BARUA
 

Jibu kwa Bw. Salum Ali kuhusu Zanzibar ni nchi au mkoa?

Ndugu Mhariri

NIMEPENDA kukufahamisha kutokana na makala yako iliyoandikwa katika gazeti la ANNUUR tarehe 5-11, 1999 kichwa cha habari "Zanzibar ni nchi au mkoa" Kwa kweli kichwa chako cha habari kilikaa kiswali mno na wala si kimaelezo. Najibu lake linafahamika kuwa Zanzibar si nchi.

Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'an, Wakristo wanawaogopa Waislamu kuliko wanavyomuogopa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo Wakristo Tanzania Bara hawawezi kukubali kukaa na adui Muislamu karibu yake pale Zanzibar. Wakristo wafahamu hivyo. Kinyume chake, Waislamu walio wengi hawafahamu hivyo, na badala yake wanamuogopa Mkristo kuliko wanavyomuogopa Mwenyezi Mungu.

Jambo la kusikitisha kwa Zanzibar ni kwamba ina watu wachache sana wenye kuona mbali na wenye uwezo wa kujadili tukiwaondoa wale waliowahi kushika ngazi za juu za utawala. Watu wenye elimu zao wanashindwa kusema kwa khofu ya kuiogopa serikali yenyewe ya Zanzibar ikizidishiwa nguvu na serikali ya Muungano.

Imekuwa wengi wetu hatuna uwezo wa kufikiri haraka na kujadili ajenda mezani papo kwa hapo pindi wakiweka mada iliyotayarishwa kwa madhumuni yaliyofichwa. Tukaweza kuchambua yaliyofichwa na kuuona ubaya au uzuri wa mada hiyo.

Kutokana na ubovu huo ndio imepelekea kufutwa katika Katiba ya Muungano kipengele Rais akitoka Bara baada ya muda wa miaka 10 ya Urais ukiisha, awamu inayofuata Rais atoke Zanzibar. Kipengele hicho muhimu Wazanzibari wamekubali kifutwe. Na wakakubali ugombea mwenza usiokuwa na serikali. Madaraka ya serikali akapewa Waziri Mkuu.

Wakati huo huo mabadiliko ya katiba hiyo yakasema serikali ya Zanzibar itakuwa na kiongozi wa serikali ambaye ndiye atakuwa Rais. Huyo kiongozi wa serikali ya Zanzibar hana madaraka katika serikali ya Muungano.

Hivi sasa inakuja katiba ya serikali moja, hakuna serikali mbili wala serikali tatu. Kutakuwa hakuna baraza la Mapinduzi wala serikali ya Mapinduzi kutakuwa hakuna baraza la wawakilishi kutakuwa na Bunge moja tu, Waziri Mkuu mmoja, Rais mmoja, labda na Makamu wa Rais ambaye ni Mwenza asiyekuwa na serikali. Jibu lako wakati huo litakuwa limejibika kikamilifu.

Na hakuna Mzanzibari atakayeweza kufurukuta, kujadili wala kuhoji. Athari mbaya kabisa za Muungano kwangu mimi naziona ni nyingi kabisa, lakini hapa nitazitaja mbili tu, nazo ni:

Kufa kwa Uislamu Zanzibar, mfano mmoja uliopo vijana wengi wa Kiislamu watokao Zanzibar wengi wa waliobahatika kuingia katika vyuo vya elimu ya juu bara hawaujuwi siasa.

Zanzibar ilikuwa nchi kamili yenye uchumi wake na uwezo wa kujitegemea, leo Zanzibar haina serikali kabisa, na kama inalo jeshi basi halina silaha za kutosha kupambana na yeyote atokae nje ya mipaka yake. Na uchumi wake unategemea ruzuku na uhisani.

Wakati nchi za Ulaya Magharibi na Ulaya Mashariki zilizounganishwa kwa malengo maalumu ya kuudhibiti Uislamu zimesambaratika na miungano yao kuvunjika, nchi ambazo zilikuwa na maendeleo makubwa ya kila hali.

Eti nchi changa na masikini kama Tanganyika na Zanzibar ziungane na kufanya serikali moja na historia mbele ya macho yao. Je katika Muungano huo haki itatendeka? Au matarajio ni Kosovo na Yugoslavia nyingine katika Afrika?

Sheikh Aboud Jumbe alikuwa hana haja ya kuandika kitabu alichokiandika na kukiita : Miaka 30 ya Dhoruba", Wazazibari wengi hawakuweza kumuelewa na hawataweza. Wameinamiwa na jinamizi.

Ibrahim Kera,
S.L.P. 317,
Kigoma.



Tuwakumbuke Waislamu wenzetu wa vijijini

Ndugu Mhariri

HIVI sasa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kufanya uonevu na dhulma ya wazi kabisa dhidi ya Waislamu. Waislamu wanakamatwa ovyo, wanawekwa ndani, wanateswa sana mpaka wengine wanapoteza maisha yao kwa mateso wanayoyapata sambamba na hilo imefikia hatua ya kuwauwa Waislamu hadharani kama wanyama tena wasio na thamani yoyote.

Ni jambo la kila Muislamu anayejua kumfikishia ujumbe Muislamu mwenzie asiyejua juu ya dhulma hii ili nae aweze kuifahamu kisha jukumu ni lao kuamua nini cha kufanya kwa sababu Muislamu amekatazwa kudhulumu na kukubali kudhulumiwa. Hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa dhulma dhidi ya Waislamu inaondoka kwa gharama yoyote ile.

Jukumu la kuelimisha na kufikishiana ujumbe wa Uislamu ni la kila Muislamu. Tatizo lililopo, Waislamu wengi kama sio wote tumeng'ang'ania kuishi mjini na hivyo kuwaacha Waislamu wa vijijini mwetu na hali mbaya, hawana wanachokijua kuhusu Uislamu wao na uadui uliopo dhidi ya Waislamu pote ulimwenguni.

Napenda kuwakumbusha ndugu zangu Waislamu tusiwasahau Waislamu wenzetu waliopo vijijini au hata nje ya mji huu huu wa Dar es Salaam.

Tumeng'ang'ania mjini wakati Waislamu wenzetu wa nje tu ya mji huu wana hali mbaya.

Nilijaliwa siku moja kutembelea ndugu zangu Waislamu wa Mbagala Kongowe, hali niliyoikuta huko inatisha na kusikitisha sana, Waislamu walikuwa wanatolewa ngomani kuja kusikiliza ujumbe niliokuwa nataka kuwafikishia, ukweli ni kwamba maswali waliyoniuliza akinamama hao wa Kiislamu yalikuwa yanaonyesha wazi kuwa hakuna wanalojua lihusulo Uislamu na kwa wanayoyajua hawana elimu sahihi juu ya mambo hayo.

Walikuwa hawana habari yoyote kuhusu Mwembechai, waliona kuwa kama vile ninawahadithia hadithi zilizotokea zamani. Kama hapo Mbagala hali ndio hiyo inaonyesha wazi kuwa nje zaidi hali ni mbaya sana.

Hivyo Waislamu wakati ni huu wa kuona kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwafikishia ujumbe ndugu zetu hawa, kinyume chake hawa ndio watakaouza kura za Waislamu mwaka 2000 kwa thamani ndogo.

Na kama hilo likitokea Waislamu wote tunaojua tutakuwa masul mbele ya Allah (s.w.) juu ya suala hili.

Bi. Fatma bint Mussa,
Box 14041,
Dar es Salaam.



Pongezi Rais Mkapa

Ndugu Mhariri

NAOMBA nafasi katika gazeti lako hili tukufu nitoe yangu niliyonayo. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Rais Benjamin Mkapa kwa kukubali kuwa mgeni katika Baraza la Idd la mwezi 1 Mfungo Mosi 1419 lililofanyika Jijini Dar es Salam.

Nampongeza tena kwa yote aliyoyasema katika hafla hiyo. Lakini kubwa kuliko yote ni pale alipotamka kuwa serikali yangu haina nia baadhi ya watu wajiamini ni wanyonge wala wajione ni watu wa tabaka la pili.

Kwa kuwa Mheshimiwa Rais amesema hivi na Waislamu muda mrefu sana tulikuwa na mawazo hayo, sasa mimi ninataka tuone vitendo.

Maalim Haj. S. Ngalinga,
S.L.P. 66 Liwale.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook