MAKALA MAALUM
 
Sehemu ya hotuba ya Prof. Lipumba kwa vijana wa Dar katika ukumbi wa Starlight Tarehe 4/4/1999
 

WANANCHI hawawezi kukichagua chama wanachokiona hakipo miongoni mwao. CCM imekuwa inashinda katika chaguzi za marudio. Wachunguzi wa siasa lazima wanastuka vipi, itakuwaje watu wana njaa, watu wanadhiki, watu wamepoteza matumaini. Wanachi hao hao wachague chama tawala ambacho ndicho chanzo cha matatizo yao, cha dhiki yao. Si kwamba wananchi wanakipenda chama tawala. Watakipendaje chama tawala hali hawana amani katika matumbo yao. Mtu mwenye njaa hana amani na utulivu. Kila wakati unatazama Yaarabil'amina chakula cha mchana na watoto wangu nitakipata wapi, utakuwaje na amani na utulivu.

Lakini kwanini chaguzi za marudio CCM inatangaza kwamba imeshinda. Kwa sababu vyama vyetu vya upinzani, vyetu vingine vya kisiasa havifanyi kazi ya kisiasa miongoni mwa uma (Makofi). Na ikiwa hatutafanya kazi hiyo ya kisiasa basi hatuwezi tukachukua nafasi ya kuweza kuiongoza nchi.

Pamoja na matatizo yote yaliyomo ya Kikatiba, pamoja na kwamba Dola inasaidia sana chama tawala lakini vyama vyetu na hasa chama chetu, ukikutana na wananchi wanaeleza kwamba chama chetu kinakubalika sana. Mimi napata mialiko kila wakati naambiwa hivi Tanga, Tabora, Mwanza, Moshi mialiko mingi inakuja pale ofisini. Wananchi wengi wana hamu kubwa na chama chetu lakini uongozi hauwaendei wananchi hao (makofi). Kwa hiyo lazima kujisahihisha ndani ya chama, na wakati wa kujisahihisha ni huu wakati wa chaguzi za viongozi wa chama ndani ya chama. Kwa hiyo hilo ilikuwa jambo langu la kwanza la kusisitiza.

Lazima wananchi wajiulize kama chama hakiwezi kusimamia mambo yake ndani ya chama kitawezaje kusimamia mambo ya taifa. Sio kwamba CCM inaweza kusimamia mambo ya taifa, CCM ni chombo cha Dola, CCM wakipoteza Dola wanasambaratika. Hawana chama (makofi). Hivi sasa CCM hawana chama, haya matatizo tuliyonayo yalikuwa madogo sana, hata matatizo yaliyopo NCCR yataonekana madogo sana kama CCM wakiwa nje ya serikali (makofi). Wao ndio watashikana makoo kwelikweli yanazibwazibwa kidogo tu kwa sababu wana serikali. Na hata nani awe mgombea na nani alistahili kuwa mgombea wa mwaka 95, vijana wa CCM bado wanajiuliza hili swali bado halijapatiwa jibu. Nani aliyestahili kuwa mgombea wa CCM mwaka 95. Kwa hiyo wenzetu wana matatizo ni chama tawala, chama cha Dola....

Sasa sisi tuna bahati hatuna Dola, tuna nafasi nzuri zaidi ya kujenga chama ambacho kitaridhisha nyoyo za wananchi (makofi). Na chama kitaridhisha nyoyo za wananchi kwa sababu ni chama kinashughulikia mambo ya wananchi, kinaendeshwa kwa njia ya kujitolea. Sio kwa kasma, sio kwa ruzuku, wananchi wenyewe wana kipenda chama wanakiendesha kwa njia ya kujitolea. Wazee wetu walipokuwa wakigombea uhuru katika chama cha TANU na hasa katika huu ukanda wa Pwani, wanakumbukumbu nzuri kwa ile michango ya thumuni thumuni kila mmoja senti hamsini hamsini ndizo zilizoendesha chama. Chama kilikuwa cha wananchi wenyewe, wakati ule wafanyakazi wa serikalini walikuwa hawaruhusiwi kuingia katika chama, na ukweli wakati ule waliokuwa wakifanya kazi serikalini maslahi yao yalikuwa kwa mkoloni.

Ni Waswahili ndio waliokuwa nguzo ya chama katika kugombea uhuru wa nchi hii, basi na sisi ni hao hao mababa Kabwela wa sasa, ni hao hao vijana wa sasa ambao wametupwa na serikali ya CCM, ndio watakuwa uti wa mgongo wa chama chetu (makofi).

Lakini hatuwezi kuwapata vijana ikiwa kama taratibu zetu za ndani ya chama ziko shaghabaghala, hazina muelekeo, huna uhakika wa mipango ... vijana wa Dar es Salaam ni jukumu lenu, Dar es Salaam ndio Makao Makuu ndio kitovu cha siasa (makofi). Ni lazima tuwe na chama imara hapa Dar es Salaam.

Baada ya kuzungumza kidogo hayo mambo ya chama, nilikuwa naomba kidogo nizungumzie hali zetu, hali ya kisiasa na hali ya kiuchumi.

Nchi yetu demokrasia yake bado ni changa sana, tuna nafuu kidogo Tanzania Bara, Zanzibar demokrasia haipo. Wenzetu Zanzibar walioko madarakani wana nia ya kuua upinzani. Viongozi wetu, wanachama 17 ama 18 wamo ndani kwa kesi ya jinai ambayo inachukua muda mrefu kusikilizwa. Mgombea mwenza ambaye katika uchaguzi wa 1995 tulikuwa naye, Mh. Juma Duni Haji, mzalendo Mzanzibari mwenye uchungu na nchi yake. Viongozi wa CCM Zanzibar wanawafahamu watu hawa, wana uhakika kabisa katika nafsi zao kama wakitaka kusema kweli. Hawa sio watu wahaini, ni watu wanaosimamia haki, wanaohitaji siasa za wazi wazi. Juma Duni Haji hafichi mtu, anakueleza analolifikiria, Mimi nilikuwa na bahati toka tukiwa Chuo Kikuu.

Ni watu wanatiwa ndani kisiasa kwa nia na lengo la kutaka kuua, kuvunja chama cha CUF. Sisi huku Bara wakati mwingine hatuoni hili kama ni tatizo la Tanzania yote kwa sababu hatuna tatizo hili hatufuatwi fuatwi kwa kiasi ambacho chama chetu cha CUF kinavyodhalilishwa na kukandamizwa, na wanachama wetu wa CUF wanavyodhalilishwa na kukandamizwa Zanzibar.

Kwa hiyo tunaweza tukajisahau tukasema kwamba hilo ni tatizo la Zanzibar lakini kama na sisi bara tungeibana CCM kama CUF ilivyoibana CCM Zanzibar basi matatizo yaliyoko huko Zanzibar huenda yangetokea huku bara (makofi). Kwa hiyo tusilione hilo ni tatizo la Zanzibar tu ni tatizo la kukosa demokrasia katika taifa letu kwa ujumla.

Na ikiwa tunahitaji kujenga taifa lenye haki sawa kwa wote basi jambo la msingi, jambo la kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba tuna demokrasia katika nchi yetu. Na demokrasia haipewi watu kama tende kwenye kisahani. Huipati demokrasia kwa kugawiwa na watawala. Watawala kwa kawaida yao wanapenda ukiritimba wa madaraka. Demokrasia inapiganiwa, lazima watu wawe tayari kujitoa muhanga,ndio kizazi cha kesho kitakuwa na demokrasia ya kimsingi (makofi). Ni lazima tuelewe tukiwa katika vyama ambavyo hivi sasa vinaitwa vya upinzani mbinu mbalimbali zinatumika kutudhalilisha, utafunguliwa mashitaka ya kila namna ili udhalilishwe, nia usishiriki katika mapambano ya kuleta demokrasia katika nchi yetu.

Hivi sasa serikali katika kuwabana wananchi, kuibana demokrasia ina waraka namba moja wa mapendekezo ya Katiba badala ya kuanzia tume ya Nyalali ilipoishia ya kuweza kuunda tume huru au kamati huru ambayo itashirikisha wananchi wote kwa ujumla ikiwa ni pamoja na vyama vingine vya kisiasa. Serikali inategemea kutumia wingi wa wabunge katika bunge kupitisha mambo ambayo hanaya ridhaa ya wananchi.

Hivi sasa tuna miaka 35-36 ya muungano, badala ya kutazama kimsingi matatizo yetu ya muungano na namna yakuyatatua kuna mawazo na haya mawazo si ya wanachama wa CUF tu, kuna wanchama wa CCM, kuna wanachama wa vyama vingi vya siasa, kwamba muundo wa muungano ulivyo hivi sasa si muundo muafaka, si muundo mzuri. Itakuwa vizuri tuwe na serikali tatu, kuna wazo, inaweza ukalikubali unaweza ukalikataa. Kuna wana CCM nadhani ilikuwa inatiwa G55 ambao pia na wao hata wengine wamo katika Baraza la Mawaziri walitoa wasiwasi wao na muundo wa muungano.

Sasa serikali imesema toeni maendekezo lakini serikali hiyo hiyo inasema kamwe hapatakuwa na serikali tatu, sasa kweli wewe una nia nzuri ya kuwaomba wananchi watoe mapendekezo yao ikiwa msimamo tayari umeshatoa, umeshatoa msimamo wa kwamba hapatakuwa na serikali tatu, sasa watu watoe mapendekezo ya nini? Ikiwa msimamo tayari unao, unasema tuletee vyama, Watanzania wana uhuru wa kuunda vyama vyao. Wananchi wanaunda vyama, wanafanya shughuli za kisiasa unawatukana, unawaambia hivi vyama vingine ni vyama haramu au wanaharamu ndio wamo katika vyama hivi. Je, wewe unahitaji demokrasia katika nchi yetu? Kwa hiyo tuna tatizo la ujenzi wa demokrasia ya msingi katika taifa letu. Hivi sasa hatuna, na tutaijenga demokrasia ya msingi ikiwa tutaimarisha chama chetu na tukashiriki katika chaguzi zote. Hata ikiwa wenzetu wanatuwekea mbinu kutuibia kura tusikubali kutoshiriki katika shughuli za kisiasa.

Lazima tushughulike nao tuhakikishe kwamba panawekwa taratibu ambazo zitaweza kuleta ushindi kwa vyama vinavyopendwa na wananchi (makofi). Vijana tunakazi kubwa, wenzetu nadhani mimi si mtaalamu wa mambo ya dini lakini nadhani katika dini mbalimbali kukata tamaa kunatazamwa kama ni dhambi.

Mtu hata ukiwa na matatizo siku hizi waandishi wa Kasheshe sijui wako hapa huwa wanalitangaza gazeti lao kuwa ukilikosa ujimalize. Sasa ukiwa na matatizo katika dini zote tunazozifahamu ukaamua matatizo yamekuzidi basi ujimalize, hiyo ni dhambi, dhambi kubwa (makofi).

Tuna matatizo ndani ya nchi yetu, hatuna demokrasia na wanaojaribu, wanawekewa vizingiti vikubwa lakini tusikate tamaa (makofi). Itakuwa kosa kubwa kukata tamaa. Na namna ya kuweza kuongeza madai yetu ya kuleta demokrasia ya msingi ni kuimarisha vyama vyetu, ishiriki katika chaguzi mwaka huu kuna uchaguzi wa vitongoji lakini haujaelezwa utafanyika vipi, utakuwa wapi, unakuwa kama vile unahitaji kushtukizwa.

Serikali haijaeleza huu uchaguzi wa vitongoji utafanyikaje, lakini tusiususie uchaguzi wa vitongoji pamoja na matatizo yaliyopo (makofi) kwa sababu ikiwa hatuna watu wetu katika vitongoji chaguzi za madiwani, chaguzi za wabunge, chaguzi za Rais. Tusipokuwa na sauti kwenye vitongoji, mitaa na vijiji, basi tutapata shida namna ya kusimamia kwa kuwataka wananchi ama wana CUF au wapenzi wa CUF washiriki katika chaguzi hizo tuwe na viongozi mtaani na vitongojini ndivyo tutakavyoweza kukijenga chama ndani ya jamii kwa hiyo vijana chaguzi za vitongoji zikitangazwa, tuwe tayari kushiriki.

Tutazame katika sehemu tunakoishi, wananchi gani wanaweza kuwa viongozi wazuri katika vitongoji vyetu. Kwa sababu tukiwa na wananchi ambao wanakubalika ... basi hata chaguzi zinazokuja itakuwa ni rahisi zaidi kusimamia tusiibiwe kura zetu...

Vijana tatizo letu kubwa nchini petu hivi sasa ni tatizo la uchumi. Tulipokuwa tunafanya kampeni mwaka 95 tulieleza kama tutaichagua CCM na kuirudisha madarakani, basi nilikuwa na uhakika dhiki na madhara yatakuwa zaidi kuliko yalivyokuwa mwaka 95 (makofi).

CCM haina sera wanadiriki kujisifu kwamba wanasimamia shughuli za uchumi vizuri. Rais anaeleza kwamba katika miaka yake mitatu na sasa huu ni wa nne, mambo ambayo amesimamia, juzi hapa nilieleza alipokuwa Chuo Kikuu akizungumza na wanajumuiya pale, alianza hotuba yake kwa kusema kama mngeniuliza kwa miaka mitatu na nusu hii, jambo gani ambalo limenipotezea muda wangu mwingi sana kushughulikia, anawaeleza vijana na waalimu wa Chuo Kikuu, jibu la kwanza lingekuwa ni uchumi, jibu la pili lingekuwa ni uchumi, jibu la tatu lingekuwa ni uchumi.

Kwamba hali yetu tuliyonayo ni matokeo ya Rais wetu kila kukicha anashughulikia tatizo la uchumi wa nchi yetu. Sasa katika kulishughulikia tatizo hili matokeo yake katufikisha hapa. Tulizungumza na wazee wa Bagamoyo, wazee wa Bagamoyo wakaeleza, basi afadhali angeshughulikia magazeti akaacha uchumi (makofi). Tungekuwa na magazeti mazuri zaidi kama hiyo miaka mitatu angejishughulisha na kuhakikisha kwamba Kiswahili na Kiingereza kinachotumika katika magazeti yetu kinakuwa Kiswahili kizuri na Kiingereza kizuri (Makofi).

Hali imekuwa ngumu na wenzetu hawana dira, hawana muelekeo wa namna gani ya kujenga uchumi ulio bora. Uchumi ambao ukiutazama unajua huu ni uchumi unaoingia karne ya 21. Hawana dira hiyo. Kuna tatizo la kihistoria, ilani ya uchaguzi wa CCM, nadhani ukurasa wa nane wa ilani ya uchaguzi, inasema wazi serikali ya CCM itaongozwa na siasa ya ujamaa na kujitegemea, inayolingana na wakati tulio nao. Sasa hali yetu ya uchumi inavyotafsiriwa na CCM hivi sasa tunatekeleza ujamaa na kujitegemea unaolingana na mwaka 1999. Huu ndio ujamaa wa sasa!

Wanaeleza katika ilani ya uchaguzi kwamba serikali yao itasimamia uzalishaji wa viwanda vitakavyotoa ajira kwa wananchi wa Tanzania. Kazi yao kubwa ya uchumi itakuwa kusimamia uzalishaji na ukuzaji wa viwanda vitakavyotoa ajira nyingi kwa wananchi.

Ukurasa wa 17 wa ilani ya CCM serikali ya CCM itamotisha viwanda vitakavyoongeza ajira ya wananchi kwa kutumia malighafi inayopatikana nchini na kusukuma uuzaji wa bidhaa za viwandani nchini na nchi za nje ili kuongeza pato la fedha za kigeni.

Tuwaulize CCM, Rais anapozungumza kuwaeleza watumishi wa serikali kazi yao ni kutekeleza ilani ya CCM, tunawauliza wana CCM ni viwanda vingapi mmeanzisha toka uchaguzi wa mwaka 95 ulipomalizika. Wananchi wangapi, vijana wangapi wameajiriwa kwenye hivi viwanda vipya vilivyoanzishwa kwa matokeo ya sera za CCM toka mwaka 1995 (makofi).

Wananchi hivi sasa tunalolijua ni kupoteza kazi kwenye viwanda vya uma, viwanda vinabinafsishwa, wafanyakazi hawalipwi haki zao, idadi ya wafanyakazi inapungua. Wananchi wengi hawapati kazi, nimekutana na vijana wa Chuo Kikuu waliomaliza Chuo Kikuu hawana kazi, miaka mitatu miaka minne na siyo tu masomo ya sayansi ya jamii na sanaa, kuna mainjinia wamemaliza Chuo Kikuu hawana kazi, CCM haina sera ya kuongeza ajira (makofi).

Wananchi Dar es Salaam tulivyo hali yetu, barabara zetu hazina mifereji ambayo inasaidia kupeleka maji. Barabara zote zina maji isipokuwa chache. Hizo ni kazi ambazo zinaweza zikafanywa kwa kuajiri watu wengi zaidi kuweka mazingira ya barabara zetu zisiwe zinaweka maji kama zinavyofanya hivi sasa. Unaongeza ajira kubwa kwa kuwa na taratibu za kuweka miundo mbinu ya mji wako. Tuseme Manzese, Temeke, Tandika, Sinza, sehemu zote hizi zikisimamiwa kutengeneza mifereji ili barabara ziwe bora, ajira kiasi gani unavyoweza kuiongeza (makofi). Watu nao watakaoajiriwa katika kazi hizi za nguvu kazi kipato watakachokipata watatumia kununua vitu. Kwa hiyo wataongeza biashara.

Watu wakiwa na fedha, wanapofanya biashara, wanaponunua vitu, ndiyo unavyoongeza ajira ya wengi na ikiwa kila mtu hana kitu basi ajira haiwezi ikaongezeka, lakini nilikuwa najaribu kutazama makaratasi ya serikali yana mpango gani wa kuongeza ajira. Pamoja na kwamba mji wetu una sehemu nyngi unazohitaji matengenezo ya kimsingi ya kuongeza ajira. Matokeo yake vijana mnayaelewa mtu hapati uzoefu wa kufanya kazi, umemaliza shule, hufanyi kazi popote pale nidhamu ya kufanya kazi huwezi ukaijenga. Kama kijana hajapata ajira yoyote alikaa miaka mingi bila ya kupata ajira, itafika wakati inakuwa haajiriki. Hajajenga nidhamu alfajiri inabidi uamke ujitayarishe kwenda kazini, kama huna kazi ni vigumu sana kuwa na nidhamu ya kuweza kuamka asubuhi kujua kwamba siku yako utaitumia namna gani. Unachoweza leo Yarabbi alamiin kikombe cha chai utakipata wapi. Sasa ukiwa katika hali hiyo mwaka mmoja, miaka miwili, miaka mitano, miaka kumi unakuwa na vijana ambao hawajapata nidhamu ya kuanya kazi. Kwa hiyo tunaanza kupoteza vijana wetu. Suala la ajira na taratibu za kuongeza ajira ni suala la msingi kabisa.

Itaendelea toleo lijalo
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook