KUTOKA MAGAZETI YA ZAMANI
 

'Majizi yatandikwe viboko mbele ya hadhara'

Mwafrika Jumatano Juni 12, 1963

MAJIZI, wanyang'anyi, waendeshao rushwa na magendo,watandikwe viboko hadharani na kukatwa mikono yao, hayo ni madai yaliyotolewa na Wajumbe wa Baraza la Taifa lilipokutana hivi leo.

Dai hilo lilitolewa na Wajumbe kadhaa wakati wa majadiliano ya hati ya sheria inayoweka kima cha adhabu kwa wahalifu hao kuwa miaka miwili jela pamoja na viboko 24. Wajumbe wote waliosema wanaunga mkono sheria hiyo.

Waziri wa Usalama, Bw. Job Lusinde, akianzisha majadiliano ya hati hiyo ya sheria, aliliambia Baraza kuwa wanaohusika katika sheria hiyo ni wanaonyang'anya kwa nguvu, wavunjao majumba, wezi wa mifugo, wezi wakiwa watumishi, waendeshao rushwa na magendo.

Akaongeza kusema kuwa kadiri ya marekebisho yaliyofanywa sheria mpya hiyo pia itawaruhusu wanaoiba mali ya serikali au vyama na wavunjaji wa maduka au stoo.

Bw. Lusinde akazidi kusema kuwa kima cha adhabu inayotolewa kwa wahalifu hao na sheria mpya jela miaka miwili pamoja na viboko 24; ambavyo mhalifu atatandikwa 12 anapoanza kifungo na 12 mwishoni mwa kifungo.

Katikati

Lakini, aliendelea Bw. Lusinde, mahakimu wanaachiwa hiari ya kuongeza adhabu hiyo kwa kufuata ukubwa wa uhalifu. Ikiwa hivyo, basi viboko vinavyozidi, mfungwa atatandikwa katikati ya kifungo chake.

Sheria mpya, alisema Bw. Lusinde, haihusu watoto; hali kadhalika, viboko havitatolewa kwa watu wazima wanaozidi umri wa miaka 45 pamoja na wanawake wote.

Hali kadhalika, ikiwa mhalifu ndio mara yake ya kwanza kuiba kitu chenye thamani isiyozidi shilingi 100, korti inaweza kumpa viboko 10.

Waheshimiwa wajumbe wengi waliunga mkono hati ya sheria hiyo, Bw. Peter Wala. Kamishna wa Jimbo la Kaskazini (Mjumbe wa kuteuliwa) alisema: "Majizi wanaotumia silaha ili kunyang'anya mali ya watu ni wauaji, hivyo wanastahili kutandikwa viboko sokoni, ili waombe radhi; na watu wengine na raia wawe na imani kuwa adhabu hizo zinatolewa.

Bw. majaj wa Iringa alisihi kwamba kabla ya kumtandika mfungwa viboko, apimwe kwanza na daktari kama anaweza kustahimili adhabu hiyo.

Mjumbe Wilji wa Moshi alidai kuwa wanaopokea mali ya wizi nao watandikwe viboko hadharani.

Wakatwe

Mjumbe Mhannah wa Bukoba alidai kuwa adhabu ya viboko haitoshi, ila majizi yakatwe mikono yawe na alama ya kuonyesha kwa watoto na wajukuu kuwa ni waizi.

Mjumbe Chifu Fundikira wa Tabora alisema: Mfungwa aliekaa vizuri na kuonyesha kabadili tabia yake katika jela, asitandikwe vile viboko 12 mwishoni mwa kifungo.

Mjumbe Siyovelwa wa Iringa: Wanawake nao wakiwa majizi watandikwe viboko. Hali kadhalika wanaume wenye umri kati ya miaka 40 hadi 50 wana nguvu za kutosha, hivyo wakiiba watandikwe.

Mjumbe Sarwatt wa Mbulu: Majizi yasipunguziwe siku za kifungo chao.

Wazomewe

Mjumbe Kapilima wa Mahenge: Majizi yasipewe uhuru wa kusafirisafiri baada ya kutoka jela.

Mjumbe Mbarnot wa Umasaini: Wamasai wanasingiziwa na kufanywa ndio peke yao majizi ya ng'ombe kumbe wako wachache tu wanaoiba mifugo. Wengi wako tayari kusaidia serikali kukomesha wizi huo.



Mshitakiwa hakuja ofisini siku ya mauaji - Shahidi

Uhuru Ijumaa, Agosti 15, 1969

MASHAHIDI kadhaa, maofisa polisi na raia, walitoa ushahidi hapa jana kuhusu shughuli na safari za mtu anayeshitakiwa kwa mauaji ya Bwana Tom Mboya, Waziri wa zamani wa Mipango ya Uchumi wa Kenya hapo Julai 5.

Bwana Francis Gachero, Mkurugenzi wa Kampuni moja ya Nairobi aliiambia Korti kwamba anamjua mshitakiwa kuwa mmoja wa Wakurugenzi wa kampuni yake. Siku ya Jumamosi Julai 5 hakumuona mshitakiwa ofisini lakini alimuona kwenye tafrija ya karamu iliyofanywa katika kijiji cha Wakikuyu, maili 13 kutoka Nairobi, ambako mshitakiwa alifika na kukaa kwa muda wa kama dakika tano au kumi hivi.

Shahidi mwingine, Bwana John Fernandes, meneja wa duka moja la kuchapisha vitabu mjini Nairobi aliiambia Korti kwamba anamjua mshitakiwa sana kabisa. Alikuwa mnunuzi wa kawaida katika duka lake. Bw. Fenandes alieleza kwamba mshitakiwa huyo, Nashon Issac Njenga Njoroge aliagizia karatasi za kupigia 'taipu za KANU' ambazo mpaka sasa hajazichukua.

Usikilizaji wa mwanzo wa kesi hiyo unaingia katika siku yake ya sita leo. Mpaka sasa mashahidi 48 wameshatoa ushahidi wao. Korti iliambiwa jana kwamba mashahidi zaidi pamoja na wataalamu wa silaha kutoka Uganda na "mashahidi muhimu ambao sasa wako Tanzania watapatikana wiki ijayo".



Mwalimu kortini kwa kunajisi

Mwafrika Jumatano Juni 12, 1963

WASICHANA wawili ambao ni wanafunzi wa shule ya TAPA iliyoko Temeke, mjini Dar es Salaam, leo (Jumanne) wamedai kortini kuwa wamenajisiwa kwa nguvu na mwalimu wao.

Mbele ya Hakimu, Bwana A. Erakwu alisimama Mwalimu Joseph Gumbo, Mzingua mwenye umri wa miaka 32 aliyeshitakiwa kwa kunajisi .......... na ......., wakiwa na umri wa miaka 16 kila mmoja.

Akianza kutoa ushahidi. Zainabu Saidi aliiambia korti kuwa siku moja asubuhi mwezi Februari alipewa barua ya kumtongoza na mwalimu huyo. Alipokataa, aliendelea kueleza msichana huyo, "mwalimu aliniambia kuwa ikiwa nitamkatalia, ataniroga macho nisiweze kuona ubaoni na pia wazazi wangu watakufa; na hata kama nitashinda mtihani ataniangusha".

Alinifuata

Halafu akasema kuwa wakati wa alasiri siku hiyo, alipokwenda kwenye choo cha shule, alifuatwa na mwalimu.

"Nilipopiga kelele alinitisha kuwa atanikaba koo. Hapo akaniziba mdomo kwa mkono wake, akaniangusha chini na kuninajisi kwa nguvu", alisema............

........... aliendelea kuiambia korti kuwa baada ya kitendo hicho cha mwanzo, mwalimu aliendelea kumwambia waende chooni, na alipokataa alinaswa vibao ovyo ovyo wakati kwa mafundisho.

'Tuliendelea'

"Hivyo niliogopa, ndipo tulikuwa tunaendelea kutembelea pamoja mpaka mwezi Aprili tulipokamatwa na mtu wa TANU Yusi Ligi", alisema ..............

Msichana wa pili, .........., alimwambia Hakimu kuwa Aprili 14, wakati mshitakiwa alipokuwa anafundisha. "Aliniita mezani kwake na kuniambia twende chooni tukatembee pamoja".

Akaongeza kusema: "Nilikataa na kwenye nafasi, baadaye nilipokwenda, mwalimu alinifuata na kuninajisi kwa nguvu".

Alipoulizwa na Hakimu ikiwa safari hiyo ilikuwa ya kwanza. Akajibu kuwa siyo mara ya kwanza ila ulipita muda mrefu tangu kitendo cha kwanza kupita.

Kesi imeahirishwa hadi Juni 20, naye mshitakiwa yumo ndani.



Matatizo ya Wamasai yanakumbukwa- Kundya

Uhuru Alhamisi, Septemba 30, 1965

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Bw. M.R. Kundya amesema kuwa Wamasai katika Mkoa huo hawajasahauliwa na shida yao ya maji inaeleweka sana na serikali ya Tanzania. Aliyasema haya majuzi alipokuwa akiwahutubia viongozi 15 wa Kimasai kutoka Kiberashi, wilaya ya Handeni.

Bw. Kundya aliendelea "maji ni shida inayokabili mkoa mzima wa Tanga hasa kwa wilaya ya Handeni, lakini shida ya Kiberashi ni kubwa zaidi hata ilibidi serikali kujishughulisha kwanza na Wamasai wa Kiberashi kuwapatia visima vya maji yakitolewa na bomba la kusukuma maji kunyweshea mifugo na kwa matumizi ya nyumbani".

Viongozi hao wa Wamasai pia walitoa maombi ya kupatiwa shule na hospitali ndogo, katika sehemu yao. Wote walikubaliana kuwa mara baada ya maji kupatikana, shida yoyote ile inaweza kutekelezwa kwa urahisi.

Kutokana na sheria za bei za mifugo zilizopokelewa na Wamasai, Bw Kundya aliwashauri kuunda chama cha ushirika ambacho kitawasaidia kupata bei nzuri kwa mifugo yao. Na akaeleza kuwa chama cha ushirika kitawasaidia vikubwa katika kuinua hali yao ya maisha na hali ya mifugo.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwaeleza Wamasai tofauti iliyopo kati ya kodi ya tawala za mitaa na kodi ya kichwa, ambazo zote mbili zilionekana kuwatatanisha, na viongozi walikubali kuwa watashirikiana na serikali.

Bw. Kundya ambaye alikuwa akitembelea wilaya ya Handeni kwa muda wa siku mbili, alifuatana na mjumbe wa Halmshauri Kuu ya TANU, Alhaj Abdallah Sembe, Mkuu wa Wilaya ya Handeni pia alihudhuria mkutano huo.



Sheria ya Jamhuri imenitoa Ubalozi - Kassanga Tumbo

Jumatatu Septemba 17, 1962

BWANA Kassanga Tumbo, Rais wa PDP alisema katika mkutano uliofanywa katika Jumba la Arnatoglu juzi kuwa sheria ya Jamhuri inayomfanya Rais wa Tanganyika awe sawa na dikteta ni sababu mojawapo iliyomfanya ajiuzulu Ubalozi.

Aliongeza kusema kuwa hakuweza kuvumilia yasiyofaa. "Mimi sijasema uongo", alitamka na nitaongoza chama changu kwa vitendo wala sio kwa methali.

Bwana Tumbo alisema kuwa yeye alipinga kwa nguvu zake zote ile sheria ya uraia. Lakini ilipitishwa kwa sababu alikosa kura za kutosha.

Akijitetea kwa nini ametumia jukwaa la TRAU katika mkutano alipotangaza kwamba anajiuzulu kutoka TANU na kuwa Rais wa PDP, Bw. Tumbo alisema alitumia jukwaa hilo ili kuwaaga watu wala hakuhutubia mambo ya siasa.

Mapema, Bw. Lifa Chipaka, mweka hazina wa chama hicho alisema kuwa serikali inalaumu chama chao kuwa kila wakati wanasahihisha tu baada ya kufanya vitendo.

'PDP ilishauri serikali isikope shilingi 12,000,000 za kujengea hoteli mjini Dar es Salaam, bali kila raia atoe shilingi 1 tu. Lakini serikali haikujibu.

Bw. Chipaka alisema kwamba serikali imeshindwa kutimiza ahadi zake aliposema hakutakuwa na ada za shule na kumbe hivi sasa ada zimepanda na kufikia kipeo cha shilingi 960.

Bwana Chipaka alijigamba kwamba kila siku wanapata 100, na hivi sasa jumla yao ni zaidi ya 1,500.

Hotuba zikamalizika kwa kueleza kwamba matawi 10 ya chama yatafunguliwa hivi karibuni katika Tanganyika, na tawi la kwanza likiwa Ilala mjini Dar es Salaam.



Khomeini afafanua kuhusu watakaopewa adhabu ya kifo

Uhuru, Jumanne, Mei 15, 1979

TEHERAN, Iran

KIONGOZI wa Iran, Ayatollah Ruhollah Khomeini ameamuru kwamba watu watakaofikishwa kwenye mahakama za Kiislamu kwa mashitaka ya kuua pamoja na kutesa ndio watakaohukumiwa adhabu ya kifo.

Shirika la Habari la Iran (Pars) limeeleza kwamba Khomeini ametoa watu wa aina mbili ambao watastahili adhabu ya kifo. Hao ni pamoja na walioua wenzao na walioamuru mauaji ya watu wengine kwa kuwatesa wanapokufa.

Sheria hii imetolewa baada ya kikundi cha watu 114 walioongoza maandamano ya kuupinga utawala wa Shah miezi michache iliyopita kufikishwa kwenye mahakama iliyoko kusini mashariki ya mji wa Kerman.

Wengi kati ya waliofikishwa mahakamani kwa mashtaka ya kuua, wamepatikana na makosa ya kutesa na kuamuru mauaji.

Mkuu wa mahakama ya Tehran, Ayatollah Sadiq Khalkhali aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba kiongozi wa zamani wa Iran. Shah, familia yake pamoja na wasaizidi wake wanafikiriwa na watu wa Iran kwamba wanastahili adhabu ya kifo.

"Mtu yeyote atakayewaua popote pale walipo hatashtakiwa kwa kosa la kuua", Ayatollah Khalkhali alisema.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook