Uadui na chuki yenu ni mauti kwa Taifa letu
 

Na Maalim Mwalim

AMESEMA kweli Mwenyezi Mungu pale aliposema juu ya wanafiki kuwa "Na wanapoambiwa msifanye uharibifu katika ardhi. Husema sisi ni watengenezaji". Na akaendelea kusema :Hao ndiyo waliohiari upotofu kuliko uongofu, lakini biashara yao haikupata faida wala hawakuwa wenye kuongoka". (Qur'an 2:11,16).

Unafiki katika lugha ya kawaida ni sifa ambayo mtu au kikundi cha watu hujitwalia kutokana na tabia yake ya kutaka watu wamwone na kumjua vile ambavyo sivyo alivyo.

Mara nyingi tumeambiwa na viongozi wetu kuwa Tanzania ni yetu sote, Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa misingi ya haki na usawa kwa wote, Tanzania ni nchi inayothamini haki za binadamu, Tanzania ni nchi ambvayo haina dini, Tanzania ni nchi ambayo katiba yake ndiyo sheria mama n.k.

Jambo la kushangaza ni kule kuwaona wale wanaotukumbusha kila siku juu ya sifa hizi za Tanzania wakienda kinyume na maneno yao wenyewe pale wanapotakiwa kutekeleza jambo. Na hapo ndipo fat'wa ya kuwa wao ni wanafiki inapokuwa wazi na bayana kabisa. Wanakuwa ni wanafiki kwa vile kusema uongo, hawatimizi ahadi na kuchezea dhamana tuliyowapa hasa ile ya kulinda katiba ya nchi.

Hawa watu wa aina hii mimi nimechagua kuwaita 'Waserbia' wa Tanzania. Nawaita hivi kwa sababu wameshafanikiwa kupanda chuki miongoni mwa Watanzania, chuki ambayo inatishia kuisambaratisha nchi kama hatua zinazostahiki na za haraka hazitachuliwa.

Chuki yenyewe inapandikizwa ili iwatenge Watanzania katika misingi ya dini zao. Leo hii mtu mwenye elimu, madaraka, mali, hadhi n.k. anatarajiwa awe Mkristo. Na kinyume chake ni Muislamu. Kiasi kwamba hashangai mtu kuiona hali hii bali mtu atashangaa sana anapoona kinyume chake. Hali hii imeasisiwa, imelelewa, imekuwa na kukomaa.

Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya kuwepo kwa Watanzania wenye nia na mtazamo wa Waserbia wa Yugoslavia dhidi ya Watanzania wenzi wao.

Mosi, ni kwamba Tanzania imefika mahali kwamba watu wengine wamejichukulia madaraka yanayowawezesha kuwapa Watanzania wenzi wao wa dini nyingine tafsiri ya dini yao na namna ya kuifuata. Maneno ya kuchonga kama Mujahidina, msimamo mkali, siasa kali na mengine yameibuka kwa msingi huu wenye lengo la kuwagawa na kuwakandamiza Waislamu wa Tanzania.

Hali hii imetufikisha mahali kuwa mwalimu wa shule ya serikali anaingia hofu na kutumia nguvu nyingi sana kupinga mwanafunzi Muislamu Mtanzania kuvaa vazi la dini yake. Pia tunafika mahali maafisa wa Manispaa kubwa kama ya Dar es Salaam chini ya uongozi wa Tume ya Jiji wanajipa mamlaka ya kutoa aina ya hijab anayopaswa kuvaa binti Muislamu shuleni, hijab ambayo inapingana na zile zilizopo katika Qur'an 33:59 na 24:31 na pia katika Hadith sahihi za Mtume (s.a.w.).

Kwa mujibu wa barua ya Tume ya Jiji kwa Maafisa Elimu wa Kanda ya tarehe 24/3/1999 mabinti wanatakiwa wavae mashati maupe ya mikono mifupi! Je, uamuzi huu unaonyesha ujinga (kutojua) kwa watu wa Tume? Jibu ni hapana kwani walikuwa na nafasi ya kutosha kutaka ushauri kwa viongozi wa dini na hawakuona haja.

Kwanini basi wafanye hivi? Jibu lake ni ule Userbia niliosema mwanzo. Userbia huu humfanya mtu aone kuwa yeye anayo mamlaka ya kuamua ni sehemu gani ya Uislamu ifuatwe na sehemu gani isifuatwe. Wala hana wasiwasi kuwa anaweza akatokea Muislamu yeyote kumhoji. Na ikiwa atatokea basi ule mtandao wao utamtafutia moja ya yale majina niliyoyataja hapo juu na dola itashughulika naye.

Pili, hivi karibuni Rais alipata kutembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salam sehemu ya Mlimani. Katika ziara hii Rais alijionea mwenyewe Userbia uliopo Mlimani. Hali hii ilijitokeza pale mmoja wa wanafunzi alipouliza swali kuhusu matumizi ya nguvu ya polisi yaliyopelekea kuuliwa Waislamu Mwembechai tarehe 13/2/1998. Kilichojitokeza ni kuwa 'Waserbia' hao ndani ya ukumbi wa Nkrumah hawakuweza kusubiri muulizaji amalize swali lake bali walianza kuzomea hadi Rais alipoingilia kati na kuwatuliza 'Waserbia' hao. Baada ya swali Rais alijibu kuwa suala la Mwembechai lipo mahakamani. Japo siyo kweli kuwa wale polisi walioua Waislamu pale Mwembechai wameshakamatwa na kufunguliwa mashitaka na japo ni kweli kuwa wasomi wa Chuo Kikuu wanaufahamu ukweli huu, jibu la Rais lilishangiliwa sana!!

Kisha Rais akaombwa amfukuze kazi mara moja Katibu wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu kwa kile walichokiita kutowajibika kwa Katibu huyo. Waziri ambaye ni Mkristo katika Wizara hizo, kama ilivyokwishajengeka yeye hana tatizo. Kinachofanya yote haya kutokea ni Userbia uliopo miongoni mwa Watanzania.

Tatu, hali katika mashule ya sekondari na vyuo vingine hapa nchini ni hiyo hiyo. Ni aghalabu mwanachuo/mwanafunzi Muislamu kupigiwa kura ya kuwa kiongozi katika ngazi ya shule au chuo. Matangazo yote yanayohusiana na mambo ya Waislamu hayadumu katika mbao za matangazo vyuoni. Kila linapowekwa 'Waserbia' hulibandua. Haya mtu yeyote anaweza kuyathibitisha. Nenda Mlimani, nenda Chang'ombe T.T.C., nenda IFM n.k.

Hatuwezi kuitaja mifano yote. Hali ilivyo sasa hivi inachekesha. Mtandao wa 'Waserbia' hapa nchini kila siku unabuni mbinu mpya yakuwakandamiza na kuwadhibiti Waislamu. Iko mifano hai yakuchekesha. Miezi kumi na nne baada ya mauaji ya Mwembechai leo agenda kubwa ni kumsaka na kumkamata Ponda (dead or live)! Kwa hiyo lengo hapa ni kuwalinda wauaji; kufukia ukweli wa jambo na kumfanya Ponda ndio (issue) suala la kushughulikiwa.

Wakati wa kuwadanganya Waislamu umepita, Rais keshapewa malalamiko yetu. Suala la Mwembechai ni miongoni mwa yale aliyopewa Rais na kuahidi kulishughulikia. Suala la kumtafuta Ponda kwetu si nyeti. Wala halitushangazi huu ni mtazamo wa Kiserbia uliojijenga na kusitawi. Tunachoweza sisi Waislamu kukielewa ni kuwepo kwa Userbia ambayo hata siku moja polisi hawafikirii kuwakamata wauaji wa Mwembechai na kuwafikisha mahakamani. Wala hawafikirii kumkamata Padri Lwambano mzushi na mchochezi wa mauaji ya Mwembechai aliyeishinikiza serikali hadi ikapelekea kuua watu Mwembechai.

Ni kwa mtaji huu huu wale watu wanaghushi hati na kukabidhiwa nyumba za wakfu hulindwa na polisi na kuhatarisha usalama wao. Waislamu tujihadhari na Waserbia hawa. Leo tumekabidhi madai yetu kwa Rais lakini mtandao wa Kiserbia unazusha matatizo na kuyaeneza ili kututoa katika lengo. Mara tunasikia jamani tujihadhari na watu wanaovamia Misikiti, mara sisi Waislamu hatuna umoja. Haya siyo matatizo yetu bali yametengezwa ili kututoa katika lengo. Laiti yangekuwa matatizo yetu basi tungeyakabidhi kwa Rais.

Ni bora ieleweke kwamba Muislamu havamii Msikiti. Uvamizi unaozungumziwa usifichwe ukweli wake. Huu unatokana na sera za maadui wa Uislamu waliamua kuvamia taasisi zao kama Bakwata. Hawa ndiyo wanaovamia Misikiti ili kuweka chini ya Bakwata na hivyo chini ya maadui wa Uislamu.

Propaganda nyingine ya maadui wa Uislamu ni kueneza uongo wenye madhumuni ya kuwavunja moyo Waislamu katika mapambano yao dhidi ya maadui zao. Uongo huo ni hili dai kuwa Waislamu hawana umoja. Waislamu umoja tunao. Sote tunaswali swala tano. Sote tunaelekea Qibla. Sote tunafunga Ramadhani. Sote tunahiji wakati mmoja. Na sote hatupendwi na makafiri.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook