Watu wakiwa na fedha, wanapofanya biashara, wanaponunua vitu, ndiyo unavyoongeza ajira ya wengine na ikiwa kila mtu hana kitu basi ajira haiwezi ikaongezeka, lakini nilikuwa najaribu kutazama makaratasi ya serikali yana mpango gani wa kuongeza ajira. Pamoja na kwamba mji wetu una sehemu nyingi unazohitaji matengenezo ya kimsingi ya kuongeza ajira. Matokeo yake vijana mnayaelewa, mtu hapati uzoefu wa kufanya kazi, umemaliza shule, hufanyi kazi popote pale, nidhamu ya kufanya kazi huwezi ukaijenga. Kama kijana hajapata ajira yoyote alikaa miaka mingi bila ya kupata ajira, itafika wakati inakuwa haajiriki. Hajajenga nidhamu alfajiri inabidi uamke ujitayarishe kwenda kazini, kama huna kazi ni vigumu sana kuwa na nidhamu ya kuweza kuamka asubuhi kujua kwamba siku yako utaitumia namna gani. Unachowaza leo Yarabbi alamiin kikombe cha chai utakipata wapi. Sasa ukiwa katika hali hiyo mwaka mmoja, miaka miwili, miaka mitano, miaka kumi unakuwa na vijana ambao hawajapata nidhamu ya kufanya kazi. Kwa hiyo tunaanza kupoteza vijana wetu. Suala la ajira na taratibu za kuongeza ajira ni suala la msingi kabisa. Endelea...
HIVI sasa Dar es Salaam hapa pana mabenki mengi, lakini hatuna mabenki ambayo yanawasaidia wananchi wa kawaida. Ukiuliza hapa petu katika mkutano wetu au mwananchi yeyote wa kawaida ukimuuliza ni wananchi wangapi ambao wamekuwa na mradi wao wakaweza kupata mkopo ili kuukuza huo mradi, na hapana ambaye ameweza kuja akapewa mkopo na benki yoyote. Utakuta toka kuzaliwa Watanzania wengi hawajapata nafasi yoyote ya kupata mkopo wowote ule hata kama wakiwa na mawazo mazuri ya kuweza kufanya biashara.
Hatuna vyombo vya fedha vya kuweza kuwasaidia wananchi wakaweza kujiajiri, wakaweza kufanya shughuli zao. Sasa CCM inatueleza kwamba aa!! Vijana tujiajiri sisi wenyewe. Hivi kweli kijana anayemaliza darasa la saba,ametoka tu amemaliza darasa la saba anauwezo gani wa kujiajiri mwenyewe? Ukiwauliza viongozi wetu wana watoto wenye umri mkubwa, waulize nyie wenyewe ni wazazi mna watoto wenye umri mkubwa wangapi, vijana wenu walipomaliza shule tu wakajiajiri wenyewe (Makofi). Wakajiajiri wenyewe wakaweza kupata manufaa ya kawaida, ya kuweza kukimu maisha yao, ni wangapi.
Jibu ni kwamba kijana anapomaliza shule hana uwezo wa kujiajiri mwenyewe, lazima pawe na taratibu za mafunzo. Nchi zote hakuna vijana wanaojiajiri wenyewe wakimaliza darasa la saba. Mtu ana miaka 15 - 16 akawa na uwezo wa kujiajiri mwenyewe. Hizi shughuli zinazofanywa za biashara ndogo ndogo, hizi ni shughuli za kujaribu kujikimu (Survival tacticts), ni katika hali maisha yamekuwa magumu inabidi mtu atazame mbinu za kuweza kuishi. Lakini kijana anayemaliza darasa la saba umweleze jiajiri mwenyewe unamfanyia dhihaka. Sasa mabenki tuliyonayo sio mabenki ya kutoa mikopo ya kuweza kuwasaidia wakulima wadogo wadogo, wafanya biashara wadogo wadogo. Na vijana, suala la kujenga uchumi wa kisasa, huwezi ukahimiza bila ya kuwa na vyombo vya fedha. CCM haina sera ya vyombo vya fedha (Makofi).
Katika ilani ya uchaguzi ya CCM ... Uk. 19 kuhusu mashirika ya umma. Ilani ya uchaguzi inasema hivi: CCM itaendelea kuhimiza urekebishaji waliogopa kutumia neno ubinafsishaji, wakatumia urekebishaji wa mashirika ya umma ambao utazingatia sera za CCM. Kwa mashirika ya umma ambayo serikali itaamua kuyaendeleza CCM itahakikisha kuwa mashirika hayo yanaimarishwa na kupatiwa mtaji, wataalamu na teknolojia muafaka ili kuyawezesha kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kwa kuongeza mapato ya serikali, kwa kutoa ajira kwa wananchi na kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi. Hii ni ilani ya CCM kuhusu mashirika ya umma.
Inaendelea kusema kwamba Mashirika ambayo ni ya msingi; bandari, reli, posta, simu, mabenki ya umma na nishati kwa maendeleo ya taifa, yanaendelea na yataendelea kumilikiwa na dola. Wananchi wanaweza kununua sehemu ya hisa katika mashirika hayo ambayo pia yanaweza kuingia ubia na makampuni binafsi mradi tu uwiano wa hisa unalifanya shirika kuwa la Dola.
CCM inaeleza kwamba mabenki ya umma ni msingi wa uchumi, mabenki hayo yataendelea kumilikiwa na Dola. Ndivyo walivyoeleza mwaka 95. Sasa wanafanya nini kwenye mabenki hayo? Haya mabenki hivi sasa yanauzwa, yanapigwa bei. NBC inauzwa, Microfinance inatafutiwa kama kuna mtu anahitaji kununua ainunue. Sasa mimi siulizi kama sera ya kurekebisha NBC, je, NBC iuzwe au isiuzwe, nasema CCM hawana Dira (makofi). Wanayoyaeleza kwenye ilani ya uchaguzi na wanayoyatenda ni mambo mawili tofauti.
Wanaendelea ukurasa wa 21 wanasema sera ya kurekebisha mashirika ya umma itakwenda sambamba na hatua ya kuwalinda wafanyakazi wa mashirika yatakayohusika. CCM iliwaeleza wafanyakazi mwaka '95 kwamba katika kutekeleza sera ya kurekebisha mashirika ya umma wafanyakazi watalindwa. Leo wafanyakazi wa NBC inabidi wapeleke malalamiko yao serikalini kwamba mishahara yetu na haki zetu tuhakikishiwe kwamba tutalipwa kabla hamjauza. Kama mnauza shirika la umma mmeamua kufanya hivyo, basi msituuze na sisi, haki zetu zilipwe. Inawabidi waende mahakamani pamoja na kwamba Ilani ya uchaguzi ya CCM imeeleza kwamba katika kurekebisha mashirika ya umma, wafanyakazi watalindwa. Sasa wafanyakazi inawabidi wajiulize je, serikali ya CCM inawalinda?
Vijana hatuwezi tukajenga uchumi ulio imara ikiwa kama hatuna vyombo vya fedha vya kitaifa. Nchi yetu bado changa, uchumi wetu bado mdogo. Wananchi wengi wakulima wadogo wadogo, wafanya biashara wadogo wadogo,watu wenye viwanda vidogo vidogo hawapati mitaji yoyote. Kwa hiyo ni lazima kujenga vyombo vya kitaifa ambavyo vitahusika na matatizo yanayowakabili wakulima na wafanya biashara wadogo wadogo.
Mabenki ya nje hayatakupa mkopo mkulima wa korosho, mkulima wa nazi hawezi akaenda City Bank kutafuta mkopo, kwanza wala hawatakuruhusu, huwezi ukaweka fedha pale. Ukiwa na chini ya dola 25,000 huwezi kufungua Account. Dola 25,000 kwa sasa ndio karibu zaidi ya shilingi milioni 20 zenyewe hii ni kiwango cha chini cha Account yako. Pamoja na kwamba tunasema hizi hela zetu za madafu, lakini zinapokuwa shilingi milioni 20 ni za kusikia tu hizo. Kwa hali hiyo, hivi vyombo vya nje vinavyokuja haviwezi vikatusaidia wananchi wadogo wadogo, wazalishaji wadogo wadogo. Halafu imekuwa hatuna utaratibu mzuri. Mwaka '95 kulikuwa na Benki hapa Meridian Biao; ikaanguka. Baada ya kuelezwa kuwa Benki ile ni nzuri lakini ikaanguka Serikali ikabidi iingie hasara, lakini mpaka leo hamna tathmini ya kina iliyofanywa na kuwekwa wazi sababu gani iliangusha Benki ile. Hamna tathmini yoyote ya kina iliyofanywa na kuweka wazi kuwaeleza walipa kodi wa nchi hii ambao ilibidi wapate hasara kwa kuanguka kwa Benki ile. Na hapa katikati Benki nyingine zimekuwa zikipata matatizo.
CCM haina dira ya namna gani ya kujenga vyombo vya fedha vya kuweza kuwasaidia wananchi wa Tanzania (Makofi).
Mwaka '95 kuna wataalamu walikaa wakafanya utafiti wa kina, kuna jamaa yangu mfanyabiashara maarufu anaitwa Mutaguzi alikuwa Mwenyekiti wa Kamati hii. Wakaandika ripoti inayotoa mikakati ya kutuwezesha kuongeza bidhaa tunazouza nchi za nje. Katika ripoti hiyo, wataalamu hawa wakasema inawezekana kabisa kwa Tanzania kuongeza bidhaa zake inazouza nchi za nje tokea Dola za Kimarekani milioni 600 mwaka '95 mpaka kufikia Dola za Kimarekani Bilioni 1.7 (1,700,000,000) mwaka 2000. Wameeleza wamechambua sehemu mbalimbali na mazao mbalimbali ambayo tunaweza tukayaongeza. Kama kawaida yetu ripoti hiyo ikawekwa kwenye madawati, wakaiweka kwenye mafaili mpaka leo haijafanyiwa kazi. Uendelezaji wa kuuza hizi bidhaa nchi za nje ulikuwa wa manufaa si tu ya kuongeza bidhaa, lakini pia kuongeza ajira. Ripoti hiyo mpaka hivi leo haijafanyiwa kazi na Rais anadiriki kuwaeleza Watanzania kwamba kila kikucha anachofikiria namna ya kukuza uchumi!
Tuna matatizo ya kimsingi wenzetu hawana dira. Ukitazama Bajeti ya serikali kwa muda wa miaka mitatu na huu wa nne, Rais anajisifu kwamba tumeongeza kukusanya kodi, lakini hajisifu kwamba ukienda hospitali unapata dawa. Kama unakusanya kodi basi tueleze hiyo kodi inakwenda wapi (Makofi).
Bajeti yetu hivi sasa ya serikali, asilimia 30 inapangwa kutumika katika shughuli za maendeleo, asilimia 70 ni matumizi ya kawaida, ndivyo inavyopangwa lakini inavyotumika karibuni asilimia 90 zinatumika kwenye shughuli za kawaida na asilimia 10 tu ndizo zinazotumika katika shughuli za maendeleo. Kila mwaka katika miaka mitatu hii iliyopita ya bajeti, bajeti ya maendeleo imekuwa ndogo lakini pamoja na kuwa ndogo ni nusu tu ya bajeti ya fedha zilizotengwa na bajeti ndizo zilizotumika katika miradi ya maendeleo.
Unasema kwamba unapanga shilingi 100 katika mradi huu ambao utaniwezesha kuzalisha zaidi miaka ijayo ndio serikali inalieleza Bunge, lakini pamoja na kuwaeleza Wabunge namna hiyo, matumizi halisi yanakuwa ni asilimia 50 tu. Na fedha zote hizo ni fedha za wafadhili.
Tunajisifu tunakusanya fedha za kodi, lakini hatuna mchango wowote katika miradi yetu ya maendeleo na hata hizo fedha kidogo zinazopangiwa miradi ya maendeleo hazitumiki katika miradi ya maendeleo. Matokeo yake miundo mbinu yetu inazidi kudidimia.
Vijana tuna matatizo ya kimsingi, lakini hatuna sababu ya kukata tamaa ila tuna uhakika CCM hawana uwezo wa kuleta mabadiliko ya kimsingi ya kuweza kuinua hali za wananchi wa Tanzania (makofi). Uwezo huo hawana. Sasa ikiwa tutawarudisha basi tujue kwamba hali zetu zitaendelea kuwa duni.
Vijana na nyie wenyewe mnaelewa hali halisi ya elimu. Elimu yetu ilivyoanguka, elimu yetu ilivyokuwa ya chini. Vijana wengi hivi sasa, hata hilo darasa la saba hawalimalizi, na hili tatizo limekuwa gumu hasa ukanda, ukitoa Dar es Salaam, ukanda huu wa Pwani. Na moja ya sababu mazingira ya shule, maana unaweza kuwa unakwenda kwenye shule mazingira yake ni ya kupata ugonjwa kuliko kupata elimu (makofi). Maana shule hazina vyoo, shule ziko katika hali mbaya, vitendea kazi havipo, mpaka watu wanakata tamaa wanaona kwamba kumpeleka mtoto shule ni kupoteza muda. Na kweli imefika kiwango ambacho watu wenye uwezo wanapeleka vijana wao kwenye shule za kulipa. Wakubwa wenyewe mpaka wanawapeleka vijana shule ya msingi unampeleka kijana wako Kenya au Uganda! Unatia saini kabisa kwamba unajua shule zetu zimekuwa hazitoi elimu.
Bila elimu kwa uchumi wa kidunia hivi sasa ni hatari kabisa. Hivi sasa shughuli nyingi za kiuchumi zinaenda kwa kutumia Kompyuta. Watu wanafanya biashara, ukitazama kwenye Kompyuta; hivi sasa unaweza ukaenda kutazama ukamkuta jamaa anahitaji embe dodo yuko London zimfikie katika wiki mbili. "Je, kuna mtu mwenye hizo embe aniletee". Taarifa hizi ziko kwenye Kompyuta. Mtu unaweza kuona hii embe hii sio biashara. Mabibo haya, taarifa za biashara zinapatikana katika teknolojia ya Kompyuta.
Kuna wakati nilikuwa niko Helsinki kuna baadhi ya magazeti yetu hapa, unazipata habari za nyumbani kwenye Kompyuta. Sasa Tanzania yetu ya leo vijana wetu wangapi ambao wanapata nafasi ya kuweza kujielimisha na kuweza kupata ni jambo rahisi, unaenda maktaba unaikuta Kompyuta ambayo unaweza kuitumia ukapata habari mbalimbali. Vijana wanamaliza Chuo Kikuu Tanzania hawajatumia Kompyuta.
Nilikuwa nafundisha Chuo kimoja Marekani kinaitwa Williams College, nilitokea hapa Dar es Salaam nilikwenda huko ilibidi nitumie muda mrefu niwe na uhakika wa kujua taratibu hizo, kwa sababu wanafunzi unaowafundisha, unawapa zoezi, ukiwapa zoezi wanalifanya hilo zoezi halafu wanakutumia wako vyumbani mwao, wanakutumia kwa Komputa ulisome kwa Kompyuta yako. Yeye ameshafanya zoezi, umempa kazi kafanya amemaliza, kama ni page sita, kumi kaandika halafu amekutumia. Sasa wewe mwenyewe ufungue usome, umsahihishie umueleze amepata "grade" hiyo, huna haja ukutane naye uso kwa uso. Sasa vijana wenu hapa hawana hali ya uzoefu wa kutumia Kompyuta. Tuna sera gani ya kusaidia vijana walioko Secondary Schools waweze kuwa na uzoefu wa kuwasiliana kwa kutumia Kompyuta.
Tunaingia karne ya 21, mwakani ni karne ya 21, mwaka 2000. Ilani ya uchaguzi inazungumzia sayansi na teknolojia, lipi serikali inafanya walau kwa kuanzia tu, kufanya shule zetu hizi hapa za Dar es Salaam vijana wapate elimu ya kuwawezesha wawe wabunifu katika karne tunayoingia. Kuna makampuni yanasaidia saidia kuendeleza ujuzi wa matumizi ya Kompyuta katika nchi zetu hizi. Kuna mashirika yanasaidia saidia lakini waulize viongozi wa CCM wanafanya nini ili na sisi tuwe katika mkumbo huo wa maendeleo ya sasa.
Wanasema sasa Bwana wewe unazungumzia mambo ya Kompyuta sisi vijana wetu hawana madawati. Tena wanakueleza "unazungumzia mambo gani". Madawati hawana, watu wanakaa chini, wewe unazungumzia kompyuta. Umeme sio wa uhakika, utakuwaje na mawasiliano ya kompyuta. Kompyuta hazitumii umeme mwingi lakini uwe wa uhakika basi.
Vijana tatizo letu la msingi ni kwamba CCM haina dira (makofi). CCM haina sera (Makofi).
Wanasema kwamba tujaribu tupigane, maadui wetu wakubwa ni umaskini. Tuufute umasikini. Palikuwa na kongamano nzima ya serikali Dodoma, kama kawaida watu ambao sio wa CCM hawapewi nafasi katika kongamano hizo. Lakini utakuwaje na sera ya kufuta umasikini ikiwa hujui una Watanzania wangapi katika nchi yako! Hata kuhesabu watu ili tuwe na uhakika kwamba tuko wangapi, vijana wangapi wa kwenda shule ili tuwe tunajua kwa uhakika ni asilimia ngapi ya vijana wetu wanaoenda shule, kuna uwiano gani kati ya watu na ardhi katika sehemu mbalimbali za taifa letu. CCM inakataa hata kuhesabu watu!
Kama kuna suala muhimu kwa serikali ni kuelewa idadi ya wananchi ulionao katika taifa lako. Tena wako watu wanasaidia kazi hizo. Mashirika ya kimataifa yanatoa misaada, yametoa magari, yametoa kompyuta. Serikali inasema imeahirisha mpaka itakapotangazwa baadaye kwa sababu ya kukosa fedha. Tunazo fedha za Tume ya Waraka Namba Moja wa kuhalalisha matakwa ya CCM. Lakini hatuna fedha za kusimamia sensa kuweza kupanga mipango ya maendeleo ya nchi yetu.
Wala tusistaajabu kwamba hizi ni serikali za vipi, miaka 40 baada ya uhuru watu hawahitaji, na suala hili linajulikana toka mwaka 88 tunaelewa kwamba ifikapo mwaka 98 inatubidi kufanya sensa. Haya serikali ya awamu ya tatu '95 unaingia katika madaraka jambo kubwa la msingi unalojua lazima ulifanye katika kipindi chako ni kujua una watu wangapi. Tuna dhoruba kubwa zimekupitia hapa, pana tatizo la ukimwi, linatumaliza, linapunguza vijana. Hatutaki hata kujua matokeo ya madhara haya? Vijana, vijana wenzetu hawana dira. (makofi)
Na mwisho ambalo nilikuwa nalihitaji kuzungumza kwa ujumla ni huduma za afya. Hivi sasa katika nchi yetu wastani wa maisha anayoishi kijana toka mtoto akizaliwa leo, wastani wa miaka yake ukilinganisha na mtoto aliyezaliwa mwaka 90 wastani wa maisha umepungua. Nadhani tulikuwa tumefikia wastani wa miaka 52, hivi sasa tutakuwa na bahati ikiwa tuna miaka 48. Wastani wa maisha umepungua.
Mwalimu alipokuwa anasherehekea miaka 75 ya maisha alisema kwamba yeye atafikisha miaka 100... lakini tunahitaji vijana wanaozaliwa leo nao wafike huko ... lakini hali ya huduma zetu za afya zimekuwa finyu sana. Na hii dhoruba iliyotupata ya ukimwi tumeonea aibu kuizungumza. Miaka ya '80 ilikuwa inaonekana labda ni mbinu tu za mataifa ya Magharibi kutudhalilisha Waafrika na mpaka leo hapa petu huwezi ukathubutu kueleza fulani anaumwa ukimwi hadharani. Huthubutu. Ni jambo tunalionea aibu, tunalionea haya, lakini matokeo yake tunamalizika. Na vijana ndio wanaoteseka zaidi. Inatubidi tuwe wazi na tatizo hili, tuwe wazi, na vijana wenyewe tusiwe na hisia za kisiasa. Tuwe na taratibu ya vijana wote wa Kitanzania kuweza kulijadili na kulikabili jambo hili... (makofi), kwa sababu ni hatari kubwa. Na tuwe na vituo vingi basi upande wa serikali... Vijana kwenye vikundi vyetu, na hili halina chama, halina itikadi na ndio maana ni vizuri pamoja nakuwa vyama vya siasa kuwa na vijana wao ni vizuri kuwa na jumuiya za vijana ambazo hazina muelekeo wa kisiasa. Pawepo na vijana wa chama washughulikie mambo ya chama, lakini kama taifa wawe na jumuiya ya vijana isiyokuwa na muelekeo wa kiitikadi kushughulikia matatizo ya vijana. (Makofi).
Hivi sasa vijana hawana ajira sio vijana wa CUF tu, wa CCM hawana ajira, wa CHADEMA, UDP hawana ajira, ni vizuri kuwa na jumuiya hizo ambazo zitatazama matatizo ya vijana bila ya kuwa na muelekeo wa kisiasa. Tatizo la ukimwi ni tatizo baya sana kwa vijana.
Vile vile kina mama, wenzetu wanahitaji sana ukiritimba kutumia kina mama kisiasa. Wakati umefika kwa jumuiya hizi za kina mama zisiwe za vyama tu. Ziwe zile Jumuiya ambazo zinatazama matatizo ya kinamama, matatizo ya vijana bila kujali itikadi (Makofi). Lakini la msingi vijana wenzangu ni kwamba tumefika mahali ambapo ikiwa tutaendelea na sera zenye njaa basi tuwe na uhakika kabisa hali zetu zitaendelea kudidimia. (Makofi).
Kazi tuliyo nayo ni moja ... vijana tuhakikishe chama chetu kinapendwa na wananchi kwa sababu ya vitendo vya chama chetu miongoni mwa jamii. (Makofi)...
Ahsanteni Sana.
|
|