Maoni yetu
 
Kutufanya kondoo wa kafara ni kuiletea nchi maafa
 

MACHI 28, mwaka huu wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walishuhudia hali ya kutisha ambapo nguvu iliyokithiri ya vyombo vya dola ilimwagwa eneo la Kinondoni kana kwamba kulikuwa na msako wa wahaini. Tukio hilo pamoja na mazingira ambayo yamekuwa yakijengwa yanalenga kuhalalisha kukamatwa kwa Waislamu, kuteswa na hata pengine kuuliwa huku wahalifu wakiachwa.

Hili linalomkuta Ponda hivi sasa si tukio pekee bali latoa sura yenye kujirudia rudia inayothibitisha jambo moja: Kumejengeka uhuru wa polisi kila wanapojisikia kuwakamata Waislamu kuwaweka ndani na kuwaachia wakifurahi.

Sheikh Omar Bashir alizuliwa uhalifu akasakwa mitaani kama jambazi akatishwa hadi akavunjika mguu katika purukushani.

Sheikh Mbukuzi imekuwa ni zoezi la kujirudia kila polisi wakitaka kujijua uchapa kazi wao humchukua na kumweka ndani.

Mahabusu wenye maradhi wamekuwa wakinyimwa dawa hadi wengine hufia humo kama ilivyokuwa kwa Bw. Mohammed Omar na hakuna chochote kilichofanyika.

Akina mama wamenyanyaswa na kudhalilishwa, watoto wadogo wasio na hatia waliwekwa mahabusu na watu wazima na mwanafunzi Chuki akatiwa kilema huku akisingiziwa makosa ya kuhalalisha udhalimu aliofanyiwa.

Hayo yote yanatosha kuwapa polisi kibri na kufanya watakavyo. Kama nchi hii ingekuwa na uhuru, haki na usawa kwa wote, Ponda angetafutwa kwa kuenziwa sio kama mhalifu.

Katika kadhia ya Mwembechai wachochezi na wahalifu wote wanajulikana. Lwambano wa Kanisa Katoliki ndiye aliyezua uzushi wa kichochezi; uchochezi huo ukadakwa na redio moja ya binafsi ya kidini kabla Mh. Yusufu Makamba kuupokea kwa kishindo kilichoviacha vyombo vya dola vikihamanika hadi kuua wananchi wasio na hatia.

Ulimwengu wa sayansi na teknolojia ukanasa sura na sauti za walioua. Aidha, sura za baadhi ya waliouliwa kwa amari ya "piga yule" zimehifadhiwa katika mkanda wa video.

Kama lipo alilolifanya Ponda ni kushirikiana na Waislamu wenzake Februari 13, 1998 kusafisha damu, masalia ya mabomu na uchafu mwingine ulioachwa na polisi waliounajisi Msikiti. Pili aliongea na waandishi wa habari kuelezea ukweli wa kadhia ya Mwembechai kinyume na uzushi, uongo na Propaganda iliyokuwa ikisambazwa. Tatu kusaini Waraka ulioelezea tukio hili na madhila mengine dhidi ya Waislamu.

Inashangaza kusikia Mh. Rais akisema yeye binafsi asingependa kusikia baadhi ya raia wananyanyaswa na kuonewa, lakini wachochezi na wauaji wanaachwa ilihali wanajulikana, wanasakamwa na kusakwa wasio na hatia.

Almaruhum Sheikh Kassim Juma hakuwahi kuwa Mhadhiri wa Biblia wala sakata ya mabucha ilipotokea Dar es Salaam hakuwepo, lakini alizuliwa aliyozuliwa na kuwekwa ndani kwa miezi kadhaa. Mzee Chata Mungu amrehemu ameteswa mahabusu na kufa muda mfupi baada ya kutolewa huku mahakama ikisema hana shitaka la kujibu. Kosa lake Muislamu!

Uhuru huu ni wa kidhalimu, kwamba mtu anatungiwa shitaka ilimradi ipatikane sababu ya kukaa jela na kunyimwa dhamana hadi polisi wenyewe watakapofurahi!

Katika hali kama hii hofu ya Waislamu kama ilivyoelezwa katika barua yao kwa Mh. Rais ina msingi kwamba endapo serikali itaendelea na mtindo wake huu wa kuwanyanyasa na kuwadhalilisha Waislamu huenda ikaitumbukiza nchi hii katika mauaji ya kutisha.

Mzee Katambo hakuendesha muhadhara; kipi kilimuweka ndani! Mzee Chata hakuwa mhadhiri, kawekwa ndani takriban miezi 6 afya yake ikaathirika na akakosa matibabu. Katoka ndani mgonjwa wakati kaingia mzima. Hakuchukua muda akafa.

Hali iliyojengeka hivi sasa; raia tuna hakika kuwa hakuna yeyote kama vile vyombo vya kupigania haki za binadamu, wanasheria n.k. vitakavyosimama kututetea. Navyo vimejenga tabia ya kukaa kimya wanapodhulumiwa Waislamu.

Kwa mantiki hii hofu ya Kamati ni ya kweli, kuwa kumkamata Ponda kutaleta maafa kwa vile itawawajibikia Waislamu wenyewe kuchukua hatua za kiusalama za kujihami. Tusingependa hayo yatokee.

Tunajua ni vigumu kuwashawishi Waislamu kuwa haki ipo polisi; mahakamani (kesi ya Simbaulanga na Magezi) au kuna tegemeo lolote kutoka katika ofisi za wanasheria wakuu kuwa watajitokeza kuwatetea kama ilivyokuwa kwa mbwa "Immigration".

Kimbilio lao basi kwa Mheshimiwa Rais Mkapa lina mantiki na limesadifu. Na kwa vile Mheshimiwa Rais ndiye kiongozi pekee wa juu aliyewathibitishia wananchi kuwa hayupo tayari kuona baadhi ya raia wanadhulumiwa' hatuna sababu ya kudhania kuwa ataifumbia macho dhulma hii ya kutaka kuwafanya Waislamu wasio na hatia kuwa kondoo wa kafara.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook