Na Dkt. Abdallah J. Saffari
Hati ya kuitwa Shaurini
BAADA ya mashitaka kufunguliwa rasmi upande wa mashitaka hutoa majina ya mshitakiwa na mashahidi ambao unawahitaji katika uendeshaji wa kesi. Kufuatana na taarifa hiyo, mahakama huandika hati za kuwaita shaurini watu hao. Hivyo kuna hati za kuita shaurini washitakiwa na mashahidi.
Kila hati ya kuita mshitakiwa lazima iandikwe nakala mbili, itiwe saini na kugongwa mhuri na Hakimu au Afisa mwingine aliyepewa uwezo wa kufanya hivyo kama vile Msajili wa Mahakama na kadhalika. (F.100, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Hati hiyo itaandikwa na kupelekwa kwa mshitakiwa kumtaka ahudhurie mahakamani katika saa na siku iliyotajwa. (F.100(2), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Lazima pia ionyeshe kosa ambalo anakabaliwa nalo, pamoja na fungu la sheria linaohusu. (K.h.j.). Kwa mfano: Unatakiwa (mshitakiwa) kufika Mahakama ya Wilaya Kisutu saa tatu ya asubuhi Mei 10, 1995 kujibu shitaka la wizi dhidi ya fungu la 265 la Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania). Hati ya kumwita shahidi mahakamani itamtaka shahidi awasilishe mahakamani hati au vielelezo vyote alivyonavyo mntaarafu ya shauri linalohusika.
Polisi ndiyo hutumiwa kupeleka kwa wahusika hati za kuitwa shaurini. Lakini mtumishi yeyote wa umma au hata mtu yeyote tu yule anaweza kupeleka hati hiyo. Kila inapowezekana hati hiyo inatakiwa kuwasilishwa mikononi mwa mhusika mwenyewe kwa kumpa nakala moja ya hati yenyewe. (F.101(1),Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Iwapo atatakiwa na mpelekaji wa hati hiyo, mhusika itabidi atie saini yake nyuma ya nakala ya pili ya hati hiyo kuthibitisha kuwa ameipokea. (F.1010(2), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Kama mhusika hapatikani binafsi basi hati ya kumwita shaurini inaweza kuachwa kwa jamaa au mtumishi wake muradi awe mtu mzima. (F.102, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Na mtu huyo aliyeipokea hati hiyo kwa niaba ya mhusika atatia saini yake nyuma ya nakala ya pili ya hati hiyo iwapo atahitajika kufanya hivyo na mpelekaji. (K.h.j).
Na iwapo njia zote hizo zilizoelezwa hapo juu hazikuwezekana basi nakala moja ya hati ya kuita shaurini itaandikwa au kuwekwa katika sehemu ya nyumba yake ambapo mhusika ataiona kwa urahisi. (K.103, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Dhana ni kuwa mhusika atakuwa ameipata hati hiyo. Kama mhusika ni mtumishi wa serikali mahakama yatapeleka hati ya kuita shaurini kupitia kwa mkuu wake wa kazi. (K.h.j). Nakala mbili za hati hiyo zitapelekwa kwa mkuu huyo ambaye atawasilisha hati hiyo kwa mhusika na kumtaka atie saini yake nyuma ya nakala moja ya hati hiyo. Nakala yenye saini ya mhusika itarejeshwa katika mahakama iliyoitoa kama ushahidi kuwa imepokewa na mhusika.
Ikiwa kampuni au shirika linatakiwa kufika mahakamani hati ya kuita shaurini itapelekwa kwa njia ya rejesta kwa Katibu wa Kampuni au Shirika hilo au Afisa wake Mkuu. (F.105, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Dhana ni kuwa mawasiliano kwa njia ya Posta huwa kamili wakati barua imepostiwa.
Ikiwa kuna mabishano iwapo hati ya kuita shaurini imepokewa na mhusika au la, kiapo cha mpelekaji kuwa aliwasilisha hati hiyo kwa mhusika kwa namna inayotakiwa na sheria pamoja na nakala ya hati hiyo yenye saini ya mhusika vitakuwa ushahidi kuthibitisha uwasilishaji wa hati hiyo mpaka pale itakapothibitishwa vinginevyo. (F.108, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Hati ya kutia Nguvuni
Isipokuwa kwa sababu zitakazoelezwa baadaye, mtu atatiwa nguvuni kutokana na hati rasmi ya kufanya hivyo.
Karibuni hati za kutia nguvuni zote hutolewa dhidi ya washitakiwa ambao wanashindwa kuhudhuria mahakamani katika siku na wakati ambao wametakiwa kufanya hivyo kwenye hati ya kuita shaurini.
Hati ya kutia nguvuni itatolewa na Katibu Kata, Katibu wa Baraza la Kijiji, Hakimu au Jaji baada ya kukubali maombi ya kiapo kutoka kwa mlalamikaji. (F.13(1), 110 NA 112(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Mara nyingi polisi, kwa niaba ya Jamhuri, ndiyo hufanya maombi hayo. Inasikitisha tu kuona kuwa aghalabu hawafanyi hivyo kwa kiapo. Hakimu anayetoa hati hiyo atatia saini yake pamoja na mhuri wa mahakama. (F.112(1) na 112(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Kila hati ya kutia nguvuni lazima ieleze jina la mshitakiwa na shitaka ambalo anakabiliwa nalo. (F.112(2) Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Aidha itaonyesha wazi majina ya watu ambao watatekeleza amri ya hati hiyo. Polisi ndiyo hupewa jukumu la kukamata washitakiwa. Lakini iwapo hapana budi mtu yeyote tu anaweza kutekeleza amri ya kumkamata mhusika. (F.114(1) Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Iwapo mshitakiwa anakabiliwa na shitaka ambalo si la mauaji au uhaini, mahakama yaweza kuamuru mshitakiwa huyo apewe dhamana kwa masharti ambayo mahakama yataeleza nyuma ya hati hiyo ya kutia nguvuni. (F.122(3), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Masharti hayo yataonyesha idadi ya wadhamini, kiasi cha fedha ambazo wao pamoja na mshitakiwa mwenyewe watatakiwa kutoa kama dhamana, na mwisho, saa ambayo watahitajika kufika mahakamani. (F.113, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j)..
Mshitakiwa ana haki na lazima aelezwe kwanza sababu za kukamatwa, (yaani kutiwa nguvuni). Kama mshitakiwa atasisitiza basi aonyeshwe hai yenyewe ya kumtia nguvuni. (F.117, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Hata hivyo, polisi au raia anaweza kumtia nguvuni mtu bila ya hati ya kufanya hivyo kama mtu ameonekana akitenda kosa la jinai. Hii inatoa fursa ya kuzuia utendaji wa makosa ya jinai na kurahisisha upelelezi wake. Vinginevyo ni vigumu kumkuta mhalifu anasubiri akamatwe baada ya kutenda kosa.
Utiaji nguvuni, yaani ukamataji unafanyika kwa namna mbili kutegemea mazingira yenyewe. Moja ni kumkamata kabisa mhusika. ((F.11, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Wakati mwingine pingu hutumika kumfunga mtu anayekaidi kutiwa nguvuni. Njia nyingine ni ya matamshi kwamba mtu huyo amekamatwa rasmi na kuwa yuko chini ya ulinzi wa kisheria. (K.h.j). Amri kama hiyo ina uzito wa kisheria na ni kosa kutoitii. (F.22. Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Njia hii ya pili ni ya kiungwana zaidi na hutumika mara nyingi isipokuwa kwa wale wakorofi tu. Mkamataji anaruhusiwa kutumia kiasi cha nguvu kinachotosha kumweka mkamatwaji chini ya ulinzi, na wala sio zaidi.
Nguvu inaweza kutumika dhidi ya mkamatwaji ikiwa ni lazima lakini kwa kila hali nguvu hizo zisikiuke kiwango kinachotosha kutekeleza ukamataji wenyewe. Kwa mfano jambazi laweza kupigwa kirungu ikiwa linakataa kutiwa mbingu, au linaweza hata kupigwa risasi ya miguuni kama linakimbia kutiwa nguvuni. Hata hivyo matumizi ya bunduki yanatakiwa kufanyika baada mkamataji kutoa onyo kwa mkamatwaji kuwa anakusudia kuitumia silaha hiyo kama hatasimama. Onyo sahihi zaidi ni kupiga hewani rasasi moja kabla ya kumlenga mkamatwaji.
Mkamatwaji anaweza kupekuliwa na vitu ambavyo vinashukiwa kuhusiana na uhalifu vinaweza kuchukuliwa na kuhifadhiwa kungojea kukamilika kwa upelelezi dhidi yake. (F.24(b), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Nguo alizovaa mkamatwaji hazitavuliwa. Ikiwa mkamatwaji atakutwa na silaha zozote za hatari zitachukuliwa na kuhifadhiwa mahakamani au kwenye kituo cha polisi. (F.27,Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j)
Mtu anayekamatwa na polisi bila ya hati ya kufanya hivyo ni lazima afikishwe mahakamani, au kama amekamatwa na raia, afikishwe kituo cha polisi haraka iwezekanavyo katika muda usiozidi saa ishirini na nne. (F.30 na 32(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Kumuweka mkamatwaji chini ya ulinzi kwa muda mrefu bila ya kumfikisha mahakamani ni kosa. ( Dutto v. West Nile District Administration (1968) E.A..428).
Dhamana
Mtu aliye chini ya ulinzi wa kisheria anaweza akaweka na kupewa dhamana na kuachiwa huru hadi wakati wa siku ambayo atahitajika kufika sehemu anayotakiwa kama vile kituo cha polisi au mahakamani.
Dhamana huweza kuombwa na kutolewa katika hatua tatu tofauti: wakati wa upelelezi wa shauri (F.64(2), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j) usikilizaji wake (F.148, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j) na mwisho, kabla ya rufani kusikilizwa. (F.368, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
Wakati wa upelelezi wa kesi polisi wanaweza kumkamata yaani kumtia nguvuni mtuhumiwa ili awasaidie na upelelezi wa shauri linalohusika. Baada ya mahojiano wanaweza kumwachia mtuhumiwa huyo kwa dhamana. (F.64, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Hii hujulikana zaidi kama dhamana ya polisi. Dhamana haiwezi kutolewa iwapo mshitakiwa anashitakiwa kwa kosa la mauaji au uhaini. (F.148(5) Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Hata hivyo baadhi ya mahakama duniani yamewahi kutoa dhamana katika kesi za mauaji licha ya sheria kukataza jambo hilo. Mathalan katika Owusu and Another v. The Public, (1980) GLR 469. Angalia pia Seida and Others v. The Ruplic (1978 1 GLR 67), Mahakama Kuu ya Ghana yalitoa dhamana kwa vile ilidhihirika kwamba shauri lenyewe lingechelewa mno kusikilizwa. Hadi wakati wa maombi ya dhamana, tayari mshitakiwa alikuwa amekaa rumande kwa zaidi ya miaka mitatu. Ilidhihirika pia kuwa hali yake ya afya ilizidi kuwa mbaya. Lakini sababu muhimu kupita zote ni kuwa mahakama yaliridhika kuwa hakukuwa na ushahidi unaotosheleza kufungua shitaka la mauaji ya kukusudia. Sababu kama hiyo pia ilitumiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania kumpa dhamana mshitakiwa wa mauaji ya kukusudia katika R. v. Daimu Mkando na Wenzake (Maombi Maalum ya Jinai Na. 24, 1985, Mahakama Kuu, Arusha) na R. v. Patrick Soka na Wenzake( Uchunguzi wa Awali Na. 16, 1989, Mahakama Kuu, Arusha).
Licha ya makosa ya mauaji ya kukusudia dhamana pia haitatolewa iwapo mshitakiwa aliwahi kuvunja masharti ya dhamana au ameshitakiwa kwa kosa alilolitenda akiwa katika dhamana. Dhamana pia itakataliwa iwapo Mkurugenzi wa Mashitaka, atapinga kwa hati maalum kwamba dhamana isitolewe kwa vile itahatarisha usalama au manufaa ya taifa. (F.. 148(4) Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j. Angalia pia F.35(2), Sheria ya Makosa ya Kiuchumi, Na. 13, 1984).
Katika Daud Pete v. R (Shauri Maalum la Jinai Na. 80, 1989, Mahakama Kuu, Mwanza) uwezo huu wa Mkurugenzi wa Mashitaka kupinga dhamana ulionekana kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa vile unamnyima mshitakiwa haki yake ya kibinadamu ya kujitetea kabla hajakataliwa dhamana. Kwa bahati mbaya baadaye Mahakama ya Rufani ya Tanzania hayakulijadili suala hili kwa undani katika R. v. Daudi Pete (Shauri la Jinai la Rufani Na. 28, 1990, Mahakama ya Rufani ya Tanzania) wakati ambapo Jamhuri ilipania kutengua hukumu ya awali ya Mahakama Kuu katika shauri hilo.
Mtuhumiwa alipofunguliwa mashitaka rasmi hatua nyingine huanza, ambayo inamkabidhi mikononi mwa mahakama kuanzia wakati huo mpaka shauri lake litakapomaliza kusikilizwa.
Dhamana huweza kutolewa kwa washitakiwa wa makosa yote isipokuwa yale yaliyotajwa punde tu. Vinginevyo mahakama bado yana uwezo wa mwisho kumwachia mshitakiwa kwa dhamana au la. Na vile mshitakiwa sio mhalifu hadi inapothibitishwa hivyo, dhamana hukataliwa pale tu kunapokuwa na sababu za msingi sana.
Masuala kadhaa hutiliwa maanani na
mahakama yanapofikiria kukubali au kukataa ombi la dhamana. Uzito wa kosa
ambalo mshitakiwa anakabiliwa nalo ni moja ya masuala hayo. Hofu ni kwamba
iwapo mshitakiwa atapatikana na hatia anaweza kupewa adhabu kali, jambo
ambalo huweza kumtisha au kumshawishi kutoroka akiwa nje ya dhamana.
|
|