Na Mwandishi Wetu
KITENGO cha Huduma ya Kikristo ya Haki za Binadamu kimeeleza kwamba muda wowote kuanzia Aprili 21, askari wa kutuliza ghasia (F.F.U) watatumika kuutwaa Msikiti wa Masjid Mwinyi ambao Bw. Daniel Zakaria anadai kwamba ni nyumba yake ya urithi.
Akiongea na gazeti hili kwa njia ya simu juzi, Mchungaji Elias Kibela alisema kwamba waumini wa Masjid Mwinyi wamepewa siku 21 toka Aprili 21 kuhama Msikiti huo vinginevyo wamlipe Bw. Daniel shilingi milioni 20 au wamtafutie nyumba nyingine nzuri ya vyumba sita katika eneo la Ilala au Kariakoo.
Mchungaji Elias ambaye amejitaja kama Afisa Mahusiano wa The Liberty Desk ya Mchungaji Mtikila amelifahamisha gazeti hili kwamba endapo masharti hayo hayakutekelezwa F.F.U watatumika kuwatimua waumini ndani ya Msikiti na kuurejesha Msikiti huo kuwa nyumba binafsi ya Bw. Daniel.
Nakala ya Ilani ya kuwataka waumini wa Masjid Mwinyi uliopo Ilala zimetumwa kwa Wizara ya Sheria (Administrator General); Mawakili wa South Law Chambers (Advocates) na Afisa Ardhi Kanda ya Ilala.
Alipohojiwa juu ya uhalali wa madai ya Bw. Daniel kuwa Msikiti huo ni nyumba yake; Mchungaji Elias alieleza kwamba zipo nyaraka za kuthibitisha madai hayo.
Akifafanua alieleza kwamba Bw. Daniel ana nyaraka zinazothibitisha kwamba nyumba hiyo ilikuwa mali ya Hajat Aziza Omar ambapo Bw. Daniel alirithishwa na mahakama.
Mchungaji Elias alipoulizwa haoni kwamba kitengo chake kikiwa cha kidini kutumika katika suala hili kutaleta mapambano baina ya waumini wa Kiislamu na Kikristo. Alidai kwamba hilo haliwezi kutokea kwani wao wanamsaidia Bw. Daniel kama Kitengo cha kupigania haki za kibinadamu.
Msikiti wa Masjid Mwinyi, nyumba Na. 58 iliyopo mtaa wa Somali na nyumba Na. 59 iliyoko mtaa wa Mchikichi awali zilikuwa miongoni mwa nyumba za Hajat Aziza Omar ambaye kabla ya kufa alizitoa Wakfu nyumba hizo.
Hata hivyo, katika mazingira yasiyoeleweka mahakama ya Kisutu ilimpa Bw. Daniel usimamizi wa nyumba hizo ambapo amezifanya ni zake.
Katika siku za hivi karibuni pamoja na kudai kwamba ana haki zote za kimahakama kumiliki nyumba hizo, Bw. Daniel amemualika Mchungaji Mtikila amsaidie kuzitwaa nyumbaa hizo. Katika hatua ya awali Mchungaji Mtikila aliripotiwa na vyombo vya habari akidai kwamba moja ya nyumba hizo za Wakfu ni Kanisa lake.
|
|