Kuna jambo latafutwa
Simanzi zimenishika, Ponda
kusakwa nchini,
Mikono yatetemeka, nashindwa
kushika peni,
Amekuwa kama paka, mwizi
wa nyama jikoni,
Kuna jambo latafutwa, ukweli
kuupotosha.
Kwake kusema ukweli, kumekuwa
uchochezi,
Atafutwa kweli kweli, kuliko
hata jambazi,
Lengo kubwa kubadili, ukweli
ulio wazi,
Kuna jambo latafutwa, ukweli
kuupotosha.
Lengo lao si zuri, hilo nimelibaini,
Rundo la maaskari, walijaa
Mtambani,
Wengine kwenye magari, na
bunduki mabegani,
Kuna jambo latafutwa, ukweli
kuupotosha.
Awe hai wamesema, au mfu
wamtaka,
Askari hima hima, sasa wanahangaika,
Kweli kuna usalama, siku
watayomshika?
Kuna jambo latafutwa, ukweli
kuupotosha.
Anaachwa mchochezi, vifo
alosababisha,
Tena huku wamuenzi, kama
kawafurahisha,
Kumbe kaacha majonzi, nyoyoni
yatukondesha,
Kuna jambo latafutwa, ukweli
kuupotosha.
“Piga huyu piga yule”, kauli
ilisikika,
Askari mteule, kauli akaitika,
Aliuwa pale pale, wale aliowataka,
Kuna jambo latafutwa, ukweli
kuupotosha.
Hawa hawana makosa, huru
wameachiliwa,
Wanapita “wakitesa”, bila
ya kusumbuliwa,
Atafutwa asokosa, hatiani
anatiwa,
Kuna jambo latafutwa, ukweli
kuupotosha.
Hapa mwisho kituoni, peni
ninaachilia,
Islamu chunguzeni, ukweli
kuugundua,
Ponda yupo msakoni, yapo
“maiti” sheria?
Kuna jambo latafutwa, ukweli
kuupotosha.
Hamisi M. Rutengo,
Ubungo Islamic High School,
P.O. Box 55105,
Dar es Salaam.
Bismillahi awali, kwa jina
lako Karima,
Ninakuomba mwalali, tena
kwa taadhima,
Ambaye wasitahili, dua kwangu
kulisema,
Mola wangu nakuomba, nijalie
mke mwema.
Atoke pande za kwetu, hata
kama ugenini,
Kilicho bora ni utu, ndicho
kilicho thamani,
Walio roho za kutu, Rabi
waweke pembeni,
Mola wangu nakuomba, nijalie
mke mwema.
Isilamu yangu dini, na wala
siyo pagani,
Mke wangu kuamini, isiwe
ni ubishani,
Asije kufanya kani, miye
tamuona duni,
Mola wangu nakuomba, nijalie
mke mwema.
Nijalie ewe Mola, roho yangu
itulie,
Upweke kwangu madhila, hapa
usiishilie,
Unalingana na jela, ni nani
akimbilie,
Mola wangu nakuomba, nijalie
mke mwema.
Picha na barua zenu, wenye
sifa zitumeni,
Nina haja si fununu, namtafuta
mwandani,
Ndoa si jambo la tunu, ni
sheria ya Manani,
Mola wangu nakuomba, nijalie
mke mwema.
Arubaini na moja, miaka nimeshatimu,
Msije kujenga hoja, utuli
wanilazimu,
Kuowa japo mmoja, Mola wangu
nikarimu,
Mola wangu nakuomba, nijalie
mke mwema.
Beti saba nashiliza, machache
haya yanatosha,
Mola nifutie kiza, taa njema
kwangu washa,
Naomba nisikiliza, upweke
kuniondosha,
Mola wangu nakuomba, nijalie
mke mwema.
Khamis Lali Pashua (Mwangwena)
Kijiji cha Mavumbi Pande,
S.L.P. 5332,
Tanga.
Walishasema wahenga, kuuliza
si ujinga,
Zuberi wataka mwanga, swali
lako sitapinga,
Majibu sasa napanga, kusudi
upate mwanga,
Mungu yeye ni wa wote, dua
za dini ni zako.
Wapumbavu duniani, ni wasomjua
Mungu,
Kwanza wao wanadhani, kwamba
hakuna Mungu,
Bunge letu ni makini, mambo
huanza na Mungu,
Mungu yeye ni wa wote, dua
za dini ni zako.
Aleta jua na mvua, kwa wema
na wachawi,
Na hapendi kubagua, japo
hapendi uchawi,
Wote anawatambua, awapenda
wastani,
Mungu yeye ni wa wote, dua
za dini ni zako.
Wabunge hawana dini, lakini
wanaye Mungu,
Kuwavisha upagani, Zuberi
umekufuru,
Waweza kuwa na dini, lakini
ukakosa Mungu,
Mungu yeye ni wa wote, dua
za dini ni zako.
Dua za dini ni nini, hata
shetani anazo,
Kwanza kaanzisha dini, aomba
mfululizo,
Tena akiwa gizani, kwake
hafanyi mchezo,
Mungu yeye ni wa wote, dua
za dini ni zako.
Tamati natamatisha, wenye
macho wameona,
Dunia sasa yaisha, tusibaki
kubishana,
Tuyaandae maisha, kwa kumuabudu
BWANA,
BWANA Mungu ni wa wote,
wamwombao kwa imani.
Mwinjilisti B.E. Dettu,
S.L.P. 60474,
Dar es Salaam.
Allah aliye Alimu, naja kwako
nikirimu,
Unipatie mwalimu, anifunze
nifahamu,
Kwenye sira ya Hashimu,
huyu Abali Kasimu,
Mafundisho ya muhimu, nipate
kuyafahamu.
Jamii yake Nabia, gizani
alizamia,
Dhuluma iliwajaa, haki waliipotoa,
Nuru iliwakimbia, njia wakipotea,
Twafautiana nini, malenga
niambieni.
Allahu mwenye uwezo, katoa
maelekezo,
Kwenye wake mwongozo, kwamba
Nabia kigezo,
Awe ni kielelezo, kinachotoa
mafunzo,
Ili pasiwe kikwazo, tukafuata
uozo,
Tangu utotoni mwake, machafu
hakufahamu,
Hakupata uso wake, kuabudia
sanamu,
Mkweli wasifu wake, watu
walimuheshimu,
Nipeni fundisho lake, malenga
nawaombeni.
Biashara kaifanya, alipokuwa
kijana,
Dhuluma hakuifanya, wateja
walijazana,
Hakuweza kudanganya, apate
kuuza sana,
Hapa kuna funzo gani, malenga
niambieni.
Kwa uaminifu wake, watu walimthamini,
Kwa ule ukweli wake, watu
walimwamini,
Kweli waliweka kwake, vitu
vyao vya thamani,
Kipi twajifunza kwake, malenga
niambieni.
Moyoni aliungua, dhuluma
kutoridhia,
Kutwa alifikiria, namna
ya kuing’oa,
Mapesa alitumia, watumwa
kuwakomboa,
Tunapata funzo gani, malenga
niambieni.
Chamani akaingia, cha wanyonge
kutetea,
Apate kupigania, wanyonge
kuwaokoa,
Haki wapate kupewa, utu
wao kuinua,
Hapa twajifunza nini, malenga
niambieni.
Matatizo ya jamii, yeye hakuyamezea,
Machafu kwenye jamii, hakuwa
kayaridhia,
Mejitenga na jamii, dawa
kuyatafutia,
Twajifunza kitu gani, malenga
niambieni.
Dini za wakati ule, yeye
alizikataa,
Dhuluma za wateule, macho
ziliyafumbia,
Mejaa uongo tele, wakubwa
zawatetea,
Hapa kuna funzo gani, malenga
niambieni.
Pangoni kaelekea, mlima Jabar
Hira,
Jibrili kamjia, ZANA akampatia,
Karudi kwenye jamia, maovu
kuyafyagia,
Hapa twavuna nini, malenga
niambieni.
Bado ninajisomea, sira ya
wetu Nabia,
Pale nisipoelewa, malenga
nitawajia,
Maswali tawatupia, ili nipate
kujua,
Hapa sasa natulia, majibu
natarajia.
Idd S. Kikong’ona,
Morogoro.
Bwana Meena hujambo, Dettu
ninakusalimu,
Mungu anilinda sijambo,
na wanangu nawakimu,
Umeniletea jambo, wataka
niwe hakimu,
Nami sisemi kwa fumbo, nakujibu
ya muhimu,
Mungu wetu ni mmoja, aloumba
mbingu na nchi.
NAFSI tatu sihofu, siwaze
kibinadamu,
Akili zetu hafifu, kuelewa
ya muhimu,
Kwanza tumejaa hofu, ya
Mungu hatufahamu,
Hata tunavyomsifu, ni kama
wendawazimu,
Mungu wetu ni mmoja, Muumba
wa mbingu na nchi.
Ona mkono mmoja, una vidole
vitano!
Bado mkono mmoja, na si
mikono mitano,
Vipi mkono mmoja, useme
ipo mitano?
Kwetu Mungu ni mmoja, ndiye
mwisho wa maneno,
Mungu wetu ni mmoja, Muumba
wa mbingu na nchi.
Wewe unawaza sokoni, kwenye
mafungu ya nyama,
Kisha waleta mizani, kumpanga
kama nyanya!
Tuna wasema kwa nini, yu
mafungu kama nyanya,
Hivyo Mungu hamuoni, taona
mafungu ya nyanya!
Mungu wetu ni mmoja, Muumba
wa mbingu na nchi.
Na ndiye huyo mmoja, aliyefanya
Sabato,
Mungu moja Dini moja, katuwekea
Sabato,
Jumamosi ya faraja, tufurahi
na Sabato,
Na hiyo haina hoja, yake
BWANA wa Sabato,
Mungu wetu ni mmoja, Muumba
wa mbingu na nchi.
Huyu Mungu wa Rehema, si
Mungu wa kujadili,
Bora tu nimesema, machache
yenye adili,
Ilimpasa kusema, kukujibu
lako swali,
Basi miye nasimama, nenda
Pasaka kusali,
Mungu wetu ni mmoja, Muumba
wa mbingu na nchi.
Mwinjilisti B.E. Dettu,
S.L.P. 60474,
Dar es Salaam.
Maulana yarabuka, Mola ulie
mbinguni,
Kila unalitaka, hakuna wa
upinzani,
Mauwa kakuitika, hayuko
ulimwenguni,
Mlaze pema peponi, Mauwa
Mbwana Ngowa.
Siku aliyoandika, lipofika
kasaini,
Ndipo alipoitika, akatutoka
machoni,
Nasi zetu zikifika, twaja
huko masikani,
Mlaze pema peponi, Mauwa
Mbwana Ngowa.
Likuwa mswali hina, kutwa
mpaka jioni,
Funga zote paka suna, alizifunga
yakini,
Ee Mola Maulana, mama mweke
peponi,
Mlaze pema peponi, Mauwa
Mbwana Ngowa.
Mazoeya ni mabaya, Ngare
tamwambia nani,
Mema ama mabaya, nikienda
Bomandani,
Sasa nitawayawaya, nipeni
pole jamani,
Mlaze pema peponi, Mauwa
Mbwana Ngowa.
Ombi nakuomba Mola, siwaombi
mashetani,
Mauwa alipolala, pajengee
busitani,
Na siku ya palapala, awe
mbali na motoni,
Mlaze pema peponi, Mauwa
Mbwana Ngowa.
Nyuma kaacha watoto, waume
na wana ndani,
Na wajukuu tomito, watiaji
wa ubani,
Mke wangu ni mtoto, wa tano
mwao tumboni,
Mlaze pema peponi, Mauwa
Mbwana Ngowa.
Namba saba naishia, naofia
gazetini,
Ningetunga beti mia, wenzangu
ningewahini,
Hili pia nahofia, litachakaa
kapuni,
Mlaze pema peponi, Mauwa
Mbwana Ngowa.
J.S. Ngare (Liwalo),
P.O. Gombero,
Tanga.
|
|