Hakuna Uislamu wa mguu nje mguu ndani - Sheikh Bashir
 

Na Abu Zuberi, Dodoma

SHEIKH Omar Bashir amewausia Waislamu juu ya kuingia katika hukumu zote za Kiislamu bila ya kuchagua lipi la kufanya na lipi la kuacha, pia aliwaeleza Waislamu kuwa hakuna khiyari katika kufuata amri za Allah (s.w.) wala hakuna Uislamu wa nusu nusu.

Aliyasema hayo alipokuwa akiwahutubia mamia ya waumini wa Kiislamu waliofurika Masjid Al-Hudaa (Chamwino) baada ya sala ya magharibi mjini Dodoma hivi karibuni.

Sheikh Omar Bashir ambaye alikuwa mjini Dodoma katika shughuli za Da'awah aliwahutubia waumini hao katika mada zake mchanganyiko zenye mtitiriko wa aya nyingi za Qur'an na Hadith za Mtume (s.a.w.).

Alisema, Uislamu unazo sheria zake na utamaduni wake, hivyo Waislamu hawapaswi kuvutwa na kuiga tabia za matwaghuti ambazo zitawapelekea kumuasi Mola wao na hivyo kujikuta wanaangamia siku ya kiyama.

Sheikh Bashir aliwajulisha Waislamu kuwa wanapaswa kuulinda Uislamu kwa hali yoyote iwe kwa mali au nafsi zao na wawe tayari kuwa wavumilivu kwa misukosuko itakayowapata kwa kuifanya kazi hiyo.

Sheikh Bashir alilaani baadhi ya matangazo ya biashara ambayo yanyanayotangaza pombe, na kudai kuwa ndio urithi wa mtanzania na alikemea vikali mashindano ya warembo kwani mavazi yanayovaliwa na wahusika humdhalilisha mwanamke.

Aidha Sheikh Bashir aliwaonya wazazi wa Kiislamu wenye kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika mashindano hayo "wafurahie kwa kipato kidogo wanachokipata na wasubiri fedheha kubwa siku ya kiyama".

Sheikh Bashir aliwasisitiza Waislamu hususan vijana kushikamana pamoja kwa kuitetea dini ya Allah (s.w.) kwa jitihada zote.

Alisema kuwa miongoni mwa maswali mazito yatakayotakiwa yajibiwe siku ya kiyama ni juu ya kijana alivyotumia ujana wake kuisimamisha dini ya Allah (s.w.).

Aliueleza umati huo wa Waislamu waliofurika hadi nje ya jengo la Msikiti kuwa misukosuko katika kuusimamisha Uislamu ni ya kawaida na inakwenda sambamba na kazi hiyo, kwani hilo limethibitishwa na Allah (s.w.) katika Qur'an Tukufu, na vile vile Mtume (s.a.w.) yalimpata hayo.

Wakati huo huo, Sheikh Omar Bashir alitoa sikitiko lake kwa kutopewa nafasi ya kuwahubiria Waislamu katika Msikiti maarufu wa Nunge wa mjini Dodoma.

Sheikh Bashir alisema sababu zilizotolewa ni kuwa wadhamini wa Msikiti hawakuwepo ambao imedaiwa ndio wahusika wa kuruhusu nani atoe na nani asitoe mawaidha.

Alisema kuwa zoezi kama hilo likizidi kukumbatiwa kwa Masheikh na waumini wao kuwaenzi wadhamini kiasi hicho, basi litaharibu kabisa dira ya Waislamu katika mshikamano.


Kanda ya mauaji Mwembechai yaliza wanawake Dodoma

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAMIA ya wanawake wa Kiislamu walijikuta wakitokwa na machozi pale walipokuwa wakishuhudia mauaji ya kikatili yaliyofanyika Mwembechai Februari 13, mwaka jana dhidi ya raia wasio na hatia.

Katika kusherehekea sikukuu ya Idi el Haji, akina mama wa Kiislamu wa mjini Dodoma waliungana kufanya baraza la Idi katika shule ya Sekondari ya Jamhuri, akina mama hao baadaye walielekea Area 'A' kujionea wenyewe kwa kile kilichofanywa na askari wa uongozi wa awamu ya tatu, kwa kuwaua Waislamu zaidi ya wanne kadri kanda ilivyoonekana.

Akina mama hao ambao waliiweka taswira ya siku hiyo sawa na Hija ya mwisho ya Mtume (s.a.w.) kwa kuwakumbusha kauli ya Mtume (s.a.w.) aliyosema pale Arafa kuwa "damu zenu na mali zenu ni vitu vitakatifu kamwe msikubali vichezewe". Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi Bi Kuruthum alihoji kuwa "leo hii damu ya Waislamu imekuwa si chochote hasa kuhusiana na matokeo ya Mwembechai

Akina mama hao na wengine ambao kimaumbile huathirika sana hasa pale wanapoona damu ya mtu ikimwagika hata kwa kukatwa jeraha, wameazimia kujitoa muhanga na kuwa na umoja madhubuti utakaowafanya wawe na mwelekeo mmoja mwaka 2000 kwani walisema ni kura ya pamoja itakayotoa badiliko la sura hii iliyopo sasa nchini.

Kanda ya mauaji ya Mwembechai ambayo imeshafika mjini Dodoma inategemewa kunakiliwa na kusambazwa wilayani na vijijini ili wananchi waone yale yaliyopotoshwa na vyombo va habari vya binafsi na vya serikali kuhusiana na kadhia ya mauaji ya Mwembechai.

Wakati huo huo Bi Fatma Ramadhani Mwanada'awah kutoka Gongo la Mboto (Markaz) amewataka akina mama wa Kiislamu waliokusanyika katika Baraza la Idi waitikie wito wa kuwavalisha watoto wao hijabu.

Aliwaeleza akina mama hao kuwa wanondokane na usingizi mzito wa woga usiyo na kipimo kwani suala hilo limebaki mikononi mwa wazazi na siyo serikali tena.

Bi Fatuma alisema "Pale mtakapopambana na mwalimu mkorofi unganeni na kuidai haki yenu; kwani bado wapo walimu wakorofi ambao hawakubaliani na uamuzi wa serikali kuhusiana na suala la hijabu.


Wanafunzi Kilakala Moro hatarini kulishwa nguruwe
 

Rajab Rajab na Havijawa Charles, Morogoro

WANAFUNZI wa Kiislamu wa shule ya sekondari ya wasichana ya Kilakala mjini hapa wapo hatarini kulishwa nyama ya nguruwe kufuatia uongozi wa shule hiyo kuchinja nyama hiyo shuleni hapo na kupelekwa mabwenini na wanafunzi wasiokuwa Waislamu.

Wakiongea na gazeti hili hivi karibuni, wanafunzi hao (Waislamu) ambao hawakupenda majina yao yawepo gazetini kwa hofu ya kufukuzwa shule wamesema kuwa kitendo cha shule hiyo kufuga nguruwe katika mazingira ambapo wanaishi Waislamu kimewafanya waishi bila ya kujiamini kukwepa madhara ya wanyama hao.

Wameendelea kusema kuwa katika siku za nyuma ufugaji wa nguruwe shuleni hapo kidogo ulikuwa wa kistaarabu kwa vile haikuwa rahisi kuwaona nguruwe wakizurura ovyo tofauti na hivi sasa ambapo kumeongezwa na kuchinjwa kwa wanyama hao kila mwishoni mwa wiki.

Wamebainisha kuwa wanafunzi wasiokuwa Waislamu mara nyingi wamekuwa wakinunua nyama hiyo na kupeleka mabwenini na wakati mwingine hutumia vyombo vya wanafunzi wa Kiislamu wakiwa hawapo au katika mazoea ya kushirikiana kutumia vitu.

Pia wanafunzi hao wa vidato mbalimbali wamelalamikia mabanda yanayofugiwa nguruwe shuleni hapo kutokuwa imara na kufanya nguruwe hao kutoka na kuzagaa jikoni wakitafuta mabaki ya vyakula.

Wametoa mfano kuwa mnamo Machi 13, mwaka huu alitoka nguruwe mmoja na kuvinjari mpaka sehemu wanayoanika nguo zao chini ya nyasi fupi ambapo nguruwe huyo kama vile ametumwa alikanyaga nguo hizo na kuziendea haja kubwa na ndogo.

Wamesema kuwa kufuatia tukio hilo ambalo limewaudhi hata wanafunzi wasiokuwa Waislamu wakaamua kumtaarifu mwalimu anayehusika na miradi ambaye aliwaambia kuwa hiyo ni bahati mbaya na haiwezi kutokea tena.

Wamedai kuwa wakati wanamueleza mwalimu huyo kuhusu tukio hilo majira ya asubuhi, ilipofika jioni siku hiyo hiyo wakawaona watoto wa nguruwe wakiranda randa maeneo ya jikoni hali ambayo wamedai iliwasononesha na kujiona kwamba hawakutakiwa kusoma katika shule hiyo isipokuwa uongozi wa shule hiyo unawalazimika tu kuwapokea.

Mbali na wanafunzi hao kumfikishia malalamiko hayo mwalimu anayehusika na miradi shuleni hapo, pia wamewaeleza walimu wanaofundisha somo la dini ya Kiislamu shuleni hapo ambapo wameahidiwa kuwa litashughulikiwa haraka iwezekanavyo.

Aidha wanafunzi hao wametoa kilio kwa serikali kupitia Wizara ya Elimu na Utamaduni kufanyia utafiti suala hili na kulipatia ufumbuzi wa kudumu ili wanafunzi wa madhehebu yote waweze kusoma bila ya kuathirika kimazingira.

Gazeti hili lilijaribu kuwatafuta walimu wa dini ya Kiislamu wanaofundisha shuleni hapo kama wanazo taarifa hizo. Kwa kupitia Ustadh Mohamed walimu hao walithibitisha kupokea taarifa hizo na kudai wanazifanyia kazi na wanatarajia mapema wiki ijayo kuonana na uongozi wa shule ili kuweza kuliweka sawa jambo hili.

Juhudi za gazeti hili kuwasiliana na mwalimu mkuu wa shule hiyo kwa njia ya simu hazikuweza kufanikiwa kutokana na simu (namba 2196) kuita bila ya kupokelewa.


Korogwe washuhudia mauaji ya Mwembechai

Na Masoud Mohamed, Tanga

WAISLAMU mjini Korogwe wameungana na wenzao ambao hawakuweko Mwembechai mwaka jana katika kushuhudia udhalimu uliotendwa na polisi na serikali yao.

Hilo lilikuwa tukio muhimu la maadhimisho ya Idul-Adhha ya mwaka huu lililotanguliwa na Baraza la Idd ambalo lilifanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya mji.

Mara baada ya baraza; saa kumi na mbili na nusu jioni Waislamu walielekea kwenye Msikiti Mkuu wa Manundu kushuhudia yale waliyokuwa wakiyasikia kwa zaidi ya mwaka sasa.

Mkanda ulipoisha majira ya saa tatu usiku, karibu kila mmoja kati ya umati uliohudhuria alisikika akilalamika kivyake. Wengine walitaka Waziri Ameir, Mkuu wa Mkoa Makamba, Kamanda wa polisi Gewe wawajibishwe kutokana na mauaji hayo, wengine walimtaja Rais na wengine CCM.

Pamoja na kila mtu kulalamika kivyake, wengi walionekana kupanga kutoa hasira zao kwenye uchaguzi wa mwakani, pindipo tume ya kushughulikia mkasa huo haitoundwa mapema.

Uongozi uliosimamia onyesho hilo lililotia huzuni siku ya furaha, unapanga kwenda kuonyesha kwenye kijiji cha Muhezangulo, tarafa ya Magoma alikozaliwa Bwana Yusufu Makamba.

Aidha, ratiba inaonyesha kuwa Msikiti mmoja kabla ulikwishaangalia na Misikiti mingine pia itapata fursa hiyo wilayani humo.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook