(d) Suala la maisha ya Akhera
Kutokana na mtihani huu historia ya mwanadamu haiwezi kuishia katika maisha haya ya hapa ulimwenguni tu, bali haina budi kuendelea kwenye maisha mengine baada ya haya, maisha ya Akhera, ili mwanaadamu avune kulingana na alichokipanda hapa ulimwenguni. Atalazimika mtu kutoa hisabu yake mbele ya Bwana wake ni vipi na ni kiasi gani aliishi kulingana na lengo la maisha yake. Je, aliishi maisha ya kumtii na kumnyenyekea Allah (s.w.) katika kuendesha kila kipengele cha maisha yake au aliishi kwa kumkanusha Allah na kumuasi? Kila mtu atalipwa kwa uadilifu kulingana na utendaji wake hapa ulimwenguni. Tunakumbushwa katika Qur'an:
"Na bila shaka tulimpeleka Mtume katika kila umma ya kwamba muabuduni Allah (s.w.) na mwepukeni mwovu (Twaghuti)". (16:36)
Historia ya Mitume huanzia kwa binadamu wa kwanza Adam. Yeye alikuwa mwanadamu wa kwanza kuletwa duniani na Mtume wa kwanza pia; hii yathibitisha kuwa hapakuwa na kipindi cha historia kilichompitikia mwanadamu bila ya kuwa na mwongozo wa Allah.
Hivyo historia ya Uislamu, kwa kufuata mpangilio wa ujaji wa Mitume ni mwigo wa uyakini wa mageuzi ya jamii na watu wake wote, wema na waovu. Ni Kumbukumbu ionyeshayo kupanuka kwa dini (mfumo wa maisha) ya Allahh na ibada zake; siasa, uongozi, hali ya kijamii, kihisia, na tabia, pamoja na mahitaji mbalimbali. Aidha ni somo linaloonyesha jinsi ambavyo Mtume alivyokidhi mahitaji ya wakati wake, na jinsi alivyowajibika kuwaweka watu sawa katika njia sahihi ya maisha na kuonyesha majaribu na vikwazo alivyopitia kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa Allah (s.w.) pamoja na kuonyesha sifa alizokuwa nazo yeye na wafuasi wake.
Hata hivyo historia inayobainishwa na Qur'an inaonyesha kuwa kila alivyokuja Mtume na ujumbe kutoka kwa Allah watu waligawanyika katika (makundi mawili). Wale waliupokea ujumbe na kuufuata na wale walioukanusha na kuleta upinzani. Hali hii ilijitokeza na inaendelea kuwepo kutokana na ukweli kwamba Allah (s.w.) amempa mwanadamu uhuru wa kuamini au kukufuru. Lililo muhimu ni njia ya haki kubainishwa na ya upotofu kubainishwa pia. Ama uchaguzi unabakia kwa mwanadamu mwenyewe.
Uhuru huu wa kuchagua ni mtihani kwa mwanadamu, atakaye chagua njia ya sawa' atakuwa na malipo mazuri mbele ya Allah na atakayefuata potofu makazi mabaya ya motoni itakuwa ndio marejeo yake. Qur'an inatufahamisha:
Kwa hakika tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyochanganyika (ya mwanaume na mwanamke) ili tumfanyie mtihani (kwa amri zetu na makatazo yetu). Kwa hiyo tukamfanya ni mwenye kusikia (na) mwenye kuona. Hakika sisi tumemuongoa (tumembainishia) njia (zote) mbili hizi, kuwa hii ndiyo ya kheri na hii ndio ya shari). Basi (mwenye tena atakuwa mwenye shukrani au awe mwenye kukufuru. hakika sisi tumewaandalia makafiri minyororo na makangwa na moto mkali (76:204).
Hakuna kulazimishwa (kuingia) katika dini. Uongofu umeshapambanuka na upotofu. Basi anayemkataa shetani na amwamini Mwenyezi Mungu bila shaka yeye ameshika kishiko chenye nguvu kisichokuwa na kuvunjika. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua... (2:256).
Historia yaonyesha kuwa kila alipokuja Mtume na kuondoka, watu waliyaacha mafundisho yake kidogo kidogo na kuyachanganya na upotofu hadi ujumbe ukapotea. Inapofikia hali hii Allah (s.w.) huleta Mtume mwingine kuuhuisha ujumbe wake. Mkondo huu wa historia uliendelea hadi alipokuja Mtume Muhammad (s.a.w.), kufikia kipindi hiki cha historia, haja ya kuja Mtume kila baada ya muda iliondoka. Hii ni kwa sababu Allah alichukua ahadi ya kuhifadhi mwongozo aliokuja nao, yaani Qur'an.
Haki sisi ndio tulioteremsha mawaidha (haya) (hii Qur'an) na hakika sisi ndio tutakaoyalinda (15:9)
Sababu ya pili ya kukatika Utume baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.) ni kuwa ujumbe uliokusudiwa uje kwa wanadamu ulishakamilishwa.
"...Leo nimekukamilishieni dini yenu, na kukutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe dini yenu (5:3).
Kuna baadhi ya Mitume walipelekwa kwa watu wa taifa maalumu au nchi fulani lakini tunaona kuwa Mtume (s.a.w.) aliletwa kwa walimwengu wote.
Sema (Ewe Nabii Muhammad): Enyi watu. Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi nyote" (7:158).
Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu wote (21:107).
Hii ndio sababu nyingine
ya kufanya haja ya kuja Mtume mwingine baada ya Mtume (s.a.w.) iondoke.
Msingi wa hoja hizi ni ukweli kwamba lililo muhimu si kuwepo Mtume kimwili
bali kufikisha kwake ujumbe uliokusudiwa. Kwa hiyo kama ujumbe wa Allah
(s.w.) upo katika usahihi wake kuwepo kwa Mtume kimwili si hitajio la lazima.
|
|