Na. Hassan Omar
TEKNOLOJIA inayohusiana na kompyuta inabadilika kila sekunde! Kama si mtu unayeifuatilia teknolojia hiyo kwa karibu sana, ujuzi uliokuwa nao mwezi uliopita tu basi si hasa ukawa umepitwa na wakati vibaya sana leo hii. Na hali inakuwa ngumu zaidi kwa watumiaji wa kawaida wa kompyuta wanapotaka kununua kompyuta mpya.
Mambo yanayohusiana na kompyuta ni mengi sana, na mengi kati ya hayo ni magumu kuyaelewa. Madhumuni ya makala hii ni kujaribu kumsaidia kidogo mtu anayetaka kununua kompyuta sasa hivi ili aweze kuelewa maana ya maneno mbalimbali yanayotumiwa na wauzaji wa kompyuta na hivyo kuweza kununua kompyuta yenye sifa nzuri na kwa bei nzuri.
Kompyuta ya aina ya PC (personal computer) si kitu kimoja bali ni mkusanyiko wa vifaa kadhaa vyenye kufanya kazi mbalimbali ambavyo kwa pamoja vinaifanya kompyuta ifanye kazi inayotarajiwa kufanya. Kompyuta yenye sifa ya kuitwa "multimedia computer", yaani yenye uwezo, pamoja na mambo mengine, wa kuonyesha picha na kutoa sauti, ina viungo muhimu vifuatavyo ambavyo vyote nimeviandika hapa chini kwa Kiingereza, lugha inayotumiwa zaidi na wauzaji wa kompyuta.
Ukiona jina IBM, au Compac, au DELL, n.k. usidhani kuwa kila kifaa kilicho ndani ya kompyuta hizo kimetengenezwa na kampuni hizo - si kweli kabisa! Watu wengi kikawaida wanapenda tu kununua PC za "brand name" yaani zilizotengenezwa na kampuni maarufu, lakini haina maana kuwa PC hizo zitakuwa tofauti sana kiubora kupita, kwa mfano, PC niliyoitengeneza mimi mwenyewe kwa kutumia vifaa vile vile vilivyotumiwa na kampuni hizo maarufu. Tofauti muhimu ni kuwa kampuni hizo hufuata taratibu nzuri sana za kudhibiti ubora (quality control) wa PC wanazozitengeneza kwa kuzifanyia majaribio (tests) mbalimbali.
Kwa hivyo, kitu muhimu kabisa cha kukielewa ni sifa za vifaa mbalimbali vinavyojenga PC, ili uweze kutofautisha ubora wa PC zinazouzwa na kampuni mbalimbali. Unahitaji pia kujua tofauti ya sifa hizo ili uweze kuchagua aina ya PC itakayokidhi mahitaji yako ya sasa na ya miaka kadhaa ijayo. Kama unahitaji PC ya kukusaidia kuandika barua tu, huna lazima ya kununua PC yenye uwezo mkubwa sana wa kutosheleza kurushia roketi! Kompyuta yenye sifa za msingi, kama tutakavyozieleza hapa chini, inaweza kutosheleza mahitaji yako hayo.
Sasa tuanze kuvichambua viungo
tulivyovitaja hapo juu, kimoja baada ya chengine ilI tuweze kuvielewa zaidi.
Lakini kwa kuanzia, ili kurahisisha maelezo yangu, hapa chini nimeorodhesha
sifa za kompyuta ninayoitaka kuinunua sasa hivi, ambayo ni kati ya kati,
na yenye uwezo wa kutosha kutimiza mahitaji yangu:
Na sasa tuanze uchambuzi wetu tutakaojaribu kuelezea maana ya maneno mbalimbali yaliyotajwa hapo juu.
CPU:
CPU (Central Processing Unit), au wengine wanaiita kwa ufupi "processor', ndio akili (brain) ya kompyuta. CPU ndio kiungo cha msingi na muhimu kabisa kiasi kwamba kompyuta hupewa jina kwa mujibu wa aina ya CPU iliyonayo. Ndio maana unawasikia watu wanasema, "Ah, kompyuta yangu ni Pentium", n.k.
CPU zimeanzia mbali sana lakini katika zama za leo cha muhimu kukijua ni kuwa kuna kampuni nne maarufu zinazotengeneza CPU za kutumika kwenye PC zinazotumia programu-mama (operating system) maarufu ya Windows. Kampuni hizo ni Intel, Advanced Micro Devices (AMD), Cyrix Corporation na IBM.
Bila shaka Intel ndiyo inayoongoza kwa umaarufu na hata kwa umadhubuti wa CPU wanazozitengeneza. Lakini, hawakukosea Waswahili waliposema, "Avumaye baharini ni papa, kumbe wengine wapo!" AMD katika miaka ya karibuni wameweza kutengeneza CPU zinazofikia kiwango cha ubora wa CPU za Intel na uzuri wa mambo, CPU zao zinapatikana kwa bei nafuu zaidi ukilinganisha na CPU za Intel. Cyrix yenyewe inajikokotakokota, na CPU zao za bei nafuu zaidi ya AMD. IBM wao ni maarufu zaidi kwa CPU zinazotumika kwenye kompyuta za mikononi za aina ya laptop.
Jingine la kulijua ni kuwa sasa hivi watu wanazungumzia zaidi CPU za Intel za ukoo wa Pentium II na za AMD za ukoo wa K6-2-3D. CPU za Intel za ukoo wa Pentium, Pentium Pro, na zinazoafikiana nazo kutoka kwa watengenezaji wengine, bado zinaendelea kuuzwa lakini kwa uchache sana na kwa bei ndogo sana. Kama unataka kununua kompyuta hivi sasa, haipendekezwi kununua kompyuta yenye CPU hizo zinazozidi kupitwa na wakati kila uchao. Hii ni kwa sababu, baada ya muda si mrefu CPU za aina hizo hazitakuwa zikiuzwa kabisa na kama kompyuta yako itaharibika na kuhitaji kubadilishiwa CPU (jambo ambalo, hata hivyo, ni nadra kutokezea), itakuwa kazi ngumu sana kupata CPU hizo kiasi cha kuhitajia kompyuta nyingine mpya!
Hivi nikiandika makala hii tayari CPU za ukoo wa Intel Pentium II Xeon, na Intel Pentium III, zimeshaanza kuuzwa lakini kwa ushauri wangu, ni vyema kungojea kwanza (kama huna mahitaji ya haraka) mpaka bei ya CPU hizo ianze kushuka kwani hivi sasa zinauzwa kwa bei mbaya sana.
Jina la ukoo wa CPU linaashiria ubora fulani. Pamoja na jina la ukoo, kuna na kasi ya saa ya ndani ya CPU (internal clock speed) ambayo hupimwa kwa megahertz (MZh). CPU za miaka ya karibuni kuanzia na zile za ukoo wa Pentium zinatumia clock speed ya kuanzia 100 MHz hadi kufikia 500 MHz. Kila clock speed ikiwa kuwa ndivyo CPU inavyokuwa na kasi kubwa zaidi ya kufanya mambo. Ukiona Pentium II 350 (mara nyingine huwa hawaweki MHz), ujue kuwa CPU hiyo inatumia clock speed ya 350 MHz.
Mara nyingine utaona CPU imeandikwa kwa mfano, AMD K6-2-3D-333MMX, ikionyesha kuwa K6-2-3D ni jina la ukoo wa CPU hiyo iliyotengenezwa na kampuni ya AMD, na neno MMX ni ufupisho wa Multi Media eXtensions. CPU zinazotumia teknolojia ya MMX zimefanywa ndani yake kuwa na namna maalum ya kuzifanyia kazi kwa ufanisi mkubwa data zinazotokana na sauti ya picha. Lakini takriban CPU zote za miaka ya karibuni zinatumia teknolojia hiyo hata kama kwenye tangazo neno MMX halikuandikwa.
Hapa chini ni majina ya koo mbalimbali za CPU, zinazoendelea kutumika hivi sasa, zilizotengenezwa na Intel na zile zilizotengenezwa na AMD. Majina hayo yamepewa kwa ubora kwa kila kampuni, kwa kuanzia na CPU yenye uwezo wa wastani na kumalizikia na CPU yenye uwezo mkubwa sana:
AMD K6-3D-300MMX
AMD K6-3D2-333MMX
AMD K6-3D2-350MMX
AMD K6-3D2-366MMX
AMD K6-3D2-380MMX
AMD K6-3D2-400MMX
Intel Pentium 200 MMX
Intel Celeron 266
Intel Celeron 300
Intel Celeron 300A
Intel Pentium 233 MMX
Intel Celeron 333
Intel Celeron 366
Intel Celeron 400
Intel Pentium II 300
Intel Pentium II 333
Intel Pentium II 350
Intel Pentium II 400
Intel Pentium II 450
Intel Pentium III 450
Intel Pentium III 500
Intel Pentium II Xeon 400
Intel Pentium II Xeon 450
CPU za AMD K6-2-3D zinasemekana kuwa na sifa sawa na CPU za ukoo wa Intel Pentium II zenye clock speed sawa lakini zenyewe zinauzwa kwa bei nafuu sana. Hiyo ndiyo iliyokuwa sababu ya kampuni zinazotengeneza kompyuta kama vile Compac kuamua kutengeneza kompyuta kwa kutumia CPU hizo za AMD badala ya CPU za Intel kwenye baadhi ya kompyuta zao.
CPU za Intel Celeron, ni za asili moja na CPU za Intel Pentium II lakini Celeron 266, na 300 hazina kitu kinachoitwa Level 2 (L2) Cache, na Celeron 300A, 333, 366, na 400 zimewekwa L2 Cache ya 128KB tu ambayo tofauti na L2 Cache ya ukubwa wa 512KB iliyo kwenye CPU za Intel Pentium II za kawaida. L2 Cache ni hifadhi yenye kasi kubwa kushinda RAM ya kawaida ambayo husaidia sana kuifanya kompyuta ifanye kazi kwa kasi kubwa zaidi. CPU za Intel Pentium II Xeon zinakuja na L2 Cache kubwa zaidi ya kuanzia 1MB hadi 2MB na kompyuta zenye CPU za aina hiyo hutumika zaidi kwenye server kubwa kubwa. CPU za Celeron baadhi yao zina hitilafu ndogo ndogo (manufacturing defects) na ndio maana zikawa zinauzwa kwa bei nafuu zaidi.
CPU za kasi kubwa hutoa joto jingi sana linalozidi hata 100 degrees Celsius juu yake! Ili kurefusha uhai wa CPU hizo pamoja na vifaa vingine vilivyomo kwenye kompyuta, ni muhimu sana kuwa na feni nzuri juu yake pamoja na heatsink ya kupozesha joto hilo. Hii ni muhimu zaidi kwenye nchi yenye hali ya hewa ya joto.
Itaendelea toleo lijalo
|
|