Sheikh Ponda awahutubia Waislamu
 

Na Mwandishi Wetu

KATIBU wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu, Sheikh Ponda Isa Ponda Jumapili iliyopita alihutubia maelfu ya Waislamu waliofurika katika Baraza la Idd lililoandaliwa Msikiti wa Mtambani Jijini.

Akitoa hutuba yake kupitia mkanda wa Video, Bwana Ponda aliwataka Waislamu kuzidisha mshikamanao walionao katika kukabiliana na uadui unaoendelezwa dhidi yao kwa muda mrefu hapa nchini.

Aidha, alisisitiza dai la Waislamu kuitaka serikali iwachukulie hatua wale walioua Waislamu Mwembechai na iunde Tume huru itakayochunguza kwa kina chanzo cha mauaji ya Mwembechai.

Katika hotuba yake hiyo iliyosikilizwa kwa utulivu mkubwa na waumini, Sheikh Ponda alifanya marejeo katika historia ya nchi kabla na baada ya uhuru.

Alisema harakati za kupigania haki nchini kabla ya uhuru zilitokana na serikali za kikoloni kutowatendea haki Waislamu.

Akitoa ushahidi kutoka maandiko kadhaa, Sheikh Ponda alisema hata serikali ya Tanganyika huru iliandaliwa iendeleze mkondo huo wa kuwakandamiza Waislamu kidini na kijamii.

Alisema kamata kamata ya Masheikh mwaka 1964 ilidhihirisha mpango huo mbaya dhidi ya Waislamu.

Kuvunjwa kwa Jumuiya ya Kiislamu mwaka 1968 na kuundwa Bakwata alilieleza kuwa ni katika harakati hizo za kuwabinya Waislamu pamoja na kuwa ni wao walioongoza harakati za kudai uhuru.

Sheikh Ponda alielezea kuundwa kwa kamati yake mwaka 1993 kwamba kulitokana na kadhia hiyo ambapo mwaka huo yalihusiana na uvunjwaji wa mabucha ya nguruwe.

Alifahamisha umati huo kuwa kamati yake ambayo wakati huo ilikuwa chini ya Uenyekiti wa marehemu Amiri Awalina ilijishughulisha na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kusimamia kesi zilizokuwa zikiwakabili Waislamu waliokamatwa.

Alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka Waislamu wachukue hadhari juu ya hali ya chuki na uadui inayowakabili.

"Waislamu tumefikishwa mahali ambapo tunalazimishwa kuchagua ama kukaa kimya tuendelee kudhulumiwa, tuhame nchi au tuamue tukose wote", alimalizia Sheikh Ponda.

Baadhi ya watu Jijini wamesikika wakisema dai la kumsaka Sheikh Ponda lililotolewa na polisi jijini Dar es Salaam ni ushahidi mwingien wa kisayansi ambao Rais Benjamin Mkapa aliuhitaji wakati akipokea malalamiko ya kukandamizwa kwa Waislamu hapa nchini.

Waliochochea kudhulumiwa Waislamu, walioamrisha kuvamia Msikiti na waliofanya mauaji Mwembechai wako huru na familia zao, Sheikh Ponda na familia yake wanaendelea kutishiwa usalama wao kwa kuitaka serikali ifanye uadilifu", amesema kwa uchungu Bwana Salum Almasi mara baada ya kusikiliza mkanda huo.

Hotuba ya Sheikh Ponda iliacha gumzo kubwa miongoni mwa waumini Jijini Dar es Salaam wiki hii. 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook