Na Mwandishi Wetu
MSHAURI Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Prof. Lipumba amewataka wazee wa Dar es Salaam kufikiria mustakabala wa nchi yao kwa kuzingatia hali ngumu inayowakabili Watanzania hivi sasa hasa walio mitaani.
Akizungumza na Wenyeviti wa chama hicho na wazee wa Dar es Salaam katika ukumbi wa Starlight Jumamosi iliyopita, Prof. Lipumba ambaye alikuwa mgombea wa kiti cha Urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita, amesema uchumi wa nchi umeporomoka na hakuna mipango makini kurekebisha hali hiyo.
Prof. Lipumba ambaye ni mtaalamu wa uchumi, alitaja sababu kadhaa zilizoangusha uchumi wa nchi, kubwa ikiwa ni sera ya "uchumi kutumikia siasa" ambayo amesema chama tawala imedumu nayo tangu nchi ipate uhuru.
Alihoji vipi Watanzania wadumu na umasikini wakati nchi yao ina utajiri wa maliasili.
Aliitaja Burkina Faso ambayo huko nyuma ilikuwa na matatizo makubwa ya kiuchumi lakini baada ya kuufanyia kazi utafiti wa kilaatamu leo hii imeondokana na tatizo hilo licha ya kutegemea maliasili ya bandari peke yake.
Akikariri hotuba ya Rais Mkapa aliyoitoa wakati akizungumza na wanafunzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu katika ukumbi wa Nkrumah hivi karibuni, Prof. Lipumba alisema Rais alirejea mara kadhaa azma ya serikali yake kurekebisha hali ya uchumi ya nchi.
Hata hivyo, Prof. Lipumba alionyesha kuzorota maeneo kadhaa yanayoweza kuchangia kuinua uchumi huo.
Alitolea mfano wa ukusanyaji wa kodi na jinsi serikali inavyojigamba kufanikiwa katika zoezi hilo.
Alisema haitakuwa na maana yoyote kwa serikali kutangaza mafanikio ya ukusanyaji wa kodi wakati hospitali hazina dawa, barabara mbovu, walimu hawalipwi mishahara kwa wakati na kuzorota maeneo mengine kadhaa ambayo huendeshwa na kodi hiyo.
Aliwataka wazee hao kutafakari kwa kina hali yao ya maisha hivi sasa kulinganisha na ile ya miaka ya mwanzo ya muongo huu (1990) kisha watafute namna ya kuondokana nayo kwa taratibu za kidemokrasia.
Awali katika hotuba yake hiyo, Prof. Lipumba aliwapongeza wenyeji wa mkoa wa Dar es Salam kwa tabia yao ya ukarimu ambayo imepelekea wananchi wa mikoa mingine kuhamia mkoa huo na kuanzisha makazi ya kudumu.
Akitilia mkazo hilo Prof. Lipumba alirejea historia ya nchi hii na kusema kwamba wenyeji wa Dar es Salaam ndio walioongoza mapambano ya kumng'oa mkoloni.
Aidha, alisema amani ambayo Tanzania inajivunia hii leo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na wenyeji wa Dar es Salaam ambapo wameweza kuwakaribisha; kuwapa maeneo na kuishi vizuri na watu kutoka sehemu nyingine.
Wakijibu mazungumzo ya Profesa Lipumba, Wazee hao walikiri kukabiliwa na hali ngumu ya maisha kiasi cha kuwafanya wakate tamaa.
Wazee hao walimtaka Prof. Lipumba ashirikiane nao kisiasa hivi sasa ili apate fursa baadaye ya kutafuta dawa ya tatizo la uchumi linaloikabili Tanzania hadi kuiweka katika nafasi ya pili kutoka mwisho kiuchumi duniani.
|
|