Na Mwandishi Wetu
CCM haina dira wala sera inayoeleweka kuweza kuwaletea maendeleo Watanzania na haina sera ya kuwanusurisha wananchi na hali ngumu inayowakabili.
Hayo yamesemwa na Prof. Ibrahimu Lipumba wakati akihutubia mkutano wa hadhara Mbagala Zakheem wilayani Temeke hivi karibuni.
Mkutano huo wa hadhara ulifuatia ziara ya Profesa huyo ambaye ni Mshauri Mkuu wa CUF kutembelea matawi ya chama hicho Jumatatu wiki hii.
Prof. Lipumba aliuambia umati uliokuwa ukimsikiliza kuwa nchi haiwezi kupata maendeleo bila ya kuwepo sera zenye kueleweka.
Aliwakumbusha wananchi hao kuwa chama chake kilishaeleza huko nyuma kuwa kuirejesha CCM madarakani ni kuendelea na dhiki kwani alidai kuwa chama hicho hakina sera ya kuwaletea maendeleo.
"Mwaka 1995 tulieleza kuwa mkichagua CCM mnachagua dhiki; dhiki itaongezeka, sasa mnayaona?", Prof. Lipumba aliuliza umati huo na kuitikiwa ndiyoo!!
Alisema hakuna sababu ya msingi mji kama Dar es Salaam wakazi wake wawe katika maisha ya dhiki ilhali wamezungukwa na jiografia nzuri.
Alisema pamoja na kwamba Mwenyezi Mungu amejaalia ardhi kubwa lakini CCM imeshindwa kutumia wasaa huo kuwaondolea wananchi njaa na hali ngumu.
Jiji la Dar es Salaam alitoa mfano Prof. Lipumba, lina bandari, uwanja wa ndege wa Kimataifa, vituo vya reli viwili vikubwa vinavyounganisha Tanzania na nchi za jirani pia umezungukwa na mkoa wa Pwani ambao una ardhi asilimia 20 tu inayotumika.
"Lakini serikali ya CCM imeshindwa kutumia jiografia hii kuendeleza hali za maisha ya wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam", alisema huku akishangiliwa kwa makofi na wakazi wa Mbagala.
Aidha, aliongeza kusema kuwa CCM kwa miaka kadhaa sasa imeshindwa kueleza ukweli kama zipo jitihada inazochukua katika kurekebisha hali ya nchi kiuchumi.
Prof. Lipumba aliwaeleza wananchi wa Mbagala kuwa kama zingalikuwepo jitihada zozote makini wangeshuhudia kwa macho yao badala ya kuelezwa na viongozi kupitia vyombo vya habari.
"Miundo mbinu imeharibika, hali ya barabara madimbwi kila mahali, mnaelewa wazi mbu wanavyozaliana katika madimbwi, kipindupindu, vijana hawana kazi, tazama masoko yalivyo machafu", alisema Prof. Lipumba katika hotuba iliyoonekana kumgusa kila aliyehudhuria mahali hapo.
Alizitaja baadhi ya njia zinazoweza kusaidia kurekebisha Jiji la Dar es Salam na kusema kwamba vyombo vya fedha kama vile mabenki ingetumika vyema na serikali ingeweza kumaliza tatizo hilo.
Alisema pamoja na kuweza kutengeneza mabarabara pia ingepelekea kupatikana ajira kwa vijana na mji kuwa msafi zaidi.
"Unapoongeza ajira unaongeza uwezo wa kununua bidhaa za watu wengine wanaozitengeneza", alisisitiza Prof. Lipumba.
Alitoa mfano wa Jiji la New York, kwa kueleza jinsi linavyotumia dhamana ya Jiji kwenye mabenki kuhakikisha barabara zinakuwa katika hali ya usafi na upatikanaji wa maji mzuri kuwawezesha wawekezaji kuwekeza vizuri.
"Tujifunze namna mji unavyoweza kutumia vyombo vya fedha kuwekeza katika kuhakikisha miundo mbinu imara, Prof. Lipumba aliwaeleza wananchi hao sambamba na kuishauri serikali iliyopo madarakani.
Kuhusiana na tatizo la maji Dar es Salaam, Prof. Lipumba alisema hivi karibuni alialikwa nchini Namibia ambako alisema mji mkuu wa nchi hiyo (Windhoek) ni jangwa na maji hupatikana kilomita zaidi ya mia moja, hata hivyo alisema jiji hilo halina tatizo la maji kutokana na mipango kamambe ya serikali ya huko.
"Dar es Salaam sio jangwa lakini maji hayapatikani miaka 40 baada ya uhuru, hatuna sababu ya kukosa maji wakati tukiingia karne ya 21", alisisitiza prof. Lipumba.
Katika hotuba yake hiyo iliyochukua takriban dakika 45 alizungmzia pia haki ya kuchagua madiwani badala ya Jiji kuongozwa na Tume, tatizo la rushwa na namna ambavyo kodi inayo kusanywa na serikali hivi sasa ingetumika.
Kuhusu tatizo la Rushwa nchini alisema limekuwa kubwa kiasi kwamba kitengo cha kimataifa kiitwacho transparency international katika orodha yake ya mwaka 98 kimeiorodhesha Tanzania kuwemo katika nchi zinazoongoza kwa rushwa duniani.
Alisema serikali haiwezi kudai kupambana na rushwa huku yenyewe ikifungulia mianya ya rushwa.
"Tatizo la rushwa kubwa kubwa ni kukosa sera ya uwazi ya uchumi", alisema Prof Lipumba.
Alitoa mifano kadhaa kuonyesha kwamba utoaji na upokeaji wa rushwa nchini kwa kiasi kikubwa husababishwa na serikali yenyewe.
"Mkuu wa mkoa anasema kwamba wafanya biashara ambao hawatapanda miti hawatapewa leseni, huko ni kufungulia mifereji ya rushwa", alisema Profesa Lipumba.
Aidha alitilia mkazo suala la upandaji
wa miti kwa kusema kwamba wananchi wahamasishwe kupanda miti, lakini uhamasishaji
usiunganishe leseni za biashara na upandaji wa miti kwani hayo ni mambo
mawili tofauti ambayo yakiunganishwa huanzisha mifereji ya rushwa.
|
|