Na Abeid Poyo
KUPOTEA kwa hadhi ya Msikiti kama taasisi mama katika Uislamu kumepelekea Uislamu kudidimia na kushuka hadhi yake kulinganisha na ilivyokuwa wakati wa Mtume (s.a.w.) na masahaba. Misikiti ni taasisi mama na muhimu sana katika Uislamu, ndiyo maana Mtume alipohamia Madina kwanza alijenga Msikiti kwani mambo yote ya Uislamu yangeanza na yenye kumalizika hapo.
Msikiti wakati wa Mtume (s.a.w.) ulikuwa si mahala pa kuswalia tu bali shughuli zote, Ikulu, mahakama, kituo cha elimu, ukumbi na kadhalika.
Lazima ikumbukwe kuwa ni baada ya Msikiti kutumika kwa shughuli hizi, Uislamu uliweza kustawi. Lakini leo hii ni kinyume cha mambo. sio tu kwamba shughuli hizi hazifanyiki tena Misikitini bali hata Waislamu hawajui kama haya yanatakiwa yafanyike Msikitini.
Misikiti leo hii imekumbwa na matatizo mengi sana ambayo sio tu yanaurudisha nyuma Uislamu, pia kuupa picha isiyo yake. Misikiti mingi mijini na vijijini imekuwa ndio mahala pa kuchochea migogoro na tofauti ya madhehebu, Misikiti kuongozwa na watu wasio na elimu pana na hivyo kushindwa kuiathiri jamii.
Uchafu katika Misikiti yetu, kuanzia ujenzi holela, uchakavu wa majengo, maliwatoni na sehemu za kuchukulia udhu zinaleta picha mbaya ya Uislamu wakati Uislamu unasisitiza usafi.
Leo hii, Maimamu na Makhatibu wetu kwa kukosa elimu zote kwa upana wake wameshindwa kuiathiri jamii, hawa ndio waliotakiwa kufanya kazi ya kuwa viongozi wa jamii.
Msikiti unashindwa kuwa hata na wahasibu wa kudhibiti mapato na matumizi ya Msikiti wakati kila kukicha michango inatolewa!
Misikiti imekimbiwa na vijana wetu wanaoathirika na Umagharibi kwa sababu Misikiti imeshindwa kuwahudumia. Kama Misikiti ingekuwa na maktaba zenye vitabu na magazeti kutoka kila fani, vijana hawa wasingepata fursa ya kwenda kuharibiwa "British Council au American Library".
Hata watoto wetu imewalazimu kwenda kumsifu Bwana na kula mkate mtamu wa Bwana kwa sababu Misikiti imeshindwa kuwaandalia madarasa ya chekechea.
Kama tulivyoona mwanzoni kuwa kupotea kwa hadhi ya Msikiti kumechangia katika kudidimia kwa Uislamu, hivyo ili kurudisha hadhi hii, ni lazima Waislamu waifanye Misikiti yao kuwa ya kisasa zaidi, itakayoweza kutumika kwa shughuli zote kama tulivyoona.
Msikiti mbali ya kuwa ni sehemu ya kuswalia tu, kama ilivyozoeleka na wengi pia uwe ni kituo (centre) hivyo tunaposema mathalan "Masjid Aqsa" tumaanishe kituo chenye mambo yafuatayo, sehemu ya kuswalia yenyewe, shule, maktaba, kliniki (kama sio hospitali), ukumbi, hosteli na mengineyo.
Kama alivyosema ndugu yangu Mwapwani kuwa Misikiti ni mahala wanapotakiwa Waislamu kukutana pamoja kuangalia mambo yao na kujadili matatizo yanayoikabili jamii na hii ndiyo siri ya kuswali vipindi vitano Misikitini tena kwa jamaa.
Misikiti ya kisasa ni lazima iwe na mikakati ya kujiendesha kifedha badala ya kusubiri tu michango ya waumini, hivyo kwa Misikiti inayojengwa au itakayojengwa nasaha inatolewa kwa wahusika kubuni mipango na mikakati itakayowezesha Misikiti kujiendesha, haiyumkiniki kwa Misikiti yenye wasaa wa nafasi kushindwa kuwa na vitega uchumi kama maduka, maofisi n.k.
Wito vile vile unatolewa kwa Waislamu kufanya kila liwezekanalo kuanzisha Misikiti kwa maana ya vituo katika sehemu zenye wasaa wa ardhi kama pembezoni mwa miji au vijijini badala tu ya kung’ang’ania mijini kwenye ufinyu wa ardhi. Hivi hatujifunzi kwa wenzetu ambao kila kukicha wanahodhi maelfu ya eka huko vijijini.
Tumekuwa tukisema kama sio kulalamika kuwa wenzetu wana ardhi kubwa huko vijijini, wamejenga viwanja vya ndege, mahospitali n.k. Je, sisi Waislamu tumejaribu hata kuomba ardhi katika mapori ya vijijini tukanyimwa?
Hebu tujaribu kufanya jaribio la kutembea toka mkoa wa Morogoro hadi Dodoma tukisha hebu tuangalie majengo yaliyojengwa na wenzetu. Hivi sisi tunashindwa nini? Hatuna fedha, hatuna imani, kumbe!
Ieleweke kuwa sio lengo la makala kuwataka Waislamu kuiga na kujenga majengo makubwa kama ya wasiokuwa Waislamu, isipokuwa makala ina lenga kuwakumbusha Waislamu kuifanyia mabadiliko Misikiti yetu ya karne ya 5 kuwa ya kisasa zaidi kihali na kiutandaji.
Ni jambo la aibu kwa Misikiti kukosa vitu vidogo vidogo kama simu, shule ya chekechea au zahanati angalau ya kutoa huduma ya kawaida.
Ni fedheha pia kuona Waislamu wakifanya ibada zao kama mikutano ya dini, mabaraza ya Idd na mihadhara katika kumbi ambazo ndani yake Mwenyezi Mungu huasiwa na najisi (pombe) kunywewa, eti kwa kuwa Waislamu hatuna kumbi za mikutano.
Ikumbukwe vile vile kuwa katika kuifanya kazi hii nzito ya kuihuisha Misikiti yetu, wahusika wawe ni wale wanaotajwa katika aya ifuatayo:
"Wanaoamrisha Misikiti ya Allah ni wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho na kusimamisha swala na kutoa zaka na hawamuogopi yeyote ile Mwenyezi Mungu, basi hao ndio wanatarajiwa kuwa miongoni mwa waliongoka". (9:18)
|
|