Na Mwandishi Wetu
HIVI karibuni polisi walifika nyumbani kwa Sheikh Mbukuzi wakidai kuwa wanamtafuta Bw. Ponda.
Naye Bwana mmoja aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Bakwata Makao Makuu anasemekana amekuwa akiwapigia simu baadhi ya Waislamu akidai kwamba yeye anataka Bw. Ponda ajitokeze na kwamba atamhakikishia usalama wake.
Aidha, amedai atampeleka kwa Mh. Rais. Hata hivyo hafafanua kwa Rais anampeleka kufanya nini na vipi atamhakikishia usalama wake na akiwa kama nani.
Wakati huo huo, Waislamu wamekuwa wakihoji nafasi ya Kamati iliyowasilisha malalamiko ya Waislamu kwa Mh. Rais, Kamati hiyo ambayo sasa inadai kuwa "Halmashauri Kuu ya Waislamu" katika Baraza la Idd Machi 28, mwaka huu ilieleza hatua ambazo Mh. Rais ameanza kuzichukuwa kufuatia risala ya awali.
Waislamu wengi wameshangazwa ni vipi Kamati hiyo ielezee ya kule badala ya kueleza na kuyaweka wazi zaidi yale yanayowasibu Waislamu.
Bw. Jabir Ahmad aliyeongea na gazeti hili mara baada ya Baraza la Idd alikuwa na maoni kuwa ilikuwa kazi ya serikali yenyewe kueleza kila inachofanya na wala sio Kamati kuisemea serikali.
Naye mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Hafswa alisema kwamba inabidi hii Kamati inayodaiwa kuwakilisha madhehebu zote iwaeleze wazi Waislamu ipo kule serikalini au kwa Waislamu.
"Vipi ichukue nafasi ya kuisemea serikali badala ya kuwasemea Waislamu", alihoji mama Hafswa.
|
|