TAHARIRI
 
Ulaaniwe unyanyasaji wa raia
 
WIKI iliyopita Kamati ya Kupigania Haki za Waislamu ilisambaza kwenye vyombo vya habari nakala ya barua iliyotumwa kwa Mh. Rais. Maudhui ya barua hiyo ilikuwa ni kuikumbusha serikali itumie sheria za nchi kuwachukulia hatua wahusika wa mauaji ya Mwembechai badala ya kuwasaka watu wasio na hatia.

Karibu vyombo vyote vilipiga kimya isipokuwa Majira. Ofisi za gazeti hilo zimevamiwa na mmoja wa waandishi wake kuchukuliwa kwa nguvu na polisi. Hiyo ilikuwa Jumapili Aprili 4, mwaka huu.

Kufuatia tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa Bw. Alfred Gewe amekataa kutoa taarifa yoyote japo maelezo yake yanakiri tukio hilo kufanyika, hali inayopelekea kuibuka kwa hisia na maswali mengi.

Kama gazeti la Majira linatiwa msukosuko kwa vile linaripoti taarifa za malalamiko ya Waislamu kwa Mh. Rais; Je; kuna sera inayopiga marufuku kuandika habari zinazohusu masuala ya Waislamu?

Hoja kuu ya Kamati ni kuwa: Kama serikali inawataka waliohusika na vurugu na mauaji ya Mwembechai, watu hao wanajulikana na kuhoji mbona hawachukuliwi hatua!

Aidha Kamati inatoa nasaha kwamba tabia hii ya kuvuruga sheria za nchi kuwalinda wauaji na kuwasakama raia wasio na hatia ndiko kunakoweza kusababisha mauaji.

Profesa I.G. Shivji katika kongamano la kujadili mauaji ya Mwembechai alisema alipoona televisheni ikionyesha mauaji yale alidhani ni Afrika ya Kusini ya Makaburu. Akaonya kuwa vitendo hivyo visipokemewa kwa nguvu zote basi si muda mrefu itakuwa ni kawaida ya polisi kuwanyanyasa raia.

Pengine tujiulize ni matukio mangapi ya kuwanyanyasa na kuwaonea raia yamefanywa na polisi kinyume cha sheria baada ya tukio la Mwembechai.

Tungependa kuungana na wale wote waliolaani kitendo cha polisi kuvamia ofisi za gazeti la Majira na kumkamata mwandishi wa gazeti hilo.

Lakini tunalaani pia vitendo vyote vya kuwanyanyasa wananchi kwa sababu yoyote ile iwayo.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook