Maoni yetu
 
Serikali ijisafishe
Isiwakumbatie wauaji
 
  KUMEKUWA na kauli za kuwataka Watanzania kudumisha amani ili kuepuka mauaji kwa misingi ya kidini

Balozi wa Rwanda nchini Bibi Joy Mukanyange ameripotiwa na vyombo vya habari akiionya Tanzania kuwa inaweza kujikuta katika lindi la mauaji ya halaiki, iwapo haitakuwa makini katika kudhibiti mgawanyiko wa kidini.

Bibi Joy Mukanyange alizishutumu Ubelgiji na Ufaransa kwamba ndizo zilizosababisha mgawanyiko katika Watutsi na Wahutu ambapo Watutsi

walionekana wageni na Wahutu wakifanywa waamini kuwa Watutsi hawakuwa na haki katika nchi hiyo na kwamba hawakustahili kuongoza nchi.

Je, kuwaruhusu watawa wa Kikatoliki wanafunzi kuvaa sare zao za kitawa na kuzuia hijabu nini tunajenga; je, kuruhusu Wakristo wasali siku mbili Jumamosi na Jumapili na kuwanyima wanafunzi Waislamu masaa mawili ya kuswali Ijumaa ni kustawisha nini baina ya Waislamu na Wakristo!

Kudaka uchochezi wa Wakristo hadi ukaua Waislamu na ukakataa kuwafikisha mahakamani wachochezi na wauaji kinyume chake ukaendelea kuwasaka na kuwatisha Waislamu wadhulumiwa; unataka Wakristo wajihisi vipi na kuwadhaniaje Waislamu!

Nafasi zote muhimu serikalini zinapokuwa milki ya watu wa dini moja, kipi kinastawishwa? Ni umoja au mbegu ya uhasama.

Nasaha kama hizi zimetolewa pia na Bw. Walted Bugoya akisisitiza kwamba Tanzania ijifunze toka Rwanda.

Jambo ambalo tungependa kusisitiza hapa ni kwamba amani na dhulma havitangamani. Dhulma haiondoki kwa propaganda na wala amani haidumishwi kwa kukandamizwa madai ya wadhulumiwa.

Mara nyingi wanasiasa na vyombo vya habari wamekuwa wakizungumzia hatari ya chuki za kikabila na kidini katika jamii. Na katika kusherehesha wamekuwa wakitoa mifano ya yale yanayotokea Rwanda, Burundi, Lebanon, Palestina n.k. Lakini ajabu ya mambo asili ya chuki hizo haielezwi na lipi lingetakiwa lifanyike; kinyume chake mifano hiyo hutumika kama propaganda ya kuwatisha watu na kuzima madai ya wale wanaodai kudhulumiwa.

Katika Tanzania lipo kundi kubwa la raia Waislamu linalodai tena kwa muda mrefu kuwa katika nchi yetu ipo dhulma ya wazi dhidi ya Waislamu. Kauli hizo zimefika hadi Bungeni. Badala ya kufanya juhudi za kweli za kuyatafiti madai hayo ili kuondoa dhulma, kumekuwa na juhudi za kuwakejeli wanaoonesha dhulma.

Kwa mfano katika tukio la hivi sasa agenda imehamishwa wanadaiwa Waislamu kuleta uchochezi; kuleta vurugu, kuhatarisha amani, kutumiwa na wanasiasa n.k. Wakati wao ndio walioshambuliwa Msikitini kwao na kuuliwa.

Kila mtu yuajua kwamba mauaji ya Mwembechai yalikuwa kilele cha fitna iliyoibuliwa na Paroko wa Kanisa Katoliki; Paroko Camilius Lwambano na kusambazwa na Radio ya Kanisa hilo hilo.

Kwa bahati mbaya viongozi wa serikali nao walizipokea taarifa hizo za fitna na uchochezi na kuzifanyia kazi ambapo matokeo yake ni kuuliwa watu.

Haikutosha chama tawala CCM na serikali yake kujipongeza baada ya hatua hiyo, lakini fitna ikarejea kule kule ilipoibukia. Kiongozi Mkuu kabisa wa Kanisa Katoliki nchini akaunga mkono mauaji hayo.

Shirika la Habari la B.B.C. Jumanne Aprili 6, 1999 asubuhi (B.B.C. World Service) lilielezea taarifa ya shirika moja la Haki za Binadamu juu ya Mauaji ya Rwanda. Taarifa hiyo imeonyesha mchango wa Kanisa Katoliki katika mauaji na jinsi baadhi ya Maaskofu walivyohusika.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kiongozi mmoja wa Kanisa Katoliki aliyehusika sana na mauaji ya kuangamiza huko Rwanda amehamishwa na kufichwa huko Paris.

Taarifa ya shirika hilo la Haki za Binadamu ikasema kwamba huko ni kuwalinda wauaji na kulivunjia heshima Kanisa Katoliki na kulitaka lijisafishe angalau kwa kuwatoa wauaji washitakiwe.

Waislamu tuna uchungu na nchi yetu; tunaipenda na tunatamani idumu katika hali ya amani na utulivu. Waislamu tunathamini uhai, heshima na haki ya kila Mtanzania na kila binadamu. Lakini tunajua vile vile kwamba penye dhulma amani haidumu. Amani haiwezi kudumishwa kwa kuwalinda wachochezi na wauwaji huku shutuma kubwa ikielekezwa kwa wadhulumiwa.

Tunatamani kudumu na Tanzania yetu yenye amani na utulivu ambapo kila raia anapata haki yake na haonewi kwa namna yoyote ile. Ni kwa ajili hiyo basi tunaisihi serikali ijisafishe angalau kwa kuwatoa wauaji washitakiwe.

Kauli za kuhimiza amani, amani na kuwatisha watu na matukio ya Rwanda hayatusaidii na pengine zimepitwa na wakati. Litakalotusaidia ni kuyafanyia kazi yale ya Waraka wa Abu Aziz, Waraka wa Ponda, Kamati ya kupigania haki za Waislamu, Kamati ya akina mama na yale aliyozungumza Mh. Kitwana Kondo Bungeni.

Kuwaita Waislamu wachochezi kwa kudai hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wauaji ni kuiweka rehani amani ya nchi yetu. Amani ya kweli ni ile yenye haki kwa wote. Tusiwe weledi wa kutoa mifano ya Rwanda, Burundi, Lebanon na sasa Indonesia huku tunaendekeza yaleyale yaliyozitosa nchi hizo katika janga.

Hofu ya kupungukiwa na manufaa yanayotokana na kuhodhi nafasi zinazowapa fursa baadhi ya watu kufanya wawezavyo dhidi ya Waislamu isituangamizie nchi. Wala isidhaniwe yupo Mtanzania wa kukubali kuendelea kuona anadhulumiwa na kuonewa daima dumu. Vinginevyo tusingekuwa na akina Mkwawa, Mirambo, Chifu Kimweri, Mashujaa wa Majimaji n.k.

Tuitambue haki, tuitende na kuidumisha kwa wote ili tudumishe amani. Sote tupo ndani ya jahazi moja; tusipomkemea anayetaka kulitoboa tutaangamia sote. Ni jukumu letu sote wananchi kuikemea dhulma na kuhimiza haki na uadilifu. Na kwa muktadha huu kama Kanisa Katoliki lilivyopewa nasaha kuwa liwatoe washiriki wa mauaji ya Rwanda washitakiwe, tunainasihi serikali yetu tukufu iwafikishe mahakamani walioitikia na kutoa amri ya "Piga shaba", "piga yule".

Juu RUDI

Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook