaka kama hafanyi kazi ya halali, vile vile Mtume (s.a.w.) amesema kuwaambia maswahaba kuwa mja mwema ni yue anaye fanyakazi kwa mikono yake iliyo halali na nzuri.

Hotuba iliendelea kusema Mtume (s.a.w.) alikuwa akimuomba Mwenyezi Mungu kila siku amuepushe na huzuni na machungu pia amuepushe na uzembe na uvivu, kwani hata ndege hutoka asubuhi kutafuta riziki na kuudi jioni hali ya kuwa wameshiba na hivyo Waislamu wasikae kwenye jiviwe, mabaraza ya karata, bao na zumna huku wakilalamika hali mbaya ya maisha.

Hotuba hiyo ilisema kwani Mtume (s.a.w.) ailfanya biashara kwa Bi. Khadija na kukubali kuajiriwa ili apate halali ya jasho lake na aidha Mtume (s.a.w.) alifanya kazi ya kuchunga mbuzi bila ya kujali wala kuona vibaya, hivyo Masheikh wote na Waislamu ambao wanakaa katika mabaraza ya Misikiti na kutunga mbinu za kuwadhulumu waumini kwa kuwaletea ibada hewa ambazo hazina asili na dini ya Uislamu wa kupokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.) na maswahaba watukufu.

Hotuba hiyo ilimalizia kwa kuwasisitiza Masheikh na Waislamu kuacha mara moja kuishi maisha ya kijanja janja ambayo yanategemea hitima, talakini, maulid na mahakiki yanayoambatana na kuchoma ubani kama dua maalum za kuwadanganya Waislamu ambao hawajasoma dini yao, mambo ambayo ni dhuluma kubwa.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook