TAHARIRI
 
Iwe muhali kutii yanayokiuka imani
 

UNAPOTAMKA Kalimah (shahada): La ilaha illallah, Muhammadur Rasulullah, inamaanisha kuwa sambamba na kukiri kwako kwamba kwako Sharia ni ile ya Mungu, Mfalme wako ni Mungu tu, Mtawala wako ni Mwenyezi Mungu tu, inakulazimu kumtii Mungu tu, kilicho cha kweli na sahihi ni kile alichokibainisha Mwenyezi Mungu katika Qur'an na kupitia kwa Mtume Muhammad (s.a.w.).

Hii ina maana kuwa unaacha uhuru wako kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mara tu unapoingia katika Uislamu. Pia umesamehe haki yako ya kusema: "Rai yangu ni hii, utamaduni wa dunia ni huu, mila za mababu ni hizi, muungwana yule au sharifu yule anashauri hivi."

Mbele ya Qur'an na Sunnah huwezi kutoa vijisababu kama hivyo. Sasa jukumu lako ni kuamua kila jambo kufuatana na mwongozo wa Qur'an na Sunnah. Kama vile kipofu asivyoweza kusema kuwa ana macho, hivyo hivyo hamna mtu awezae kujiita Muislamu ambapo anakataa kuyaongoza mambo yake yote ya maisha kufuatana na Qur'an na Sunnah, na badala yake anafuata utashi wa nafsi yake, utamaduni wa taifa, au amri za awadhaniao wakubwa au watukufu.

Yeyote asiyetaka kuwa Muislamu, hamna wa kumlazimisha na kumkarahisha kutenda dhidi ya ridhaa yake. Yu huru kufuata dini yoyote aipendayo na kujiita jina lolote alitakalo. Lakini baada ya kujiita Muislamu, lazima aelewe fika kuwa anaweza tu kubaki Muislamu madamu yupo katika mipaka ya Kiislamu.

Mipaka ya Kiislamu ni: Kuikubali Qur'ani na Sunnah kuwa ni kipambanuzi kati ya haki na batili na kukichukulia kila kitu kilicho dhidi ya Qur'ani na Sunnah kuwa ni upotofu. Yeyote anayebaki ndani ya mipaka hii ni Muislamu na yeyote anayechupa mipaka hii hutoka katika Uislamu.

Na kama baada ya kutoka katika Uislamu kwa kuchupa mipaka bado atajiita Muislamu basi anajidanganya mwenyewe na anaudanganya ulimwengu.

"...Na wasiohukumu kwa yale Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio makafiri". (5:44)

Haya ndiyo majukumu ya Muislamu na ndiyo msimamo wake katika mazingira yoyote awayo. Kwa hiyo wale walio kinyume naye wasishinikize kufuata nadharia, mila au utamaduni unaokwenda kinyume na msimamo wa dini yake. Na iwe muhali kwa Muislamu kutii yanayopingana na imani yake.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook