Na Abu Halima Sa Changwa
KATIKA jamaii yoyote ile ya kitwaghuti, kwa vile msingi mkuu wa maisha ni kujilimbikizia vitu vya kuifaidia dunia, kila mmoja hutaka kuota mbawa na kuwa juu zaidi ya wengine. Jamii inakuwa katika mashindano ya kihali, kila mtu, kila familia na kila kundi linataka kuwa na hali nzuri zaidi ya jingine. Hapa ndipo inazaliwa hali ya watu kutaka kujikweza. Kukosa kitu fulani kinachothaminiwa na jamii kunakuwa ni fedheha. Hali hii huwafanya watu wapate hiki kichaa cha kujikweza, waonekane wao ni bora zaidi kuliko wengine, na kwamba wao ndio wanaostahili kushika hatamu kuliko wengine, na kwamba wao ndio wanaostahili kuwa mabwana, na wengine wote wawe watwana, na mwishowe kuna vitu au mambo wanastahili kuwa nao wao tu, lakini binadamu wengine hawastahili. Kichaa hiki kimo katika jamii zetu leo.
Makundi ya watu mbalimbali yameathirika na kichaa hiki. Kuna makundi ya watu ambayo yamekuwa yakinyimwa hadhi sawa na makundi mengine yamepewa jina la Minorities (vikundi vya watu wa hadhi ya chini). Ubaguzi wa aina hii umekuwa ukilengwa katika nyanja za rangi za watu (racial minorities) na nyanja za asili ya watu kwa lugha zao, dini zao, utaifa, ulaji wao au historia yao (ethnic minorities).
Mara nyingi vichaa wa kujikweza huwa wameshika madaraka na wao ndio wanaamua hadhi ya kuwa binadamu wengine, hususan katika huduma za jamii, uwakilishi madarakani, na hata mahusiano ya watu binafsi kimaongezi, yaani mmoja lazima awe na hadhi ya chini ya kuitikia "hewala bwana" na mwingine awe na hadhi ya kuamuru tu kwa kunyooshea kidole, wengine watende.
Jamii ya wenye vichaa vya kujikweza huwa ina maradhi ya kiakili yaitwayo Prejudice, maradhi ya kuwaona wengine si kitu katika lolote lile, na hawastahili kupewa hadhi kama walio nayo wao katika nyanja yoyote ya kiheshima, isipokuwa mambo ya kawaida tu na ya hovyo hovyo.
Jamii ya watu waliopewa jina la minorities nayo huwa na watu wengi wasio na uoni mzuri, ambao hukubali hadhi walio nayo na wakaona kuwa wanastahili kuwa hivyo, au wengi huwa kisaikolojia wameathirika na falsafa ya "kuzabwa kofi shavu la kulia na kugeuza la kushoto", wakiamini kuwa huo ndio utiifu na utu, na ndio kudumisha "amani".
Mara nyingi jamii ya wabaguliwa Minorities hupata madhara mbalimbali kutoka kwa vichaa wa kujikweza. Kwa mfano wabaguliwa huwa ni scapegoats, yaani watu wanaoangukiwa na hasira za vichaa wa kujikweza, hasa watu vichaa hawa wanaposhindwa na mambo fulani (Hii niliielezea katika toleo lililopita kama displaced aggression).
Zahma kubwa inayowaangukia wabaguliwa kutoka kwa vichaa wa kujikweza waliobahatika kukwapua madaraka ni kile kinachoitwa Stereotyping. Hii ni tabia ya watu kuwapachika sifa watu wa kundi jingine, hususan sifa mbaya na halafu kuchukulia kwamba kila mtu wa kundi hilo ana sifa hiyo. Mifano ya Stereotyping ni kama ile tuliozoea kuisikia, kwamba Wachagga wanapenda sana pesa, Wapare ni mabahili, Wagogo ni ombaomba n.k. na sifa hizi akapewa kila mtu wa kabila hilo.
Mara nyingine stereotyping inaweza kuwa na ukweli kiasi fulani, lakini vichaa wa kujikweza huikuza, huipotosha au huitumia mahala pasipostahili.
Katika jamii zetu, Waislamu walio wengi wamekumbwa na mtihani wa kuishi ndani ya jamii ya kitwaghuti ambazo zimeshikwa kimadaraka na vichaa wa kujikweza. Waislamu wamekuwa wakihesabiwa kama minorities. Mara wamekuwa ni scapegoats, na kubwa zaidi linalohalalisha kubaguliwa kwao na kuteswa kwao na kuuawa kwao ni stereotyping. Hapa Waislamu wamepewa sifa ya uvivu wa kupenda pilau tu na kukaa kwenye vibaraza vya bao na kahawa (umwinyi), kutokuthamini elimu, kutokuelimika na mambo ya dunia, ushirikina wa majini na uganga wa kienyeji, Uswahili (yaani kutokuwa na mipangilio ya kimaisha, kutojali muda na kuwa hohehahe) n.k. Sifa hizi zimewapa mwanya vichaa wa kujikweza kuhalalisha ubaguzi wa Waislamu kwenye elimu, utendaji wa kiutawala na hata madaraka. Kazi za Waislamu za heshima, angalau zikawa ni za balozi nyumba kumi, wazee wa vyama vya siasa, pamoa na labda ukuu wa mabaraza ya michezo.
Stereotyping nyingine mbaya zaidi inayohalalisha kufungwa hovyo na kuuawa Waislamu ni ile ya kuwagawanya Waislamu katika makundi mawili: Siasa poa na siasa kali. Wale wanaokubaliana na sera za vichaa wa kujikweza hata kama zinaenda dhidi ya Waislamu ndio wanaitwa Waislamu safi, na futari wanaandaliwa na wakubwa. Ama wale wanaoutangaza au kujaribu kuufuata Uislamu kama unavyoelezwa kwenye Qur'an na maelezo ya Mtume (s.a.w.) hawa huwa wanahatarisha amani ya vichaa wa kujikweza, na hivyo hufukuzwa Misikitini, hukamatwa na kutiwa jela, na pia huuawa na haya hutokea baada ya stereotyping kufanya kazi.
Hali hii ya Waislamu sasa hivi dunia nzima. Historia inaonyesha kwamba ukiona vichaa wa kujikweza wanafunga watu zaidi, wanatesa watu zaidi, na wanaua watu zaidi, basi ujue shughuli imeanza na wabaguliwa wameshaanza kukataa kuzabwa kofi shavu la kushoto na kugeza la kulia.
Hali ilikuwa hivyo hivyo kwa weusi wa Marekani, hivyo hivyo kwa Waafrika wa Afrika ya Kusini, hivyo hivyo kwa Waislamu wa Sudan, hivyo hivyo kwa Waislamu wa Bosnia, na hivyo hivyo kwa...
Matokeo yake ni kutimia kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwainua wanaodhoofidhwa katika ardhi:
|
|