DODOSO LA KUTAFAKARI
 
‘Utamaduni wa kuku’
Chambua habari kabla ya kuikubali, acha kuropoka
 

Na Kipondo wa Changarawe

NI makosa makubwa kwa mtu mwenye mwongozo wa Qur’an akawa anakokotwa kibubusa na kuzitekeleza sera za watu wanaotazama maisha kwa jicho moja la kushoto. Ni makosa kwa Muislamu akiwa analishwa maneno na kutumika kama kipaza sauti cha matwaghuti; akageuzwa kuwa ‘kasuku’ mwenye kamba na kucheza ngoma asizozijua. Ni vibaya na makosa makubwa Muislamu kutekwa nyara na kufanywa kuwa chanzo cha habari, akawachoma nduguze hali ya kuwa yeye bado anaonekana kuwa ni adui, wa adui.

Ulimwengu tunao kwenda nao umekamatwa na watu wenye siasa na sera za nguvu mali; asilimia kubwa ya vyombo vya habari viko kwenye mikono ya watu ambao wana mtazamo butu kuhusu maisha haya ya mpito ya kidunia.

Mnakumbuka kuwa katika tafakari ya dodoso letu lenye anuani ya "Cheo kilichotelekezwa", tuliangalia kwa pamoja msingi utumikao kuwaandaa ambao wamekuwa ndiyo kitovu cha mkorogeko wa amani katika uso wa dunia na kutokomea kwa uadilifu katika maisha ya jamii. Pia tuliangalia namna mwongozo wa Qur’an unavyowaandaa viongozi wenye huruma, wakweli, waaminifu, waadilifu ambao hutaabika kwa kufanya kazi kwa manufaa ya jamii. Nikasema kuwa Muttaq ni mtu mwenye dhima ya kuhakikisha kuwa haki na uadilifu vinatawala maisha ya jamii.

Uharibifu mkubwa unafanywa duniani bila ya kukutana na pingamizi lililo la kweli wala kuwaokoa wanaoathiriwa na kudhulumiwa kutokana na ukweli usiopingika kwamba Waislamu tumeuweka uchagoni mwongozo wetu Qur’an; unaendelea kufunikwa na mavumbi wakati sisi tunapapatikia kujitia utumwani kwa hiari na kufuata mifumo ya maisha ya kubuni tukidhani kuwa ndiyo itakayoinua hadhi na utu wetu.

Vipi Bwana Kipondo, mbona dodoso limeanza kwa maneno makavu mno hali ambayo inafanya maandishi yaonekane kama mekundu? Na huu utamaduni wa kuku unaiwakilisha dhana gani hasa? Uhalisia wake uko vipi katika maisha yetu ya kila siku na itatufikishaje mpaka tujikwamue na haya makosa uliyoyataja?

Kwa kweli nimekasirika mno! Ndiyo sababu iliyonifanya nililete dodoso katika staili ya sura ya tisa, Surat Tawbah. Inakasirisha kuona tunaswali mara tano kwa siku, tunafunga, tunafunga safari kwenda kuhiji; tunasoma Qur’an katika khitma, kwenye maulid na kufanya mashindano ya kuhifadhi Kitaj-wid na Mughna lakini bado tunainamisha vichwa mbele ya matwaghuti na kuramba viatu vyao.

Inakuwaje twaghut akatuvishe kitambaa usoni akawa anatukokota na kutugeuza geuza anakotaka na anavyotaka? Iweje kila anachotuamuru tunakiona kuwa ni sahihi na kuitekeleza kila sera anayotuletea? Tumekuwa ‘mandondocha’ kiasi gani!? Ni ipi basi hekma ya Qur’an kufanywa kuwa mwongozo na kipambanuzi?

Utamaduni wa kuku ni anuani inayowakilisha utaratibu wa kuzichambua kwa kina habari zozote unazozipata kutoka kwa mtu binafsi, kikundi cha watu na vyombo vya habari, kabla ya kuzisadikisha na kuziweka kwenye utendaji. Kwa upande mwingine, utamaduni wa kuku unawakilisha utaratibu wa kuyachambua masuala mbalimbali kabla ya kuyasambaza katika jamii.

Habari yoyote inayokufikia, hakikisha kuwa unaiandama kwa kuiulizia maswali na ukichambua kabla ya kuikubali na kuifanyia kazi. Unaweza ukanishangaza ukaniuliza kuwa habari utaiulizaje maswali.

Ngoja nikupasulie kwa kukupa mfano: Umebahatika kuokota kipande cha gazeti kilichoandikwa hivi: "Mwanafunzi Chuki Athumani amepigwa risasi na polisi pale Mwembechai kwa sababu amekutwa na makaratasi ya uchochezi". Jalia kwamba wewe ni mtu wa kawaida kama mimi Kipondo ambaye huna fursa ya kukutana na aliyesema wala aliyeandika. Utamwuliza nani?

Kilichobakia ni kuikomalia habari yenyewe kwa kuiuliza maswali na kuichanganua ili uibuke na ukweli wake au upogo wake. Na hii ndiyo njia rahisi zaidi. Hebu tuanze kwa pamoja:

Hivi hawa mapolisi walijuaje kwamba Chuki Athumani alikuwa na makaratasi ya uchochezi? Walimwona kwa mbali akiwagawia watu makaratasi pale Mwembechai, wakajua kuwa ni ya hatari, hivyo wakamuwahi kumpiga risasi? Aliwagawia mapolisi na kuanza kukimbia hivyo wakamtwanga risasi ili wamkamate baada ya kugundua kuwa makaratasi ni ya uchochezi? Je, walimuwasha risasi kwanza na baadaye wakamsachi na kumkuta na makaratasi hayo?

Ukiiandama habari kwa maswali namna hii na kuanza kuchanganua kwa tafakari, utagundua upogo uliopo ndani ya habari, hivyo hutafanya kosa la kuungana na upande wa propaganda. Daima iulize mswali habari kabla ya kuisadiki na kuitekeleza.

Vile vile usiwe mkarimu sana wa kumwaga kila habari ya mipango, mikakati pamoja na harakati bila ya kuzingatia aina ya mtu, kiwango chake cha kuelewa uzito wa mambo, uwezo wa kuhimili vishindo na tabia yake ya kuzungumza. Lazima uzingatie kuwa ni habari gani, apewe nani, wakati gani na katika mahali gani, na kwa nini.

Kuna watu wengine hawatulii mpaka waseme hata kama hajaulizwa, anaposema huwa hachagui wala haangalii yupo kwenye mazingira gani, anazungumza na nani. Wengine wakiulizwa jambo moja ataeleza mambo chungu nzima.

Unapaswa kuzingatia kuwa si wakati wote unatakiwa useme, si kila swali unapaswa kujibu au kutoa jibu linalostahiki. Kwa sababu kuna watu wa ‘kanzu’ wafanyao kazi kwa maelekezo ya wale wenye sera ya nguvu mali.

Kuna mwenzangu mmoja alikuwa na tabia iliyonikera sana. Alikuwa anapenda kunitambulisha kwa kila mtu kuwa: "Huyu ndiye Kipondo". Wakati mwingine niko katikati ya kundi la watu asiowafahamu, anakurupuka kunitolea salamu na kutaka tushikane mikono au ananiita kwa jina langu. Kwani ni makosa kufanya hivyo? Hapana! Lakini yazingatiwe mazingira. Kuna watu wana ajira ya kuwapelemba wale wanaoaimsha jamii na kutetea haki. Nikimwambia. "Shika mwenendo wa kati na kati!" Akanielewa na akabadili tabia yake.

Tunatakiwa tuwe wakarimu sana, lakini ukarimu wa kusema kila jambo ni hatari. Vivyo hivyo ukarimu wa kuchemka ni hatari mno! Inakuwaje nduguyo unaesali naye kila siku humkirimu na kumsaidia kama utakavyomsaidia mtu aliyesilimu? Unamkaribisha mazingira yako ya ndani kabisa. Inatakiwa tuwatahini kwanza ili tuwatambue kabla hatujawakumbatia. Utamaduni wa kuku ni muhimu sana kuzingatia katika mazingira tunayo kwenda nayo.

Habari ni muhimu mno katika maisha, lakini tunapaswa kutambua kuwa kuna mitandao inayomilikiwa na madhalimu ambayo kazi yake ni kuzisuka habari katika mlengo wanaoutaka wao na kuziingiza vichwani mwa watu ili waelewe na kutenda kama walivyopangiwa. Mitandao mingine kazi yake ni kupotosha ukweli wa matukio mbali ya dhulma zinazofanywa na wababe. Huwapachika majina mabaya wale wanaodhulumiwa na kumpaka matope kila atakayejitokeza kutaka kuwatetea.

Angalia unyama na dhuluma uliofanywa na jeshi la polisi wa serikali ya chama tawala katika sakata ya Mwembechai dhidi ya wasiokuwa na hatia.

Angalia jinsi walivyoandamwa wale waliojitokeza kuikemea dhuluma hiyo na kuitaka serikali iwachukulie hatua za kisheria wale wote waliohusika katika kuidhinisha mauaji ya raia wasiokuwa na silaha.

Wakati tunakaribia kulifunga dodoso letu, ni vyema tukakumbuka kuwa ni muhimu kuiuliza maswali habari na kuichanganua kabla ya kuisadikisha na kuifanyia kazi. Usiwe mkarimu wa kutoa habari bila kumzingatia unayempa, wakati, mazingira pamoja na habari yenyewe. Ukarimu wa kuchemka ujiepushe nao.

Ni wakati muafaka sasa wa kulifunga dodoso kwa kuzitafakari, kuzikariri na kuzihifadhi aya zinazotufunza utamaduni wa kuku:

"Enyi mlioamini! Kama fasiki akikujieni na habari, ipelelezeni, msije mkawadhuru watu kwa ujinga na mkawa wenye kujuta juu ya yale mliyoyatenda". (49:6)

"Basi hakukaa sana mara (Hud-Hud) akasema: Nimegundua usilogundua, na ninakujia hivi kutoka Sabaa na habari zenye yakini. Hakika nimemkuta mwanamke anawatawalia; naye amepewa kila kitu na anacho kiti cha enzi kikubwa..." Akasema (Suleiman) :Tutatazama kama umesema kweli au umo katika waongo". (27:20-27)

"Basi mtumeni mmoja wenu na fedha yenu hii mjini na atazame chakula kipi ni tahara akuleteeni katika hicho. Na afanye mambo haya kwa busara wala asikutajeni kabisa kwa yeyote. Kwani wao wakikujueni watakupigeni mawe au watakurudisheni katika dini yao; na hapo hamtafaulu abadan". (18:19-20).

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook