Vijana tuunde jamii ya Kiislamu
 

Na F. Mkombozi

JAMII bora ya Kiislamu ni ile inayotokana na familia bora ya Kiislamu. Kama inavyojulikana ni kwamba familia inaanzia kwa mume na mke waliotangamana kwa mafungamano ya ndoa na watoto waliozaliwa nao. Hii ndio maana fupi ya familia, ingawa katika Uislamu maana yake ni kubwa zaidi ni yenye kuingiza wazazi, ndugu na kadhalika.

Kwa misingi hiyo jamii bora chanzo chake ni mke na mume waadilifu. Hivyo basi anayetaka kuunda jamii, jambo la kwanza la kuzingatia ni kutafuta mwenza atakayekuwa naye sawa katika maadili mema. Hivyo ni lazima kutafuta mke ama mume wa sawa ambaye atakuwa ni nguzo muhimu katika kuunda jamii na mainukio yake.

Mara nyingi familia zinaundwa kwa makosa kwa sababu ya kushindwa kuchagua mwenza. Hali ikishakuwa hivyo watoto wa jamii hiyo hukua wakiwa wabaya. Na hili linatokana na vijana kutozingatia mafunzo ya Mtume (s.a.w.) ya kuchagua mwenza bora. Badala yake mke au mume huchaguliwa kwa uzuri ama utajiri wake. Na ile sifa njema ya ucha Mungu imewekwa kando!

Jambo lipi linalotarajiwa kwa watoto ambao baba au mama au wote wawili ni walevi, hawana mshikamano wa dini, au ni wahalifu? Linalotarajiwa kwa familia hii ni kuharibikiwa. Ni wajibu wa kila mmoja anayetaka kuunda familia amchague yule atakayeshirikiana naye katika kuunda familia ya kicha Mungu. Mtume Muhammad (s.a.w.) amesema, "asili yapiga mbali".

Maana yake mtu aliyezaliwa na mtu au watu wabaya ile damu mbaya itaenda kwa mmoja kati ya wazazi wake. Hii ndio sababu Mtume (s.a.w.) akaamrisha Waislamu wanapotaka kuoa kwanza wachague watakayemuoa kwa kusema, "chagueni pahala pakuweka tone la maji yenu". Vile vile akasisitiza tena kwa kusema, "Chagueni pahala pa kupanda mbegu zenu. Chagueni mwanamke wa kuoa ambaye ndiye mbegu ya jamii inayopandwa".

Kinachosikitisha hivi sasa ni jinsi ulimwengu ulivyoparaganyika kutokana na wimbi la mabalaa mbalimbali yapelekayo maangamizi makuu. Mabalaa hayo hapo wazi na sioni umuhimu wa kuyataja. Na chanzo chake ni ukosefu wa maadili mazuri. Na hii ndio iliyonishikiza kuandaa makala hii. Kwa sababu vijana ndio watarajiwao kuikwamua hali hii. Hivyo lazima tutambue kuwa chanzo ni ukosefu wa mafunzo mema hususan kwa wazazi waadilifu haswa mama.

Kuna msemo wa watu wenye hekima usemao. "ukimlea mwanamke vizuri huwa umelea taifa zima". Msemo ni sawa kwa sababu mwanamke ni shule ya kwanza ambayo kila mtu lazima aingie kwanza kabla hajaenda nyingine yoyote. Iwapo basi shule hii itakuwa si barabara matarajio ni kila apitiae lazima aambulie ‘uvundo’ ambao hupelekea kuundwa kwa jamii mbaya yenye wazinifu wengi, vibaka, wavuta madawa ya kulevya, walevi, wezi, walaghai na wachafuzi wote wa jamii.

Leo hii tumekuwa tukikabiliwa na matatizo mengi kuanzia kiuchumi, siasa na hata kimaadili kwa ujumla. Chanzo ni ukosekanaji wa uundaji wa familia ipelekayo jamii bora. Leo hii imefikia wazazi kuwatafutia watoto wao wazazi wengine, utakuta mzazi analalamika kwa uchungu "hawa watoto wa siku hizi bwana!" Sasa utashangaa hiyo "siku hizi" mwenyewe yuko, lakini bado hawajabaini chanzo ni nini.

Suala la hijabu mashuleni limekuwa ni kielelezo hai cha kudhihirisha ufinyu wa maadili utolewao na wazazi/walezi. Tangu mwaka 1995 ruksa ya hijabu ilitolewa, lakini wazazi wamekuwa kimya na kupelekea baadhi ya vijana kutumia muda mwingi kuhamasisha kutumia matangazo mbalimbali, mihadhara, semina, taalimu na vikao mbalimbali vya Kiislamu lakini bado amri hiyo kutekelezwa imekuwa ngumu mno!

Sasa mzazi kama huyu asiyefahamu hata ubora wa vazi hili. Ni vigumu kutoa malezi bora ya mfumo wa Uislamu kwa watoto anaowalea. Hivyo basi vijana tuwachukulie wazazi hao hawakupata mafunzo muafaka yatakiwayo katika Uislamu. Bali sisi hatuna utetezi. Ni muhimu sasa kuzingatia mafunzo mazuri na kujiandaa na ujenzi wa jamii ya Kiislamu. Tusikae na kuota ndoto hali ya kuwa tumesimama wima, mafaniko hayawezi kuja bila ya maandalizi mazuri.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook