NATO isizuge walimwengu
Ndugu Mhariri
Hivi karibuni majeshi ya NATO yakiongozwa na Marekani yamekuwa yakiishambilia Yugoslavia eti kwa sababu majeshi ya Waserbia (Wayugoslavia) yakiongozwa na Dikteta Milosovic yaache kuwaangamiza Wakosovo wenye asili ya Albania, ambao sisi tunatambua kuwa ni Waislamu wa Kosovo. Kinachostaajabisha ni kwamba, makombora na mizinga ya Waserbia kwa wakati huo yalikuwapo mpakani mwa Kosovo na Yugoslavia.
Katika mazungumzo ya kutafuta amani yaliyofanyika Rambuyee, Ufaransa Waislamu wa Kosovo walikubaliana walitia saini ila Waserbia walikataa na hawakutia saini na miongoni mwa masharti waliopewa Waislamu ni kutopigana kabisa, kumbuka wakati huo majeshi ya Serbia (Yugoslavia) yapo mpakani. Baada ya mkutano kuvunjika majeshi ya Serbia bila kuzuizi yalianza kuingia Yuguslavia kwa mashambulizi makali. Hii ni mfano wa kupigana na mtu wakati mikono imefungwa kwa nyuma.
Majeshi ya Yugoslavia kwa kuwa yalikuwa tayari ndani ya Kosovo yalichokuwa yakifanya ni kuwatesa mpaka kuwaua vijana. Ama kijana akifanikiwa kupata nafasi basi hukimbia, pia majeshi ya Serbia yalikuwa yakichoma moto nyumba na kuiba mali za Waislamu ama wanawake na watoto na wazee hawa walilazimishwa kuondoka na kibaya zaidi vitambulisho vyote wananyang’anywa ili itakapotokea kurudi asijulikane kuwa ni mtu wa Kosovo.
Hapa tunaona kwamba kuwazuia Wakosovo kujibu mashambulizi ni mbinu ya NATO na Marekani kuwasaidia Waserbia kuhamisha, kuwadhulumu na kuwaua Waislamu wa Kosovo kwa urahisi, na kwa miaka minne sasa vita hivi vilikuwa vikiendelea, lakini wakimbizi hawakufikia kiasi kilichopo sasa. Kwa hiyo kinachodhamiriwa Ulaya ni kutokuwepo taifa la Waislamu na hata kama litakuwepo basi watahakikisha linakuwa masikini kupita yote kwa mfano Albania, Bosnia na Wanakosovo.
Ama kwa upande wa pili, NATO na Marekani wanaishambulia Yugoslavia si kwa sababu hii inayoeleweka na mambumbumbu, bali wana wasiwasi mkubwa juu ya kuwepo silaha kali kule Yugoslavia na kuwepo kwa mitambo ya kutengeneza Nyuklia.
Kwani silaha na mitambo kama hiyo wanataka waimiliki wao wenyewe, kwa sababu hii ya NATO kupiga vituo vya kijeshi vya Waserbia, haimaanishi kuwazuia kwani mpaka sasa Waserbia na mizinga wapo ndani ya Kosovo wakiendelea na opereshani yao bila kipingamizi, wakati NATO na Marekani wanashambulia Belgrade (mji mkuu wa Yuguslavia) hii inastaajabisha zaidi wakati jambazi lipo Manzese likiendelea kuleta athari wewe unapeleka wakiwa na mabomu ya machozi Ilala kwa sababu kwao ni Ilala.
Hassan K. Himid,
P.O. Box 12621,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
NISINGEPENDA kuingilia maswala ya mavazi kwa akina mama kwani vyombo na Wizara husika ipo. Kwa kweli mimi binafsi ninaamini serikali haiwajibiki katika kuangalia suala la mavazi yanayovaliwa na baadhi ya kina mama hivi sasa.
Na suala kubwa hasa ni kuona ipo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto ikiwa haina mwelekeo katika kutoa mafunzo, maonyo au adhabu kwa baadhi ya wanawake wanaotembea wakiwa wamevaa nguo fupi zinazoonyesha sehemu nyeti za miili yao.
Kama Wizara hii inawajibika ipasavyo je, inaleta maendeleo gani kwa wanawake, inajisikia vipi inapoona wanawake wakitembea na nguo fupi?
Nyinyi wanawake mnapaswa kuona haya mnapowaona baadhi ya wanawake wasio na akili timamu wakidhalilisha miili yao kwa umalaya. Naiomba serikali kulipeleka Bungeni suala hili na adhabu zichukuliwe kwa wanawake hayawani wanaovaa nguo fupi na zinazopasuliwa sehemu ya mbele au nyuma.
Kama itaendelea basi ni bora Wizara ivunjwe na badala yake kiundwe chombo cha kuwadhibiti wanawake wanaovaa nguo za ukahaba.
Jumbe M. Mzigo,
Ubungu Islamic High School,
P.O. Box 55105,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
MNAMO Ijumaa ya Machi 12, mwaka huu hapa Mwanza tulitembelewa na ugeni adhimu wa Ustadh Salum Msabaha aliyekuwa Mwakilishi wa Mkunazini kwa tiketi ya CUF kabla hajatekwa nyara na kulazimishwa kujiuzulu kwa mujibu wa vyombo vya habari.
Mimi binafsi sikuwa namfahamu Msabaha kabla ya sakata hilo lakini nilimuweka kwenye kumbukumbu zangu sio tu kama mwanasiasa bali kama Sheikh baada ya kuona kanda ya Mdahalo kuhusu mwandamo wa mwezi uliofanyika Kibaha mwaka jana kati ya wanaokubali mwezi wa kitaifa na wale wa kimataifa, nikiwa kambi ya kitaifa niliweza kuvutiwa na hoja zake mpaka nikashawishika na hoja zake na kurudi kwenye kambi yake.
Hivyo niliposikia tangazo la ziara yake nilivutiwa nakuwa miongoni mwa maelfu ya wale waliohudhuria mhadhara wake uliofanyika Jumapili ya Machi 14, mwaka huu katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Thaqafa.
Sio nia ya barua yangu kuzungumzia kila alichozungumza Msabaha, maudhui yake makuu ya mada yake yaligusia mambo manne: Itikadi, mahusiano ya kijamii, uchumi na siasa.
Sipendi kuzungumzia haya matatu ya mwanzo kwani yanaongozwa na siasa, nilimstukia pale aliopo onya viongozi wa dini kuchanganya dini na siasa na kutoitumia Misikiti katika masuala ya kampeni kwani kwa kufanya hivyo kutawagawa Waislamu.
Vile vile aliwaonya Waislamu kwamba hakuna haja ya kuihusisha Misikiti katika masuala ya siasa kwani hata serikali tutakayoichagua haitaongoza kidini hivyo Waislamu watulie, waache jazba pale wanapohisi kutotendewa haki basi wachague kundi la viongozi mahiri wa kuwakabili viongozi kwani njia hiyo imejaribiwa na kuonekana inafaa vile vile, aliwafananisha viongozi wasiojua kama BEDUI aliyekojoa Msikitini wakati wa Mtume, maswahaba walipochachamaa Mtume aliwazuia wasiwe na jazba na kumuelimisha yule BEDUI ubora wa nyumba ya Mungu (Msikiti), BEDUI akaomba msamaha.
Hivyo hata kama Waislamu watakapo hisi hawatendewi haki lazima watumie busara na wawaelimishe wale wanaovamia Misikiti na kuingia na viatu makosa yao badala ya kuwalaumu.
Baada ya maelezo hayo napenda kumkumbusha ndugu yangu Mh. Msabaha kwamba mtu akisahau historia kila aendapo ni giza, niliwahi kusimuliwa na babu yangu kwamba "Msikiti huu ndipo tulipokuwa tunakutana katika vikao vyetu wakati wa kudai uhuru, hata kadi zetu za TANU zilihifadhiwa humo kwani kwa tabia ya mkoloni alikuwa anaheshimu sana nyumba ya ibada", mwisho wa kumnukuu.
Babu zetu walipigana kumuondoa mkoloni kutokana na dhuluma na mgao usio wa haki wa fursa zilizokuwepo kati ya Waislamu na watu wa dini nyingine, lakini hakuna nafuu iliyopatikana, baada ya uhuru Waislamu wanajiandaa kupiga kura ya pamoja kama iliyopigwa kumuondoa mkoloni, kitu ninachotaka kumkumbusha ndugu Msabaha na Waislamu wote wafahamu hatumchagui kiongozi atakayeamrisha mwizi akatwe mkono la hasha, tunamchagua kiongozi atakayesimamia KATIBA na kutoa haki sawa kwa watu wa dini zote.
Hatutaki tena kauli za huyu hana mke!! Hana mtoto, kwani kakwambia nani kuwa tunataka kuchagua Imamu wa kusalisha Msikitini. Hivi Sheikh hawa wacha Mungu tunaotakiwa kuwachagua tunaweza kuwapata wapi kwani kwa wenzetu wacha Mungu wao hupatikana Kanisani na huko ndiko hutambulishwa kwa waumini wao.
Kusahau historia ni hatari. Wakati wa Mtume Misikiti ilitumikaje na nani aliyesema sasa basi. Wakati wa uhuru Misikiti ilitumika, nawaomba Masheikh waisome makala ya Alhaj Yusuph Kalala katika gazeti la ANNUUR la Feb. 28 - Machi 4, mwaka huu lenye kichwa kisemacho "Tujiandae kwa kura ya pamoja 2000", na wito wake waufanyie kazi.
Abu Kisha M,
P.O. Box 1103,
Mwanza.
Ndugu Mhariri
KWANZA nampongeza Bwana Murshidu Issa wa Dodoma kwa maoni yake yenye kichwa cha habari "pongezi mabinti wa Kiislamu" kupitia gazeti tukufu la ANNUUR Febuari 26 hadi Machi 4, 1999 Dhulkada 1419.
Hakika ni muhimu vijana wa Kiislamu sio wanawake tu bali hata wanaume kupitia gazeti hili maarufu ANNUUR waonyeshe nia zao "Nusra" ya kuonyesha utaka kuolewa au kuoa.
Hivyo isiishie kwa vijana tu bali hata wanawake wa umri mkubwa wa miaka arobaini na kuendelea wajitokeze kwani wanaweza wakawa wamefikwa na matatizo hivyo aidha wakapoteza waume zao au wake zao katika mazingira mbalimbali, hivyo wanahitaji wenzao wengine wa kuwaenzi. Jitokezeni msiogope ndio namna ya kuwapata waadilifu wenzenu.
Twaha Bakari,
Tabora.
Ndugu Mhariri
NATOA wito kwa Taasisi na Jumuiya zote za wananchi na hata zile za kidini kulaani kitendo cha polisi kuvamia ofisi za Gazeti huru la kila siku Majira.
Ni uonevu mtupu na matumizi mabaya ya vyombo vya dola, kwani lingekuwepo kosa basi polisi ingetoa maelezo.
Tusipolaani vitendo hivi basi uhuru wetu na amani ya nchi yetu ipo mashakani.
Hussein Kingaru,
Morogoro.
Ndugu Mhariri
GAZETI la Majira la Jumamosi Aprili 3, liliripoti kuwa Rais Mkapa ametumiwa mkanda wa mauaji ya Mwembechai. Mkanda huo unaelezwa kuwa kiambatanisho cha Waraka unaoikumbusha serikali iwashughulikie Paroko wa Kanisa Katoliki Lwambano na Polisi walioua badala ya kuwasaka watu wasio na hatia.
Kilichofuata ni Ofisi hizo kuvamiwa na mwandishi Martin Malera kutekwa nyara kwa mtutu wa bunduki.
Kwanza ningependa nilaani kitendo hicho kwa nguvu zangu zote na kuwapa pole waandishi wa habari wa Majira walioathiriwa na tukio hilo.
Lakini ningependa kuhoji kosa nini maana hata Kamanda Gewe kakataa kutoa maelezo. Au tuseme madhila yanayowagusa Waislamu hayatakiwi yaandikwe?
Abu Hafsa,
Masjid Qiblatain,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
NIMESIKITISHWA sana na kitendo cha polisi kuvamia ofisi za gazeti la Majira na kumteka nyara mwandishi.
Je; ni sera na sheria gani polisi huwa wanafuata? Nchi yetu si ya kidikteta wala ya kikoloni. Wasituletee sera na utendaji kazi wa kikaburu uliopitwa na wakati.
Maua Kindamba,
Bagamoyo.
|
|