KAMATI YA KUPIGANIA HAKI ZA WAISLAMU
TANZANIA
S.L.P. 2055, DAR ES SALAAM
Machi 30, 1999
Kwa;
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania,
Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Yah: KAMPENI YA KUMSAKA SHEIKH PONDA NA KUWALINDA WAUWAJI WA RAIA
MARA baada ya mauaji ya kikatili yaliyofanywa na askari polisi katika Msikiti wa Mwembechai Machi 1998, na hasa katika siku za hivi karibuni serikali imekuwa ikiendesha kampeni kubwa ya kumsaka Sheikh Ponda Issa Ponda na kuwahimiza raia wasaidie kana kwamba Sheikh Ponda ni mhaini, jambazi sugu au mhalifu mzoefu. Waislamu wanazitafsiri kampeni hizi kama ni ishara ya wazi kuwa serikali hii ina chuki na uhasama na raia ambao ni Waislamu. Siku ya Jumapili ya tarehe 28 Machi, 1999 kwa mfano, serikali ilisambaza maaskari wengi sana wenye silaha katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam katika harakati za kumsaka Sheikh Ponda.
Serikali inatumia gharama kubwa kuendesha kampeni hiyo dhidi ya Sheikh Ponda hali ya kuwa inawajua na kuwalinda watu waliochochea na kushiriki katika mauaji ya raia pale Mwembechai. Ni Paroko Lwambano wa Kanisa Katoliki Mburahati ndiye aliyetoa taarifa za uzushi na za kiuchochezi. Na Radio Tumaini inayomilikiwa na Kanisa Katoliki ndiyo iliyozirudiarudia na kuzisambaza taarifa hizo za kichochezi bila ya kuzichuja kwanza. Ni Mheshimiwa Yusuf Makamba, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliyechukua ahadi ya kuwashughulikia Waislamu kwa kutegemea kauli zile za uzushi.
Mkanda wa video ya mauaji hayo unaonesha sura za wauaji hao upo na umesambaa ulimwengu mzima. Lakini badala ya kusakwa wauaji hao ambao wanajulikana, leo serikali inamsaka Sheikh Ponda. Sheikh Ponda baada ya mauaji ya Mwembechai alifanya mambo matatu: Kwanza alishiriki katika kusafisha damu na najisi nyingine katika Msikiti ule kufuatia uvamizi na uharibifu wa polisi. Pili, alikutana na waandishi wa habari na kuwaonesha vifaa vya ujenzi ambavyo awali Mheshimiwa Makamba alidai ni "silaha" zilizokuwa Msikitini. Na la tatu alilolifanya ni kusaini waraka ulioelezea chanzo cha mauaji ya Mwembechai.
Mheshimiwa Rais, tunachukua fursa hii kutanabahisha kuwa kampeni zinazoendeshwa hivi sasa kwa vishindo dhidi ya Sheikh Ponda zinatishia kuchochea ghasia kubwa za kidini nchini iwapo serikali inayowalinda wauaji itamkamata Sheikh Ponda. Inasikitisha sana Sheikh Ponda anasakwa na kusakamwa baada ya ahadi nzuri ulizotoa Mheshimiwa Rais kuwa serikali itafanya uchunguzi na kuwachukulia hatua wauaji. Amani katika nchi hii itapatikana kwa kuwatendea haki raia wote. Zoezi la hivi sasa la kuwanyanyasa Waislamu na kuwalinda wanaowaua au kuwadhalilisha Waislamu huenda likaitumbukiza nchi hii katika mauaji ya kutisha. Tumetimiza wajibu wetu kwa "Kutahadharisha" juu ya tishio la maafa linaloikabili nchi yetu. Kinachobakia ni uamuzi wa serikali. Ama kuendelea na kiini macho cha kumsaka mtu asiye na hatia yoyote au kuukabili ukweli na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliohusika na mauaji ya mwembechai.
Pamoja na barua hii tumeambatanisha nakala ya mkanda wa video unaoonesha mauaji ya kinyama yaliyofanywa na askari polisi Februari, 1998 na yenye mazungumzo ya Ponda na waandishi wa habari.
Kaimu Katibu,
A. Ahmad
Nakala kwa:
Waheshimiwa Wabunge,
Usalama wa Taifa,
Vyama vya siasa,
Jumuiya ya Wanasheria Tanganyika,
Jumuiya ya Wanataaluma Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam,
Vyombo vya habari,
|
|