MASHAIRI
 

Mungu mlaze peponi

Kilio kimetufika, watoto wa Khalfani,
Kaka yetu katutoka, katuachia huzuni,
Daima twakukumbuka, akurehemu Manani,
Marehemu kaka yetu, Mungu mlaze peponi.

Pemba alikozaliwa, sehemu za Kikunguni,
Kalelewa akakua, akapelekwa chuoni,
Elimu akapatiwa, ya kumjua Manani,
Marehemu kaka yetu, Mungu mlaze peponi.

Akasomea elimu, ya Kizungu darasani,
Hadi alipohitimu, masomo yake shuleni,
Akawaaga walimu, karudi zake nyumbani,
Marehemu kaka yetu, Mungu mlaze peponi.

Alioa marehemu, mtoto wa Selemani,
Jina lake Mariamu, na mtoto Khalfani,
Awarehemu Rahimu, akhera na duniani,
Marehemu kaka yetu, Mungu mlaze peponi.

Ilipofika ahadi, ya kuhama duniani,
Ikawa hakuna budi, kwenda kwa Rabi Manani,
Kamchukua Wadudi, yu mgonjwa kitandani,
Marehemu kaka yetu, Mungu mlaze peponi.

Amezikwa marehemu, kijijini Magodini,
Bado tuna kwake hamu, tuwe nae duniani,
Bali kwa wanaadamu, akhera ndo maskani,
Marehemu kaka yetu, Mungu mlaze peponi.

Tunakushukuru nyote, ndugu pia majirani,
Wa Unguja na wa Wete, mlofika msibani,
Na rafiki zake wote, mtalipwa na Manani,
Marehemu kaka yetu, Mungu mlaze peponi.

Zuena Khalfan Salim,
P.O. Box 5478,
Usagara,
Tanga.



Mwenye shamba (jibu)

Zuberi jibu pokea, kwa swali uliuliza,
Nakujulisha sawia, sipendi kukutatiza,
Majibu yako sikia, wazi wazi nakweleza,
Shamba hilo lamhusu, yule alolima kwanza.

Na huyu mtu wa pili, inafaa tumcheke,
Kafanya kazi thakili, na shamba wala silake,
Katwaa ya watu mali, akayafanya ni yake,
Shamba hilo lamhusu, yule alolima kwanza.

Wa tatu akili hana, kafanana na wa pili,
Akapalilia sana, akatoka jasho mwili,
Mazoeya yakafana, shamba kwake si halali
Shamba hilo lamhusu, yule alolima kwanza.

Mwenye haki ni wa kwanza, kama nilivyobaini,
Ndie yeye aloanza, kulima hapo shambani,
Kufungwa kwake si manza, kwa kuwekwa gerezani,
Shamba hilo lamhusu, yule alolima kwanza.

Wawili ni wavamizi, kupora haki ya watu,
Wanastahili wizi, adhabu imethubutu,
Ni ya bure yao kazi, malipo hawana katu,
Shamba hilo lamhusu, yule alolima kwanza.

Nimefika kwenye safu, tamati kwa kuandika,
Ndugu usiwe na khofu, moyoni kuhuzunika,
Soma kwa ukamilifu, nadhani utatosheka,
Shamba hilo lamhusu, yule alolima kwanza.

Suleiman Khamis
P.O. Box 571,
Arusha,
Tanzania.



Kitakuziba mdomo (tahadhari)

Si kila kilo kinono, kipanuliwe mdomo,
Vyengine vina ndoano, vitakuziba mdomo,
Tena jihadharini mno, wazi kuweka mdomo,
Chakula chenye ndoano, kitakuziba mdomo.

Ya kwangu haya maono, nimepima kwa kipimo,
Dhalimu mbaya mno, achimba yake mashimo,
Akukite kisigizo, ukatumbukie humo,
Chakula chenye ndoano, kitakuziba mdomo.

Hatoi bure vinono, zingatia hili somo,
Hataki mshikamano, kuwepo na msimamo,
Akutega kwa ndoano, upigepige midomo,
Chakula chenye ndoano, kitakuziba mdomo.

Ndugu usiwe mfano, baada ya hili somo,
Usirukie vinono, ukaja kwenda mchomo,
Nimetafakari mno, nasema kwa mtizamo,
Chakula chenye ndoano, kitakuziba mdomo.

Hasa kwenye mapambano, yahitaji msimamo,
Mibaya mifarakano, jengo yabomoa bomo,
Mafunzo ya sala tano, yajenge wetu mfumo,
Chakula chenye ndoano, kitakuziba mdomo.

Nyuma rudisha mikono, wako zuia mdomo,
Yakate mahusiano, sijali zake ngurumo,
Akitaka michuano, mtupie misukumo,
Chakula chenye ndoano, kitakuziba mdomo.

Nakoma kuwamba wino, nimekwisha toa somo,
Nakoma yangu maneno, yapimwe kimtazamo,
Nakoma onyo vinono, uchunge wako mdomo,
Chakula chenye ndoano, kitakuziba mdomo.

IDD S. Kikong’ona,
Morogoro.



Serikali hii vipi?

Bismillahi naanza, kwa jina la Mola wetu,
Ambaye dniye wa kwanza, hilo halipingwi katu,
Elimu ametufunza, hakuacha hata kitu,
Serikali hii vipi, mbona haitendi haki.

Matukio mbalimbali, yenyewe yasababisha,
Kisha inaruka mbali, ukweli kuupotosha,
Inajifanya ukali, kwa kauli za kutisha,
Serikali hii vipi, mbona haitendi haki.

Mfano Mwembechai, vurugu ilianzisha,
Harafu ikajidai, uongo kuvumisha,
Ilijifanya ni chui, mabomu kuyatupisha,
Serikali hii vipi, mbona haitendi haki.

Iliuwa Islamu, kwa makusudi hakika,
Kwa risasi na mabomu, roho za watu kutoka,
Harafu inashutumu, eti haikuhusika,
Serikali hii vipi, mbona haitendi haki.

Nguruwe sasa halali, hilo wamelitamka,
Kufugwa kila mahali, mtu anapopataka,
Bila hata ya kujali, mipaka waliyoweka,
Serikali hii vipi, mbona haitendi haki.

“Kiti Moto” mabuchani, hilo halivumiliki,
kuuzwa hadi sokoni, Isilamu hatutaki,
Mtasema ni udini, hilo hatuliafiki,
Serikali hii vipi, mbona haitendi haki.

Sasa ni mtasema, kuhusu hizi hijabu,
Ni mavazi ya heshima, katuamuru Wahabu,
Kwa mwanamke lazima, kulivaa si ajabu,
Serikali hii vipi, mbona haitendi haki.

Hapa mwisho ninakoma, mbele sitaendelea,
Islamu hima hima, serikali twaijua,
Tusiregee daima, itakuja kutuua,
Serikali hii vipi, mbona haitendi haki.

Hamisi M. Rugengo,
Ubungo Islamic High School,
S.L.P. 55105,
Dar es Salaam.



Iwache yako dhihaki (machale)

Natafakari bunduki, kulengwa kwa kijana Chuki,
Moyoni sifurahiki, upumbavu siutaki,
Sipendipendi muziki, vichupi na ushabiki,
Iwache yako dhihaki, sipumbazwi kwa muziki.

Tena nasema sitaki, mipango ya kishabiki,
Jazba zenye mikiki, za kimuziki muziki,
Upambe na chukichuki, usinifanye rafiki,
Iwache yako dhihaki, sipumbazwi kwa muziki.

Nyimbo nyimbo sishiriki, kwangu hazistahiki,
Kwa upambe sipambiki, nawapasha halaiki,
Usije kujenga chuki, vipi kwangu hupendeki,
Iwache yako dhihaki, sipumbazwi kwa muziki.

Bora nikamate chaki, au nicheze na biki,
Niwaseme wenye chuki, walotupiga bunduki,
Upotee ufisasikia, dhuluma haki ibaki,
Iwache yako dhihaki, sipumbazwi kwa muziki.

Nataka niwashitaki, walouwa bila haki,
Mpaka itendeke haki, walouwa wahaliki,
Jahadi haizimiki, kwa vishindo vya bunduki,
Iwache yako dhihaki, sipumbazwi kwa muziki.

Siupendi unafiki, na kufanywa mamluki,
Ikiwa huambiliki, utakong’otwa kwa biki,
Usije ukahamaki, gazeti kulishitaki,
Iwache yako dhihaki, sipumbazwi kwa muziki.

Tambua sibadiliki, kwa vinyimbo na miziki,
Naitaka yangu haki, nipate kuimiliki,
Mikononi idiriki, si huku kunidhihaki,
Iwache yako dhihaki, sipumbazwi kwa muziki.

Ulingo nautariki, nyimbo miziki sitaki,
Ulingo nataka haki, agendani sibanduki,
Ulingo naweka biki, mekasirika sicheki,
Iwache yako dhihaki, sipumbazwi kwa muziki.

Idd S. Kikong’ona,
Morogoro.



Dua Bungeni (swali)

Naona ni adhuhuri, mchana wa jua kali,
Imekuwa ni vizuri, kuwaulizeni swali,
Sitakuwa na kiburi, jibu nitalikubali,
Linalosomwa Bungeni, ni dua la dini ipi?

Husomwa kwa lugha nzuri, na unyenyekevu kweli,
Wabunge hukaa turi, wakiwa wanakubali,
Kikao huwa kizuri, likisha somwa awali,
Linalosomwa Bungeni, ni dua la dini ipi?

Nchi hii ipo huri, dini si za serikali,
Ajabu inashamiri, dua kusomwa halali,
Au ni masihari, wapagani wanasali,
Linalosomwa Bungeni, ni dua la dini ipi?

Msekwa ni mlozari, hilo mimi silijali,
Vipi hii Jamhuri, ndio muje kujadili,
Nataka mutafakari, Bungeni wanakosali,
Linalosomwa Bungeni, ni dua la dini ipi?

Dodoma mnishauri, pamoja nanyi wa mbali,
Nataka watu mahiri, wamchao Mungu kweli,
Majibu kwa Mhariri, wa AN-NUUR jabali,
Linalosomwa Bungeni, ni dua la dini ipi?

Kwangu mimi si vizuri, kuombewa na jahili,
Mungu kwake ni sifuri, hamfahamu wa kweli,
Vipi iwe desituri, Wabunge mnakubali,
Linalosomwa Bungeni, ni dua la dini ipi?

Huwa halisomwi siri, Redioni kunakili,
Kipindi kikiwasiri, utafikiri maswali,
Leo katika Bungeni, Wabunge wanajadili,
Linalosomwa Bungeni, ni dua la dini ipi?

Hapa mwisho wa shairi, njoo Dettu Muinjili,
Nijibuni si zohari, wote wake na rijali,
Nitakuwa na fahari, jibu likiwa kamili,
Linalosomwa Bungeni, ni dua la dini ipi?

Zuberi Mohammed Mwinyi (Amir),
S.L.P. 61428,
Dar es Salaam.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook