Ijue Madrasat Maamur

Na Abeid Poyo

MADRASATUL Maamur ni madrasa mchanganyiko iliyopo katika majengo ya Msikiti wa Temeke Mwisho wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam.

Madrasa hii ilianzishwa mwaka 1989 muasisi wake akiwa ni Sheikh Alhad bin Mussa. Ilianza na wanafunzi 28 wasichana 16 na wavulana 12.

Kwa mujibu wa maelezo ya muasisi huyo ambaye pia ndiye Mudir Mkuu kwa sasa, madrasatul Maamur ilianza katika mazingira magumu na mitihani kadhaa, hata hivyo akishirikiana na Makamu wake Ustadh Zuberi Idd Mahambi waliweza kuikomboa na kuiweka katika hali ya kuridhisha.

Madrasa hii ilianzishwa kwa lengo la kuwafundisha na kuwalea vijana kuanzia ngazi ya chekechea na kuendelea. Kwa sasa masomo yanayofundishwa ni pamoja na Fiqh, Siira, Tawhiid, Hadith, Lugha ya Kiarabu na Maarifa ya Uislamu kwa ujumla.

Hivi sasa madrasa hii ina wanafunzi wapatao 196 chini ya uangalizi wa walimu wanne ambao ni Sheikh Alhad Musa (Mudir), Zuberi Idd (Naibu Mudir), Abbas Charles na Mohamed Khatib.

Tangu kuanzishwa kwake madrasa imefanikiwa kutoa vijana kadhaa ambao kwa sasa ni Makhatibu na Maimamu wasaizidi katika Misikiti kadhaa wilayani humo. Vile vile imekuwa ikiandaa hafla ya kusherehekea mazazi ya Mtume (s.a.w.) kila mwaka mfungo saba, ambapo mwaka jana madrasa iliandaa hafla kubwa iliyowajumuisha Masheikh toka sehemu kadhaa za ulimwengu. Vile vile madrasa imeanzisha darasa la kinamama ambalo kwa sasa lina wanafunzi wapatao 26.

Akitaja matatizo yanayoikabili madrasa yake, Sheikh Alhad amesema ni pamoja na uhakika wa ajira kwa walimu, ambapo walimu wamekuwa wakikimbia kufundisha, wazazi kushindwa kuchangia ada za kila mwezi, vile vile utoro kwa wanafunzi ambao wengi wao wamekuwa wakihudhuria masomo ya ziada (tuition) mashuleni mwao.

Akimalizia, Sheikh Alhad alitoa wito kwa wazazi kuwa na ushirikiano wa karibu na walimu.


Ijue Taasisi ya Iqra Islamic Centre
 

IQRA Islamic Centre ni Taasisi ya Kiislamu inayoshughulika na masuala ya Da’awah kuufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu (s.w.) ili kuuzindua ummah na kukumbusha. Iliasisiwa na kuzinduliwa rasmi Machi 1, 1998 mtaa wa Wailes wilaya ya Temeke, mkoa wa Dar es Salaam nyumba namba 39 kwa Ustadh Farid.

Muasisi wa jina hili la Iqra ni Ustadh Ahmed Mzoa na Ustadh Farid Mohamed. Wasisi wa kwanza walikuwa watu wawili chini ya uongozi wa ustadh Ahmed M. Mzoa (Amir Mkuu) na Hamad Nadhifu (Katibu Mkuu).

Tasisi hii ni ya Waislamu, hivyo ni kila Muislamu anakubaliwa kujiunga nayo kwa kufuata taratibu zilizowekwa na uongozi na kuwa (Members). Ili kuimarisha taasisi, ilibidi kuhamia mtaa wa Rusende Temeke kufanya makao mapya ya muda, hiyo ilikuwa Oktoba 2, 1996. Katika madrasda iliyokuwa ikiitwa Madrasa Tulnnajah iliyopo ubavuni mwa nyumba ya marehemu Mohamed Kindamba na marehemu Rashid Mweleka nyumba Na. 21023. Na tarehe hiyo ndipo ilianzishwa kituo (shule) cha watoto wadogo (Nursery) kuwapa elimu ya Kiislamu, pamoja na masomo ya hesabu, Kiingereza (English) n.k. Kwani ni kutekeleza moja ya malengo ya taasisi hii kutokana na maazimio ya wanatasisi (waanzilishi).


Ijue Madrasat Madinat Munawara Mkulazi Ngerengere Morogoro

Na Dibagula, Morogoro

MADRASA hii ipo nje ya mji wa Ngerengere mkoani Morogoro. Muasisi wake D.A. Dibagula mzaliwa wa Mkulazi na mwalimu wake ni Ustadh Abas Athuman.

Ilianzishwa mwaka 1998 mwezi tatu ikiwa na wanafunzi 30, muda mfupi idadi hiyo ikaongezeka hadi kufikia 50.

Matatizo inayoikabili madrasa hii ni pamoja na kibanda ambacho ni cha nyasi, vitabu, mikeka na walimu. Kijiji ni kikubwa lakini kuna mwalimu mmoja tu. Huduma zisizoridhisha anazopata mwalimu kutokana na ukata wa aliyemleta yaani muasisi wa madrasa.

Mwito umetolewa kwa Waislamu kupeleka nguvu zao vijijini ambako Uislamu umekufa. Wenye kupenda kutoa msaada apige simu No. 184559 ama akipenda atapelekwa akajionee mwenyewe hali halisi ilivyo.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook