Na Maalim Bassaleh
KAMA kuna wakati ambao umoja baina yao basi hakuna wakati muafaka kama huu tulio nao. Lakini kutafuta njia za kutufikisha katika umoja huo, sisi tumekuwa tukijishughulisha zaidi na mambo madogo madogo yenye ikhitilafu baina yetu, ambayo hayana faida yoyote kwetu, isipokuwa kutuongezea uhasama na utengano.
Sala ya Idi ni Sunna lakini umoja wa Waislamu ni wajibu. Sisi tumeacha kulishughulikia lile jambo la wajibu, ambalo ni umoja wa Waislamu na tumeamua kutowafikiana katika kusali sala ya Idi siku moja bila ya kuwa na sababu yoyote ya msingi.
Maswali ya lini tuanze kufunga Ramadhani na lini kufungua pamoja na swali la saumu ya Arafa yameleta ikhtilafu kubwa baina ya wanazuoni wetu. Kundi moja linadai kwa kuwa dunia ni moja na mwezi ni mmoja, basi mwezi ukiandama katika nchi yoyote ulimwenguni inabidi nchi nyingine zote zifuate. Kundi la pili linasema hatulazimiki kufunga kwa ajili ya kuandama mwezi bali kwa kuuona mwezi. Kundi hili linategemea sana kile kisa mashuhuri cha Kurayb, kilichotajwa katika Sahih Muslim, kinachoelezea kuwa Ibn Abbas (R.A.) alikataa mwezi ulioandama Sham. Wafuasi wa kundi hili wanasema kila nchi itafuata kuandamana kwa mwezi katika nchi inayohusika.
Aidha, katika swali la saumu ya Arafa, kundi la kwanza linaona saumu hiyo inatokana na kisimamo wanachosimama mahujaji katika viwanja vya Arafat huko Makka, kwa hvyo inawalazimu watu wa nchi zote ulimwenguni kufuata Arafa ya Saudi Arabia. Na kundi la pili linadai kuwa Arafa huwa ni tarehe 9 Dhul Hijja, basi kila nchi itategemea kuandama kwa mwezi wa Dhul Hijja katika nchi inayohusika.
Wanazuoni wa pande zote hizo mbili wanatoa hoja na dalili zao kutoka katika Qur’an Tukufu na Sunna ya Mtume (s.a.w.). Mimi sitakuwa tayari kuzielezea hoja na dalili hizo katika makala haya nisije nikaamsha ushabiki baina ya hizi pande mbili znazotofautiana. Kwa vyovyote vile wanazuoni wa upande mmoja ndio waliosibu katika hoja zao na wanazuoni wa upande wa pili wamekosea. Haiyumkiniki kabisa kuwa pande zote hizo mbili zimekosea.
Jambo la msingi hapo ni kurejea katika mafundisho ya Mtume (s.a.w.) tuone anasema nini inapotokezea hali kama hiyo. Mwanazuoni mmoja amelitolea hukumu jambo akasibu na mwingine akalitolea hukumu jambo akalikosea.
Katika makala yangu ya mwisho katika gazeti hili nilieleza kuwa Mtume (s.a.w.) alisema: "Akijitahidi mwanazuoni akasibu basi atapata malipo mara mbili. Na akijitahidi akakosea basi atapata ujira mara moja". (Bukhariy na Muslim).
Maana ya Hadith hiyo iko wazi kabisa. Mwanachuoni anayelitolea Fat’wa jambo basi Allah (s.w.) hukubali ile ijtihadi yake na kumlipa ujira kwa ijtihadi hiyo, hata kama amekosea katika hukumu yake.
Hii ina maana kwamba katika kila jambo Allah (s.w.) hutazama nia ya huyo mwenye kulitenda hilo jambo na siyo hilo jambo lililotendwa. Kama nia ya kutenda jambo hilo ni kumtii Mwenyezi Mungu (s.w.) na Mtume wake, basi jambo hilo hukubaliwa na kama nia ni nyingine basi hukataliwa.
Seyyidna Umar Ibn Al Khattaba (ra) amesema, " Nilimsikia Mtume (s.a.w.) akisema: ‘Hakika matendo huhesabiwa kwa mujibu wa nia, na kila mtu atalipwa kwa kile alichokinuia. Mtu aliyenuia kuhama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi kuhama kwake kutakuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na kama nia yake ya kuhama ni kwa ajili ya dunia basi ataipata; au kama kuhama kwake ni kwa ajili ya mwanamke basi atamwoa mwanamke huyo, kwa hivyo kuhama kwake ni sawa na ile nia aliyoinuia". (Bukhariy na Muslim).
Katika Hadith hii Mtume (s.a.w.) ametupigia mfano wa watu wawili mbalimbali waliofanya nia tofauti. Wote wawili wamehama, lakini mmoja alihama kwa kuitikia wito wa Allah (s.w.) na Mtume wake na yule wa pili alihama kwa ajili ya kutafuta maslahi ya kidunia tu, basi kila mmoja wao akalipwa kwa mujibu wa ile nia yake, na siyo kwa lile tendo alilolifanya.
Basi na sisi hata kama tutahitalifiana katika siku ya kuanza kufunga na kufungua Ramadhani na pia katika siku ya kufunga Arafa, Mwenyezi Mungu (s.w.) atatulipa kwa mujibu wa nia zetu na ijtihadi za wanazuoni wetu. Haidhuru huyu amefuata Saudi Arabia na mwingine amefuata mwezi ulioandamana katika nchi yake.
Madamu nia za wote ni kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na siyo kumuasi basi watalipwa kwa hizo hizo nia zao na wala hawatapunjwa.
Inavyopendeza Waislamu wote ulimwenguni wafunge na kufungua Ramadhani siku moja, na pia wafunge Arafa siku moja, lakini kutokana na kila upande kufanikiwa kinamna vyake hilo limekuwa gumu.
Ni dhahiri kuwa tutaendelea hivi hivi kukhitalifiana katika mambo hayo. Kila upande utafuata ijtihadi yake. Aliyesibu atapata pointi mbili na aliyekosea hataondoka patupu, atapata pointi moja. Hivyo ndivyo alivyotufundisha Mtume (s.a.w.).
Tatizo linabaki katika sala ya Idi. Kwa vile kundi moja limetangulia kufunga kwa siku moja, pia litatangulia kufungua kwa siku moja. Kwa hivyo Idi itakuwa katika siku mbili tofauti, yaani kila kundi litasali sala ya Idi siku yake.
Lakini kama tulivyokwishatangulia kusema sala ya Idi ni Sunna na si faradhi, na Mtume (s.a.w) aliwahi kuiakhirisha sala hiyo; badala ya kuisali siku ile ile ya Idi ikaisali siku ya pili yake.
Safari moja mwezi ulionekana tarehe 29 Ramadhani, nje ya mji wa Madina, lakini wakazi wa Madina hawakuuona. Basi siku ya pili yake wakaamka hali ya kuwa wamefunga Ramadhani ya 30.
Wakati wa mchana akaletwa habari Mtume (s.a.w.) kuwa mwezi ulionekana jana yake. Mtume (s.a.w) akaamrisha watu wote wafungue na kwa kuwa wakati ulikuwa umekwisha pita, akawaambia watasali sala ya Idi siku ya pili yake. Na kweli akafanya hivyo.
Hii ni hoja na dalili ya wazi kuwa inapopatikana sababu nzito, sala ya pili. Kama hivyo ndivyo, kwa nini hatungojani tukasali Idi siku moja?
Kwa mfano hivi majuzi hapa kwetu, kuna waliofunga saumu ya Arafa siku ya Ijumaa kwa kufuata Arafa ya Saudia Arabia. Idi, kwa kundi hili, ilikuwa ni Jumamosi. Na kundi la pili ambalo ndilo kubwa sana lilifunga Arafa siku ya Jumamosi iliyopita, kwa kufuata jinsi ya vile mwezi ulivyoandama hapa nchini. Hawa nao, Idi kwao ilikuwa Jumapili.
Kwa kuwa sala ya Idi tunaweza kuisogeza mbele siku moja baada ya Idi kama alivyofanya Mtume (s.a.w.), basi kwa ajili ya kutafuta umoja na mshikamano baina yetu ingalikuwa vizuri zaidi kama safari hii sote tungesali Idi siku ya Jumapili, kwa pamoja, nchi nzima. Na hasa ukitilia maanani kuwa wale waliosali Jumapili ndio waliokuwa wengi sana.
Jambo la kusikitisha ni kule kuona baadhi ya viongozi wa Kiislamu wakikimbilia vyombo vya habari na kila mmoja kutangaza siku yake ya kusali Idi.
Kama upo uwezekano wa sote kusali Idi siku moja kwa nini tung’ang’anie ikhtilafu hata katika jambo lisilohitaji ikhtilafu? Kama jambo la kuthubutu mwezi lina utata, tutaendelea na ikhtilafu zetu, si neno; lakini jambo la kusali Idi halina utata wowote, sote tunaweza kusali siku moja, hoja tukubaliane tu.
Tusisahau, "Umoja ni nguvu na utengano
ni udhaifu". Waislamu kwa hivi sasa tumeandamwa na kila aina ya matatizo.
Silaha pekee itakayotuwezesha kupata ushindi ni mshikamano wetu. Umoja
wetu ni tishio kwa maadui zetu. Adui anapenda kutuona tumesambaratika;
na anatumia kila aina ya mbinu ya kutugawa. Kwa nini na sisi tumsaidie
katika kazi yake hiyo?
|
|